MAADHIMISHO YA MIAKA 25 YA JUMUIYA YA TATHIMINI AFRIKA ( AfrEA ) WAFANYIKA ADDIS ABABA-ETHIOPIA

June 16, 2025 Add Comment


*Na Mwandishi Wetu – Addis Ababa, Ethiopia*


Tanzania imeshiriki Maadhimisho ya Miaka 25 ya Jumuiya ya Tathmini Afrika (AfrEA) yanayofanyika kwa siku tatu kuanzia tarehe 16  hadi 18 Juni, 2025, katika Kituo cha Mikutano cha Umoja wa Mataifa (UNECA), jijini Addis Ababa, Ethiopia.

Ujumbe wa Tanzania umeongozwa na Mkurugenzi wa Idara ya Ufuatiliaji na Tathmini, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Bi. Sakina Mwinyimkuu.

 Washiriki wengine kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu ni Mkurugenzi wa Mipango na Bajeti Bw. Eleuter Kihwele na Mkaguzi Mkuu wa Ndani katika Ofisi hiyo Bw. Exavery Salira.


Maadhimisho hayo ya siku tatu yameandaliwa kwa lengo la kuenzi mchango wa tathmini katika maendeleo barani Afrika, na kuimarisha uwajibikaji wa sera kwa kutumia ushahidi (Evidence Based) katika kufanya maamuzi.

Aidha Washiriki kutoka nchi mbalimbali ndani na nje ya bara la Afrika wanajadili mbinu bunifu na jumuishi za tathmini kwa maendeleo endelevu yenye muktadha wa Kiafrika.




*MWISHO*

RAIS SAMIA ATEMBELEA MRADI WA REA SIMIYU

June 16, 2025 Add Comment

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametembelea mradi wa nishati safi ya kupikia wa shule ya Sekondari ya Wasichana Simiyu iliyopo Bariadi mkoani humo na kupewa maelezo na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga wakati akifungua shule hiyo leo tarehe 16 Juni, 2025

Mradi huo unahusisha usimikaji wa mfumo wa kupikia kwa kutumia gesi yaani LPG, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa, hivyo kuchangia katika utunzaji wa mazingira na kulinda afya ya wanafunzi na walimu.



Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imetoa ufadhili wa kiasi cha Shilingi Shilingi Milioni 14 kwa ajili ya ujenzi na usimikaji wa miundombinu ya nishati safi ya kupikia katika shule hiyo.

BEI YA KUJAZA GESI LPG KWA MATUMIZI YA KUPIKIA NI HIMILIVU-KAPINGA

June 16, 2025 Add Comment


*📌 Wizara ya Nishati na TAMISEMI zaendelea kushirikiana kuhakikisha  Shule mpya zinafungwa mifumo ya Nishati Safi ya Kupikia*

Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga amesema gharama ya kujaza gesi kwenye mitungi (LPG) ni himilivu ikiwa ni jitihada zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ili kuwezesha matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia.

Mhe. Kapinga ameyasema hayo leo Juni 16, 2025 katika ziara ya  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan mkoani Simiyu  wakati wa kuzindua Shule Maalum ya Sayansi ya Wasichana ya Simiyu ambayo imefungwa miundombinu ya nishati safi ya kupikia. 



“Mheshimiwa Rais ulituelekeza Taasisi ambazo zinahudumia watu zaidi ya mia moja tuzifungie miundombinu ya nishati safi ya kupikia, Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na TAMISEMI tunatekeleza agizo hilo kwa kuzifungia mifumo ya nishati safi shule mpya ambazo zinajengwa." Amesema Kapinga

Ameeleza kuwa,  uwezo wa shule hiyo ni wanafunzi 800 na mifumo ya Nishati Safi ya Kupikia iliyofungwa ina uwezo wa kuhudumia wanafunzi 800.

Ameongeza kuwa, kwa idadi hiyo ya wanafunzi 800  mtungi wa gesi katika Shule ya Wasichana Simiyu utakuwa ukijazwa kila  baada ya miezi miwili.



WIZARA YA NISHATI NA TAASISI YASHIRIKI MAADHIMISHO YA WIKI YA UTUMISHI WA UMMA DODOMA

June 16, 2025 Add Comment


Wizara ya Nishati na taasisi zilizo chini yake inashiriki Maadhimisho ya Kitaifa ya Wiki ya Utumishi wa Umma ambayo yameanza Juni 16, 2025 katika viwanja vya Chinangali, Jijini Dodoma.

Maadhimisho hayo yamebebwa na kaulimbiu isemayo "Himiza Matumizi ya Mifumo ya Kidijiti Kuongeza Upatikanaji wa Taarifa na Kuchagiza Uwajibikaji", 

Watalaam wa Wizara pamoja na kueleza mafanikio yaliyofikiwa katika Sekta ya Nishati ikiwemo ukamilishaji wa mradi wa umeme wa Julius Nyerere na usambazaji wa umeme vijijini, wanatoa elimu  kwa njia mbalimbali ikiwemo machapisho na vitendo kuhusu ajenda ya kitaifa ya  utekelezaji wa Mkakati wa Nishati Safi ya kupikia.

Taasisi za Wizara ya Nishati zinazoshiriki maadhimisho hayo ni Shirika la Umeme Tanzania ( TANESCO), Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli ( PURA),  Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania ( TPDC), Wakala wa Nishati Vijijini ( REA) na Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA).


WAACHENI WATOTO WAENDE SHULE- RAIS SAMIA

June 16, 2025 Add Comment


Na John Mapepele -OR TAMISEMI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe, Dkt. Samia Suluhu Hassan amewataka wazazi nchini kuwaachia watoto wa kike kusoma shule maalum za msingi na sekondari ambazo zimejengwa na Serikali.