RAIS SAMIA AONGOZA KIKAO CHA KAMATI KUU YA CCM KINACHOTEUA WAGOMBEA UBUNGE

August 21, 2025 Add Comment

 


Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiongoza Kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa,kilichoketi leo Agosti 21,2025 Jijini Dodoma kwa ajili ya kufanya uteuzi wa Wagombea Ubunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Wabunge wa Viti Maalum,Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Viti Maalum.  

WATUMISHI WAHIMIZWA KUJENGA MAKAZI KABLA YA KUSTAAFU

August 21, 2025 Add Comment


📌 Wasisitizwa kuzingatia Maadili ya Utumishi wa umma


📌Mramba apongezwa kwa kutatua Changamoto za Watumishi


Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, amewahimiza watumishi wa umma kutumia fursa zilizopo katika taasisi za kifedha kwa ajili ya kujiimarisha kiuchumi, ikiwemo kujenga makazi yao binafsi kabla ya kustaafu.

Ushauri huo umetolewa Agosti 20, 2025, wakati Katibu Mkuu huyo alipokutana na wafanyakazi wa wizara hiyo katika kikao cha ndani kilichofanyika jijini Dodoma.


“Tumieni fursa ya mikopo inayotolewa na taasisi za kifedha nchini ili mjenge maisha yenu mapema. Msisubiri hadi mstaafu ndipo muanze kufikiria kujenga nyumba ya kuishi,” alisisitiza Mhandisi Mramba.

Aidha, alikumbusha watumishi kuendelea kuzingatia maadili ya utumishi wa umma kwa kuwa na nidhamu, weledi, na kuepuka vitendo vya rushwa, sambamba na kutunza mali za serikali kama kompyuta na vifaa vingine vya ofisi.

“Serikali inatumia gharama kubwa kuhakikisha upatikanaji wa vifaa vya kazi kwa ajili ya kuwahudumia wananchi. Ni wajibu wetu kuvithamini na kuvitumia kwa tija,” aliongeza.


Katika kikao hicho, watumishi walimpongeza Katibu Mkuu kwa utaratibu wake wa kuwa karibu nao kwa kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili, hatua waliyoieleza kuwa imeongeza hamasa na uwajibikaji kazini.

Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. James Peter, Wakuu wa Idara na Vitengo kutoka wizara hiyo pamoja na watendaji kutoka taasisi mbalimbali za serikali.





WAZIRI KOMBO AWASILI JIJINI YOKOHAMA (JAPAN) KUSHIRIKI MKUTANO WA WAKUU WA NCHI NA SERIKALI WA TICAD 9

August 20, 2025 Add Comment
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) amewasili jijini Yokohama, Japan kumwakilisha Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mkutano wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika (Tokyo International Conference on African Development-TICAD 9) ambao unafanyika kwa ngazi ya Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika na Japan kuanzia tarehe 20-22 Agosti 2025.

KASI NDOGO YA UTEKELEZAJI MRADI WA UMEME WA CHALINZE-DODOMA YAMKASIRISHA DKT.BITEKO

August 20, 2025 Add Comment




📌 *Asikitishwa mradi huo aliouzindua Novemba 2024 kuwa nyuma kwa asilimia Saba*


📌 *Asema Rais Samia alitoa agizo mradi usichezewe kutokana na umuhimu wake katika  mikoa mbalimbali ikiwemo ya Magharibi*


📌 *Asema sababu zilizotolewa na mkandarasi  (TBEA) za kusuasua kwa mradi hazikubaliki*


📌 *Atoa maagizo kwa Mkandarasi kuwasilisha mpango kazi mpya kwa Katibu Mkuu  Wizara ya Nishati  ili kufidia muda uliopotezwa*


📌;*Aagiza TANESCO kutumia mapato ya ndani kulipa fidia wananchi wanaopisha mradi*


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amekagua mradi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilovolti 400 kutoka Chalinze  hadi Zuzu Dodoma na kueleza kutoridhishwa kwake na utekelezaji wa mradi huo ambao  ulipaswa kuwa umefikia asilimia 31 lakini kwa sasa  umefikia asilimia 24 tangu kuzinduliwa kwake Novemba mwaka 2024. 


Hali ya kusuasua kwa mradi imebainika wakati Dkt. Biteko akikagua mradi huo katika Kijiji cha Manchali wilayani Chamwino mkoani Dodoma tarehe 20 Agosti 2025 ambapo Dkt. Biteko amemuagiza mkandarasi kampuni ya TBEA ya China kuhakikisha kuwa anafidia muda wa kazi uliopotezwa wa asilimia Saba ili mradi ukamilike kwa wakati kutokana na umuhimu wake nchini.

Mwezi Novemba, 2024 Serikali ilikubaliana na mkandarasi kuwa mradi huo ufanyike ndani ya miezi 19 tu badala ya miezi 22 kwani wakati mradi unazinduliwa tayari kazi kubwa za awali zilikuwa zimeshafanyika ikiwemo za upembuzi yakinifu na utoaji wa maeneo. 

“ Leo ni miezi saba imepita tangu tuzindue mradi sawa na asilimia 32 ya muda wote tuliokuwa tunahitaji  kutekeleza mradi huu, na tulitegemea mradi kwa sasa ufikie asilimia 31 lakini katika hali ya kushangaza mradi umefikia asilimia 24 tu jambo ambalo halikubaliki.” Amesema Dkt. Biteko


Dkt. Biteko ameeleza kuwa, sababu zilizotolewa na Mkandarasi za kuchelewesha mradi ikiwemo ya wananchi kugoma kutoa maeneo kwa madai ya fidia na kukutana na miamba katika mkuza wa mradi hazikubaliki kwani  wananchi  hao wana haki na  lazima walipwe fidia.


Kutokana na hali hiyo, ameagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO)  kutumia mapato yake ya ndani kulipa fidia wananchi waliopisha mradi.


Dkt. Biteko ametanabaisha kuwa mkandarasi alishaagizwa asiutekeleze mradi huo kwa mazoea kutokana na umuhimu wake kwani kwa sasa  miundombinu inayosafirisha umeme kwenda  Dodoma kutoka mradi wa Julius Nyerere (JNHPP) kupitia kituo cha  Chalinze  inabeba umeme kidogo kwa takriban megawati 240 tu ambayo ni sawa na mashine moja tu kati ya mashine 9 za JNHPP hivyo njia hiyo mpya ya umeme ya kV 400 inayojengwa ni muhimu.

Amesisitiza kuwa njia mpya ya umeme ya kV 400 ni muhimu kwani katika Mkoa wa Dodoma mahitaji ya umeme yanaongezka kila siku huku mkoa huo pia ukiwa ni kitovu cha usambazaji umeme katika mikoa yote ya Magharibi ikiwemo Singida, Tabora, Shinyanga Mara na Kigoma ambayo inategemea utulivu wa umeme katika Mkoa wa huo na kwamba  Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan alishaagiza kuwa mradi huo usichezewe hivyo Mkandarasi ahakikishe kuwa anaupa umakini  mkubwa.


Kutokana na mradi huo kuwa nyuma katika utekelezaji,  Dkt. Biteko  amemuagiza Mkandarasi kuja na mpango mpya wa utekelezaji wa kazi ukiwemo wa kufidia muda uliopotezwa ambapo ametoa siku nne mpango wa fidia ya muda uwasilishwe kwa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati.

Vilevile, Dkt. Biteko ameagiza mkandarasi kuongeza nguvu kazi ya watu ili minara 917 ya umeme inayopaswa kujengwa kwenye mradi huo ijengwe kwani kwa sasa mkandarasi amechimba takriban  mashimo 100 tu kwa ajili ya usimikaji wa minara. Pia amemtaka Mhandisi mshauri wa mradi kuhakikisha anasimamia mradi huo kwa ufanisi na aeleze ukweli pale anapoona kuwa hauendi sawa.


Aidha amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, kutengeneza timu itakayoungana na TANESCO kuusimamia mradi huo na kila wiki taarifa itolewe kuwa umefikia wapi.

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amewaasa Wananchi kutozuia utekelezaji wa miradi pale inapopita kwenye maeneo yao na Serikali kwa upande wake itahakikisha kuwa wanapata haki wanazostahili kwani Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshaelekeza kuwa hataki wananchi wafanyiwe dhuluma ambapo wasaidizi wake wanahakikisha kuwa agizo hilo linatekelezwa.


Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amesema  mradi huo wa usafirishaji umeme wa kV 400 kunaenda kuifanya Dodoma kuwa kitovu cha usambazaji umeme nchini.

Aidha, ameahidi kuyasimamia maelekezo yote yaliyotolewa na Dkt. Biteko ya kuhakikisha kuwa mradi huo unakamilika kwa wakati ili kuwezesha umeme huo utakaofikishwa Dodoma, kusambazwa pia kwenye maeneo mengine nchini.


Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Lazaro Twange amesema Mradi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 400 kutoka Chalinze hadi Dodoma unakusudia kusafirisha umeme wote unaozalishwa kutoka katika Bwawa la kuzalisha umeme la Julius Nyerere (Megawati  2,115) na kuingiza kwenye gridi ya Taifa kisha  kuufikisha kwenye maeneo yote yenye mahitaji ya umeme.


Amesema mkataba na mkandarasi kampuni ya TBEA ulisainiwa mwaka 2024 na mradi kuanza kutekelezwa mwezi Novemba 2024 ambapo mkandarasi ameshalipwa awamu ya kwanza ya malipo ambayo ni shilingi za kitanzania bilioni 107 na mhandisi mshauri ameshalipwa asilimia 15 ya malipo yake.



Ameeleza kuwa maagizo yote yaliyotolewa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa  Nishati yatafanyiwa kazi ikiwemo ya kuhakikisha kuwa mradi unakamilika mwezi Juni au kabla ya Juni 2026 kwa mujibu wa mkataba.



Aidha, Ameishukuru Serikali chini ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa shilingi bilioni 513 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo ambao utakuwa na urefu wa kilometa 345 na kuhusisha minara ya umeme ipatayo 917 kutoka Chalinze mkoani Pwani hadi Zuzu mkoani Dodoma.


Mwisho

MKUTANO WA TISA WA WAKUU WA NCHI NA SERIKALI WA TICAD WAANZA JIJINI YOKOHAMA, JAPAN.

August 20, 2025 Add Comment
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni mojawapo ya Nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) ambazo zinashiriki katika Mkutano wa Tisa wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika unaojulikana kama TICAD 9.

Mkutano wa TICAD 9 Summit, umefunguliwa leo tarehe 20 Agosti 2025 kwa pamoja na Mheshimiwa Shigeru Ishiba, Waziri Mkuu wa Japan; Mheshimiwa João Lourenço, Rais wa Jamhuri ya Angola na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU); Mheshimiwa António Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN); Mheshimiwa Mahmoud Ali Youssouf, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AUC); Bw. Haoliang Xu, Acting Administrator and UNDP Associate Administrator; na Bw. Makhtar Diop, Mkurugenzi Mtendaji wa International Finance Corporation (IFC) kwa niaba ya Rais wa Benki ya Dunia.

Katika hotuba ya ufunguzi ya Waziri Mkuu wa Japan, Japan imeahidi kuendeleza ushirikiano wa kimkakati na Nchi za Afrika katika maeneo makuu matatu ya: Uchumi, Jamii, Ulinzi na Usalama.

Mahususi kabisa Japan imeahidi kushirikiana na Afrika katika kutatua changamoto za madeni yasiyohimilika; kuimarisha mtangamano wa Afrika; ushirikiano wa kikanda kupitia utekelezaji wa Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA); kukuza sekta binafsi ya Afrika kwa kuwezesha ushirikiano na sekta binafsi ya Japan; kuimarisha maendeleo ya rasilimali watu hususan katika kuwezesha vijana na wanawake kupitia program za mafunzo, startups, na kuunga mkono juhudi za Afrika za Huduma Bora ya Afya kwa watu wote.