WAZIRI MAVUNDE ATAKA WATANZANIA KUPEWA KIPAUMBELE KUSAMBAZA BIDHAA NA HUDUMA MIGODINI

June 17, 2025 Add Comment


▪️Aelekeza mabadiliko ya Kanuni ili kuruhusu uhaulishwaji teknolojia kwa Kampuni za Kigeni


▪️Ataka Watanzania kuchangamkia Trilioni 5.3 za usambazaji bidhaa na utoaji huduma


▪️Rais Samia apongezwa kwa uongozi wa maono


▪️Watanzania 19,371 wanufaika na ajira rasmi


▪️Kamati ya Bunge yaipongeza Wizara kwa ukuaji wa sekta



MWANZA


Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde ameitaka Tume ya Madini kuwapa kipaumbele watanzania kwenye usambazaji wa  huduma na bidhaa kwenye migodi ya madini ili kujipatia kipato, kuongeza mzunguko wa fedha nchini hivyo Sekta ya Madini kuendelea kuwa na mchango mkubwa kwenye Pato la Taifa.


Mhe. Waziri Mavunde ameyasema hayo mapema leo Juni 17, 2025 jijini Mwanza kwenye ufunguzi wa Jukwaa la Nne la Utekelezaji wa Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini linalokutanisha wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na  Wizara ya Madini na Taasisi zake, Taasisi za Serikali, Taasisi Binafsi, Taasisi za Fedha, Kampuni za Uchimbaji wa Madini na Watoa Huduma kwenye Migodi ya Madini. 

Amesema kuwa katika kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini na kuhakikisha watanzania wananufaika na rasilimali madini, Serikali imeendelea kusimamia ipasavyo Sheria ya Madini, Sura 123 Kifungu Na. 102 na Kanuni za Ushirikishwaji wa Watanzania za Mwaka 2018 ili kuweka usimamizi thabiti katika utekelezaji wa masuala ya Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini nchini.

Amesisitiza kuwa lengo la uwepo wa Kanuni za Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini ni kuhakikisha watanzania wanashiriki ipasavyo kupitia usambazaji wa bidhaa na huduma kwenye migodi ya madini badala ya kampuni kuagiza bidhaa kutoka nje ya nchi.


Aidha Mhe. Mavunde ameitaka Tume ya Madini kufanya mabadiliko ya Kanuni ili kuruhusu uhaulishwaji teknolojia kwa Kampuni za Kigeni ambapo itatoa fursa kwa kampuni za kitanzania kushirikiana na kampuni za kigeni kwenye utoaji wa huduma migodini na kujifunza teknolojia mpya kutoka kampuni za kigeni.

Katika hatua nyingine, Mhe. Mavunde amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maono yake makubwa ya kuendeleza Sekta ya Madini hali iliyopelekea mabadiliko makubwa ambapo mpaka sasa mafanikio makubwa yamepatikana.


“Mpaka sasa mafanikio makubwa yamepatikana hasa kwa wachimbaji wadogo ambapo wameanza kukopesheka kutoka kwenye Taasisi za Fedha, ushiriki wa watanzania kwenye shughuli za uchimbaji, uchenjuaji, biashara ya madini na utoaji wa bidhaa na huduma kwenye migodi ya madini umeongezeka na mchango wa wachimbaji wadogo kwenye makusanyo ya maduhuli umeendelea kuimarika,” amesisitiza Mhe. Mavunde.

Akielezea mafanikio ya utekelezaji wa kanuni za ushirikishwaji wa watanzania katika Sekta ya Madini, Waziri Mavunde amesema katika kipindi cha mwaka 2023/2024 jumla ya ajira rasmi 19,874 zilizalishwa katika migodi ya madini  ambapo ajira 19,371 sawa na asilimia 97 zilitolewa kwa Watanzania na ajira 503 sawa na asilimia 3 zilitolewa kwa wageni.

Aidha, amewataka watanzania kuchangamkia fursa za uwekezaji katika Sekta ya Madini hasa kwenye usambazaji wa bidhaa na  huduma kwenye migodi ya madini kama vile usambazaji wa vifaa, vyakula na huduma na kuzitaka Taasisi za Kifedha kuendelea kuwakopesha mitaji.


Amesema kuwa kampuni za madini zinatumia kiasi cha shilingi Trilioni 5.3 kila mwaka kwa ajili ya manunuzi ya bidhaa na huduma zinazotumika migodini na kuwataka watanzania kuchangamkia fursa hizo.


Naye Mkuu wa Wilaya Ilemela, Mhe. Hassan Masala akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Said Mtanda amempongeza Waziri Mavunde kwa usimamizi mzuri wa Sekta ya Madini hali iliyopelekea mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na ongezeko la wawekezaji nchini.


Ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji kuwekeza katika mkoa wa Mwanza hasa katika eneo la uchimbaji wa madini na utoaji wa huduma mbalimbali kwenye migodi ya madini.


Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo amesisitiza kuwa Wizara ya Madini itaendelea kufungamanisha Sekta ya Madini na sekta nyingine muhimu za kiuchumi ili kuongeza ushiriki wa watanzania kwenye shughuli za madini nchini.

 

Wakati huohuo akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Dkt David Mathayo, Mbunge wa Ilemela, Dkt. Angeline Mabula amepongeza kazi kubwa inayofanywa na Waziri Mavunde hali iliyochangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa  mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa.


“Kupitia uongozi wa Mhe. Mavunde tumeshuhudia mapinduzi makubwa kwenye Sekta ya Madini ambapo Tanzania imepiga hatua kubwa ya kihistoria kwa kufikia mchango wa asilimia 10.1 katika Pato la Taifa kwa Mwaka 2024, ikiwa ni Mwaka mmoja (1) kabla ya lengo la asilimia 10 lililowekwa kwenye Sera ya Madini ya Mwaka 2009 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026),” amesisitiza Dkt. Mabula


Naye Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Dkt. Janet Lekashingo amesema kuwa Tume imeanza kukusanya takwimu za bidhaa zinazoingizwa nchini ili kushauri Serikali kuhusu uanzishwaji wa viwanda vinavyotoa bidhaa husika na kuongeza mzunguko wa fedha nchini huku wananchi wakijipatia ajira.


Katika hatua nyingine, Kamishna wa Tume ya Madini ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini, Dkt. Theresia Numbi ameeleza mikakati iliyowekwa na Tume ya Madini  ya kuongeza ushiriki wa watanzania katika Sekta ya Madini kuwa ni pamoja na mikutano, majukwaa na vyombo vya habari.

DKT. YONAZI AMEONGOZA KIKAO CHA KAMATI YA TAIFA YA USHAURI YA SENSA YA WATU NA MAKAZI YA MWAKA 2022

June 17, 2025 Add Comment
NA. MWANDISHI WETU

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi (mwenyekiti wa kikao) cha Kamati ya Taifa ya Ushauri ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 kilichofanyika tarehe 17 Juni, 2025 katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere JIjini Dar es Salaam.

WIZARA YA NISHATI ENDELEENI KUWEZESHA UWEKEZAJI WA VITUO VYA MAFUTA VIJIJINI-WAZIRI SIMBACHAWENE

June 17, 2025 Add Comment


📌 *Atembelea Banda la Wizara ya Nishati na Taasisi zake katika Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma*


DODOMA


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,  Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.George Simbachawene ameiasa Wizara ya Nishati kuendelea kuweka mazingira wezeshi yatakayowezesha uwekezaji zaidi wa vituo vya mafuta vijijini.


 Simbachaene amesema hayo tarehe 17 Juni, 2025, jijini Dodoma wakati alipotembelea Banda la Wizara ya Nishati katika Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma  yanayoendelea katika viwanja vya Chinangali ambayo leo yamefunguliwa rasmi

" Wafanyabiashara wengi wanataka kuwekeza kwenye vituo vya Mafuta vijijini kwakuwa bado  kuna uhaba wa vituo, hivyo angalieni masharti yanayowekwa kwenye uwekezaji yasiwe kikwazo kwenye huduma hii muhimu." Amesema Simbachawene

Pia, Simbachawene  ameishauri Wizara kuongeza kasi ya upatikanaji  wa Nishati Safi ya Kupikia Vijijini pamoja na kuhamasisha uwekezaji kwenye Nishati Safi ya Kupikia.


Vilevile, ameipongeza Wizara ya Nishati na  Taasisi zake kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuendelea kutoa huduma za Nishati kwa wananchi.

TANAPA KUNADI MAENEO YAKE YA UWEKEZAJI KATIKA MKUTANO WA UWEKEZAJI ZANZIBAR

June 17, 2025 Add Comment



Na. Mwandishi wetu Zanzibar.

Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limekuwa miongoni mwa wadau wakuu wanaoshiriki kunadi fursa za uwekezaji zinazopatikana katika Hifadhi za Taifa 21 kwenye Mkutano wa Uwekezaji Zanzibar (Zanzibar Investment Summit 2025), uliofanyika kwa mara ya kwanza Kisiwani Pemba huku ukifunguliwa rasmi na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi.

Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano huo, Mhe. Dkt. Mwinyi alisisitiza umuhimu wa kutumia mkutano huo kama jukwaa la kutangaza fursa za kiuchumi zilizopo Zanzibar hususan kisiwani Pemba na maeneo mengine ya Tanganyika hasa maeneo ya Hifadhi za Taifa. 


Aidha, alitilia mkazo zaidi kwa wawekezaji wa ndani na nje kuchangamkia mazingira bora ya uwekezaji yaliyowekwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ajili ya kuvutia wawekezaji wengi zaidi.

Katika Mkutano huo ulioanza June 15, 2025 TANAPA ilijikita kutangaza fursa za uwekezeji katika mazao ya utalii pamoja na miundombinu ya malazi kwa watalii wanaotembelea vivutio hivyo vilivyosheheni aina mbalimbali ya wanyama, mimea na mandhali za kuvutia zenye uoto wa asili ikijumuisha mabonde, milima na mito.


Mbali na kunadi fursa za uwekezaji pia, Wahifadhi hao walihamasisha watanzania na wawekezaji mbalimbali waliohudhulia mkutano huo kutembelea Hifadha za Taifa mbalimbali kutokana na upekee wa kila hifadhi ili wawe mabalozi wazuri wa kuzinadi hifadhi hizo warudipo nchini kwao na kuongeza kasi ya ujio wa watalii ili kukuza pato la Taifa.

Mkutano huo unaotarajiwa kutamatika leo June 17, 2025 ukibeba kauli mbinu isemayo; *“Ni Wakati wa Pemba”* pia unawajumuisha wadau kutoka sekta za utalii, kilimo, uchumi wa buluu, miundombinu, na biashara kutoka mataifa mbalimbali.

OCTOBA KURA ZOTE KWA RAIS DKT SAMIA- UMMY MWALIMU

June 17, 2025 Add Comment


Na Mwandishi Wetu, TANGA


Kazi nzuri na miradi tele ya maendeleo iliyotekelezwa katika Jimbo la Tanga Mjini imetengeneza deni kwa wananchi wa Tanga Mjini dhidi ya Rais Dk. Samia Suluhu ambaye pia ni Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Uchaguzi Mkuu wa mwezi Oktoba, 2025.


Hayo yameelezwa na Mbunge wa Jimbo la Tanga Mjini (CCM), Ummy Mwalimu, Juni 16, 2025, alipokuwa akitoa hotuba fupi kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Tanga Mjini katika Mbio za Mwenge wa Uhuru wilayani Tanga. Katika hotuba yake, Ummy Mwalimu amesema Jimbo la Tanga Mjini limepata miradi mingi na mikubwa ya maendeleo ambayo imetatua kero za wananchi. 


Kwa msingi huo, Ummy Mwalimu amemuhakikishia Rais Dk. Samia kuwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwezi Oktoba mwaka huu, asiwe na wasiwasi wa kura kwani wananchi wa Tanga Mjini watampa asante yao kwa njia ya kumpigia kura nyingi za kishindo ili aendelee kukaa Ikulu awatumikie Watanzania.


"Kwa kazi nzuri zilizofanyika, sisi watu wa Tanga kwakweli hatuna deni na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, na Oktoba 2025, watu wa Tanga tutamlipa Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kumrejesha Ikulu," amesema Ummy Mwalimu.


Mwenge wa Uhuru wilayani Tanga umezindua miradi mbalimbali ya maendeleo ikijumuisha miradi ya afya, maji, elimu, viwanda na utawala ambapo wananchi wamepongeza miradi hiyo iliyozinduliwa kwani imegusa ustawi na maendeleo yao.