TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
A; MKUTANO MKUU AIPS
WIKI iliyopita kulifanyika Mkutano Mkuu wa Chama cha Kimataifa cha Waandishi wa Habari za Michezo (AIPS) jijini Baku, Azerbaijan.
Mkutano
huo ulishirikisha viongozi wa vyama 116 vya waandishi wa habari za
michezo duniani, ambapo Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo
Tanzania (TASWA), kiliwakilishwa na Katibu Mkuu, Amir Mhando.
Katika
mkutano huo msisitizo mkubwa umewekwa kwa nchi wanachama kutilia mkazo
program za kuwaendeleza waandishi chipukizi wa habari za michezo, lakini
pia AIPS yenyewe nayo pamoja na Chama cha Waandishi wa Habari za
Michezo Afrika (AIPS-Afrika) vimechukua jukumu la kusaidia kwa wale
watakaokidhi vigezo wanavyohitaji.
Hivyo
kila nchi mwanachama itatuma wasifu wa majina ya wanahabari chipukizi
wasiozidi watano, ambao AIPS yenyewe itaangalia wale watakaofaa na
kuwaandalia mafunzo baadaye mwaka huu.
Kwa
upande wa AIPS Afrika yenyewe itaendesha mafunzo kwa wanahabari
chipukizi 25, ambayo yatafanyika Morocco, lakini kipaumbele cha kwanza
kitakuwa kwa nchi 16 zitakazocheza fainali za mataifa ya Afrika mwakani
nchini humo na nafasi zingine zitabaki kwa nchi ambazo hazitaenda
Morocco.
Mafunzo
ni ya wazi kwa waandishi wowote chipukizi wasiozidi umri wa miaka 25,
hata wale waliopo kwenye vyuo vya uandishi wa habari wataruhusiwa
kuomba. Tanzania imewahi kupata nafasi moja mwaka 2011, ambapo Mwita
Mwaikenda wakati huo akiwa mwanafunzo wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,
alishiriki mafunzo hayo yaliyoandaliwa na AIPS akiwa miongoni mwa
Waafrika watatu tu waliopata nafasi hiyo.
Utaratibu
kuhusiana na suala hili utaelezwa vizuri baada ya kikao cha Kamati ya
Utendaji ya TASWA kitakachofanyika Jumatatu wiki ijayo kujadili masuala
mbalimbali.
B: Ziara Uganda
Kulifanyika
kikao cha viongozi wa nchi wanachama wa AIPS ambao wanatoka Afrika
Mashariki, ambapo nchi za Burundi, Kenya, Tanzania na Uganda zilishiriki
na kukubaliana kufanyike ziara ya kimafunzo itakayohusisha waaandishi
wa habari za michezo Septemba 25-29 mwaka huu Kampala, Uganda. Rwanda
licha ya kutoshiriki mkutano wa AIPS, lakini tulikubaliana nayo ialikwe.
Katika
makubaliano hayo kila nchi itakuwa na washiriki wasiopungua 20 na
wasiozidi 35, ambapo pia litafanyika kongamano kuhusiana na masuala
mbalimbali ya waandishi wa habari za michezo kwa ukanda huo na siku ya
mwisho litafanyika bonanza la michezo mbalimbali. Taarifa zaidi za ziara
hiyo itatolewa siku za usoni.
C; Ushirikiano wa kimafunzo
Baadhi
ya nchi zilizoshiriki mkutano huo wa 77 wa AIPS, zilikubaliana
kuanzisha utaratibu wa kubadilishana utaalamu wa kitaaluma kwa nchi
mbalimbali, kwa kuwatoa baadhi ya wanahabari kwenda nchi zilizo katika
makubaliano hayo kujifunza kwa gharama za nchi mwenyeji.
Hata
hivyo makubaliano hayo, yataanza kufanya kazi baada ya kila nchi kupata
baraka za Kamati ya Utendaji na kutuma majibu kwa waratibu kwamba
wanaafiki. Kamati ya Utendaji ya TASWA katika kikao chake kijacho hilo
litakuwa moja ya ajenda.
Nawasilisha
Amir Mhando
Katibu Mkuu TASWA
07/05/2014
EmoticonEmoticon