TANZIA .MCHEZAJI WA KLABU YA KIZIMBANI UNITED RASHID SERENGE AFARIKI DUNIA GHAFLA AKITOKA MAZOEZINI

May 09, 2014

Na Masanja Mabula –Pemba .
 
Tasnia ya michezo Kisiwani Pemba imekumbwa na  simanzi kufuatia kifo cha  Mchezaji wa Klabu ya Kizimbani  United Rashid Abdalla Serenge kufariki ghafla wakati akitoka kwenye mazoezi kwenye   uwanja wa Mnazi Mmoja  .
 
Mchezaji huyo ambaye amewahi  kuzitumkia  timu mbali mbali zinazoshiriki madaraja tofauti Kisiwani Pemba amefikwa na mauti hayo juzi baada ya kuanguka na kufariki dunia na kuacha simanzi kwa wapenda soka Kisiwani hapa .
 
Mmoja wa marafiki wa karibu wa Mchezaji huyo ameeleza kwamba kifo cha Serenge kimewashtua  kutokana na kwamba alikuwa ni kiungo kwa wachezaji wenzake mazoezini  pamoja na benchi zima la uongozi wa Klabu hiyo .
 
“Licha ya kwamba hatuwa katika klabu moja , lakini tulikuwa tunakutana mazoezini , kwa kweli alikuwa ni mchezaji mwenye nidhamu na mshauri wa karibu wa wachezaji na viongozi wa klabu yake , lazima tukubali kwamba hili ni pigo ” alifahamisha Hosein Omar .

Kwa upande wake mlinda mlango namba wa klabu ya Mwenge Jafar Said Talib amesema kuwa mafanikio yake katika michezo yametokana na ushawishi wa Serenge ambaye amekuwa akimhimiza kudhuruia mazoezi kwa wakati pamoja na kuzingatia suala la nidhamu uwanjani .

"Alikuwa ni mchezaji anayependa wenzake waendelee kisoka , muda wote alikuwa ananihimiza kufika mazoezi kwa wakati pamoja na kuwa na nidhamu kwa wenzangu viongozi wa klabu yangu " alieleza Jafar

Naye Meneja wa Klabu ya  Kizimbani United Juma Ali amesema kuwa pamoja na Serenge kuwa ni mchezaji wa  timu yake pia uongozi ulikuwa unamtumia kama ni Msaidizi wa Meneja na wakati wate alikuwa karibu sana na uongozi wa timu hiyo .
 
Amesema kuwa hata wakati timu ilipokuwa ikisafiri kwenda Unguja kushiriki ligi Kuu msimu uliomalizika hivi karibuni , Serenge ndiye alikuwa akiishuhulikia timu na kuongeza kwamba pengo lake haliwezi kuzibika upesi .
 
“Uongozi wa timu ya Kizimbani kwa ukweli umepoteza moja ya nguzo na muhimili  mkuu , kwani kwa kipindi ambacho timu ilikuwa inashiriki ligi kuu , Serenge alikuwa anafanya kazi kwa kumsaidia Meneja , ni pengo kwetu ”alieleza .
 
Katika uhai wake Serenge amewahi kuzichezea timu mbali mbali ambapo alianza soka kwa kuichezea timu ya Biashara iliyokuwa ikishiriki ligi ya Juvenile , African Kids daraja la pili hadi ligi Kuu Zanzibar , New Stars ya daraja la kwanza  pamoja na Kizimbani United .
 
Mwisho .

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »