BENKI YA CRDB YASHINDA TUZO YA DHAHABU YA KIMATAIFA YA UWEKEZAJI KATIKA JAMII KUPITIA CRDB MARATHON

July 04, 2025

 

Benki ya CRDB imeshinda tuzo ya dhahabu ya Kimataifa ya Uwekezaji katika Jamii (International CSR Awards 2025) kupitia mbio zake za kimataifa ya CRDB BANK International Marathon.

Tuzo hii ya hadhi ya juu imetolewa na CSR Society, shirika huru la kimataifa linalotambua na kuenzi mashirika yenye juhudi za uwajibikaji wa kijamii duniani kote lenye makao makuu yake nchini Uingereza.
Mwaka huu, Benki ya CRDB ilikuwa miongoni mwa washiriki 300 walioshindana kutoka nchi mbalimbali duniani na kushinda tuzo hiyo kwa kuonyesha ubunifu mkubwa katika uwezeshaji wa kijamii katika nyanja tofauti.

Akiiwakilisha Benki ya CRDB na kupokea tuzo na cheti cha ushindi, Afisa Uwekezaji wa Jamii, Natalia Tuwano amesema tuzo hii inaipa Benki ya CRDB heshima na hadhi ya juu katika kuiwezesha jamii na makala yake kuhusu jambo hilo kubwa yatachapishwa na Jarida la Viongozi wa Uwezeshaji Jamii Duniani – rejeleo la kimataifa la mazoea bora ya uwajibikaji wa kijamii. Hii pia inaruhusu benki kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya Green World Awards mwakani ujao.
“CRDB Bank International Marathon ni mfano wa jinsi juhudi za kijamii zinavyoweza kuleta mabadiliko chanya na kuimarisha jamii zetu,” amesema Natalia. “Tunawashukuru CSR Society kwa kutambua jitihada zetu na tunaahidi kuendelea kutekeleza mipango inayolenga maendeleo endelevu ya kijamii.”

Benki ya CRDB imekuwa mstari wa mbele katika kukuza afya, elimu, uendelevu wa mazingira, na mshikamano wa kijamii kupitia kampeni hii ambayo imevutia maelfu ya watu kutoka makundi mbalimbali.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »