SERIKALI IMETOA RUZUKU YA ASILIMIA 20 HADI 50 KWENYE MITUNGI YA GESI LAKU 4.4 MH KAPINGA

May 23, 2025 Add Comment


📌 *Asema lengo ni kupunguza gharama na kuhamasisha Nishati Safi ya Kupikia*


*📌  REA kusambaza majiko banifu 200,000 kwa punguzo la hadi asilimia 75*


📌 *Baada ya umeme kufika kwenye vijiji vyote; Serikali kuendelea kuhamasisha matumizi ya majiko ya umeme*



Naibu Waziri wa Nishati, Mhe Judith Kapinga amesema Serikali imetoa ruzuku ya asilimia 20 hadi 50 kwenye mitungi ya gesi ya LPG takribani 452,445 kwa watumiaji wa mwisho ikiwa ni jjtihada za kuhamasisha matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia.


Mhe. Kapinga ameyasema hayo leo Mei 23, 2025 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Grace Tendega aliyetaka kufahamu Serikali ina mkakati gani wa muda mfupi wa kuhakikisha Wananchi wa Vijijini wanatumia Nishati Safi ya kupikia badala ya Kuni na Mkaa.

 

"Mheshimiwa Mwenyekiti Serikali kupitia REA pia  itasambaza majiko banifu 200,000 yenye bei ya punguzo la hadi asilimia 75 pamoja na kuwezesha ufungaji wa mifumo ya nishati safi ya kupikia katika Taasisi za Umma zinazohudumia watu zaidi ya 100."  Amesema  Kapinga

Aidha, amesema Serikali imekamilisha kazi ya usambazaji umeme katika vijiji vyote hivyo kwa sasa inaendelea kuhimiza matumizi ya majiko ya kupikia yanayotumia umeme ikiwa ni njia mojawapo ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa wananchi wa vijijini badala ya kutumia kuni na mkaa.


Mhe. Kapinga ametanabaisha  kuwa, Mkakati wa Taifa wa  Nishati Safi ya Kupikia ni wa miaka kumi lakini Serikali inao mkakati wa matumizi bora ya nishati ambao unahusisha pia sekta binafsi kwa ajili ya kusaidia kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.


Akijibu swali la Mbunge wa Mbulu, Mhe. Zacharia Isaay aliyeuliza Serikali imejipangaje kuhakikisha Vitongoji vyote vilivyokusudiwa katika mwaka huu wa bajeti kufikiwa  na umeme katika kipindi cha mwezi mmoja uliobaki, Mhe. Kapinga amesema Serikali inayo mikakati na miradi mbalimbali ya kupeleka umeme katika Vitongoji. 


Amesema kuwa, moja ya mikakati hiyo ni kupeleka umeme katika Vitongoji 15 kwa kila Jimbo, na pia  Serikali imekuja na mkakati wa kupeleka umeme katika Vitongoji 20,000 ambapo   awamu ya kwanza inaanza kupeleka umeme katika Vitongoji 9000 na hatua iliyopo ni utafutajj wa wakandarasi.


Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Anatropia Theonest aliyeuliza bei ya Serikali ya ruzuku imeanza kutumika lini kutokana na mitungi ya gesi kuendelea kuuzwa kati ya 22,000/- na 25,000 na kwa mitungi mikubwa ya kilo 15 shilingi 50,000/- na 60,000/-,  Mhe. Kapinga ameeleza kuwa kwa maeneo ya mjini Serikali imepeleka ruzuku hadi asilimia 25 na maeneo ya Vijijini ni kati ya asilimia 50 hadi 75 na kutolea mfano iwapo mtungi ulikuwa unauzwa shilingi 45,000/- kwa bei ya ruzuku inapatikana kwa shilingi 17,000/- hadi 21,000/- na kusema ni zaidi ya nusu ya bei yake.


Ameongeza kuwa, katika kila Wilaya kuna takribani mitungi 3,255 inayopatikana kwa ruzuku na kuongeza kuwa ndio kwanza mkakati umeanza.


Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Yustina Rahhi alieuliza mpango wa Serikali kuwapelekea jamii ya wafugaji teknolojia ya biogas au kuwajengea majiko yanayotumia samadi ya gesi ambayo ni rahisi, Mhe. Kapinga amesema Serikali inatekeleza mradi huo kupitia umoja wa Ulaya (mfuko wa UNCDF) ambao unateknolojia alizozitaja Mhe. Mbunge.


Akijibu swali la Mbunge wa Nyang’wale, Mhe. Hussein Amar aliyeuliza kuhusu mpango wa Serikali kuzipelekea nishati safi ya kupikia  Shule za Sekondari 19 na Sekondari 12 za bweni zilizo Wilaya ya Nyang’wale ili kulinda mazingira,  Mhe. Kapinga amesema Wizara ya Nishati inaompango wa kuzipelekea nishati safi ya kupikia Taasisi za umma kwa kushirikiana na TAMISEMI.


Katika hatua nyingine Mhe. Kapinga amezishauri Halmashauri  kufunga mifumo ya nishati safi ya kupikia  katika Taasisi zilizopo katika Halmashauri wanazoziongoza kwa kutumia mapato ya ndani.

DKT .TULIA ATANGAZA KUGOMBEA JIMBO LA UYOLE

May 23, 2025 Add Comment


Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) na Mbunge wa Mbeya Mjini, Mhe. Dkt. Tulia Ackson, ametangaza nia ya kugombea Ubunge katika jimbo jipya la Uyole mkoani Mbeya katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwezi Oktoba mwaka huu.


Dkt. Tulia ametoa tamko hilo leo tarehe 23 Mei, 2025 alipokuwa akihutubia Mkutano Mkuu Maalum wa Wilaya ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambapo amesema kuwa ameamua kufanya uamuzi huo ili kuwahudumia wananchi wa Uyole kutokana na kasi ndogo ya maendeleo iliyopo katika eneo hilo.


“Maendeleo ya Uyole yanasonga kwa taratibu sana, nimeona ni vyema nijitoe kwa moyo wote kuhakikisha wananchi wa Uyole wanapata huduma stahiki na maendeleo ya haraka. Nitoe wito kwenu, watu wengi watakuja kwenu, chagueni kiongozi, chagueni mtumishi, itasaidia sana kuendelea kuyakimbiza maendeleo ya jamii," amesema Dkt. Tulia.

TBS YAWAKUMBUSHA WANANCHI UMUHIMU WA KUJIRIDHISHA NA TAARIFA ZA BIDHAA

May 22, 2025 Add Comment
Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limeendelea kutoa msisitizo kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kujiridhisha na taarifa zilizo kwenye vifungashio vya bidhaa kabla ya kununua, likisema taarifa hizo ni sehemu muhimu ya uthibitisho wa ubora na usalama wa bidhaa husika.

RAIS SAMIA APELEKA NEEMA TANGA

May 22, 2025 Add Comment


*📌Bilioni 20 kusambaza umeme katika vitongoji 180*


*📌Zaidi ya Kaya 5,940 kufikiwa*


*📌RC Tanga amshukuru Rais Samia, awasisitiza wananchi kuchangamkia fursa*


Wakala wa Nishati Vijijini (REA) unatekeleza mradi wa Shilingi Bilioni 20 wa kusambaza umeme katika vitongoji 180 utakaonufaisha zaidi ya Kaya 5,940 Mkoani Tanga.


Hayo yameelezwa na Meneja Usimamizi wa Miradi kutoka REA, Mhandisi Romanus Lwena akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy Mei 22, 2025  wakati wa kumtambulisha Mkandarasi aliyeshinda zabuni ya kutekeleza mradi, Kampuni ya Transpower Limited na International Contractor Limited Jv kwa Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Balozi Dkt. Batilda Burian.



“Leo hii tupo hapa Mkoani Tanga kwa ajili ya kumtambulisha mkandarasi ambaye atatekeleza mradi huu wenye thamani ya shilingi 20,581,548,011.20,” alibainisha Mha. Lwena.


Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Burian alimshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapelekea mradi huo ambao alisema unakwenda kuongeza kasi ya maendeleo kwa wananchi wake na alimsisitiza mkandarasi kuhakikisha anatoa ajira kwa wananchi wa maeneo ya mradi.

“Wananchi wa Tanga tujitokeze kwa wingi kuchangamkia fursa, mradi unaotekelezwa ni mkubwa hivyo mbali na manufaa tutakayopata baada ya kukamilika kwa mradi lakini pia kuna fursa nyingi wakati wote wa hatua zote za utekelezaji wake ikiwemo ajira na biashara mbalimbali,” alisisitiza Mhe Dkt. Burian.


Akizungumzia utekelezaji wa mradi, Mhandisi Lwena alisema mradi unatekelezwa katika majimbo 12 ya uchaguzi na kwamba kwa kila jimbo vitongoji 15 vitafikiwa na mradi.


Alitaja majimbo ambayo ni Jimbo la Tanga, Pangani, Mkinga, Muheza, Korogwe Mjini, Korogwe Vijijini, Lushoto, Bumbuli, Mlalo, Handeni Mjini, Handeni Vijijini na Kilindi.

Alitoa wito kwa wananchi kuchangamkia fursa ya kuunganishiwa umeme ambapo alibainisha kuwa gharama ya kuunganisha umeme kupitia mradi huo ni shilingi 27,000 pekee.


“Katika mradi huu, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa ruzuku ili kila mwananchi aweze kuunganisha umeme kwa gharama ya shilingi 27,000, tumuunge mkono kwa kuchangamkia fursa hii,” alisisitiza Mha. Lwena.


Kwa upande wake mwakilishi wa Mkandarasi kutoka Kampuni ya Transpower Ltd, Mha. Cuthbert Shirima alisema kampuni hiyo inao uzoefu wa muda mrefu na aliahidi kufanya kazi kwa weledi na kukamilisha mradi huo kwa kipindi cha miezi 18 badala ya 24 iliyoainishwa katika mkataba.

TANESCO MUHEZA: KATIKATIKA YA UMEME ILITOKANA NA WIZI WA NYAYA ZA KOPA KWENYE TRANSFOMA

May 22, 2025 Add Comment


Na Paskal Mbunga, MUHEZA.

SHIRIKA la Umeme nchini (TANESCO) katika wilaya ya Muheza Mkoani Tanga limetolea ufafanuzi katikakatika ya Umeme katika wiki mbili zilizopita ilitokana na kuibiwaa kwa wizi wa nyaya za kopa kwenye Transfoma 18 katika maeneo tofauti tofauti wilayani humo na hivyo kupelekea kuungua na kusababisha umeme kuzima.

Hayo yalisemwa na Meneja wa TANESCO wilaya ya Muheza African Chuwa wakati akizungumza na waandishi wa habari kutolea ufafanuzi suala hilo lililosababisha baadhi ya wananchi kulalamika, ambapo alisema jitahada zilifanywa ili kuurejesha umeme kwa haraka.

Alisema wakati wa zoezi la kurejesha umeme, walilazimika kufanya majaribio ili kutambua eneo lenye matatizo kwani wilaya hiyo pia inapeleka huduma ya umeme kwenye wilaya za Mkinga na Pangani.

Alibainisha kwamba kwa vile baadhi ya maeneo yanachukua umeme kutoka Muheza, na kwamba ili kubaini tatizo lipo upande upi, ilikuwa lazima kwanza kuurejesha umeme ili endapo itazima, watabaini changamoto ipo wapi. Alieleza kwamba wanaendelea kufuatilia vitendo vya wizi wa waya unaofanywa na baadhi ya watu uliosababisha b umeme kukatika mara kwa mara.

“Lakini niwaambie kwamba tatizo jingine linalosababisha umeme kukatikakatika ni matengenezo makubwa yanayofanyika pale kituo cha kuzalisha umeme Hale yanayopelekea kuzimwa kwa line inayokwenda Muheza na kusisitiza kwamba wanalazimika kuzima umeme wakati wa matengenezo wa line inayotoka Hale kwenda Songa na kwenda Muheza na line inayotoka Kituo cha Hale Songa kwenda Korogwe.

Hata hivyo alibainisha kwamba Ofisi ya TANESCO wilayani Muheza inatoa taarifa kwa wananchi ya uwepo wa matengenezo na kwamba wakati wa matengenezo hayo, umeme huzimwa. Meneja huyo wa TANESCO wilayani hapa alifahamisha kwamba kutakuwa na katikakatika kwa umeme wakati wa matengenezo yanayoendelea kwa kipindi cha miezi minne hadi mwezi Agosti, 2025 ambapo yatakuwa yamekamilika.



(Mwisho)