WENYE VYETI FEKI VYA UANDISHI WA HABARI WAONYWA

May 19, 2025 Add Comment


Na Mwandishi Wetu, JAB

Wakati Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) ikiufungua rasmi mfumo wa usajili wa Waandishi wa Habari wa https://taihabari.go.tz ili kuomba kuthibitishwa na kupatiwa Kitambulisho cha Uandishi wa Habari (Press Cards) Mwenyekiti wa Bodi hiyo Ndg. Tido Mhando amewaonya wenye nia ya kutumia vyeti visivyo halali wakati wa kujaza taarifa zao.


Mhando alitoa tahadhali hiyo tarehe 19 Mei, 2025 wakati akizungumza na Wahariri na Waandishi wa Habari wa vyombo mbalimbali vya Habari katika ofisi za Bodi hiyo zilizopo Mtaa wa Jamhuri jijini Dar es Salaam.


“Ndugu zangu Waandishi wa Habari, Bodi hii itaanza kutoa ithibati kwa waandishi wa habari wote kupitia mtandao na kutoa vitambulisho vya kidijiitali (digital Press Card).  Maombi ya ithibati Press Cards yatafanyika kupitia Mfumo unaoitwa TAI-Habari”, alisema.


Mhando alisema mahitaji muhimu wakati wa kujaza taarifa katika mfumo huo kuwa ni pamoja na namba ya simu na barua pepe vinavyofanya kazi, picha ndogo (passport size) iliyoskaniwa barua ya utambulisho kutoka taasisi anayotoka au anakopeleka kazi zake ikiwa ni mwandishi wa kujitegemea (Freelancer), nakala ya Kitambulisho cha Taifa (NIDA) na ada ya ithibati shilingi Elfu Hamsini (50,000).

“Mahitaji mengine ni vyeti vya elimu vilivyoskaniwa kwa mfumo wa PDF na kuthibitishwa na Mamlaka husika (kama chuo kikuu vithibitishwe na TCU na kama ni vyuo vya kati vithibitishwe na NACTVET), na katika hili nisisitize tafadhali sana usiweke cheti ‘feki’ jambo hilo linakiuka siyo tu linakiuka maadili ya taaluma habari, bali pia ni makosa yanatakayodhibitiwa kwa mujibu wa Sheria za nchi,” alisema Mhando.

Mhando alisema mahitaji hayo ni muhimu ili kukamilisha mchakato wa maombi kwa mafanikio na kwamba ni hatua inayolenga kuboresha huduma, kuimarisha usimamizi wa taaluma ya Uandishi wa Habari na kurahisisha upatikanaji wa vitambulisho kwa waandishi waliothibitishwa.


Aliomba Wahariri, Waandishi na wadau wote wakiwemo waajiri kutambua umuhimu wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari katika kuimarisha weledi, maadili, na uwajibikaji wa taaluma ya uandishi wa habari nchini, na hivyo watoe ushirikiano wa hali ya juu katika kukuza na kuendeleza taaluma hiyo muhimu kwa taifa.



Akijibu maswali ya waandishi wa Habari kuhusu watu walio kwenye tasnia bila kuwa na vyeti vya Elimu ya Uandishi wa Habari, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi hiyo Wakili Patrick Kipangula alisema Sheria ilitoa muda wa miaka mitano kwa watu waliokuwa hawana sifa ili wakasome na kutimiza vigezo vya kisheria.


Alisema baada ya muda huo kuisha Waziri aliongeza muda wa mwaka mmoja na kwamba tangu Waziri aongeze mwaka mmoja ni miaka miwili imeshapita na kufanya jumla ya miaka nane na hivyo hakutakuwa na muda wa nyongeza tena.

RAIS SAMIA NA RAIS MSTAAFU KIKWETE WAPONGEZWA KWA KUFANIKISHA USHINDI WA PROFESA JANABI KATIKA UCHAGUZI WA MKURUGENZI WA WHO KANDA YA AFRIKA

May 19, 2025 Add Comment


Na Mwandishi `Maalumu


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amepongezwa kwa maono yake ya mbali na uamuzi wa busara wa kumpendekeza Profesa Mohamed Yakub Janabi kugombea nafasi ya Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika wa Shirika la Afya Duniani (WHO).

Wananchi mbalimbali waliohojiwa wametaja hatua hiyo ya Rais Samia kama ishara ya kujiamini kama taifa, na uthibitisho kuwa Watanzania wanao uwezo wa kushika nafasi nyeti katika taasisi kubwa za kimataifa, wakielezea faraja yao kwa jinsi Tanzania inavyozidi kung’ara kwenye majukwaa ya kidiplomasia duniani.

Aidha, Rais Samia amesifiwa kwa kuunda kikosi kazi maalum kilichoongozwa na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, kwa ajili ya kuratibu na kusimamia kampeni ya kidiplomasia ya Profesa Janabi. 


Ushirikiano huo umeibuka na  matokeo chanya, ambapo Profesa Janabi ameibuka mshindi kwa kishindo kupitia mchakato wa uchaguzi uliopigiwa kura na nchi wanachama wa WHO Kanda ya Afrika.

Dkt. Kikwete, ambaye ana uzoefu mkubwa katika medani za kimataifa, amepongezwa kwa kutumia umahiri na uhusiano wake wa kidiplomasia kuhakikisha kampeni hiyo inafanikiwa. Mchango wake umetajwa kama kichocheo muhimu kilichowezesha Tanzania kupata ushindi dhidi ya wagombea kutoka Côte d’Ivoire, Guinea na Togo.


Katika picha iliyopigwa wakati wa harakati za kampeni hiyo, Dkt. Kikwete anaonekana akiongoza moja ya vikao vya kikosi kazi hicho, ambacho hatimaye kilitimiza azma yake mnamo Jumapili, Mei 18, 2025, kwa ushindi mkubwa wa Profesa Janabi. 

Mgombea huyo wa Tanzania alipata kura 32 kati ya 47 zilizopigwa kwa siri na wajumbe wa nchi wanachama wa WHO Afrika, kabla ya kuanza kwa Mkutano Mkuu wa WHO.


Uchaguzi huo umefanyika kufuatia kifo cha ghafla cha aliyekuwa Mkurugenzi mteule, Dkt. Faustine Ndugulile, mnamo Novemba 2024. Nafasi hiyo ilivuta wagombea mahiri kutoka mataifa kadhaa, lakini Profesa Janabi alifanikiwa kuungwa mkono kwa wingi, akionesha kuwa jina la Tanzania bado lina nguvu katika diplomasia ya afya barani Afrika.


Kwa mujibu wa taratibu za Shirika la Afya Duniani, jina la Profesa Janabi sasa litawasilishwa kwa ajili ya kuthibitishwa rasmi na Bodi ya Utendaji ya WHO katika kikao chake cha 157 kitakachofanyika Mei 28–29, 2025, mjini Geneva, Uswisi.


Iwapo atathibitishwa, Profesa Janabi ataapishwa na kuanza kutekeleza rasmi majukumu yake kwa kipindi cha miaka mitano, huku akiwa na fursa ya kuongezewa muhula mmoja zaidi kulingana na kanuni za taasisi hiyo.

WAZIRI MKUU MAJALIWA : SERIKALI IMEJIPANGA KUDHIBITI MAGUGUMAJI ZIWA VICTORIA

May 19, 2025 Add Comment


_▪️Amshukuru Rais Dkt. Samia ununuzi wa mitambo ya uteketezaji wa magugumaji

 

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema Serikali imeweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha changamoto ya uwepo wa magugumaji katika ziwa Victoria inapatiwa ufumbuzi ili kuwezesha shughuli za kijamii ziweze kuendelea katika maeneo hayo.

 



”Ninamshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia kutoa fedha za ununuzi wa mitambo mikubwa ya kuteketeza magugumaji ndani ya ziwa Victoria ili kuwezesha shughuli za uvuvi, usafiri na usafirishaji kuendelea.”

 

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatatu, Mei 19, 2025) wakati akizungumza na wananchi alipokagua shughuli ya udhibiti wa magugumaji katika eneo la Kigongo-Busisi akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Mwanza.

 


Mheshimiwa Majaliwa amesema magugumaji hayo yamekuwa yakiathiri kwa kiwango kikubwa shughuli mbalimbali za kijami na kiuchumi katika ziwa hilo, hivyo ununuzi wa mitambo hiyo utasaidia kuteketezwa kwa magugu hayo.

 

Aidha, Waziri Mkuu amewashukuru wananchi wa maeneo hayo wakiwemo wavuvi ambao wamejitolea kushirikiana na Serikali katika zoezi la kuyaondoa magugumaji hayo.

 

Wakati huo huo, Waziri Mkuu ameiagiza Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira iendelee na kazi ya kuyaondoa magugumaji hayo hadi pale yatakapomalizika ili kuhakikisha shughuli za kijami zinaendelea bila ya kikwazo chochote.

 

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhandisi Cyprian Luhemeja akitoa taarifa kuhusu shughuli ya kuteketeza magugumaji hayo kwa Waziri Mkuu amesema kwa sasa wanaendelea na kazi ya kuyaondoa magugumaji ya asili ambayo yamesambaa katika eneo la ukubwa wa ekari zaidi ya 300.

 

Amesema magugumaji hayo ambayo yamegawanyika katika aina tatu (salivinia molesta ambalo ni jipya, water hyacinth na gugumaji la asili aina ya Lutende) yameathiri mfumo wa ikolojia, shughuli za usafiri na usafirishaji na shughuli za uvuvi katika baadhi ya maeneo ndani ya Ziwa Victoria

 

Katibu Mkuu huyo amesema wanatarajia kumaliza kazi ya kuyateketeza magugumaji mwezi Julai, 2025 na hivyo kuwezesha shughuli za uvuvi, usafiri na usafirishaji kuendelea katika ziwa Victoria kama ilivyokuwa awali.

BIASHARA YA MAZAO YA MISITU NA NYUKI YAPAA – MAUZO NJE YA NCHI YAONGEZEKA KWA ASILIMIA 333%

BIASHARA YA MAZAO YA MISITU NA NYUKI YAPAA – MAUZO NJE YA NCHI YAONGEZEKA KWA ASILIMIA 333%

May 19, 2025 Add Comment

 MH CHANA.jpg

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana akiwasilisha akadirio ya bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
-----
WhatsApp Image 2025-05-19 at 10.42.45.jpeg

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Kutoka kushoto ni Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Prof. Dos Santos Silayo, akiwa na makamishna wengine wa uhifadhi wafuatilia kwa makini hoja mbalimbali, ikiwemo mafanikio makubwa ya TFS katika usimamizi endelevu wa rasilimali za misitu na nyuki Mei 19,2025—ikiwa ni sehemu ya dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kujenga uchumi shirikishi wa kijani.

Serikali imebainisha mafanikio makubwa katika biashara ya mazao ya misitu na nyuki nchini, ikiwemo ongezeko la uzalishaji, viwanda na mauzo nje ya nchi, ikiwa ni matokeo ya uwekezaji wa kimkakati unaofanywa kwa kushirikiana na sekta binafsi.

Akizungumza leo Mei 19, 2025 bungeni jijini Dodoma wakati wa kuwasilisha makadirio ya bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha 2025/2026, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana alisema kuwa ndani ya miaka mitano, sekta hizo mbili zimeonyesha ushahidi wa wazi wa kuimarika kwa msingi wa uchumi wa kijani nchini.

Aliongeza kuwa, katika kipindi cha kuanzia mwaka wa fedha 2020/2021 hadi 2024/2025, uzalishaji wa mbao kutoka mashamba ya miti ya Serikali unaolimwa kibiashara umeongezeka kutoka mita za ujazo 1,108,791 hadi 1,264,535, ikiwa ni ongezeko la zaidi ya 155,000 m³.

Aidha, viwanda vya kati na vikubwa vya kuchakata na kuongeza thamani ya mazao ya misitu vimeongezeka kutoka 636 mwaka 2020 hadi 1,671 mwaka 2025, huku viwanda vidogo vidogo kama vya useremala vikifikia zaidi ya 7,000 kote nchini.

Waziri Chana alisema kuwa thamani ya mauzo ya mazao ya misitu nje ya nchi nayo imepanda kwa kasi, kufikia Shilingi 458.47 bilioni mwaka 2024/2025, kutoka Shilingi 105.68 bilioni mwaka 2020/2021. Ongezeko hilo ni sawa na asilimia 333.8, jambo alilolieleza kuwa ni matokeo ya kuimarika kwa viwango vya usimamizi na ubora wa bidhaa zinazozalishwa.

Katika upande wa nyuki, Serikali imewezesha ujenzi wa viwanda nane (8) vya kati na vikubwa vya kuchakata na kuongeza thamani ya mazao ya nyuki, kutoka kiwanda kimoja (1) mwaka 2020. Viwanda hivyo vimejengwa katika mikoa ya Tabora, Kigoma, Singida, Iringa, Katavi na Geita.

Mpaka kufikia Aprili 2025, Tanzania imeuza nje ya nchi jumla ya tani 1,321.35 za asali zenye thamani ya Shilingi 15.86 bilioni, ikilinganishwa na tani 430.61 za mwaka 2020/2021 zenye thamani ya Shilingi 5.17 bilioni — ikiwa ni ongezeko la asilimia 206.9.

Kutokana na mafanikio haya, Shirika la Wafugaji Nyuki Duniani limeiteua Tanzania kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Dunia wa Wafugaji Nyuki (APIMONDIA) utakaofanyika mwaka 2027 na kuhudhuriwa na watu zaidi ya 4,000 kutoka mataifa mbalimbali duniani.
“Kuongezeka kwa uzalishaji na thamani ya mauzo ya mazao ya misitu na nyuki ni ushahidi wa mafanikio ya ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi. Tunajenga msingi wa uchumi wa kijani unaozingatia uhifadhi, maendeleo ya viwanda na ajira kwa vijana wetu,” alisisitiza Waziri Chana.

Katika hatua nyingine, Waziri Chana amewakaribisha wabunge wote na wadau wengine wa sekta ya maliasili kushiriki maonesho ya Siku ya Nyuki Duniani ambayo yanaendelea jijini Dodoma, na kufikia kilele chake kesho Mei 20, 2025 katika katika viwanja vya Chinangali Jijini Dodoma.


--

Tulizo Henry Kilaga I A Brand Communication Strategist,

Located: Dodoma I Dar es Salaam - Tanzania. 

Call/WhatsApp: +255 765 888887

www.thestrategist.co.tz

RC DKT BATILDA AFUNGUA MAADHIMISHO YA NNE YA SIKU YA KIMATAIFA YA WANAWAKE KATIKA SEKTA YA BAHARI ATOA NENO

May 19, 2025 Add Comment




Na Oscar Assenga,Tanga

kuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dk Batilda Burian amesema maendeleo ya Taifa hayawezi kupimwa kwa kiwango cha uwekezaji au ujenzi wa viwanda pekee, bali kwa namna serikali na jamii zinavyoweka fursa za usawa wa kijinsia katika ajira, hususan kwa watoto wa kike na wa kiume.

Dk Burian ameyasema hayo alipokuwa akifungua maadhimisho ya nne ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake katika Sekta ya Bahari yaliyofanyika jijini Tanga  (Jumapili) Mei 18/2025.


Akimnukuu mwanafalsafa maarufu Plato, aliyewahi kusema kuwa "Kilimo cha jamii yoyote ni jinsi inavyowathamini wanawake", Dk Burian alisisitiza kuwa taifa linapaswa kujipangia malengo ya kuhakikisha usawa wa kijinsia unatekelezwa kikamilifu.

"Tusiache mwanamke abaki ufukweni bali tunataka aingie ndani ya bahari," alisema kwa msisitizo..

Alieleza kuwa licha ya juhudi zinazofanywa na serikali na wadau mbalimbali, sekta ya bahari bado inatawaliwa na wanaume, huku takwimu zikionyesha kuwa wanawake wanaofanya kazi katika sekta hiyo ni asilimia 1.2 pekee.

Katika hatua ya kutia moyo, Dk Burian alipongeza Umoja wa Wanawake Wanaofanya Kazi katika Sekta ya Bahari katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika (WOMESA) kwa kuanzisha programu ya 'Wakamate Wangali Wadogo' (Catch them Young) inayolenga kuelimisha na kuwahamasisha wanafunzi wa kike kujiunga na fani zinazohusiana na bahari.

Alisisitiza kuwa wanawake ndio uti wa mgongo wa sekta hiyo, akibainisha kuwa juhudi kama hizo zinaunga mkono maono ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan ya kuwekeza kwenye elimu ya sayansi kwa watoto wa kike, ikiwemo kuanzishwa kwa shule maalum."

Hapa Tanga, kupitia uwekezaji wa Rais, tumeanzisha shule maalum ya watoto wa kike wilayani Kilindi ambayo imepewa jina la aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo, Beatrice Shelukindo," alisema.

Dk Burian pia alitoa wito kwa sekta binafsi inayohusika na bahari kuhakikisha usawa wa kijinsia unazingatiwa katika ajira.


"Nifahari yetu Kuwaona Wanawake wa Kitanzania wakiongoza na kushiriki miradi mkubwa ya maendeleo ya bandarini,fukwe zetu wakifundisha kwenye vyuo vya Bahari kama Chuo Cha Bahari Dar es salaam(Dar es salaam Maritime INstute-DMI)kufanya kazi kwenye Meli za kitaifa na Kimataifa Kwa hakika Hawa ni vinara na fahari yetu ni lazima tuwapongeze"alisema Burian.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa WOMESA, Bi Fortunata Kikwaya, alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, kwa uwekezaji mkubwa walioufanya katika sekta ya bahari."


Sherehe hizi za nne zinaashiria maono yetu kuwa wanawake si wa kushirikishwa tu, bali ni wadau wakuu katika maendeleo ya sekta hii," alisema.

Bi Kikwaya alitaja mafanikio ya WOMESA kuwa ni pamoja na ongezeko la wanachama kutoka 24 mwaka 2021 hadi kufikia 174 mwaka huu, pamoja na kudhamini mafunzo ya muda mfupi na mrefu kwa wanawake.


Kuhusu mpango wa 'Catch them Young', alisema tayari wametembelea shule 35 na kuanzisha vilabu tisa vya wanafunzi, vitatu kati yake vikiwa jijini Tanga.

Hata hivyo, alieleza kuwepo kwa mwamko mdogo wa wanawake kujiunga na WOMESA pamoja na uelewa mdogo kuhusu fursa zilizopo katika sekta ya bahari.

Aliiomba Serikali kuanzisha utaratibu wa kutoa ufadhili wa masomo kwa watoto wa kike wanaotaka kusomea taaluma zinazohusiana na sekta ya bahari na kusaidia kuendeleza juhudi za kuwahamasisha kuingia katika sekta hiyo.



Mwisho