SADC:SEKTA YA NISHATI IWE KICHOCHEO CHA KUIUNGANISHA AFRIKA KUJENGA UCHUMI

July 04, 2025 Add Comment


📌 *Yasisitiza utekelezaji wa miradi ya kipaumbele ya Nishati*


📌 *Kapinga ataka SADC kuweka dhamira thabiti na mikakati madhubuti ya utekelezaji wa Ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia*


Mawaziri wanaoshughulikia masuala ya Nishati na Maji wa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wametaka Sekta ya Nishati kuwa kichocheo cha kuiunganisha Afrika katika kujenga uchumi wake.


Wamesema hayo leo Julai 4, 2025  wakati wakihitimisha mkutano wa SADC jijini Harare nchini Zimbabwe ambao ulilenga kuimarisha na kujadili masuala mbalimbali yatakayowezesha mtangamano wa Kikanda katika sekta za nishati na maji.

Akizungumza wakati akihitimisha mkutano huo, Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Umeme wa Zimbabwe, Mhe. Dkt. July Moyo, ameitaka jumuiya hiyo ya SADC kuipa kipaumbele sekta ya nishati na maji ili kuifanya kuwa na tija kwa wananchi katika kukuza uchumi wao kwa kuwa nishati  ni chanzo kikubwa cha maendeleo. 

Aidha, ameipongeza Tanzania kwa kuandaa na kuwa mwenyeji wa kufanikisha Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Nishati Afrika wa Misheni 300 (M300) ambao ulifanyika kwa mafanikio. Pia, Dkt. Moyo amezishukuru Nchi wanachama zilizohudhuria katika mkutano huo muhimu uliofanyika jijini Dar es Salaam. 

Kwa upande wake, Waziri wa Nishati wa Malawi, Mhe. Ibrahim Matola ameitaka SADC kuhakikisha inaiendeleza miradi yote ya kipaumbele katika jumuiya ili kuifanya sekta ya nishati kuwa kimbilio katika kujenga uchumi wa nchi zao. 

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga ameitaka SADC kuhakikisha inakuwa na mikakati madhubuti ya utekekezaji wa maazimio mbalimbali wanayofikia  katika makongamano ya umoja huo ili yawe na tija kwa wananchi na taifa kwa ujumla na kuifanya sekta ya nishati kuwa chachu na mkombozi ndani ya SADC. 

Kuhusu utekelezaji wa nishati safi ya kupikia katika jumuiya hiyo, Mhe. Kapinga ameitaka SADC kuweka dhamira thabiti na mikakati madhubuti ya utekelezaji wa ajenda ya nishati safi ya kupikia ili kuwafikia watu wengi zaidi katika SADC. 


Mkutano huo uliohitimishwa leo, umehudhuliwa na Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe, Mhe. Suzan Kaganda, Wataalam mbalimbali kutoka Wizara ya Nishati akiwemo Kamishna Msaidizi wa Maendeleo ya Umeme, Mha. Styden Rwebangila, Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mha. Hassan Saidy, Mkurugenzi wa  Mipango na Uwekezaji (TPDC), Derick Moshi, Mkurugenzi wa Mifumo ya Udhibiti Umeme (TANESCO) , Mha. Deogratius Mariwa, Mkurugenzi wa Udhibiti Uchumi (EWURA), Msafiri Mtepa na  Wataalam kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.




NISHATI SAFI YA KUPIKIA NI AGENDA YA DUNIA,WIZARA INAITEKEKEZA KWA VITENDO - DKT.KAZUNGU

July 04, 2025 Add Comment


*📌Apokea Magari Mawili kutoka Umoja wa Ulaya kwa ajili ya kuanza kampeni ya kutoa elimu ya uhamasishaji wa nishati safi ya kupikia nchi nzima*


*📌 Amshukuru Dkt Samia kwa kuwa kinara wa nishati safi na kuibeba ajenda hiyo*


*📌 Umoja wa Ulaya waridhishwa na jitihada za Tanzania kwenye kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia*


*📌UNCDF yaahidi kushirikiana na Wizara kuhakikisha watanzania wanafikiwa na elimu ya nishati safi*


Naibu katibu Mkuu Wizara ya Nishati anayeshughulikia umeme na nishati Jadidifu, Dkt Khatibu Kazungu leo 04 Julai, 2025 amepokea magari mawili yatakayotumika kwa ajili ya kampeni ya kuhamasisha na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia chini ya kampeni ya nishati safi ya kupikia Okoa Maisha na Mazingira itakayoendeshwa nchi nzima na Wizara ya nishati kwa kushirikiana na UNCDF.

‘’ Ajenda ya Nishati safi ya kupikia ni ajenda ya Dunia na sisi Wizara ya Nishati tuko tayari kwa utekelezaji ili kumuunga mkono Mhe. Rais Samia’’ Amesema Dkt. Kazungu

Aidha, ameishukuru Umoja wa Ulaya, na UNCDF kwa kutekeleza mradi wa nishati safi ya kupikia chini ya mfuko wa Cook fund kwa kuwa umesaidia kubadili maisha na mitazamo ya wananchi kuhusu  utekelezaji wa miradi ya Nishati safi.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo,  Balozi wa Umoja wa Ulaya Mhe. Balozi Christine Grau amesema umoja wa Ulaya uko tayari kuendelea kuisaidia Tanzania kwenye utekelezaji wa Nishati safi ya kupikia na tayari EU imetoa kiasi cha Euro Milioni 19.4 sawa na shilingi Bilioni 59 kutekeleza miradi ya nishati safi ya kupikia kwa mikoa ya Dar es salaam, Dodoma, Pwani, Morogoro  na Mwanza. 

Kuhusu magari amesema magari hayo mawili yana thamani ya Euro 130,000 na amewataka wizara ya Nishati kuhakikisha wananchi wa vijijini wanafikiwa na nishati safi ya kupikia

Tanzania inajipanga kutekeleza kwa vitendo mkakati wa Taifa wa Nishati safi ya kupikia chini ya mkakati wa Mawasiliano wa Taifa ili kutoa elimu kwa wananchi na kufikia lengo la Serikali la asilimia 80 ya watanzania kuanza kutumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.




ASKOFU DKT.SHOO AKEMEA UPOTOSHAJI MCHANGO WA RAIS SAMIA KWA TAASISI ZA DINI

July 04, 2025 Add Comment

Mwenyekiti wa CCT, Askofu Dkt. Fredrick Shoo amesema kuwa baadhi ya watu kwa sababu zao binafsi wamekuwa wakidai kuwa msaada wa Rais, Dkt. Samia ni sehemu ya hongo, madai ambayo yamekuwa yakimuumiza sana kama kiongozi wa dini. Niendelee kumsihi Rais Samia asirudishwe nyuma na watu hao bali aendelee kuwa na hofu ya Mungu katika kusaidia huduma za kiroho nchini. 

Askofu Mkuu Shoo amebainisha hayo Julai 03, 2025 Jijini Dodoma wakati wa Mkutano Mkuu wa 32 wa Jumuiya ya Kikristo nchini Tanzania - CCT ambapo Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko alimuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano huo.

BENKI YA CRDB YASHINDA TUZO YA DHAHABU YA KIMATAIFA YA UWEKEZAJI KATIKA JAMII KUPITIA CRDB MARATHON

July 04, 2025 Add Comment

 

Benki ya CRDB imeshinda tuzo ya dhahabu ya Kimataifa ya Uwekezaji katika Jamii (International CSR Awards 2025) kupitia mbio zake za kimataifa ya CRDB BANK International Marathon.

Tuzo hii ya hadhi ya juu imetolewa na CSR Society, shirika huru la kimataifa linalotambua na kuenzi mashirika yenye juhudi za uwajibikaji wa kijamii duniani kote lenye makao makuu yake nchini Uingereza.
Mwaka huu, Benki ya CRDB ilikuwa miongoni mwa washiriki 300 walioshindana kutoka nchi mbalimbali duniani na kushinda tuzo hiyo kwa kuonyesha ubunifu mkubwa katika uwezeshaji wa kijamii katika nyanja tofauti.

Akiiwakilisha Benki ya CRDB na kupokea tuzo na cheti cha ushindi, Afisa Uwekezaji wa Jamii, Natalia Tuwano amesema tuzo hii inaipa Benki ya CRDB heshima na hadhi ya juu katika kuiwezesha jamii na makala yake kuhusu jambo hilo kubwa yatachapishwa na Jarida la Viongozi wa Uwezeshaji Jamii Duniani – rejeleo la kimataifa la mazoea bora ya uwajibikaji wa kijamii. Hii pia inaruhusu benki kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya Green World Awards mwakani ujao.
“CRDB Bank International Marathon ni mfano wa jinsi juhudi za kijamii zinavyoweza kuleta mabadiliko chanya na kuimarisha jamii zetu,” amesema Natalia. “Tunawashukuru CSR Society kwa kutambua jitihada zetu na tunaahidi kuendelea kutekeleza mipango inayolenga maendeleo endelevu ya kijamii.”

Benki ya CRDB imekuwa mstari wa mbele katika kukuza afya, elimu, uendelevu wa mazingira, na mshikamano wa kijamii kupitia kampeni hii ambayo imevutia maelfu ya watu kutoka makundi mbalimbali.