Kg 178 za Bangi zakamatwa Tanga.

April 20, 2013
Na Oscar Assenga, Sussan Uhinga, Tanga.
JESHI la Polisi Mkoa wa Tanga limefanikiwa kukamata kg 178 za madawa ya kulevya aina ya bangi zenye thamani ya sh.milioni 2,670,000 katika matukio mawili tofauti mkoani hapa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana,Kamanda wa Polisi mkoa wa Tanga,Constatine Massawe alisema katika tukio la kwanza lilitokea Aprili 19 majira ya 2.45 usiku kufuatia taarifa toka kwa wasamaria wema na askari walifika eneo la Mwanzang’ombe Chumbageni jijini Tanga, kwenye nyumba ya Hemed Salum Hugo ambaye alifanikiwa kutoroka kabla ya polisi kufika eneo hilo.

Alisema baada ya polisi kufika katika eneo hilo walianza kupekua nyumba hiyo na kukuta madawa ya kulevya aina ya bangi kg 100 ambayo ilikuwa imepakiwa kwenye vifurushi na nyengine ilikuwa imehifadhiwa katika maeneo mengine ndani ya nyumba hiyo.

Aidha kamanda Massawe alisema Jeshi hilo linaendelea kumtafuta mtuhumiwa huyo ili kuweza kujibu tuhuma zinazomkabili pamoja na kufikishwa mahakamani.

Hata hivyo kamanda Massawe alitoa wito kwa wananchi wanaojishughulisha na biashara ya uuzaji wa bangi kuwaonea huruma wenzao na kuacha mara moja kwani ina madhara makubwa kwa watumiaji.

Alisema madawa mengine ya kulevya aina ya bangi kg 78 yalikamatwa katika eneo la barabara iendeyo horohoro wakati polisi wakiwa katika doria na walikutana na mwendesha baiskeli ambaye alikuwa amebeba gunia lenye madawa ya kulevya aina ya bangi ambapo alipowaona polisi alilitupa gunia hilo na kukimbia

Wakati huo huo,Jeshi la Polisi mkoa wa Tanga linamshikilia kondakta wa basi lenye namba za usajili T.398 CEK Juma Salehe (32) kwa kosa la kukutwa na kg 52 za madawa ya kulevya aina ya mirungi katika basi hilo.

Kamanda Massawe alisema tukio hilo lilitokea Aprili 18 mwaka huu majira ya saa kumi na moja jioni eneo la Zingibari kufuatia polisi wa usalama barabarani kulisimamisha basi hilo na kuanza kulipekua na kukuta madawa hayo.

Alisema baada ya askari hao kuanza kulipekua basi hilo ilikutwa mirungi yenye kg 55 ambayo alikutwa nayo Juma Salehe ambaye ni msafirishaji na kueleza kuwa mtuhumiwa huyo anashikiliwa na jeshi hilo kwa ajili ya kufikishwa mahakamani.

Mwisho.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »