MBEKI AWAASA VIONGOZI WA AFRIKA KUWA WAZALENDO KATIKA KULINDA MASLAHI YA BARA LAO

May 24, 2025 Add Comment

 Rais Mstaafu wa Afrika Kusini, Mheshimiwa Thabo Mbeki, amewahimiza viongozi wa Bara la Afrika kuwa wakweli na waaminifu katika kulinda maslahi ya bara lao, ili kufanikisha malengo ya kukuza uchumi na kuboresha maisha ya Waafrika.


Mheshimiwa Mbeki ameyasema hayo katika hafla ya chakula cha jioni iliyofanyika tarehe 23 Mei, 2025 jijini Dar es Salaam .

Mheshimiwa Mbeki amesisitiza kuwa maendeleo ya Bara la Afrika yatapatikana endapo viongozi wataweka mbele maslahi ya nchi zao na kuongoza kwa uadilifu, uwazi, na dhamira ya dhati ya kuleta mabadiliko chanya kwa Waafrika wote.

“Tunapoadhimisha Siku ya Afrika mwaka huu kwa kaulimbiu ‘Haki kwa Waafrika na Watu wa Asili ya Kiafrika Kupitia Fidia: Kuangazia Historia Yetu, na Kuunda Mustakabali Wetu,’ tunakumbushwa kuwa haki siyo mwisho, bali ni dai endelevu la ukweli, heshima, na uongozi unaoakisi hali halisi za watu wetu. Tuwekeze katika elimu, ubunifu, ushirikishaji wa vijana katika maamuzi, na kupambana na ufisadi unaoharibu maendeleo,” alifafanua Mheshimiwa Mbeki.

Ameongeza kuwa Bara la Afrika lina utajiri na uwezo mkubwa ambao unahitaji Viongozi wanaowaza zaidi ya uchaguzi, wasioogopa uwajibikaji, wenye maono, na wanaotanguliza maslahi ya wananchi wao na Taifa, kuliko matakwa yao binafsi.

Awali Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo alisema kila mwafrika lazima atakafari mafanikio, changamoto na matarajio ya kuinua maendeleo ya Afrika kwa amani ya utulivu.

Amesisitiza umuhimu wa kuwaenzi viongozi walioendeleza fikra za Uafrika na wanaoendelea kupigania ukombozi wa kiuchumi na mshikamano wa Bara la Afrika kwani wameacha urithi mkubwa kwa kizazi cha sasa na kizazi kijacho.

“Kwa niaba ya Serikali na Wananchi wa Tanzania, nichukue nafasi hii kusema kuwa tunawakumbuka na kuwapongeza waanzilishi wa Umoja wa Afrika (OAU) — ambao ndoto yao ya kuunganisha na kushirikisha zaidi mataifa ya Afrika imeendelea kuishi hadi leo. Tunawakumbuka pia kwa heshima kubwa viongozi waliowafuata, ambao waliendeleza dhima ya Uafrika (Pan-Africanism) na wanaoendelea kupigania ukombozi wa kiuchumi na mshikamano wa bara letu tukufu,” alisema Mhe. Kombo

Hafla hiyo iliwakutanisha pamoja mabalozi , viongozi wa Serikali, Mabalozi wastaafu, viongozi wa serikali, wanadiplomasia, wasomi, pamoja na wawakilishi wa asasi za kiraia na kijamii kwa ajili ya kusherehekea mshikamano, utofauti na maendeleo ya Afrika.

Usiku huo ulipambwa na burudani mbalimbali za kitamaduni, vyakula kutoka nchi za Afrika, pamoja na tafakuri juu ya mchango wa mataifa ya Afrika katika historia na maendeleo ya sasa kuelekea amani na kujitegemea.

Hafla hiyo ilifanyika sambamba na maadhimisho ya miaka 62 ya Umoja wa Afrika, ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za kuelekea maadhimisho ya Siku ya Afrika ambayo huadhimishwa tarehe 25 Mei ya kila mwaka.
.







RAIS DKT. SAMIA ATOA BILIONI 42.34 KULIPA FIDIA KWA WANANCHI WA MKOA WA ARUSHA

RAIS DKT. SAMIA ATOA BILIONI 42.34 KULIPA FIDIA KWA WANANCHI WA MKOA WA ARUSHA

May 24, 2025 Add Comment








Na Prisca Libaga RAS Arusha

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Paul Christian Makonda, amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa kiasi cha shilingi bilioni 42.34 kwa ajili ya kulipa fidia kwa wananchi wa Mkoa wa Arusha ili kumaliza migogoro ya ardhi na uendelezaji wa maeneo mbalimbali katika mkoa huo.

Akizungumza na wananchi wa Kata ya Moshono, Jijini Arusha, Mhe. Makonda amesema fidia hiyo imetolewa kwa maeneo kadhaa yaliyoguswa na miradi ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa barabara, uwanja wa ndege, maeneo ya jeshi, na uchimbaji wa madini.

Katika Jiji la Arusha, eneo la Losirwa lililokuwa chini ya matumizi ya Jeshi limepewa fidia ya shilingi Bilioni 2.27, ambapo fidia hiyo imekwishalipwa, eneo la Oloresho kwaajili ya maandalizi ya mashindano ya AFCON, limetengewa fidia ya shilingi bilioni 7.27, barabara ya Mianzini – Ngaramtoni nayo imelipwa fidia ya shilingi bilioni 3.49 ambapo fedha hizo zimelipwa tayari pamoja na eneo la barabara ya Mirongoine – Olmot limepokea fidia ya shilingi milioni 591.64 ambayo nayo imelipwa.

Aidha, Wilaya ya Arumeru, fidia kwa eneo la Jeshi lililopo Duluti imetolewa kwa kiasi cha shilingi bilioni 7.9 na tayari imelipwa yote kwa walengwa.

Wilaya ya Karatu imepata fidia ya shilingi bilioni 5.9 kwa ajili ya uwanja wa ndege wa Manyara uliopo katika eneo hilo, hatua inayolenga kufanikisha uboreshaji wa miundombinu ya usafiri wa anga.

Kwa upande wa Wilaya ya Monduli, eneo la Engaruka, ambalo linahusishwa na shughuli za uchimbaji wa madini ya magadi soda, limetengewa fidia ya shilingi bilioni 14.9, ikiwa ni sehemu ya uwekezaji wa kimkakati katika sekta ya madini.

Katika hatua nyingine, Mhe. Makonda amewataka viongozi wote wa Mkoa huo kuacha mara moja tabia ya kuwaondoa wananchi kwenye maeneo yao bila kuwapa fidia stahiki, akisisitiza kuwa serikali ya awamu ya sita inalenga haki, usawa na maendeleo ya watu na ndiyo dhamira ya Rais Dkt. Samia katika kulinda haki za wananchi na kusukuma mbele ajenda ya maendeleo ya Taifa.

RAIS DKT.SAMIA AWAAPISHA VIONGOZI ALIOWATEUA HIVI KARIBUNI IKULU JIJINI DAR LEO

May 24, 2025 Add Comment

 


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akimuapisha Prof. Tumaini Joseph Nagu kuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia masuala ya Afya kwenye hafla fupi iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 24 Mei, 2025.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akimuapisha Dkt. Blandina Bugazi Kilama kuwa Naibu Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango anayeshughulikia biashara na ubunifu kwenye hafla fupi iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 24 Mei, 2025.


Viongozi wateule wakiapa Kiapo cha Maadili kwenye hafla ya uapisho iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 24 Mei, 2025.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akimuapisha Jaji Mstaafu John Samweli Mgetta kuwa Mjumbe wa Baraza la Maadili kwenye hafla fupi iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 24 Mei, 2025.

RC BALOZI BATILDA :TAKWIMU NI NGUZO MUHIMU KATIKA MAENDELEO YA NCHI

May 24, 2025 Add Comment

 



Na Oscar Assenga,TANGA

MKUU wa Mkoa wa Tanga Balozi,Dkt Batilda Burian amesema kwamba takwimu ni nguzo na nyenzo muhimu katika kupanda utekelezaji wa mipango mbalimbali maendeleo duniani.

Dkt Batilda aliyasema hayo leo Jijini Tanga wakati akifungua mkutano wa kwanza wa Baraza la Saba la Wafanyakazi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu nchini (NBS) ambapo alisema kwamba mabazara hayo yana maada mkubwa kwa wafanyakazi.

Ambapo alisema kwamba Serikali inatambua jukumu hilo kubwa la (NBS) kuzalisha na kusambaza pamoja na kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa takwimu rasmi kwa ajili ya kupanda utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo katika nchi.

Alisema kutokana na hilo wanamshukuru Rais Dkt Samia Suluhu kwa utashi wake mkubwa wa kisiasa alionao katika kuendeleza Tasnia ya Takwimu nchini na wote wameona mafanikio yake .

“Wote tunaona kwa namna ya kipekee  Serikali ya awamu ya sita  imekuwa mstari wa mbele kuwezesha uzalishaji wa takwimu rasmi pamoja na matumizi ya takwimu katika mipango mbalimbali ya maendeleo na Dira bila takwimu hakuna kinachoendelea”Alisema

Hata hivyo aliipongeza timu ya  Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa  umoja na mshikamano kutokana na takwimu huanzia katika uzalishaji,uchakataji wake,uhakiki wake mpaka usambazaji wake kutokana na kwamba  mtu moja hawezi kufanya pekee yake hivyo lazima wafanye kazi kwa ushirikiano.

Alisema kwamba wanaendelea kuhamasisha wenzao wajiunge kwebye vyama vya wafan yakazi hasa tughe ili waweze na kauli kubwa ambavyo itakuwa na maslahi mapana kwa nchi na sisi wenyewe.

Aidha aliwataka kuhakikisha wanafanya kazi kwa tija na uzalendo na kuongea nao waelewe dira na dhima ya taasisi zao na mambo ambayo hawataji kuyaona kwenye taasisi zao ikiwemo uvujaji wa siri.

“Katika mambo ambayo tunawapongeza sana NBS ni usiri mkubwa mlionao kwa kweli mnafanya kazi kubwa na sasa wanakwenda kwenye teknolojia ya habari tunaweza kuwa na usiri lakini mkaingiliwa kuna viti ya kimtandao inabidi tuendelee kujiimarisha sana kwa maana nyie ndio wamebeba roho ya nchi”Alisema

Mkuu huyo wa Mkoa alisema kwa sababu taarifa zote zipo kwao kwa hiyo wajipange na moja ya maeneo ambayo watapaleka watu wengi kusoma ni masuala ya ulinzi wa kimtandao ili kuungana na kikosi kazi cha Serikali  ili kuhakikisha kwamba taarifa zinakuwa salama na hakuna jambo ambalo litaingizwa.

Awali akizungumza Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi (NBS) na Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dkt Amina Msengwa alimshukru Rais Dkt Samia Suluhu kwa kumteua kuwa Mtakwimu Mkuu wa Serikali anatambua heshima kubwa aliyopewa na kuhaidi kuendelea kusimamia ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa maelekezo na waledi mkubwa ili kuhakikisha majukumu ya NBS yanakwenda sambamba na kasi ya maendeleo ya Rais.

“Nimshukuru Kamisaa Anna Makinda kwa kuendelea kutusaidia katika ushauri lakini kusimamia mkakati wetu wa usambazaji wa matokeo ya Sensa na tunaendelea kujivunia kutoka kwake”Alisema

Aidha alisema kwamba kupitia ofisi ya Taifa ya Takwimu wanataka kuijenga Tanzania yenye maendeleo ya juu kabisa huku akieleza kwamba wamekuwa wakitekeleza sheria na kanuni za zinazoongoza uundaaji na uendeshaji  na u vikao vya mabaraza la wafanyakazi .

Naye kwa upande wake Kamisa wa Sensa na Spika wa Bunge Mstaafu Anna Makinda alisema  baraza la wafanyakazi ndio roho muhimu ambayo inaunganisha wafanyakazi na menejimenti ambapo alitumia wasaa huo kuwataka watumishi kujiunga kwenye mabaraza hayo kutokana na uwepo wa manufaa mbalimbali.

Mwisho

WANAJAMII TUJIPANGE KUEPUSHA MIGOGORO - DKT.BITEKO

May 23, 2025 Add Comment


📌 Dkt. Biteko azindua kitabu cha miaka 35 ya TAWLA


📌 Rais Samia aipongeza TAWLA kushiriki kampeni za kisheria


📌 TAWLA yaipongeza Serikali miradi ya kimkakati 


Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewataka wanajamii kujiepusha na mazingira yanayoweza kusababisha migogoro baada ya wao kufariki

Dkt. Biteko amesema hayo Mei 23, 2025 Jijini Dar es Salaam alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kufungua Kongamano na Mkutano Mkuu wa mwaka wa Chama cha Wanasheria Wanawake nchini - TAWLA

Amesema endapo wanajamii watajiandaa na kuweka mazingira mazuri, wataepusha migogoro isiyo ya lazima na jamii itaishi kwa amani na kupunguza gharama zinazotumika kurekebisha jamii yenye migogoro

Aidha, ameipongeza TAWLA kwa kazi nzuri iliyodumu kwa miaka 35 tangu kuazishwa kwake mwaka 1990


“ Tangu mlipoanzishwa kuna vyama vingi vya kijamii vilianzishwa sambamba na chama chenu, lakini vingine vilikufa baada ya mwaka mmoja, vingine vilikufa baada ya miaka mitano na vingine vilisambaratika baada ya miaka 10. Ninyi mmeimarika na kukua hadi leo na mnaendelea kufanya kazi nzuri,” ameoongeza Dkt. Biteko

Pia amewasilisha pongezi za Rais Samia kwa TAWLA kupitia kushiriki kampeni ya msaada wa kisheria ya Samia Legal Aid na kusisitiza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana nao kuhakikisha jamii inaishi kwa amani na upendo kama ilivyo ndoto ya TAWLA ya kuwasaidia watu wenye uhitaji.

“Bila mchango wenu, mafanikio yanayozungumzwa serikalini huenda yasingekuwa yanazungumzwa kwa kiwango hicho, amesema Dkt. Biteko


Ameutaka uongozi wa TAWLA kuendelea kuwashawishi na kuwavutia wanachama wapya watakaoweza kutoa msaada bila kusita katika jamii yao.

Amesema Serikali imechukua hatua mbalimbali za kuhakikisha wanawake wanakuwa katika nafasi mbalimbali za maamuzi ikiwemo kuongeza uwiano wa majaji wanawake na wanaume katika mahakama za rafani na mahakama Kuu Akizungumzia Uchaguzi Mkuu ujao, Dkt. Biteko amewahimiza wajumbe wenye nia kujitokeza na kugombea uongozi ili kuwakilisha wananchi hususan wanawake wanaongezeka

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila ameipongeza TAWLA kwa kazi ya kutetea kundi maalum la wanawake na kuliwezesha kupata msaada wa kisheria

“TAWLA inafanya kazi kubwa ya kufanyia kazi tabia za watu na kazi hiyo inahitaji mawanda mapana” amesema na kuongeza kuwa wadau wa sheria wanashughulia watu wenye malezi na makuzi tofauti hivyo, kazi yao ni kubwa inayohitaji kufanyika kwa weledi wa hali ya juu


Mwenyekiti wa TAWLA Wakili Suzan Ndomba ameipongeza Serikali kwa hatua zake za kulinda haki na kushughulikia changamoto za zinazowakabili wanawake na watoto nchini

Amesema hatua ya Serikali kuwekeza katika utekelezaji wa miradi ya nishati, maji na elimu ni fursa zaidi kwa kundi la wanawake wa Tanzania ambao wamekuwa waathirika wakubwa madhara yanayotokana na ukosefu wa miundombinu hiyo

Amefafanua kuwa tangu kuanzishwa kwa TAWLA, chama hicho kimeshiriki kutoa mafunzo kwa baadhi ya mawakili, kuanzisha huduma ya simu ya bure kwa ajili ya wateja wake kurupoti vitendo na matukio ya ukatili, kuwatetea wateja wake mahakamani, kushiriki katika kuandaliwa na kutungwa kwa sheria ya mtoto ya mwaka 2009 pamoja na kutungwa kwa kifungu maalum cha makosa ya kujamiiana SOSPA (2008)


TAWLA ilianzishwa mwaka 1990 ikiwa na wanachama 40 na idadi yao imeongezeka hadi 420 miaka 35 baadaye.


MWISHO