UDSM yawaita Wadau wa Elimu kushiriki maadhimisho Wiki ya Utafiti na Ubunifu

June 05, 2025 Add Comment

 

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.

CHUO  Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimeutaarifu umma wa Watanzania na kuwaalika wadau wa elimu na maendeleo, kwa ujumla kushiriki katika Maadhimisho ya kumi ya Wiki ya Utafiti na Ubunifu ya UDSM yatakayofanyika kuanzia Juni 9- 11, 2025 katika Viwanja ya Maktaba ya Chuo.

Akizungumza na Waandishi  wa Habari Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo-Utafiti, Prof. Nelson Boniface (Pichani) amesema kuwa Maonesho hayo yanatarajiwa kuhitimishwa Juni 11, 2025 na mazungumzo ya mashirikiano ya kimkakati, kongamano, maonesho na mawasilisho ya watafiti na wabunifu likiwa ni jukwaa la washiriki kupata fursa ya kubadilishana maarifa na ushirikiano.

Aidha, Prof.  Boniface amesema kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni: "Kutumia teknolojia ya Dijitali ili kukuza utafiti, ubunifu na ubiasharishaji,".

Ameongeza kuwa miradi mingi itakayooneshwa ni ile ya wanafunzi na Wanataaluma huku akitanabaisha kuwa mtoa Mada Mkuu ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), Mhandisi Peter Ulanga na Profesa Lilian Kaale Mkurugenzi katika masuala ya Ubunifu UDSM.

Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kinatumia fursa hiyo kujipambanua kwa jamii kwa kuonesha shughuli zake za utafiti, ubunifu, huduma kwa umma na ubadilishanaji maarifa kwa kuunga mkono Dira ya  Taifa ya  Maendeleo 2050.



Ukerewe yawashukuru wafanyakazi Benki ya CRDB ukarabati madarasa mawili, madawati 200

June 04, 2025 Add Comment

 


Mkuu wa Wiliya ya Ukerewe, Mheshimiwa Christopher Emily Ngubiagai amewashukuru wafanyakazi wa Benki ya CRDB kwa kukarabati madarasa mawili na madawati 200 kwa ajili ya Shule ya Msingi Hamkoko.

Akipokea msaada huo kutoka kwa Mkurugenzi wa Rasilimali Watu wa Benki ya CRDB, Godfrey Rutasingwa, mkuu huyo wa wilaya amesea mazingira mabovu ya madarasa yanasababisha utoro kwa watoto wengi jambo ambalo seriklai inashirikiana na wadau kulifanyia kazi ili watoto wote wasome kwa utulivu unaohitajika kufanikisha ndoto zao.

“Hakika leo wafanyakazi wa Benki ya CRDB mmetupa somo kwa kujitoa kwenu kuhakikisha mnaigusa jamii jamii yetu ya wana Ukerewe. Hakika huu ni upendo mkubwa sana kutoka kwa wafanyakazi ambao sio tu inatugusa jamii ya hapa Ukerewe bali Tanzania nzima kwa ujumla. Mmeonyesha kujali na alama hii ya upendo haitosahaulika. Asanteni sana kwa heshima hii kubwa mliyotupa,” amesema Mheshimiwa Ngubiagai.

Amesisitiza kuwa shule zikiwa na miundombinu mizuri huwafanya watoto wapende kusoma kutokana na kuvutiwa na mazingira mazuri na madarasa ya kisasa, madawati bora ya kukalia. Kwa kulitambua hilo, amesema serikali inafanya kila liwezekanalo kuhakikisha inajenga shule mpya popote inapohitajika nchini na kukarabati miundombinu ya hsule za miaka mingi.

Akizungumza na wazazi, walimu na wanafunzi waliokuwepo kwenye hafla ya kukabidhi madarasa na madawati hayo, Mheshimiwa Ngubiagai amesema ni muhimu kwa jamii kujitoa kuchangia kuboresha mazingira ya shule kwa ajili ya watoto wa Kitanzania kujifunza kwa umakini na akaitumia nafasi hiyo kuwapongeza wafanyakazi wa Benki ya CRDB kwa kuonyesha mfano katika kujitoa kwa jamii wanaoyoihudumia na inayowazunguka.

“Hii imekuwa bahati kwetu kwani mngeweza kwenda sehemu nyingine lakini mliona inafaa kuja Ukerewe kusaidia kutatua changamoto za madarasa na kutoa madawati haya 200. Kwa kweli mmetufundisha na kutupa deni kubwa mioyoni mwetu kwani Watanzania wengi huwa wepesi kuchangia harusi na sherehe nyingine ila wazito kujitoa kwenye elimu kama mlivyofanya wafanyakazi wa Benki ya CRDB,” amesema.

Kwa upande wake, Rutasingwa amesema msaada huo umetolewa kupitia Programu ya Employee Volunteering iliyoanzishwa mwaka 2020 ambapo wafanyakazi wa Benki ya CRDB huchanga fedha kutoka kwenye mishahara yao na kuielekeza kutatua kero iliyopo kwenye jamii katika sekta ya elimu, afya, mazingira na watu waishio katika mazingira magumu.

“Moyo huu wa kujitoa kwa wafanyakazi wetu ni mwendelezo wa jitihada zinazofanywa na Benki ya CRDB kurudisha na kuwekeza katika jamii inapotoa huduma. Benki yetu hutenga asilimia moja ya faida yake baada ya kodi kwa ajili ya kuiwezesha jamii. Tunachangia madarasa, madawati, na miundombinu mingine ya shule. tunatoa vifaatiba na kuhamasisha afya ya jamii. Kupitia kampeni ya Pendezesha Tanzania, tunashiriki kutunza mazingira ili kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi na tupo mstari wa mbele katika kuwawezesha wanawake na vijana kujitegemea kiuchumi,” amesema Rutasingwa.

Mkurugenzi huyo amefafanua kuwa utekelezaji wa Programu ya Employee Volunterring unaanzia ngazi ya mfanyakazi mmoja mmoja, matawi, ofisi za kanda mpaka idara za makao makuu ya Benki ya CRDB.

“Katika ngazi ya kanda, tayari tumeratibu na kutekeleza miradi katika kanda za Pwani, Dar es Salaam, na Kaskazini. Leo tunafungua ukurasa mpya wa jitihada hizi katika Kanda hii ya Ziwa kwa kukabidhi rasmi madarasa mawili na madawati 200 kwa shule hii ya Hamukoko hapa wilayani Ukerewe,” ameeleza Rutasingwa.

Kwa wazazi, Rutasingwa amewakumbusha umuhimu wa kuandaa mazingira haya ya kiuchumi kugharimia elimu akieleza kwamb benki ya CRDB inayo Akaunti ya Junior Jumbo inayomwezesha mzazi kuweka fedha taratibu kwa ajili y amahitaji ya mwanaye huku ikimwandaa mtoto kuwajibika kiuchumi kwa kuanza kutumia huduma za benki tangu akiwa mdogo.

“Akaunti hii haina makato na inamwezesha mzazi kuweka akiba kidogo kidogo kwa ajili ya masomo ya mtoto wake, kuanzia elimu ya awali hadi chuo kikuu. Unachohitaji ni cheti cha kuzaliwa cha mtoto, kitambulisho cha mzazi au mlezi, na shilingi 5,000 ya kuanzia ili kufungua akaunti hii,” amesema.

MHE. MCHENGERWA AWAFUNDA WALIMU

June 04, 2025 Add Comment

Na John Mapepele

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Mhe. Mohamed Mchengerwa ametoa rai kwa walimu nchini kuwa wazalendo na kuzingatia weledi ili kuongeza ufaulu wa wanafunzi.

WAZIRI MCHENGERWA AWAFUNDA WALIMU AWATAKA WAWE WAZALENDO KUZINGATIA MAADILI

June 04, 2025 Add Comment


Na John Mapepele 


Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Mhe. Mohamed Mchengerwa ametoa rai kwa walimu nchini kuwa wazalendo na kuzingatia weledi ili kuongeza ufaulu wa wanafunzi. 


Mhe. Mchengerwa ametoa rai hiyo kwenye mkutano wa walimu na wadau wa elimu  wa Wilaya ya Rufiji uliofanyika kwenye ukumbi wa shule ya Sekondari ya Wasichana Bibi Titi Mohamed, ambapo yeye mwenyewe pia alitunukiwa tuzo ya heshima ya kutambua mchango wake katika sekta ya elimu wilayani Rufiji.

"Katika hali ya kawaida  Serikali imeboresha mazingira na miundombinu ya sekta ya elimu kilichobaki ni kwa sisi walimu kutanguliza uzalendo ili kuinua kiwango cha elimu katika ngazi zote" . Amesisitiza Mhe. Mchengerwa 


Aidha, amesisitiza walimu kutambua wajibu wao na kwamba Serikali haitaweza kusita kuwachukulia hatua za kinidhamu  Walimu na Maafisa Elimu ambao watakuwa wazembe katika utekelezaji wa majukumu yao.

Katika taarifa ya Wilaya ya Rufiji kwa Mhe. Waziri, iliyoandaliwa na  Mkurugenzi Mtendaji  wa Rufiji, bwana Simon Berege, inaonyesha kuwa kumekuwa na ongezeko la wanafunzi wanaohitimu darasa la Saba kutoka 3135 mwaka 2020 hadi wanafunzi 3715 mwaka 2024.


Idadi ya shule za Awali na Msingi zimeongezeka  kutoka 48 mwaka 2021 Hadi 63 mwaka 2025 ikiwa ni ongezeko la shule 15 sawa na asilimia 31.3.


Pia vyumba vya madarasa  vimeongezeka  kutoka vyumba 377 mwaka2921 hadi vyumba566 mwaka 2025 ikiwa ni ongezeko la vyumba vya madarasa 189 sawa na asilimia 50. 1

Aidha, katika mashindano ya UMITASHUMTA ngazi ya mkoa, Halmashauri ya Mji wa Rufiji imefanikiwa kushinda kwa nafasi ya kwanza katika michezo ya mpira wa miguu, pete na riadha huku ikishika nafasi ya pili kwenye mpira wa mikono hivyo kushika nafasi ya pili ya ujumla katika mashindano hayo.

Katika mkutano huo Mhe.Waziri Mchengerwa alikabidhi makombe hayo kwa shule na baadaye kupokea msaada wa madawati 50 yaliyotolewa na Benki ya CRDB.



UTENDAJI KAZI WA WIZARA YA NISHATI NA TAASISI ZAKE WAIMARIKA KWA ZAIDI YA ASILIMIA 95

June 04, 2025 Add Comment



📌 *Dkt. Biteko apongeza; akumbusha Watendaji umuhimu wa tathmini katika kuboresha utendaji kazi*


📌 *Ataka TANESCO kuendelea kuboresha miundombinu ya umeme; kubuni vyanzo vipya*


📌 *Aziagiza Taasisi chini ya Wizara kuungana kuitekeleza Ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia*


📌 *Ofisi ya Waziri Mkuu yaipongeza Wizara kutekeleza miongozo ya ufuatiliaji na Tathmini kwa asilimia 100*


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewapongeza Watendaji wa  Wizara ya Nishati na Taasisi zake kwa kuendelea kuimarisha utendaji kazi na hivyo kuifanya Sekta ya Nishati kuwa na matokeo chanya katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

Dkt. Biteko ametoa pongezi hizo kufuatia tathmini ya utendaji kazi iliyofanywa na Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini katika Wizara ya Nishati ambayo imeonesha kuwa katika kipindi cha robo ya tatu ya mwaka 2024/2025 utendaji kazi  wa Wizara/Taasisi umeimarika kwa zaidi ya asilimia 95.


Katika kikao cha Nne cha tathmini ya utendaji kazi wa Wizara ya Nishati na Taasisi zake kilichofanyika jijini Dodoma, Dkt. Biteko amesema kuwa, tathmini hiyo inasaidia  kujiimarisha hasa ikizingatiwa kuwa Sekta ya Nishati ina muhimu mkubwa kiuchumi na kijamii.

“Sekta hii ni muhimu sana nchini kwa kuwa ni Sekta ya huduma na sekta ya uchumi hivyo ikilegalega italeta malalamiko, ningependa kuona sekta hii inaendelea kuwa na matokeo mazuri kwa wananchi.” Amesema Dkt. Biteko

Katika kikao hicho, Dkt. Biteko ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuendelea na kasi ya ukarabati wa miundombinu ya umeme pamoja na kuendelea kutafuta vyanzo vipya vya umeme.


Aidha, ameupongeza Wakala wa Nishati Vijijini (REA), kwa kasi iliyofanya ya kupeleka umeme vijijini na kuwezesha vijiji vyote kupata umeme pia kwa kuendelea na kasi ya kupeleka umeme vitongojini.

Kuhusu Nishati Safi ya Kupikia, Dkt. Biteko amezitaka Taasisi zilizo chini ya Wizara hususan, REA, TPDC na TANESCO kuunganisha nguvu katika kutekeleza Ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia ili ikue na kufanikiwa na hivyo kutimiza lengo la Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan la kuhakikisha kuwa wananchi wanahama kutoka matumizi ya Nishati isiyo safi kwenda kwenye matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia.

Dkt. Biteko amekipongeza Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini katika Wizara ya Nishati  kwa kutekeleza jukumu lao kwa ufanisi na kukumbusha Watendaji wa Wizara ya Nishati na Taasisi zake  kuwa, zoezi hilo la tathmini linapaswa kuwa  ni endelevu kutokana na umuhimu wake katika kuboresha utendaji kazi.

Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith.Kapinga kwa upande wake, amezipongeza Taasisi zote zilizo chini ya Wizara ya Nishati pamoja na Idara na Vitengo vya Wizara ya Nishati kwa utendaji kazi wenye kuleta matokeo kama ambavyo tathmini ya utendaji kazi iliyotolewa ilivyoonesha kuwa ufanisi wa kazi umeendelea kuimarika.

Aidha amezitaka Taasisi chini ya Wizara ya Nishati kuibeba Ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia ili kufikia lengo la Serikali la kufikisha asilimia 80 ya Watanzania wanaotumia Nishati Safi ya Kupikia ifikapo 2034.

Awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba alisema kuwa kikao hicho cha tathmini ya utendaji kazi wa Wizara na Taasisi zake ni cha nne kutoka vikao vivyo vimeanza kufanyika.

Alieleza kuwa, kutoka zoezi la kupima utendaji kazi wa Wizara na Taasisi lianze kufanyika limeleta ufanisi hasa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali pamoja na mipango ya Wizara.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Ufuatiliaji na Tathmini  ya Utendaji wa Serikali, kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Bi. Sakina Mwinyimkuu ameipongeza Wizara ya Nishati kwa kutekeleza miongozo iliyowekwa na Ofisi hiyo ya ufuatiliaji na tathmini ambapo ameeleza kuwa Wizara ya Nishati imetekeleza miongozo iliyowekwa kwa asilimia 100.

Pia amempongeza Dkt. Doto Biteko kwa dhamira yake ya dhati katika kusimamia utendaji kazi wa Serikali hasa Sekta ya Nishati ambayo anaisimamia akiwa ni Waziri wa Nishati.

Vilevile, ameipongeza Wizara ya Nishati kwa kutoa motisha kwa Taasisi na Idara/Vitengo zilizofanya vizuri zaidi katika tathmini ya utendaji kazi hali ambayo inaongeza ari ya kazi.

Taasisi zilizofanya vizuri Katika tathmini ya utendaji kazi iliyofanyika katika robo ya tatu ya mwaka 2024/2025 ni  Wakala wa Nishati Vijijini (REA) aliyeshika nafasi ya kwanza, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) aliyeshika nafasi ya pili na Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) aliyeshika nafasi ya tatu.  

Aidha, Idara/Vitengo vya Wizara ya Nishati vilivyofanya vizuri Katika tathmini ya utendaji kazi iliyofanyika katika robo ya tatu ya mwaka 2024/2025 ni  Kitengo cha Ugavi na Manunuzi (nafasi ya kwanza), Kitengo cha Sheria (nafasi ya pili), na Kitengo cha TEHAMA (nafasi ya tatu).

Mikoa ya Kitanesco iliyofanya vizuri katika tathmni ya utendaji kazi ni Manyara (nafasi ya kwanza), Arusha (nafasi ya pili) na Simiyu (nafasi ya tatu).

Hata hivyo ilielezwa kuwa kwa ujumla ufanisi wa utendaji kazi wa Idara na Vitengo vya Wizara pamoja na Taasisi zake umeendelea kuimarika kwa zaidi ya asilimia 95.

Kikao hicho kilihudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt, James Mataragio, Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara, Menejimenti ya Wizara ya Nishati  na Taasisi zake pamoja na   Mameneja  wa Mikoa wa TANESCO.