Na Mbonea Herman Tanga.
HOSPITALI ya Mkoa wa Tanga Bombo inakabiliwa na upungufu
mkubwa wa damu jambo ambalo linaweza kuchangia kuongezeka kwa vifo vya wagonjwa
wanaokuja kutibiwa katika hospitali hiyo.
Kufuatia jambo hilo,Club ya waandishi wa Habari Mkoa wa
Tanga(TPC)imeamua kufanya kampeini ya kuwahamasisha wananchi kuchangia damu kwa
hiari.
Mratibu wa Huduma za Maabara Mkoa wa Tanga,Mussa Juma
alisema kwamba uhitaji wa hospitali hiyo ni Unit 15 kwa siku wakati wanapatiwa wakati
mwingine Unity ishirini kwa wiki kiwango ambacho hakilingani na mahitaji.
“Sisi tunapokea mgawo wa damu kutoka kituo cha kanda ya
hospitali ya rufaa KCMC kiwango hicho ni kidogo lakini haya yote yanatoana na
uhaba wa damu uliopo katika kituo hicho,”alisema Juma.
Juma alisema kama wananchi wangejengewa utamaduni wa
kuchangia damu kwa hiari taifa lingeweza kuondokana na tatizo hilo ambalo kwa
sasa linaonekana kugharimu maisha ya watanzania waliowengi.
Juma alisema pia kwamba kitendo cha hospitali kutegemea
vituo vya damu salama vya kanda kinachangia upatikanaji mgumu wa damu katika
hospitali zile ambazo zipo mbali na kituo hicho.
Aidha Mratibu huyo alishauri kuwa na vituo vya damu
salama ngazi ya Mkoa ili kuondokana na adha ya kuifuata damu umbali mrefu
wakati yupo mgonjwa mahututi nayehitaji huduma hiyo kwa haraka.
Akizungumzia uhaba wa damu nchini Mwenyekiti wa
(TPC)Hassan Hashim alisema katika kukabiliana na swala hilo waandishi wa habari
watajikita katika kuihamasicha jamii kupitia vyombo vyao kama sehemu ya
kumaliza tatizo hilo,
Naye Katibu wa Club hiyo Lulu George alisema kazi hiyo
itaanza May 21 mwaka huu katika Wilaya za Moa wa Tanga.
MWISHO.
EmoticonEmoticon