TFS YABORESHA MIUNDOMBINU YA UTALII MSITU WA PUGU KAZIMZUMBWI KUPITIA MRADI WA BIONUWAI

TFS YABORESHA MIUNDOMBINU YA UTALII MSITU WA PUGU KAZIMZUMBWI KUPITIA MRADI WA BIONUWAI

June 14, 2025 Add Comment





Kisarawe, Pwani – Juni 2025

Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), kupitia Mradi wa Kuimarisha Ustahimilivu wa Bioanuwai ya Misitu ya Mazingira Asilia dhidi ya Matishio ya Mabadiliko ya Tabianchi, unaendelea kutekeleza hatua madhubuti za kuboresha miundombinu rafiki kwa utalii katika maeneo ya hifadhi ya misitu nchini.

Katika Hifadhi ya Msitu wa Pugu Kazimzumbwi, moja ya misitu ya asili ya pekee inayopatikana karibu kabisa na Jiji la Dar es Salaam, mradi huu unajenga jengo la kisasa la mbao kwa ajili ya mapumziko ya watalii. Jengo hilo, lenye ukubwa wa mita za mraba 72, litakuwa na sehemu tatu za kupumzikia wageni na lina uwezo wa kuhudumia hadi watu 50 kwa wakati mmoja.

Kazi ya ujenzi imefikia asilimia 55 na inatarajiwa kukamilika ifikapo tarehe 26 Juni 2025 kwa gharama ya shilingi milioni 120. Kukamilika kwa jengo hili kutakuwa hatua muhimu ya kuboresha huduma kwa wageni na kuongeza mvuto wa utalii wa misitu katika Ukanda wa Pwani.

Akizungumza wakati wa ukaguzi wa maendeleo ya kazi, Msimamizi wa Ujenzi, Bw. Fredrick Chakyi alisema kuwa mradi sasa unasonga mbele kwa kasi baada ya changamoto za mvua zilizokuwepo awali kupungua.

“Awali mvua zilikuwa changamoto kubwa, lakini hali sasa ni shwari. Tunatarajia kukamilisha kazi ndani ya muda uliopangwa,” alisema Chakyi.

Kwa upande wake, Mhifadhi wa Misitu wa Wilaya ya Kisarawe, Bw. Baraka Mtewa, alieleza kuwa uwekezaji huo ni sehemu ya mkakati mpana wa TFS wa kuimarisha utalii wa misitu na kuhifadhi bioanuwai kwa njia endelevu.

“Mradi huu utasaidia kuvutia watalii wa ndani na nje ya nchi, kuongeza mapato ya hifadhi, na kuchochea maendeleo ya kijamii kwa wakazi wa maeneo yanayozunguka Msitu wa Pugu Kazimzumbwi,” alisema Mtewa.

Kwa msaada wa UNDP na ufadhili wa Mfuko wa Dunia wa Mazingira (GEF), mradi huu unalenga kulinda mazingira ya asili, kuimarisha uthibiti wa mabadiliko ya tabianchi, na kukuza ushirikiano kati ya Serikali, jamii, na wadau wa maendeleo.

TFS inaendelea kushirikiana na sekta mbalimbali ili kuhakikisha kuwa rasilimali za misitu si tu zinahifadhiwa, bali pia zinatumika kwa njia endelevu katika kuleta tija kwa taifa – kijamii, kiuchumi, na kimazingira.






MHE MCHENGERWA AWATAKA MA RC, DC KUONGOZA JOGGING KWENYE MAENEO YAO

June 14, 2025 Add Comment

Na John Mapepele

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Mhe. Mohamed Mchengerwa amewataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya nchini kuwaongeza wananchi katika maeneo yao kufanya "jogging" na mazoezi ili kuimarisha afya.

KAMISHNA WA UMEME NA NISHATI JADIDIFU AFANYA ZIARA YA UKAGUZI WA MIRADI YA UMEME JIJINI DAR ES SALAAM

June 14, 2025 Add Comment


▪️Aridhishwa na hatua ya utekelezaji wa miradi


▪️Awataka wakandarasi kuzingatia viwango na TANESCO kuongeza usimamizi ili kuepuka ongezeko la gharama


▪️Aisisitiza dhamira ya Serikali ya kuhakikisha Watanzania wanapata umeme wa uhakika


Na. Agnes Njaala, Dar es Salaam


Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu kutoka Wizara ya Nishati, Mhandisi Innocent Luoga, tarehe 12 Juni 2025, amefanya ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme ya Gridi Imara inayoendelea katika Jiji la Dar es Salaam, na kutoa maelekezo muhimu kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) pamoja na wakandarasi wanaotekeleza miradi hiyo.


Miradi hiyo inalenga kuimarisha upatikanaji wa umeme kwa kuboresha miundombinu ya usafirishaji na usambazaji wa umeme nchini, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuhakikisha huduma bora na ya uhakika kwa wananchi.

Akizungumza mara baada ya ziara hiyo, Kamishna amesema ameridhishwa na hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa miradi hiyo, licha ya changamoto mbalimbali za kimazingira, na kusisitiza umuhimu wa kuendelea na jitihada za kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati.


“Nimeridhishwa na hatua zilizofikiwa, lakini nimeagiza wakandarasi waharakishe kazi, vifaa vipatikane kwa wakati, na viwango vya kazi vizingatiwe ili miradi hii itoe matokeo yaliyokusudiwa kwa wananchi,” amesisitiza Mhandisi Luoga.


Akifafanua amebainisha kuwa miradi hiyo ya kimkakati, inayotekelezwa na TANESCO kwa ufadhili wa Serikali, inalenga kuboresha huduma ya umeme kwa wakazi wa Dar es Salaam na maeneo mengine nchini. Aidha, ametoa pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuidhinisha rasilimali fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo muhimu.


Katika maagizo yake, ameitaka TANESCO kuongeza usimamizi kwa wakandarasi katika kuhakikisha upatikanaji wa vifaa kwa wakati, na kusimamia ubora wa kazi ili kuepuka ongezeko la gharama zitokanazo na ucheleweshaji.

Kwa upande wake, Mhandisi Abdallah Chikoyo, Meneja wa Miradi ya Kuzalisha Umeme TANESCO aliyemwakilisha Mkurugenzi Mtendaji , ameahidi kuongeza juhudi katika usimamizi wa miradi na kuweka mipango kazi inayotekelezeka kwa wakati.


“Tumejipanga kuongeza nguvu katika usimamizi wa miradi hii, na kuimarisha ushirikiano na wadau wa maendeleo ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati na kwa ufanisi, tukitimiza wajibu wetu katika kuboresha huduma ya umeme nchini,” amesema Mhandisi Chikoyo.


Ziara hiyo ilikuwa sehemu ya utekelezaji wa wajibu wa Serikali katika kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ambapo Kamishna Luoga alitembelea vituo vya umeme vya Ubungo I, Mabibo, Kinyerezi na Gongo la Mboto. Katika vituo hivyo, kazi ya ufungaji wa mashine umba zenye uwezo mkubwa  (transformers) inaendelea kwa kasi ya kuridhisha, ikiwa ni hatua ya kuimarisha miundombinu ya usambazaji wa umeme jijini Dar es Salaam.

MWENGE WA UHURU 2025 KUPITIA MIRADI YENYE THAMANI YA BILIONI 3 WILAYA YA TANGA

June 14, 2025 Add Comment










Na Paskal Mbunga,TANGA

MWENGE wa Uhuru unatarajiwa kuwasili katika wilaya ya Tanga Jumatatu June 16 mwaka huu na upitia katika miradi saba ya maendeleo yenye thamani ya Sh.Bilioni 3,058,289,671.99.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati akitoa taarifa za ujio wa Mwenge huo,Mkuu wa wilaya ya Tanga Dadi Kolimba alisema wataupokea ukitokea wilayani Mkinga katika uwanja wa shule ya Msingi Mabambani Mtaa wa Mpirani Kata ya Chongoleani.

Aliitaja miradi ambayo itapitiwa na Mwenge ni ujenzi wa madarasa 4 ya Ghorofa ,matundu 13 ya vyoo na ofisi shule ya Msingi Mbuyuni yenye thamani ya Milioni 388,769,596.80 na Ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa ya awali ya mfano shule ya msingi Mwakidila yenye thamani ya Milioni 70,100,000.00.

Mkuu huyo alisema pia miradi mingine ni ujenzi wa ofisi ya mtendaji kata ya Tongoni uliogharimu kiasi cha sh.Milioni 85,000,000.00,ujenzi wa barabara ya Sahare awamu ya kwanza na ya pili yenye urefu wa mita 600 kwa kiwango cha lami uliogharimu Sh.Milioni 489,606,700.00.

“Lakini pia Mwenge utapita katika ujenzi wa Jengo la X-Ray kituo cha Afya Makorora wenye thamani ya Sh.Milioni 84,721,640.00 pamoja na mradi wa ufungaji wa dira za maji za malipo ya kabla awamu ya kwanza wenye thamani ya Sh. 1,872,091,735.00 “Alisema.

Hata hivyo alisema kwamba mradi mwengine ambao utapitiwa na mwenge ni mradi wa kikundi cha vijana cha kutengeneza gypsum wenye thamani ya Sh.Milioni 68,000,000.00

Alisema mbali na miradi hiyo saba mwenge wa uhuru utakagua shughuli za maandalizi ya uchaguzi,kongamano la vijana pamoja na maswala mtambuka.

Mwisho.

KAMPENI YA PIKA SMART INAYOHAMASISA MATUMIZI YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA YAZINDULIWA

June 13, 2025 Add Comment


*📌 Kamishna Luoga asisitiza matumizi ya umeme katika Nishati Safi ya Kupikia*


Kamishina wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga amezindua kampeni ya kitaifa ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ya umeme inayokwenda na kaulimbiu ya PIKA SMART.


Mha. Luoga amezindua kampeni hiyo leo Juni 13, 2025 jijini Dar es Salaam akimwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi  Mramba. 


Kampeni hiyo imeandaliwa na Shirika la Modern Energy Cooking Services (MECS) chini ya ufadhili wa UKAID kwa kushirikiana na Serikali kupitia Wizara ya Nishati.


Mhandisi Luoga amesema kampeni hiyo imezinduliwa ikiwa ni mojawapo ya jitihada za Serikali kuhakikisha inawahamasisha wananchi kutumia nishati safi ya kupikia ili kufikia lengo la asilimia 80 ya watanzania kutumia nishati safi ya kupikia ifikapo 2034. 

Luoga amewatoa hofu wananchi kuhusu kutumia nishati safi ya kupikia ya umeme akitanabaisha kuwa ni salama na gharama nafuu na kuongeza kuwa Tanzania Ina Umeme mwingi na wa kutosheleza mahitaji.

"Kama tunavyofahamu bwawa la kufua umeme kwa maji la Julius Nyerere limekamilika na hivyo kupelekea umeme uliopo nchini hadi sasa kufikia takribani megawati 4,031,  umeme huu umeshafika  katika Vijiji vyote 12, 318 vya Tanzania  hivyo kuna kila sababu kwa wananchi kutumia nishati safi ya umeme kupikia." amesema Mha. Luoga



Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji TANESCO, Mkurugenzi wa Mipango na uwekezaji TANESCO, Mhandisi Henryfried Byabato amesema Shirika hilo limekuwa likihamasisha wananchi kutumia nishati safi ya kupikia ya umeme kutokana na uwepo wa kutosha wa nishati hiyo nchini.

Ameongeza kuwa, teknolojia  zimeboreshwa hivyo majiko ya umeme yanatumia nishati kidogo na kwa ufanisi mkubwa.

Kampeni hii ya kuhamasisha matumizi ya pika smart imekuja wakati muafaka ambapo Wizara ya Nishati imezindua mkakati wa Taifa wa Mawasiliano wenye lengo la kutoa mwongozo kwa wadau kuendeleza kampeni ya uhamasishaji matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kuunga mkono jitihada za Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan ambaye ni kinara wa nishati safi ya kupikia kuhakikisha watanzania wanahama kutoka kwenye matumizi ya nishati isiyo safi kwenda kwenye nishati safi