MSHABIKI MBARONI KWA MADAI YA TIKETI FEKI

February 03, 2014
Release No. 018
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Februari 3, 2014

Mshabiki mmoja anashikiliwa na Jeshi la Polisi akidaiwa kukutwa na tiketi bandia kwenye mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kati ya Yanga na Simba iliyochezwa jana (Februari 2 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Matei Cosmas (28) ambaye ni mkazi wa Buza Njiapanda Kitunda, Dar es Salaam amefunguliwa jalada namba CHA/IR/900/2014 kwenye Kituo cha Polisi Chang’ombe akidaiwa kupatikana na tiketi bandia.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) leo asubuhi (Februari 3 mwaka huu) limeamkia Kituo cha Polisi Chang’ombe kusaini hati ya maelezo dhidi ya mtuhumiwa.

Ni imani ya Shirikisho kuwa mtuhumiwa atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria za nchini.

Tunatoa mwito kwa washabiki wa mpira wa miguu kuepuka kununua tiketi kutoka mikononi mwa watu, kwani kufanya hivyo ni kosa. Tiketi zinauzwa kwenye sehemu maalumu zenye chapa ya TFF.

RAIS WA TFF ATEMBELEA RUANGWA
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi ametembelea Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi.

Katika ziara hiyo aliyoifanya jana (Februari 2 mwaka huu), pia alikuwa mgeni rasmi mechi ya kugombea Kombe la Majaliwa kati ya Hull City na Mbagala City, na kuahidi kuwa TFF itaandaa kozi za awali za ukocha na uamuzi kwa Wilaya ya Ruangwa.

RAMBIRAMBI MSIBA WA OMARI CHANGA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha aliyekuwa mchezaji wa Vijana, Moro United na Yanga, Omari Changa kilichotokea juzi (Februari 1 mwaka huu) jijini Dar es Salaam.

Msiba huo ni mkubwa katika familia ya mpira wa miguu kwani Changa wakati wake uwanjani akichezea timu mbalimbali alitoa mchango mkubwa ambao tutaukumbuka daima.

TFF tunatoa pole kwa familia ya marehemu Changa, klabu ya Moro United na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.

Katika maziko TFF itawakilishwa na mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Kidao Wilfred, na imetoa rambirambi ya sh. 200,000.

Boniface Wambura Mgoyo
Ofisa Habari na Mawasiliano
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »