OFISI YA WAKILI MKUU WA SERIKALI KUENDESHA MAFUNZO MAALUM KWA MAWAKILI WA SERIKALI

May 28, 2025 Add Comment
NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

OFISI ya Wakili Mkuu wa Serikali inatarajia kuendesha mafunzo kwa Mawakili wa Serikali kutoka Tanzania Bara na Visiwani Zanzibar ambapo mafunzo hayo yatafanyika Juni 2 hadi Juni 4, 2025 katika ukumbi wa mikutano wa AICC mkoani Arusha.

WAZIRI DKT.GWAJIMA AINISHA VIPAUMBELE VITANO WIZARA YA MAENDELEO YA JAMII 2025/2026

May 28, 2025 Add Comment


Na WMJJWM, Dodoma 


Waziri wa Maendeleo ya Jamii. Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima ameainisha vipaumbele vya Wizara vikubwa vitano katika utekelezaji wa Bajeti kwa mwaka wa fedha 2025/2026.


Mhe. Dkt. Gwajima ameainisha hayo wakati akiwasilisha Bajeti ya  Wizara hiyo kwa Mwaka husika wa Fedha leo Mei 27, 2025 Bungeni jijini Dodoma.


Ameeleza kuwa Wizara kupitia Idara na Taasisi zilizo chini yake zitatekeleza vipaumbele hivyo  ambavyo ni kukuza ari ya Jamii kushiriki katika kupanga na kutekeleza miradi ya maendeleo kwa ngazi ya msingi, kuratibu na kuimarisha utoaji wa huduma za ustawi wa maendeleo ya jamii, kutambua pamoja na kuratibu maendeleo ya ustawi kwa Makundi Maalum.

Mhe. Dkt. Gwajima ameongeza kuwa vipaumbele vingine ni pamoja kuboresha mazingira ya kufundisha na kujifunzia katika Taasisi na Vyuo vya Ustawi na Maendeleo ya Jamii na kuimarisha mazingira ya ushiriki na mchango wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika Maendeleo ya Taifa.


Amesema Wizara imeendelea kuratibu utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Kuhamasisha na Kusimamia Maendeleo katika Ngazi ya Msingi (2022/23 – 2025/26) ambao unalenga kuwawezesha wananchi kuwa kitovu cha maendeleo na kuchochea mageuzi ya kifikra, mtazamo na kiutendaji kwa timu ya wataalam ngazi ya msingi ili kuboresha utendaji na utoaji wa huduma kwa wananchi.


Katika kuhakikisha Watoto wanalindwa na ukatili Waziri Dkt. Gwajima amesema Wizara imeratibu na kusimamia Kampeni ya Taifa ya Usalama wa Mtoto Mtandaoni (Child Online Protection - COP) katika Mikoa 26 ya Tanzania Bara. Kampeni ilikuwa na lengo la kuelimisha Wazazi au Walezi na Watoto wenyewe kuhusu Usalama wa Mtoto anapokuwa anatumia mitandao.


Aidha Mhe. Dkt. Gwajima amefafanua kuwa Wafanyabiashara ndogondogo 601 (Me 274; Ke 327) wamekopeshwa mikopo yenye thamani ya Shilingi Bilioni 1,101,650,000 na zoezi hilo linaendelea. Vilevile maombi 2,092 yanaendelea kuchakatwa yenye thamani ya Shilingi Bilioni 3,590,477,000.


"Wizara kwa kushirikiana na OR - TAMISEMI imeendelea kuratibu na kufuatilia maendeleo ya ya Ujenzi wa Ofisi za wafanyabiashara ndogondogo katika ngazi ya mikoa ambapo hadi kufikia Aprili 2025 mikoa 17 kati ya mikoa 26 imekamilisha ujenzi wa Ofisi hizo" ameeleza Mhe. Dkt Gwajima. 


Akichangia hoja, Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Dkt. Thea Ntara amesizitiza Serikali kuchukua hatua na kusimamia maadili nchini, kutokana na kuwepo kwa matukio mengi ya uvunjifu wa maadili.


Naye Mbunge wa kuteuliwa Dkt. Shukurani Manya ameshauri  kuongezeka kwa juhudi za kuelimisha Jamii kuhusu elimu ya malezi ili kuepusha kutelekezwa kwa watoto ili waweze kupata malezi ya baba na mama.


MWISHO

WAZIRI MKENDA AVALIA NJUGA SAKATA LA MADEREVA KWENDA QATAR

May 28, 2025 Add Comment
Watu wanaowapeleka madereva kufanya kazi nje ya nchi wanawajibu wa kufanya utafiti kujua mahitaji ya eneo wanaloenda ni yapi tofauti na mahitaji ya magari ya Tanzania.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe Profesa Adolf Mkenda amesema hayo jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya Wizara hiyo katika miaka minne ya serikali ya awamu ya sita.

Waziri Mkenda amesema wahitaji hao wa madereva wanatakiwa kujua aina ya magari yaliyopo Tanzania ni ya namna gani, yanayoenda Kongo ni ya namna gani, madereva wa Tanzania wanajifunza nini, hivyo mtu akiwachukua watu nchini na kuwapeleka Qatar ni vizuri kwanza akaangalie, asiwachukue na kuwakimbiza kule halafu wakaenda kupimwa hilo ni jambo la muhimu kulifanya.

“Lakini pia tuna haja ya kuwafundisha magari yote hata yale ambayo hayajaingia nchini lakini sisi tulishatoa maelekezo miaka miwili iliyopita kwamba Chuo cha Ufundi Arusha kiingie makubalianao na makampuni ya magari na tayari wameanza mazungumzo na wengine wanaingia mkataba lakini pia tulishawaambia VETA kufanya jambo hilo” Amekaririwa Prof Mkenda

Hata hivyo amesema hata kwenye magari wanahitaji siyo fundi Mechanical pekee bali wanahitaji fundi ambaye anajihusisha na shughuli zote za mfumo wa magari ya kisasa (Mechatronics).






KAFULILA ATETEA REKODI YA RAIS DKT.SAMIA SULUHU KATIKA UBIA WA SEKTA BINAFSI NA UMMA

May 27, 2025 Add Comment


Na Ashrack Miraji Tanga Raha 


Dar es Salaam, Mei 27, 2025 — Kongamano muhimu kuhusu Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi limefanyika leo katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, likikutanisha wadau mbalimbali wa maendeleo, viongozi wa serikali, sekta binafsi na wasomi mashuhuri. Kongamano hili limeandaliwa kwa ushirikiano kati ya PPPC na REDET kwa lengo la kuimarisha mjadala kuhusu mchango wa ubia katika maendeleo ya taifa.


Miongoni mwa wageni waalikwa walioshiriki ni pamoja na Prof. Rwekaza Mukandala, Prof. Abel Kinyondo na Prof. Anna Tibaijuka, ambao waliwasilisha mada mbalimbali zinazohusu mchango wa sera, tafiti na uzoefu wa nchi nyingine katika kukuza ubia wenye tija. Washiriki walijadili umuhimu wa kuweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa.

Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPC), David Kafulila, alitumia jukwaa hilo kutetea kwa nguvu rekodi ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kukuza ushirikiano wa sekta hizi mbili. Alisema kuwa tangu kuingia madarakani kwa Rais Samia, kumekuwa na mageuzi makubwa yanayolenga kuwezesha sekta binafsi kushiriki katika miradi ya kimkakati ya maendeleo.

David Kafulila alifafanua kuwa serikali haitegemei tena kodi na mikopo pekee kugharamia maendeleo, bali sasa inachochea ubia na sekta binafsi kama chanzo mbadala cha mitaji. Alieleza kuwa hadi kufikia Machi 2025, Tanzania ilikuwa na miradi 83 ya ubia yenye thamani ya zaidi ya Sh trilioni 30, hatua inayodhihirisha dhamira ya serikali katika kuchochea uchumi shirikishi.

Akigusia deni la taifa, Kafulila alisema kuwa ni himilivu na linatumika kwa uwekezaji wa maendeleo. “Deni la taifa la Sh trilioni 97 si tatizo ikiwa linachochea maendeleo. Tunapaswa kuelekeza nguvu katika usimamizi bora wa mikataba ya PPP badala ya kuogopa ubia,” alisisitiza.


Aidha, mchango wa sekta binafsi hauishii kwenye uwekezaji tu bali una nafasi kubwa katika kuongeza ajira kwa Watanzania na kukuza ujuzi wa kitaalamu. Kwa mujibu wa takwimu, zaidi ya asilimia 70 ya ajira nchini hutolewa na sekta binafsi, jambo linalosaidia kupunguza ukosefu wa ajira na kukuza kipato cha wananchi. Kupitia ajira hizi, wananchi huweza kuchangia zaidi kwenye mzunguko wa uchumi kwa njia ya matumizi, kodi na uwekezaji wa ndani.

Vilevile, sekta binafsi huchochea ubunifu na ushindani wa kibiashara, jambo linalosaidia kuboresha ubora wa bidhaa na huduma. Ushindani huu huongeza tija na kuwafanya wawekezaji kuboresha miundombinu, kuongeza matumizi ya teknolojia na kutoa mafunzo kwa wafanyakazi. Mchango huu unaiwezesha serikali kuelekeza rasilimali zaidi kwenye huduma za kijamii huku pato la taifa likiendelea kukua.


Kwa upande wake, Prof. Abel Kinyondo alitoa tahadhari kuhusu changamoto za usimamizi na ukosefu wa uelewa wa kina kuhusu PPP, akiitaka serikali kuweka mfumo madhubuti wa kuwajengea uwezo watendaji wa umma. Naye Prof. Tibaijuka aliitaka serikali kushirikisha wananchi kwa uwazi zaidi ili kuongeza uaminifu wa umma katika miradi ya ubia.

Kongamano hilo lilihitimishwa kwa mapendekezo ya kuimarisha ushirikiano wa sekta hizi mbili kupitia maboresho ya sera, uwazi katika mikataba na ushirikiano wa karibu na taasisi za elimu na utafiti. Washiriki walisisitiza kuwa ubia wa sekta binafsi na umma ni nyenzo muhimu ya kuifikisha Tanzania katika maendeleo jumuishi na endelevu ifikapo mwaka 2050.

DKT.BITEKO AKUTANA NA MTENDAJI MKUU WA PUMA DUNIANI

May 27, 2025 Add Comment


📌 Tanzania na PUMA kuimarisha ushirikiano


📌 PUMA kuendelea kuwekeza zaidi Tanzania


Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amekutana na kufanya mazungumzo na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Nishati ya PUMA Energies, Duniani Bw. Mark Russell.


Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Mei 27, 2025 jijini Dodoma, Dkt. Biteko ameipongeza Kampuni ya PUMA Energies kwa kuwekeza nchini na kutoa huduma ya viwango vya juu katika bidhaa zake pamoja na kuzingatia wazawa katika nafasi za juu za utendaji za Kampuni hiyo nchini. 


Vilevile, ametoa rai kwa PUMA Energies kuendelea kuwekeza zaidi nchini na kusema kuwa Kampuni hiyo inaweza kujenga vituo zaidi vya kuweka gesi kwenye magari ili kusaidia upatikanaji wa huduma kwa wananchi. 

Kuhusu nishati safi ya kupikia, Dkt. Biteko ametoa wito kwa Kampuni ya PUMA kuwekeza katika eneo hilo na kusema kuwa Serikali itaendelea kuimarisha ushirikiano wake kwa Kampuni hiyo.

Naye, Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Nishati ya PUMA Energies, Bw. Mark Russell amesema kuwa Kampuni yake imewekeza zaidi ya dola za kimarekani milioni 24 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vitatu vya kujaza gesi kwenye magari katika mikoa ya Dar es salaam na kimoja Dodoma.


MWISHO.