DKT.BITEKO AELEZA MAPINDUZI YALIYOFANYWA NA SERIKALI SEKTA YA ELIMU

June 08, 2025 Add Comment


📌 Ataka CWT wasigawanyike, ahimiza amani, upendo na mshikamano*


📌 Serikali kuendelea kuajiri walimu kila mwaka


📌 Serikali ya Awamu ya Sita yajenga madarasa 62,685 ya shule za msingi na sekondari, shule mpya za msingi na sekondari 2,611 na nyumba za walimu 1,792


📌 Serikali kufanyia tathmini ombi la kuwa na chombo kimoja cha kusimamia walimu nchini


📌 CWT yaipongeza Serikali kwa kuendelea kulipa stahiki za walimu


Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati

Serikali imeendelea kutambua mchango wa walimu katika maendeleo ya sekta ya elimu kwani ni wazalishaji wa watalaamu mbalimbali waliopo katika sekta zote ikiwemo afya, nishati, sayansi na teknolojia. Sambamba na kufanya maboresho yatakayowaongezea walimu ari ya kufanya kazi kwa bidii, weledi, uadilifu na kutanguliza mbele maslahi ya Taifa.


Mafanikio yaliyopatikana katika sekta hiyo yanachangiwa moja kwa moja na walimu. Hivyo, Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kina mchango mkubwa kwa jamii na kwa Taifa kwa ujumla kwa kuwa pamoja na jukumu la kufundisha na kujengea watu maarifa, mwalimu ni mzazi wa kiroho, kiongozi wa fikra, na ni mjenzi wa maadili katika jamii.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko Juni 8, 2025 jijini Dodoma wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Saba wa Chama Cha Walimu Tanzania (CWT).


Amesema katika kuimarisha sekta ya elimu ili kuongeza ufanisi na kusogeza huduma kwa jamii. Serikali imefanikiwa kujenga jumla ya madarasa 62,685 kwa shule za msingi na sekondari, shule mapya za sekondari 1,031, shule mpya za msingi 1,580 na nyumba za walimu 1,792.



Ameongeza kuwa katika kipindi cha mwaka 2020/21 hadi 2024/25, Serikali imefanikiwa kuwalipa malimbikizo ya mishahara walimu 101,596, kulipa watumishi 156,556 madeni yasiyo ya mishahara na kuongeza mshahara kwa watumishi wa umma ambapo kima cha chini kuanzia mwezi Julai, 2025 kitakuwa shilini 500,000 badala ya 370,000.


“Serikali inaendelea kutoa ajira za walimu ambapo kuanzia mwaka 2021 hadi sasa, jumla ya walimu 40,527 wameajiriwa katika maeneo mbalimbali nchini. Lengo la kufanya hivi ni kutatua changamoto mbalimbali zilizopo,” amesema Dkt. Biteko.


Amepongeza matokeo ya zoezi la ‘Samia Teachers Mobile Clinic’  kwa kuwafikia walimu 48,380 pamoja na kutatua kero zao huku akiwaomba kuongeza ubunifu utakaowawezesha kuwa na mikakati mingine yenye lengo la kuimarisha utendaji katika sekta ya elimu na kushirikiana na Serikali kwa kutekeleza miradi ya Elimu ya TEHAMA kwa walimu na miradi mingine isambae  kwenye mikoa yote nchini.

Kuhusu ombi la walimu kuwa na mwajiri mmoja anayeshughulikia masuala yote ya walimu ili kuimarisha ufanisi katika kuwasimamia. Dkt. Biteko amesema Serikali imelipokea ombi hilo na italifanyia tathmini ili kubaini endapo utaratibu uliopo sasa una changamoto zinazolazimu kutatuliwa kwa kuanzisha chombo kitakachosimamia walimu wote nchini.


Amezungumzia utekelezaji wa mtaala ulioboreshwa na kusema kuwa lengo lake ni kukuza elimu inayotolewa nchini na kuwafanya wanafunzi waweze kujitegemea wanapomaliza masomo yao. Aidha, Serikali inaendelea kuchukua hatua stahiki kuhakikisha kuwa walimu wote wanapata mafunzo ili waweze kuendana na mabadiliko hayo. 


Fauka ya hayo, kufuatia kufanyika kwa uchaguzi wa viongozi wa CWT, amewasihi wajumbe wa Mkutano huo kutumia haki yao katika kuchagua viongozi watakaowaongoza vyema na kuwataletea maendeleo pamoja  wagombea kuomba kura kwa heshimiana.

  


“ Nawasihi kuendelea kusimamia misingi ya haki, usawa na uwazi hususan wakati wa majadiliano na utatuzi wa masuala yote yanayohusu chama chenu. Niwaombe watakaoshinda msiwanange watakaoshindwa na mtakaokosa nafasi msikasirike, asitokee mtu wa kuwagawanya, msigawanyike hii ni taalamu ya pili ya uumbaji, mshikamane, mpendane na mshirikiane,” amesisitiza Dkt. Biteko.


Naye, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Ridhiwan Kikwete amesema kuwa Serikali inathamini mchango wa walimu katika mipango mbalimbali ya Taifa na kuahidi kuendeleza ushirikiano mzuri kwa ajili ya ujenzi wa Taifa na uchumi imara.

Kupitia mkutano huo, Rais wa Chama Cha Walimu Tanzania, Leah Ulaya amempongeza Rais Samia kwa utendaji kazi wake na kuahidi kuwa CWT itaendelea kushirikiana na Serikali .


Naye, Kaimu Katibu Mkuu wa Chama Cha Walimu Tanzania (CWT), Joseph Misalaba ameishukuru Serikali kwa kuendelea kulipa stahiki mbalimbali za walimu ambapo walimu wamenufaika kwa kupandishwa vyeo, ulipwaji wa malimbikizo ya mishahara na madeni yasiyo ya mishahara.


“ Kwa niaba ya watumishi wa Tanzania hususan walimu wote tunaipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kusikiliza kilio cha wafanyakazi juu ya suala la kikokotoo cha mafao ya kustaafu na kuridhia kuboresha kikokotoo kutoka asilimia 33 hadi asilimia 40. Chama cha Walimu Tanzania kinaiomba Serikali yako iendelee kufanya maboresho zaidi ili kuleta ustawi wa walimu wetu wastaafu ambao wameitumikia nchi yao kwa uaminifu mkubwa,” amesema Misalaba.

Amefafanua kuwa CWT ni chama cha wafanyakazi ambacho msingi wake mkubwa ni kutetea haki na maslahi ya wanachama wake. Kama mdau wa elimu CWT itaendelea kushirikiana na Serikali na wadau mbalimbali wa elimu katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya elimu nchini.


Aidha, Mkutano huo wa mwaka wa CWT umehudhuriwa pia na wawakilishi wa vyama vya walimu kutoka nchi za Rwanda, Burundi, Afrika Kusini na Namibia. 


Mwisho

TFS yawakaribisha wawekezaji katika vivutio vya utalii wa misitu — yaweka bayana fursa mpya za kipekee

June 07, 2025 Add Comment

 


Na Mwandishi Wetu, Arusha

WAKALA wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umeeleza mikakati na fursa mbalimbali za uwekezaji na utalii wa misitu, huku ukizindua aina mpya ya vivutio ikiwemo usafiri wa waya (zipline) katika Ziwa Duluti, ikiwa ni sehemu ya kuongeza mazao na shughuli za utalii katika kampeni ya kuvutia watalii na wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.

Akizungumza katika Maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya Karibu Kilifair 2025 yanayoendelea jijini Arusha Juni 6,2025, Yusuph Tango - Mhifadhi TFS, alisema lengo la kushiriki maonesho hayo ni kuwafikia wadau muhimu na kuwaeleza fursa zilizopo katika sekta ya utalii wa misitu nchini.

 "Tuko hapa kuwaeleza wadau wetu kuhusu mazao ya utalii tuliyonayo. Tuna maeneo mengi ya misitu nchini yenye vivutio vya kipekee vinavyofaa kwa utalii wa kimazingira na pia tuna fursa nyingi za uwekezaji wa huduma kama vile malazi, burudani (recreations) ndani ya misitu,” alisema Tango.

Aliendelea kusema, TFS kwa kushirikiana na wadau imeanzisha mazao ya kipekee ikiwemo usafiri wa waya (zipline) katika Ziwa Duluti, Arusha, ambacho kitakuwa cha kwanza nchini kupita juu ya maji, jambo linalotoa fursa ya kumbukumbu za kipekee kwa watalii.

    “Utalii huu ni sehemu ya jitihada za TFS kubuni njia mpya za kutumia fursa ya huduma
zitokanazo na misitu kama chanzo cha mapato ya taifa na ajira,” aliongeza.

Kwa mujibu wa Tango, TFS imeweka mkazo katika kukuza utalii wa misitu kwa kushirikiana na sekta binafsi kuwekeza katika maeneo yenye vivutio vya asili, huku akibainisha kuwa baadhi ya misitu tayari imeanza kunufaika na uwekezaji huo.



Akitolea mfano wa matukio yanayotarajiwa mwezi huu wa Juni, Tango alieleza kuwa TFS inaandaa matukio mawili makubwa ya utalii wa mazingira — Rubare Marathon itakayofanyika ndani ya Shamba la Miti Rubare, Bukoba, na West Kili Forest Challenge itakayofanyika katika Shamba la Miti West Kilimanjaro, jirani na geti la Londorosi linaloelekea Mlima Kilimanjaro.

    “Katika matukio haya kutakuwa na shughuli kama mbio za msituni, kuendesha baiskeli, mbio za pikipiki, pamoja na kutembelea maporomoko ya maji na vivutio vya kipekee ndani ya misitu,” alisema.

Mbali na hayo, TFS pia imetangaza kuongeza msukumo katika kukuza utalii wa nyuki (api-tourism), ambao umeanza kuonyeshwa kama zao jipya la kiutalii nchini. Kwa sasa, shughuli hiyo inatekelezwa katika maeneo ya Mlima Hanang, Vikindu (Mkuranga), na maeneo mengine yanayoratibiwa kuingizwa kwenye mpango huo.

    “Mhe. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati walionesha kuvutiwa sana na api-tourism. Walituhimiza tuiendeleze maeneo mengine ili itoe tija kwa taifa na jamii zinazozunguka misitu hiyo,” alieleza Tango.

Alisisitiza kuwa TFS imejipanga kushiriki kikamilifu katika kufanikisha azma ya serikali ya kuongeza idadi ya watalii nchini, kwa mujibu wa malengo ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama Tawala.

    “Malengo ya serikali ni kuongeza watalii. Sisi TFS tumepewa jukumu la kuchangia hilo kupitia vivutio vya misitu na huduma bunifu za utalii. Kwa hiyo, tuko tayari kushirikiana na wadau wote kuifikia Tanzania ya utalii endelevu,” alihitimisha.

Maonesho ya Karibu Kilifair 2025 yanayofanyika jijini Arusha, yamekusanya wadau wa sekta ya utalii kutoka mataifa mbalimbali, ambapo TFS ni miongoni mwa taasisi za serikali zinazotumia jukwaa hilo kuhamasisha uwekezaji na kukuza utalii wa ndani.

--

Tulizo Henry Kilaga I A Brand Communication Strategist,

Located: Dodoma I Dar es Salaam - Tanzania. 

Call/WhatsApp: +255 765 888887

www.thestrategist.co.tz


TAASISi 762 ZATUMIA NISHATI SAFI YA KUPIKIA NCHINI-DKT.MPANGO

June 07, 2025 Add Comment


📌 Taasisi chini ya Wizara ya Nishati zqpewa tuzo kutambua mchango wao katika Gesi, Umeme na Nishati Jadidifu


Makamu Wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.  Philip Isdor  Mpango ameeleza kuwa jumla ya taasisi 762 nchini zinatumia nishati safi ya kupikia ikiwa ni jitihada za kuepuka athari za kimazingira, kiafya, kijamii na kiuchumi.


Amesema hayo tarehe 5 Juni 2025 katika kilele cha Siku ya Mazingira Duniani ambayo  kitaifa imeadhimishwa jijini Dodoma katika kituo cha  Mikutano cha Jakaya Kikwete.


 "Taasisi nyingi za Serikali na Binafsi zimeanza kutekeleza katazo la matumizi ya nishati isiyo safi na  kuanza kutumia nishati safi ya kupikia ambapo  hadi Machi 2025 jumla ya Taasisi 762 zilikuwa zimeanza kutumia nishati safi ya kupikia." Amesema Dkt. Mpango


Ameongeza kuwa,  kati ya taaisis hizo, taaisisi za Umma ni 495 na taasisi binafsi ni 267.i 


 Makamu wa Rais amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa kinara wa kuendeleza na kusukuma matumizi ya nishati safi ya kupikia Tanzania, Afrika na Duniani kwa ujumla.

Sambamba na hilo Dkt. Mpango amezipongeza taasisi zote zilizotekeleza katazo hilo la kutotumia nishati isiyo safi  na kutoa rai kwa taasisi ambazo hazijatekeleza agizo hilo ziendelee kuwekeza katika matumizi ya nishati safi ya kupikia. 


Katika hafla hiyo ya Siku ya Mazingira dunian,   Dkt. Mpango ametoa Tuzo kwa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati ikiwa upande wa REA tuzo imepokelewa na Kaimu Mkurugenzi wa Usimamizi wa Rasilimali Watu na Utawala wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Bw. Renatus Msangira tuzo ya kutambua mchango wa REA katika kutunza mazingira  kupitia utekelezaji wa miradi ya nishati safi ya kupikia.

Miradi hiyo ambayo ni utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia ni pamoja na usambazaji wa mitungi ya gesi pamoja na majiko banifu kwa bei ya ruzuku kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa nishati safi ya kupikia vijijini .


Aidha, TANESCO tuzo hiyo imepokelewa na Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Bw. Lazaro Twange,ikiwa ni kutambua mchango wa TANESCO katika kuhifadhi mazingira kupitia utekelezaji wa Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP), ambao umeendelea kuzingatia misingi ya utunzaji wa mazingira sambamba na kuchangia kupunguza gesi joto.

Huku, CPA Mussa M. Makame - Mkurugenzi Mtendaji TPDC, amepokea TUZO  ya kutambua mchango wa TPDC katika kuhifadhi  na kutunza mazingiza kupitia matumizi ya gesi asilia iliyoshindiliwa (CNG).



DKT.BITEKO AWEKA JIWE LA MSINGI UJENZI WA KITUO KIKUBWA CHA GESI AFRIKA MASHARIKI

June 05, 2025 Add Comment


📌 *Tanga kuwa Kitovu cha Nishati nchini*


📌 *Dkt. Biteko Asisitiza Ajira Kwa Wazawa*


📌*Kampeni ya Rais Samia ya Nishati Safi ya Kupikia  Yavutia Wawekezaji*


📌*Matumizi ya Gesi ya Kupikia Yaongezeka Kila Mwaka*


*Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati*


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ametoa wito kwa wawekezaji nchini kutoa kipaumbele cha ajira kwa Watanzania ili kukuza kipato cha mtu mmoja mmoja na uchumi wa Taifa kwa ujumla.


Amewaomba wawekezaji wa mradi wa Kituo cha Gesi cha Tanga International Energy licha ya kuwa zitazalishwa ajira zaidi ya 300 na baadae zaidi ya 2,000, waangalie utaratibu katika ujenzi wa mradi huo ambao utawezesha wazawa kupata kazi na hakuna sababu ya kutafuta watu kutoka mbali.


Dkt. Biteko ametoa wito huo leo Juni 5, 2025 jijini Tanga wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika ujenzi wa Kituo cha Gesi cha Tanga International Energy mkoani humo.


“ Mradi huu uwe mfano wa kielelezo kila kazi anayoweza kufanya Mtanzania apewe, ili asilimia 40 ya fedha za ujenzi wa mradi zizunguke nchini. Nitasikitika nikiona kila aina ya kazi analetwa mtu kutoka nje kuja kufanya,” amesema Dkt. Biteko.

Ameendelea kutoa wito kwa wawekezaji kufikiria namna ya kupeleka huduma ya ujazaji mitungi ya gesi katika maeneo ya vijijini ikiwa ni pamoja na kuanzisha teknolojia ya kusaidia mtu aweze kulipia gesi kulingana na mahitaji yake badala ya kujaza mtungi mzima.


Dkt. Biteko amesema kwa mujibu wa taarifa ya utendaji sekta ndogo ya mafuta ya EWURA ya mwaka 2024, matumizi ya gesi ya kupikia yaani (LPG) huongezeka kwa kasi kila mwaka. Ambapo kwa mwaka 2023/24 matumizi yalifikia zaidi ya tani 403,000 ikilinganishwa na tani 293,000 mwaka wa fedha 2022/23 sawa na ongezeko la asilimia 38.


Amewahakikishia Kampuni ya Tanga Energy International Ltd kuwa mradi wao utakuwa na uhakika wa soko ndani na nje ya nchi na kuwa Serikali itaendelea kushirikiana nao  ili kufikia malengo yao ya kuleta huduma bora na nafuu kwa Watanzania.

Katika kuthibitisha hilo, Dkt. Biteko amesema kupitia Wakala wa Nishati Vijijini, Serikali inaendelea na programu ya kutoa ruzuku ili wananchi wapate mitungi ya gesi ya kupikia kwa punguzo la bei hadi kufikia asilimia 50 na kusambaza mitungi 452,445 ambapo hadi kufikia Aprili, 2025 jumla ya mitungi 154,225 imeshasambazwa.


“ Tarehe 2 Juni, 2025 pale jijini Dodoma tumezindua Mkakati wa Taifa wa Mawasiliano wa Nishati Safi ya Kupikia. Hivyo, kupitia Mkakati huu, Serikali itaendelea kutoa elimu nchi nzima na hivyo kuinua uelewa wa wananchi na hatimaye kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia ambapo LPG ni chanzo kikuu,” amesisitiza Dkt. Biteko.

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amesema Rais Samia anataka Mkoa wa Tanga uwe kitovu cha biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki, na hivyo ameendelea kufanya jitihada mbalimbali ili kutimiza lengo hilo ikiwemo kupanua mfumo wa kusafirisha umeme kutoka Majani mapana hadi Pemba kutoka kilovoti 33 hadi 132.


Pamoja na hayo ametoa wito kwa Watanzania kushiriki katika Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu kwa kuchagua viongozi wanaofaa “ Tumuunge mkono Rais Samia kwa kuwa kinara wa Kampeni ya Nishati Safi kimataifa ili Watanzania wengi watumie nishati safi ya kupikia,” amemaliza Dkt. Biteko.


Naye, Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Suleiman Jafo amesema kuwa utendaji kazi wa Dkt. Biteko umesaidia kuimarika kwa sekta ya nishati huku akisisitiza kuwa kukamilika kwa mradi huo mkubwa wa Kituo cha Gesi kutaifanya Tanzania kuwa msafirishaji mkubwa wa gesi  na kuchochea ukuaji wa viwanda nchini.


Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Balozi Batilda Burian amesema mradi huo utasaidia kuitangaza Tanga kimataifa, kuongeza ajira na pato la mkoa na Taifa kwa ujumla.

Akitoa salamu za Chama cha Gesi na Mafuta, Mkurugenzi Mtendaji wa TOAG, Abdulsamad Abdulrahim amesema mradi huo utaisaidia Tanzania kuleta mapinduzi ya nishati katika ukanda wa Afrika Mashariki, kupunguza athari zinazotokana na matumizi ya nishati isiyo safi.


Bw. Abdulrahim amebainisha kuwa Watanzania wako tayari na hiyo ni fursa kwa wawekezaji wazawa kuonesha uwezo wao na wako tayari kufanya kazi.


“Tunaishukuru Serikali kwa kuweka mazingira wezeshi ya kusaidia utekelezaji wa miradi kama hii ambayo ni zao la ushirikiano wa wageni na wazawa wenye kufanya mawazo kuwa uhalisia,” amesema Abdulrahim.


Awali akitoa maelezo ya mradi, Michael Dimond amesema LPG ni suluhu ya nishati safi ya kupikia na kuwa Kampuni ya Pretedec imefurahishwa jitihada za Rais Samia katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia na lengo la Serikali la kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.


“Leo tunajivunia kuwekwa kwa jiwe la msingi katika mradi huu wa kipekee Tanzania ambao umezingatia usalama wa usambazaji wa LPG katika ukanda wa Afrika Mashariki,” amesema Dimond.


Mwakilishi wa Kampuni ya Asas, Bw. Ahmed Asas amesema mbali na manufaa ya kiafya na mazingira mradi huo utachochea uchumi jumuishi na kuchangia katika ukuaji wa viwanda vya ndani.


Mradi wa Kituo cha Gesi cha Tanga International Energy unatekelezwa kwa ushirikiano wa Kampuni ya Pretedec na Asas ambao unatagharimu dola za marekani milioni 100 utakuwa mradi mkubwa wa LPG nchini. Aidha, kupitia mradi huo unaotarajiwa kukamilika 2027 utanufaisha pia nchi za Burundi, Kenya, Uganda, Burundi na Zambia kwa kuagiza gesi kutoka nchini Tanzania.


Mwisho