KAMATI MPYA YA UKAGUZI WIZARA YA NISHATI YAFANYA ZIARA KATIKA MIRADI YA UMEME MKOANI PWANI

May 20, 2025 Add Comment


📌 *Yapongeza Serikali utekelezaji miradi ya umeme*



Kamati mpya ya  Ukaguzi ya Wizara ya Nishati imefanya ziara  katika miradi ya umeme mkoani Pwani ili kujionea utekelezaji wa miradi hiyo hali itakayopelekea  Kamati husika  kumshauri vyema Katibu Mkuu Wizara ya Nishati  juu ya usimamizi wa rasilimali za Wizara ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa miradi.


Ziara hiyo imefanyika katika Mradi wa kuzalisha umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) na Kituo cha kupoza na kusambaza umeme cha Chalinze mkoani Pwani tarehe 19 na 20 Mei 2025

 Baada ya kujionea utekelezaji wa miradi hiyo ambayo imekamilika,  Mwenyekiti wa  Kamati,  Mhandisi Kenneth Nindie ameipongeza Serikali kwa kazi Kubwa inayofanya kwa maslahi mapana ya wananchi na Taifa kwa ujumla.


 Amebainisha kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita imewekeza fedha nyingi katika miradi ya umeme, hivyo Wizara ya Nishati wajibu wake ni kufanya usimamizi mzuri  wa miradi ili thamani ya fedha ionekane.

 Kamati hiyo pia  imewataka wakandarasi wanaopewa kazi ya kutekeleza  miradi kuwa wazalendo kwa kuzingatia viwango na ubora ili miradi inayofanyika  idumu kwa  muda mrefu na kuleta matokeo chanya kwa Watanzania.


"Tunaipongeza Serikali kwa kweli inafanya kazi kubwa ya kutekeleza miradi mikubwa katika nchi yetu kwa manufaa mapana ya wananchi, kikubwa tunawasihi wakandarasi kuwa  wazalendo katika kutekeleza majukumu yao, mikataba iliyowekwa izingatiwe kwa kutekeleza kazi kwa viwango na Ubora ili miradi hii iwe na tija kwa Taifa." Amesema Nindie


MHE. NYONGO AONGOZA UJUMBE WA TANZANIA NCHINI UBELIGIJI

May 20, 2025 Add Comment
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Stanslaus Nyongo amewasili nchini Ubeligiji kuongoza ujumbe wa Tanzania katika Kongamano la Bajeti la Umoja wa Ulaya linalofanyika mjini Brussels nchini Ubeligiji kuanzia tarehe 20 hadi 21 Mei, 2025.

Equity Group yapongezwa kwa kuwaleta pamoja wawekezaji

May 19, 2025 Add Comment

 

Dar es Salaam, 19 Mei 2025 – Equity Group, chini ya Mpango wa Afrika wa Urejeshaji na Uhimilivu (ARRP), inaongoza msafara wa kimataifa wa biashara na uwekezaji katika Afrika Mashariki, ukiaanzia nchini Tanzania (Dar es Salaam na Zanzibar) na kuendelea Uganda (Kampala). Msafara huu unalenga kuangazia fursa za kiuchumi na kukuza ushirikiano wa kikanda.

Msafara huo wa wiki moja umeandaliwa kwa kushirikiana na Equity Bank Tanzania na Equity Bank Uganda, ukiwavuta zaidi ya wawekezaji 200 kutoka nchi 15, pamoja na wajasiriamali, makampuni ya uwekezaji, na wadau wa maendeleo ili kukuza uwekezaji wa mipakani kwa kushirikisha sekta muhimu kama Kilimo-biashara, Nishati mbadala, Utalii na hoteli, Madini na miundombinu pamoja na Uchumi wa Buluu (Blue Economy) kuchangia uundaji wa ajira na ukuaji wa uchumi wa jumuishi.
Akizungumza katika kongamano la Maonesho ya Biashara na Uwekezani (Equity Trade and Investment Roadshow 2025) ameiopongeza Benki ya Equity kwa kuwaleta pamoja wawekezaji wa ndani na wa kimataifa, wajasiriamali na washirika wa maendeleo na kusema kuwa hiyo sehemu ya utekelezaji wa mpango wa ARRP chini ya nguzo ya Biashara na Uwekezaji, kwa lengo la kukuza uchumi jumuishi na shindani kikanda.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Equity Bank Tanzania, Isabela Maganga amesema Msafara huu ni jukwaa la kuiweka Tanzania kama kiungo muhimu katika mnyororo wa thamani kikanda na kimataifa, unatoa fursa ya kipekee kwa wawekezaji wa kimkakati kwenye masoko ya kikanda na uwezo mkubwa katika sekta mbalimbali na ni jukwaa la kuiweka Tanzania kama kiungo muhimu katika usambazaji wa kikanda na kimataifa.
"Tanzania ina masoko makubwa, idadi ya watu inayokua, na rasilimali kwa sekta mbalimbali. Hii ni fursa ya kipekee kwa wawekezaji." alisema.
Msafara huu unafuatia mafanikio ya misafara mingine ya awali iliyosaidia uwekezaji wa mabilioni ya dola, katika nchi mbalimbali ikiwa ni pamoja na:

Kenya–DRC
Marekani–Tanzania
India–Rwanda–Uganda
Singapore–Kenya
Athari ya Mpango wa ARRP

Kwa kusudi la kufikia watu na biashara milioni 100 ifikapo 2030. Equity Group inatarajia kurejesha asilimia 2 ya pato la taifa Afrika Mashariki kwenye sekta binafsi na kuunda ajira milioni 50 barani Afrika.


Msafara huu unaonesha jitihada za Equity Group kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kuvumbua fursa kwa wawekezaji kimataifa. Kwa kushirikiana na serikali na sekta binafsi, Afrika Mashariki inaweza kuwa kivutio kikuu cha uwekezaji na ustawi wa kijamii.

Mkurugenzi Mtendaji wa Equity Bank Tanzania, Isabela Maganga akiteta jambo na Mkuu wa Chuo Cha Elimu ya Biashara (CBE) Prof. Edda Tandi Lwoga wakati wa kongamano la Maonesho ya Biashara na Uwekezani (Equity Trade and Investment Roadshow 2025) , lililoandaliwa na Benki ya Equity Tanzania na kufanyika jijini Dar es salaam leo.
Mkurugenzi wa Biashara wa Equity Bank Tanzania, Prosper Nambaya akizungumza wakari alipokuwa akiwasilisha mada yake katika kongamano la biashara na uwekezaji katika Afrika Mashariki, lililoandaliwa na Benki ya Equity Tanzania na kufanyika jijini Dar es salaam leo.

Benki ya CRDB Yaadhimisha Miaka 30 kwa Kutoa Jumla ya Gawio Kubwa Zaidi Kuwahi Kutokea la Shilingi Bilioni 170

May 19, 2025 Add Comment

 

Arusha 17 Mei 2025 - Katika Mkutano Mkuu wa 30 wa Mwaka wa Wanahisa (AGM) uliofanyika katika kituo cha mikutano cha AICC, wanahisa walikubaliana kwa kauli moja kuidhinisha gawio la Shilingi 65 kwa kila hisa, kiwango cha juu zaidi kuwahi kutolewa katika historia ya benki hiyo.


Jumla ya gawio lililotangazwa kwa mwaka wa fedha wa 2024 ni Shilingi bilioni 170, ikionyesha uimara wa utendaji wa kifedha wa benki na dhamira yake ya kudumu ya kutoa thamani endelevu kwa wanahisa wake.
Akizungumza wakati wa mkutano huo, uliofanyika kwa mfumo wa mseto ambapo wanahisa wengine walishiriki kidijitali, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB, Dkt. Ally Laay, alielezea fahari yake juu ya safari ya mafanikio ya benki hiyo kwa kipindi cha miongo mitatu iliyopita.

"Tukiadhimisha miaka 30 ya ubora katika huduma za kibenki, gawio hili la kihistoria ni ishara ya uimara wetu wa kifedha na pia ni zawadi ya kipekee kwa wanahisa waliotuamini na kutembea nasi katika safari ya mabadiliko, ubunifu na ukuaji," alisema Dkt. Laay.

Alieleza kuwa gawio la Shilingi 65 kwa hisa, ambalo ni ongezeko la asilimia 30 kutoka mwaka uliopita, linaakisi ongezeko la faida kwa kila hisa hadi kufikia TZS 211.5 kwa mwaka 2024, likichochewa na muundo thabiti wa uendeshaji wa benki, uongozi wa kimkakati na wafanyakazi wenye moyo wa kujituma.

Faida ya Benki ya CRDB baada ya kodi ilikua kwa asilimia 30 hadi kufikia TZS bilioni 551, ikiashiria mafanikio ya mkakati wa muda mrefu wa benki na ufanisi wa uendeshaji. Dkt. Laay pia alizipongeza kampuni tanzu za benki kwa mchango wao unaoongezeka katika mafanikio ya kundi, ambapo kwa pamoja zimetoa mchango wa asilimia 6 katika Faida ya kundi.
CRDB Bank Burundi ilipata faida baada ya kodi ya Shilingi bilioni 40.3, huku CRDB Insurance ikiwa katika mwaka wake wa kwanza wa biashara, ilipata faida ya TZS milioni 343, na hivyo kuimarisha mapato yasiyotokana na riba.

Wakati huo huo, kampuni tanzu ya Benki ya CRDB DR Congo inaendelea kuonyesha mwelekeo mzuri wa ukuaji na inatarajiwa kufikia kiwango cha faida mapema kuliko ilivyotarajiwa.
Akiwasilisha ripoti yake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kundi la Benki ya CRDB, Abdulmajid Mussa Nsekela, alijivunia mafanikio ya miaka 30 ya benki hiyo na kueleza mwelekeo wa miaka ijayo: “Tukiadhimisha miongo mitatu ya kuboresha maisha na kujenga uchumi wa watu wetu na nchi zetu, mafanikio ya mwaka 2024 yanadhihirisha kuwa safari yetu ndio kwanza inaanza.

Hatua inayofuata ni ya kuleta ushirikishwaji mpana zaidi, mabadiliko ya kidijitali, na athari chanya katika ukanda wetu wa Afrika.”

Nsekela alieleza kuwa mali za benki zimeongezeka hadi kufikia Shilingi trilioni 16.7 (+25.3%), na mkopo wa jumla umefikia Shilingi trilioni 10.4 (+22.7%) kutokana na mikakati inayowalenga wateja na uwezeshaji kupitia mikopo. Benki pia iliongeza upatikanaji wa huduma kwa makundi yaliyosahaulika huduma shirikishi kama akaunti ya Sadaka na mikopo kwa wajasiriamali wadogo wadogo kupitia mifumo ya kidijitali.
Alitaja pia ushiriki wa benki katika miradi mikubwa ya kikanda kama vile uwezeshaji wa viwanda vya grafiti kwa kushirikiana na DBSA na IDC, jambo linaloifanya Benki ya CRDB kuwa kichocheo cha ongezeko la thamani na uanzishaji viwanda Afrika Mashariki na Kati.

Uwiano wa gharama na mapato wa benki uliimarika hadi kufikia asilimia 45.7, huku Uwiano wa Mikopo Chechefu (NPL) ukiendelea kuwa chini kwa asilimia 2.9, ikiashiria nidhamu madhubuti ya usimamizi wa gharama na ubora wa mikopo. Uwekezaji katika usanifu wa mfumo wa biashara, uhimilivu wa mtandao na miundombinu ya msingi ya kibenki, umehakikisha uendeshaji thabiti katika mazingira ya kidijitali yanayobadilika kwa kasi.
Nsekela alitoa shukrani kwa wanahisa kwa kuendelea kuiamini benki hiyo, huku akisisitiza maono ya muda mrefu ya benki: “Maadhimisho haya ya miaka 30 ni hatua ya kihistoria. Dira yetu haijabadilika, kuwa taasisi ya kifedha inayoaminika, yenye athari chanya, na tayari kwa siku zijazo kwa vizazi vijavyo.”

Kwa kuzingatia misingi ya utawala bora, wanahisa waliidhinisha kuteuliwa tena kwa Price Waterhouse Coopers (PwC) kuwa wakaguzi wa nje wa benki kwa mwaka wa fedha wa 2025. Aidha, wanahisa walikubaliana kwamba Mkutano Mkuu wa 31 wa Mwaka ufanyike tarehe 23 Mei 2026 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC). Mkutano huo pia uliidhinisha kuchaguliwa kwa wajumbe katika makundi yafuatayo:

• Bw. Abdul Ally Mohamed, Bi. Grace Joachim na Dkt. Donald Mmari kuwakilisha wanahisa walio na umiliki chini ya asilimia 1,
• Dkt. Fred Msemwa aliteuliwa tena kuwakilisha wanahisa wenye umiliki kati ya asilimia 1–10
• Na Dkt. Judica King’ori aliteuliwa kuwa Mkurugenzi Huru.
Akizungumza katika mkutano huo, Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Mheshimiwa Gelasius Byakanwa, alisifu mageuzi ya benki hiyo: “Benki ya CRDB imekuwa mfano bora wa thamani kwa wanahisa na uadilifu wa kifedha. Rekodi yake ya kutoa gawio kila mwaka na utendaji wake mzuri katika soko la hisa ni ushahidi wa uongozi imara usio na kifani kwa kipindi cha miaka 30.”


WENYE VYETI FEKI VYA UANDISHI WA HABARI WAONYWA

May 19, 2025 Add Comment


Na Mwandishi Wetu, JAB

Wakati Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) ikiufungua rasmi mfumo wa usajili wa Waandishi wa Habari wa https://taihabari.go.tz ili kuomba kuthibitishwa na kupatiwa Kitambulisho cha Uandishi wa Habari (Press Cards) Mwenyekiti wa Bodi hiyo Ndg. Tido Mhando amewaonya wenye nia ya kutumia vyeti visivyo halali wakati wa kujaza taarifa zao.


Mhando alitoa tahadhali hiyo tarehe 19 Mei, 2025 wakati akizungumza na Wahariri na Waandishi wa Habari wa vyombo mbalimbali vya Habari katika ofisi za Bodi hiyo zilizopo Mtaa wa Jamhuri jijini Dar es Salaam.


“Ndugu zangu Waandishi wa Habari, Bodi hii itaanza kutoa ithibati kwa waandishi wa habari wote kupitia mtandao na kutoa vitambulisho vya kidijiitali (digital Press Card).  Maombi ya ithibati Press Cards yatafanyika kupitia Mfumo unaoitwa TAI-Habari”, alisema.


Mhando alisema mahitaji muhimu wakati wa kujaza taarifa katika mfumo huo kuwa ni pamoja na namba ya simu na barua pepe vinavyofanya kazi, picha ndogo (passport size) iliyoskaniwa barua ya utambulisho kutoka taasisi anayotoka au anakopeleka kazi zake ikiwa ni mwandishi wa kujitegemea (Freelancer), nakala ya Kitambulisho cha Taifa (NIDA) na ada ya ithibati shilingi Elfu Hamsini (50,000).

“Mahitaji mengine ni vyeti vya elimu vilivyoskaniwa kwa mfumo wa PDF na kuthibitishwa na Mamlaka husika (kama chuo kikuu vithibitishwe na TCU na kama ni vyuo vya kati vithibitishwe na NACTVET), na katika hili nisisitize tafadhali sana usiweke cheti ‘feki’ jambo hilo linakiuka siyo tu linakiuka maadili ya taaluma habari, bali pia ni makosa yanatakayodhibitiwa kwa mujibu wa Sheria za nchi,” alisema Mhando.

Mhando alisema mahitaji hayo ni muhimu ili kukamilisha mchakato wa maombi kwa mafanikio na kwamba ni hatua inayolenga kuboresha huduma, kuimarisha usimamizi wa taaluma ya Uandishi wa Habari na kurahisisha upatikanaji wa vitambulisho kwa waandishi waliothibitishwa.


Aliomba Wahariri, Waandishi na wadau wote wakiwemo waajiri kutambua umuhimu wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari katika kuimarisha weledi, maadili, na uwajibikaji wa taaluma ya uandishi wa habari nchini, na hivyo watoe ushirikiano wa hali ya juu katika kukuza na kuendeleza taaluma hiyo muhimu kwa taifa.



Akijibu maswali ya waandishi wa Habari kuhusu watu walio kwenye tasnia bila kuwa na vyeti vya Elimu ya Uandishi wa Habari, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi hiyo Wakili Patrick Kipangula alisema Sheria ilitoa muda wa miaka mitano kwa watu waliokuwa hawana sifa ili wakasome na kutimiza vigezo vya kisheria.


Alisema baada ya muda huo kuisha Waziri aliongeza muda wa mwaka mmoja na kwamba tangu Waziri aongeze mwaka mmoja ni miaka miwili imeshapita na kufanya jumla ya miaka nane na hivyo hakutakuwa na muda wa nyongeza tena.