DKT.BITEKO KUZINDUA MKAKATI WA TAIFA WA MAWASILIANO WA NISHATI SAFI YA KUPIKIA

May 30, 2025 Add Comment

 


 Imeelezwa kuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko tarehe 2 Juni 2025 atazindua Mkakati wa Taifa wa Mawasiliano wa Nishati Safi ya Kupikia ambao ni nyenzo muhimu katika kuhakikisha kuwa asilimia 80 ya Watanzania wanatumia Nishati Safi ya Kupikia ifikapo 2034.


Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba amesema uzinduzi wa Mkakati utaenda sambamba na uzinduzi wa Kampeni ya Kitaifa ya Uhamasishaji na  Uelimishaji wa matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia.


Mramba ameeleza kuwa mkakati huo umeandaliwa na Wizara ya Nishati  kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Mitaji la Umoja wa Mataifa (UNCDF) chini ya ufadhili wa Umoja wa Ulaya (EU), ikiwa ni pamoja na Kampeni ya Kitaifa ya Uhamasishaji na Uelimishaji kuhusu Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia.


 Ameongeza kuwa  uzinduzi huo utaenda sambamba na Wizara ya Nishati  kukabidhiwa magari mawili kwa ajili ya  kuendesha Kampeni ya Kitaifa ya Uhamasishaji wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia ili kuwafikia wananchi hasa sehemu za vijijini.


Mhandisi Mramba amesema Mkakati unalenga masuala mbalimbali ikiwemo kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu faida za nishati safi ya kupikia katika afya, mazingira na uchumi wa kaya, kuhamasisha mabadiliko ya tabia kutoka kwa matumizi ya nishati isiyo safi ya kupikia kama mkaa na kuni, kuhamasisha uwekezaji na ushiriki wa sekta binafsi katika soko la bidhaa za nishati safi ya kupikia na kujenga mazingira ya sera na udhibiti yanayosaidia upatikanaji na upatikanaji wa nishati safi kwa wote.


Amesema mbinu mbalimbali za mawasiliano zitatumika  ikiwemo  vyombo vya habari vya kitaifa na kimataifa,  viongozi wa kimila, kidini, na kisiasa, matumizi ya mitandao ya kijamii na mafunzo kwa watendaji wa Serikali na Waandishi wa Habari na kuyafikia makundi mbalimbali  ya wananchi wa mijini na vijijini, wanawake na vijana, watoa huduma za afya, viongozi wa serikali za mitaa, mashirika ya kiraia na sekta binafsi.


Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Marc Stalmans, Mkuu wa Ushirikiano wa  Umoja wa Ulaya upande wa Tanzania na Bw. Immanuel Muro, Mtaalam Mwandamizi wa fedha kutoka UNCDF ambao kwa pamoja wameeleza kuunga mkono juhudi za Serikali katika Uhamasishaji wa Nishati Safi ya Kupikia.




TAKUKURU TANGA YABORESHA MFUMO WA HUDUMA ZA UDHIBITI TAKA NGUMU JIJINI TANGA

May 30, 2025 Add Comment


Na Oscar Assenga, TANGA

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoani Tanga (Takukuru) imesema kwamba moja ya mafanikio ya utendaji wake kazi katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia Januari hadi Machi 2025 uboreshaji mfumo wa huduma za udhibiti Taka Ngumu Jijini Tanga.

Hayo yalisemwa leo na Kaimu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Tanga Mariam Mayaya wakati akitoa taarifa kwa umma juu ya mafanikio ya utendaji kazi wa Taasisi hiyo kwa kipindi cha Januari hadi Machi 2025.

Alisema kwa upande wa uchambuzi wa mifumo katika kipindi hicho taasisi hiyo imefanikiwa kutekeleza matakwa ya sheria na kanuni za udhibiti taka ngumu nchini Tanzania kwa kutumia mfumo wa Punguza,Tumia Tena na Rejeleza taka (PTR) au Reduce,Re-use and Reycle (3R),

Aidha alisema katika mkoa wa Tanga mfumo huo ulianza katika kata ya Central,Chumbageni na Ngamiani Kati pamoja na utekelezaji wa sheria ya udhibiti wa taka ngumu,uchambuzi uliofanywa na Takukuru umesaidia mikakati na maazimio ya kulipwa kwa madeni ya wazabuni hivyo kufanya kazi ya uzoaji taka kuanza kutekelezwa kwa ufanisi.

Mariam alisema kwamba kwa ujumla zimefanyika chambuzi za mifumo 20 katika sekta za udhibiti take na usafi wa Mazingira,Afya,Kilimo na mapato ambapo wamefanikiwa kubaini mapungufu na kuwasilisha ripoti za chambuzi husika kwa wadau ambazo zimejadiliwa na maazimio yaliyofikiwa yametekelezwa na mengine yanaendelea kutekelezwa kwa ufanisi.

Akizungumzia ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo,Mariam alisema kwamba katika kipindi cha Januari hadi Machi 2025 walifanya kazi ya ufuatiliaji wa matumizi ya rasilimali za umma katika miradi 54 yenye thamani ya Bilioni 240,264,703,118.09.

Alisema katika ufuatiliaji wa miradi hiyo iliyopo katika sekta za Maji,Elimu na Afya ambapo miradi 12 yenye thamani ya Sh.Bilioni 5,468,760,058 ilibainika kuwa na mapungufu ambapo ushauri wa marekebisho yalitolewa na hatua za marekebisho ya mapungufu hayo zimechukuliwa na miradi ipo katika hali inayokidhi ubora kulingana na thamani ya fedha zilizowekezwa.

SAME KAYA SACCOS YARUDISHA KWA JAMII KWA KUTOA MSAADA WA VIFAA NA MAHITAJI MUHIMU

May 29, 2025 Add Comment

 



Na Ashrack Miraji Tanga Raha  

Katika kuendeleza uwajibikaji kwa jamii, taasisi ya kifedha ya SAME KAYA SACCOS imetoa msaada wa vifaa mbalimbali kwa makundi yenye uhitaji katika Wilaya ya Same, Mkoa wa Kilimanjaro. Msaada huo umetolewa kama sehemu ya kuadhimisha mchango wa jamii katika mafanikio ya SACCOS hiyo, ikiwa ni mfano bora wa taasisi za kifedha kurudisha kwa jamii wanakotoka.

Kwa mujibu wa Meneja wa SAME KAYA SACCOS, Bi Elvera Mdee, taasisi hiyo imetumia jumla ya Shilingi milioni tano (Tsh. Mil 5) katika kugharamia ununuzi wa bidhaa hizo, ambazo ni pamoja na vyakula, vinywaji, sare za shule (uniforms), vifaa vya usafi na vifaa vya shule (stationery).


Walengwa wa msaada huo ni pamoja na hospitali ya Wilaya ya Same, Shule ya Sekondari Chauka iliyopo Hedaru, pamoja na kituo cha kulelea yatima cha Rafiki Children Centre kilichopo mjini Same. Kila taasisi ilipokea msaada kulingana na mahitaji maalum yaliyobainishwa awali.

Katika hafla ya kukabidhi misaada hiyo, Bi Elvera Mdee alieleza kuwa SAME KAYA SACCOS inaamini katika kuijali jamii na kuwa karibu na wananchi, hasa wale walio katika mazingira magumu. Alisisitiza kuwa mafanikio ya taasisi hiyo hayawezi kufikiwa bila ushirikiano kutoka kwa wananchi wa Wilaya ya Same.

Aidha, alitoa wito kwa taasisi nyingine za kifedha na wafanyabiashara binafsi kujitokeza na kusaidia jamii, hususan katika kipindi hiki ambapo hali ya kiuchumi imekuwa changamoto kwa wengi. “Tunaamini kwamba kila mmoja wetu ana wajibu wa kusaidia kule tunakoweza. SAME KAYA SACCOS inatambua umuhimu wa mshikamano na upendo kwa jamii,” alisema.


Wazazi, walimu na walezi waliopokea msaada huo kwa niaba ya walengwa walitoa shukrani zao kwa taasisi hiyo, wakieleza kuwa msaada huo umekuja wakati muafaka na utaongeza ari ya watoto kuhudhuria shule, pamoja na kuboresha huduma za afya na mazingira ya usafi katika maeneo yao.

SAME KAYA SACCOS imekuwa mstari wa mbele si tu katika utoaji wa huduma za kifedha, bali pia katika kuhakikisha kuwa jamii inayowazunguka inanufaika moja kwa moja na mafanikio ya taasisi hiyo. Hii ni sehemu ya dira yao ya kuhakikisha maendeleo jumuishi na yenye uwiano kwa wote




 

NCAA YATOA MAFUNZO KWA WADAU WA UTALII KUHUSU MATUMIZI YA MFUMO MPYA WA SAFARI PORTAL V2

May 29, 2025 Add Comment


Na Kassim Nyaki, NCAA.


Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) imetoa mafunzo ya siku mbili kuanzia tarehe 29 hadi 30 Mei, 2025 kwa wadau wa Utalii kuhusiana na matumizi ya mfumo mpya wa *Safari Portal V2* ulioboreshwa kutoka mfumo wa zamani wa Safari Portal.


Akifungua Mafunzo hayo Kaimu Meneja wa Huduma za Utalii na masoko NCAA, Afisa Uhifadhi Mkuu Peter Makutian ameeleza kuwa mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo wadau wote wa Utalii kuhusu matumizi ya mfumo mpya wa makusanyo ya mapato yatokanayo na shughuli za Utalii ambao umeboreshwa ili kurahisisha utoaji huduma kwa wadau wote wanaofanya kazi na NCAA.

"Tumeboresha mfumo wetu wa makusanyo ya mapato ya Utalii na utaaanza kutumika kuanzia tarehe  31/05/2025, kwa hiyo ni muhimu wadau wetu wanaopata huduma kupitia mfumo huu wawe na uelewa ya maboresho yaliyofanyika na kuwasaidia namna ya kuhamisha taarifa zao kwenye mfumo mpya kabla ya tarehe ya kuanza mfumo huo" alilisitiza Makuatian.


Makutian ameongeza kuwa sababu zilizopelekea kuboresha mfumo huo ni kuendana na mabadiliko ya kukua kwa teknolojia ya habari na mawasiliano sambamba na kuzingatia mapendekezo ya Wadau wa utalii ambao ndio watumiaji wakuu wa mfumo huo.

Mafunzo hayo yameshirikisha makundi mbalimbali katika mnyororo wa sekta ya utalii ikiwemo Waongoza watalii, wamiliki wa kampuni za utalii, madereva wa utalii, wamiliki wa hoteli na wadau wengine wanaohusika na sekta ya Utalii.

Wadau wa utalii walioshiriki mafunzo hayo wametoa pongezi kwa uongozi wa NCAA kwa maboresho ya mfumo huo ambao umerahisisha taratibu za malipo bila kutumia mda mrefu wanapokuwa na shughuli za utalii na wageni ndani ya hifadhi ya Ngorongoro



DKT.BITEKO ATAJA MAENEO SITA YA VIPAUMBELE UTEKELEZAJI WA ILANI YA CCM 2020/2025

May 29, 2025 Add Comment


📌 CCM yajivunia kuimarisha upatikanaji wa huduma bora kwa jamii


📌 Rais Samia asema CCM kuzindua Ilani yake kesho


📌 CCM yazalisha ajira 800,000 kwa vijana 2020/2025


Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita aliyowasilisha ni ya mwisho katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020. 


Amesema hayo Mei 29, 2025 wakati akiwasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Mkutano Mkuu Maalum wa  CCM Taifa - 2025 jijini Dodoma kwa niaba ya Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa. 


Ametaja maeneo sita muhimu ya vipaumbele  katika utekelezaji wa Ilani hiyo ya CCM kuwa ni pamoja na kulinda  na kuimarisha misingi ya utu, usawa, haki na uongozi bora ili kudumisha amani, umoja na mshikamano wa Taifa.

Dkt. Biteko ameendelea kwa kusema kuwa eneo lingine ni kukuza  uchumi wa kisasa, fungamanishi, jumuishi na shindani  uliojengwa katika msingi wa viwanda, huduma za kiuchumi na miundombinu wezeshi.


Aidha, kipaumbele kingine “ Kuleta mageuzi ya kilimo, mifugo na uvuvi ili kuwa na uhakika wa chakula na kujitegemea kwa chakula wakati wote na kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya uchumi na kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za afya, elimu, maji, umeme na makazi vijijini na mijini na kutengeneza ajira zisizopongua milioni nane katika sekta rasmi na isiyo rasmi kwa ajili ya vijana,”  ameongeza Dkt. Biteko.

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amesema kuwa kumekuwepo na mafanikio makubwa ikiwemo nchi kuendelea kuwa na amani, umoja na mshikamano pamoja na kuendelea kuenzi Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar na kudumisha Muungano wa Tanzania.


“ Vilevile, Serikali imeendelea kuimarisha demokrasia, utawala bora na haki za binadamu kwa kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuondoa zuio la mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa na hivyo kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari ili kuwezesha wananchi kupata habari kwa wakati,” amesema Dkt. Biteko.

Ameendelea kusema  kuwa mafanikio hayo  yamechagizwa na falsafa aliyoianzisha Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya 4R ambayo ni Maridhiano, Ustahimilivu, Mabadiliko na Kujenga Upya.


Amesisitiza “ Falsafa  hiyo imekuwa dira na nguzo muhimu ya kisera katika kuijenga upya Tanzania yenye mshikamano, haki na maendeleo endelevu kwa misingi ya demokrasia na ushirikishwaji wa wananchi katika masuala ya msingi ya Taifa.”



Kupitia mkutano huo Dkt. Biteko alielezea mafanikio ya Rais Samia kitaifa na kimataifa hususan katika sekta ya nishati kwa kuwa kinara wa nishati safi ya kupikia barani Afrika.


Akihutubia katika mkutano huo, Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kuwa Mkutano Mkuu huo ni sehemu muhimu ya maandalizi ya kushiriki Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.


“ Kesho  tutafanya uzinduzi wa Ilani tutakayoinadi kwa wananchi ili kutupa nafasi nyingine ya kuongoza kwa miaka mitano,” amesema Dkt. Samia.


Amebainisha  kuwa Ilani hiyo imehusisha vipaumbele  vya Chama na kuwa kabla ya kuiwasilisha  kwa wajumbe wameona ni muhimu kupitia utekelezaji wa Ilani ya mwaka 2020 hadi 2025.


Akizungumza katika mkutano huo, Katibu Mkuu wa CCM, Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi amesema  lengo la  mkutano huo ni kupokea taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa mwaka  2020 hadi 2025, kuzindua Ilani mpya 2025 hadi 2030 na kupitia maboresho machache ya Katiba ya CCM.


Aidha, Mkutano huo ulioongozwa  na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan umehudhuriwa na viongozi wa vyama vya siasa nchini, mabalozi wanaowakilisha nchi zao Tanzania pamoja wawakilishi wa vyama rafiki kutoka nchi mbalimbali za Afrika, China na Korea ya Kaskazini na Urusi.

 

MWISHO