SERIKALI KUTOA MAFUNZO KWA WAANDISHI WA BLOGU
Na Mwandishi Wetu
Serikali imekubali kutoa mafunzo maalum kwa waandishi wa blogu kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025, hatua muhimu itakayowajengea uwezo na kuwaandaa kubeba dhamana kubwa ya usambazaji wa habari sahihi.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wizara ya Habari,Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa katika Mkutamo wa Wadau Kujadili Mchango wa Sekta ya habari Katika kufanikisha uchaguzi Mkuu 2025.
Katika mkutano huo kipindi cha majadiliano Mwenyekiti wa Chama cha Mabloga Tanzania (TBN), Beda Msimbe, aliomba serikali kuona umuhimu wa kufunza mabloga wengi ambao sio waandishi lakini wanatengeneza maudhui kuwa na weledi kuandika masuala ya siasa kuelekea uchaguzi mkuu.
Akizungumza kwenye mkutano huo uliofanyika Mlimani City jijini Dar es Salaam, Julai 9, 2025, Bwana Msimbe alisisitiza umuhimu wa kuwajengea uwezo mabloga, akibainisha kuwa, "Wao wanabeba dhamana kubwa kutokana na wingi wao na wanatengeneza maudhui, na wengine si waandishi wa habari."
Aliongeza kuwa katika ulimwengu wa sasa wa teknolojia na akili bandia (AI), vyanzo vya habari vinavyotegemewa zaidi si mitandao ya kijamii, bali maandishi yanayopatikana kwenye blogu na tovuti, hivyo kufanya uhitaji wa mafunzo kuwa mkubwa zaidi.
Bwana Msimbe alitumia fursa hiyo kupongeza uamuzi wa kuandaa kikao hicho muhimu cha wadau, akisema kuwa ni hatua inayostahili kuelekea uchaguzi wa haki na uwazi. Licha ya changamoto ya mada nyingi (tisa) kujadiliwa ndani ya siku moja, alipongeza mkutano huo na jinsi ulivyokwenda.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Ndugu Msigwa, aliiagiza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuandaa mafunzo hayo mapema iwezekanavyo.
Kauli hiyo ya serikali imetafsiriwa na wadau mbalimbali kama hatua ya kutambuliwa rasmi kwa mchango wa mabloga katika tasnia ya habari na katika mchakato wa kidemokrasia.
Chama cha Mabloga Tanzania (TBN) kina wanachama zaidi ya 200 waliotawanyika kote nchini na nchi za nje, hivyo mafunzo haya yatakuwa na athari kubwa katika kuhakikisha usambazaji wa habari sahihi, zenye vigezo vya kitaaluma, na zinazozingatia maadili ya uandishi wa habari wakati wa kipindi cha uchaguzi na baadae.
Mkutano huo ulifunguliwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dk Doto Biteko ambaye alitaka vyombo vya habari na vya usalama kuhakikisha Amani na kuvumiliana kuelekea katika uchaguzi huo.
mwisho
TANZANIA INA UMEME WA KUTOSHA -DKT.BITEKO
📌 Asema ni jitihada za uwekezaji uliofanywa na Rais Dkt. Samia
📌 Aipongeza TANESCO kwa kuhakikisha wananchi wanapata umeme wa uhakika
Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema Tanzania ina umeme wa kutosha hatua ambayo imechangiwa na kukamilika kwa Miradi mikubwa ya uzalishaji umeme ukiwemo Mradi wa Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP) ambao pekee unazalisha Megawati 2115.
Naibu Waziri Mkuu ameyasema hayo Julai 10, 2025 wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya miradi ya kuzalisha umeme kwa gesi asilia katika vituo vya Kinyerezi I, Kinyerezi I Extension na Kinyerezi II ambapo amesema licha ya kazi kubwa inayofanywa na TANESCO yapo baadhi ya maeneo yalikua na changamoto ya upatikanaji wa umeme lakini mpaka sasa yameendelea kuimarika.
Naibu Waziri Mkuu Dkt. Biteko amefafanua kuwa ili kuhakikisha upatikanaji wa umeme unaendana na mahitaji ya ongezeko la watu TANESCO inatarajia kuongeza uzalishaji umeme katika Kituo cha Kinyerezi III kutoka megawati 600 katika mpango wa awali hadi kufika Megawati 1000 mpango wa sasa.
‘’Nataka niseme mbele yenu ndugu zangu, Mhe. Rais Samia ndio Kinara wa kufanya haya yote yafanikiwe amefanya uwekezaji mkubwa kwenye Sekta ya Nishati na ndio maana kwenye bajeti iliyopita Wizara hii imepata Shilingi Trilioni 2.3 kikubwa anataka wananchi wapate umeme wa uhakika,’’ alisema Dkt Biteko.
Aidha, Naibu Waziri Mkuu pia ametumia nafasi hiyo kuipongeza TANESCO kwa maboresho makubwa yanayoendelea kufanyika ya kuwahudumia wateja hasa kwa uharaka wao wa kukabiliana na dharula zozote za umeme zinazojitokeza.
‘’Kuna maboresho makubwa yamefanyika katika kuwahudumia wananchi naona jitihada kubwa zinafanyika, mmekuwa na uharaka wa kushughulikia changamoto za umeme lakini pia niwapongeze kwa kuimarisha Kituo cha miito ya simu sasa wananchi wanahudumiwa bila gharama yoyote,’’ alisisitiza Dkt. Biteko.
Vilevile, Dkt. Biteko ametembelea Kituo cha Kupokea Gesi Asilia Kinyerezi kwa ajili ya kukagua miundombinu ya kusafirisha gesi na kuwataka kuongeza uzalishaji wa gesi ili kusaidia kukidhi ongezeko la mahitaji ya umeme.
Katika ziara hiyo Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko aliongozana na viongozi mbalimbali akiwemo katibu Mkuu wa Wizara ya nishati Mha. Felchesmi Mramba, Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Edward Mpogolo na Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Bw. Lazaro Twange.
Mwisho