WAOMBAJI MIKOPO YA ELIMU,TAFUTENI NAMBA ZA NIDA MAPEMA

May 18, 2025 Add Comment


Na: Dk. Reubeni Lumbagala, Tanga


Ni takwa la kisheria kwa waombaji wa mikopo ya elimu kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kuwa na namba ya utambulisho (National Identification Number-NIN) au kitambulisho cha uraia kutoka Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) ili kuweza kuomba mikopo ya elimu.


Pamoja na kwamba takwa hilo la kisheria kwa miaka ya nyuma kwa mwombaji ambaye hakuwa na namba ya utambulisho au kitambulisho cha uraia aliweza kuomba na kupata mkopo, lakini kwa mwaka huu wa masomo wa 2025/2026, bila namba ya utambulisho au kitambulisho cha uraia, mwombaji atashindwa kuomba mkopo na hivyo kukosa mkopo.


Bodi ya Mikopo kwa kushirikiana na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa walifanya mkutano Mei 16, 2025 ambapo mkazo juu ya kila mwombaji  wa mkopo wa elimu kuhakikisha ana namba ya utambulisho au kitambulisho cha uraia uliwekwa bayana mbele ya vyombo vya habari na Watanzania kwa ujumla.

Katika mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dk. Bill Kiwia alisisitiza juu ya umuhimu wa waombaji kuwa na namba ya NIN. "NIN itaiwezesha HESLB kuwa na taarifa sahihi na za kipekee za kila mwanafunzi. Kwa kutumia NIN kutatuwezesha kuboresha uwezo wetu wa kufuatilia wanufaika waliokopeshwa baada ya kuhitimu. Tumeunganisha mifumo yetu ili kuwezesha kuhakiki taarifa za waombaji mikopo kupitia NIN. Tayari wataalamu wa Tehama kutoka pande zote mbili (HESLB na NIDA) wanashirikiana kuhakikisha mifumo yetu iliyounganishwa inafanya kazi kwa ufanisi," amesema Dk. Kiwia.


Kimsingi, serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Dk. Samia Suluhu Hassan, imekuwa ikisisitiza mifumo ya serikali kusomana ili kurahisisha utendajikazi na ufuatiliaji kwa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama). Kabla ya maboresho makubwa yaliyofanywa na HESLB kuhusiana na mifumo ya kidigitali, kulikuwa na changamoto ya kupata taarifa za wanufaika wahitimu ambao hawajarejesha mikopo ambayo ni fedha zilizotumika kuwasomesha elimu ya juu katika taasisi mbalimbali za elimu.


Kwahiyo, maboresho makubwa yamefanyika kwa HESLB kuungana na taasisi nyingine mbalimbali ili kuwa na mfumo wa pamoja ambao utarahisisha utendajikazi na ufuatiliaji. Sambamba na hilo, kwa kuzingatia gharama zilizopo katika elimu ya kati na ya juu yaani ada, chakula, malazi, vitabu, kudurufu matini (kutoa photocopy), mafunzo kwa vitendo; Watanzania wengi wanahitaji kuwezeshwa kifedha kupitia mikopo inayoratibiwa na HESLB.


Hivyo, niwashauri waombaji wa mikopo ambao hadi sasa hawana namba ya NIN kuomba namba hizo kupitia tovuti ya NIDA au kwenda kwenye ofisi za NIDA zilizopo katika Halmashauri na wilaya zao ili kupata namba ili kuweza kuomba mikopo pindi dirisha la maombi ya mikopo litakapofunguliwa rasmi na hivyo kuwa katika nafasi nzuri ya kupata mikopo. 


Kwa upande wa Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, James Kaji, amesema NIDA wapo tayari kuwahudumia waombaji wa mikopo. "Tunafurahia wenzetu wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu wameona na kutambua jitihada zetu, pamoja na mambo mengine watatuunga mkono katika kutoa hamasa hii kwa vijana. Namba ya utambulisho wa Taifa (NIN) inapatikana ndani ya siku 5 baada ya kujisajili, na kadi ya NIDA inapatikana ndani ya siku 21 baada ya uthibitisho wa taarifa za mwombaji, hakikisha unapojisajili unapata kadi," amesema.


Dirisha la maombi ya mikopo linatarajiwa kufunguliwa mwezi Juni, 2025, ni vyema waombaji watarajiwa wasiokuwa na namba ya utambulisho au kitambulisho cha uraia wakaanza kufuatilia mapema badala ya kusubiri hadi muda wa kuomba mkopo ufike ndipo waanze kuhangaika kufuatilia. Ikumbukwe kuwa bila namba ya utambulisho, maombi ya mikopo hayataweza kukamilika. 


"Tunatarajia kufungua dirisha la maombi ya mikopo mwezi Juni, 2025, kwa mwaka wa masomo wa 2025/2026, namba ya utambulisho wa Taifa itakuwa hitaji la lazima katika kujaza fomu za maombi ya mikopo, hivyo waombaji wote wanapaswa kuwa na namba hii wakati wa kujaza maombi yao ya mkopo," alisisitiza Dk. Kiwia.


Dk. Reubeni Lumbagala ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Funguni ya wilayani Pangani mkoani Tanga.


Maoni: 0620 800 462.

NISHATI SAFI YA KUPIKIA NI KIPAUMBELE CHA SERIKALI -MHANDISI MRAMBA

May 17, 2025 Add Comment


📌 *Ashiriki Marathon ya Kuhamasisha Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia*


📌 *Asema Nishati Safi ya Kupikia itapunguza uharibifu wa mazingira na kulinda afya*


Katibu Mkuu wa Wizara Ya Nishati Mha. Felchesmi Mramba amesema kuwa, suala la upatikanaji wa nishati safi ya kupikia ni moja ya vipaumbele vya nchi na kwamba Serikali inahakikisha kuwa Mpango Mkakati wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia unatekelezwa kwa kasi na kwa umakini ili kutimiza azma ya nchi kuhama kutoka matumizi ya nishati isiyo safi ya kupikia kwenda kwenye nishati safi.

Amesema hayo tarehe 17 Mei, 2025 jijini Dar es Salam wakati akishiriki Marathon ya Nishati Safi ya Kupikia oiyofanyika katika viwanja wa Oysterbay..


“Serikali imeamua kwenda nalo kasi suala hili la nishati safi ya kupikia ili kuepusha uharibifu wa mazingira kwani nishati ambayo si salama kama kuni na mkaa inatumika kwa kiasi kikubwa kwa kupikia hivyo tukitekeleza Dira hii, kwa kiasi kikubwa tutapunguza uharibifu wa mazingira pamoja na kulinda afya za wananchi.” Amesema Mramba

Mha. Mramba, amewapongeza waandaaji wa Marathon hiyo Shirika la Wafanyabishara Wanawake (TABWA) ambayo imelenga kuhamasisha Nishati Safi ya Kupikia  kwa Wananchi.

Aidha, amewaasa  Wadau mbalimbali kuzidi kujitokeza ila kuzidi kuendeleza mikakati ya kusambaza elimu ya Nishati Safi ya Kupikia kwa Watanzania wengi zaidi.












MATHIAS CANAL ACHANGIA VIFAA VYA MICHEZO SHULE MBILI ZA MSINGI IRAMBA//AMPA HEKO DKT MWIGULU NCHEMBA

May 17, 2025 Add Comment
Mshindi wa Tuzo za SAMIA KALAMU AWARDS na Afisa Mtendaji Mkuu wa WAZOHURU MEDIA Ndg Mathias Canal amechangia vifaa vya michezo katika shule mbili za Msingi ambazo ni Kiomboi Bomani na Kiomboi Hospitali.

TPDC Yadhamini na Kushiriki Mbio za Marathoni kwa Lengo la Kuelimisha Umma Kuhusu Nishati Safi ya Kupikia

May 17, 2025 Add Comment
 Baadhi ya wanachama wa TPDC Runners Club wakiwa katika picha ya pamoja

MAJALIWA: SANAA INAMCHANGO MKUBWA KATIKA KUKUZA UCHUMI

May 17, 2025 Add Comment


_▪️Awataka wasanii wawekeze zaidi katika sanaa ili kuongeza wigo wa ajira_

 


WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema sekta ya utamaduni na Sanaa ina mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa wasanii na Taifa, kuongeza fursa za ajira, kurasimisha kazi za sekta sambamba na kuimarisha maadili ya jamii.


Waziri Mkuu ametoa wito kwa wasanii nchini waweke kipaumbele cha kuwekeza mapato yatokanayo na kazi zao katika shughuli za mnyororo wa thamani wa sanaa ili kuongeza wigo wa kuajiri vijana katika sekta hiyo na kuongeza pato la Taifa.


Ameyasema hayo leo (Jumamosi, Mei 17, 2025) alipomuwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Pili wa Wadau wa Utamaduni na Sanaa uliofanyika kwenye Ukumbi wa Millenium Tower jijini Dar es Salaam. Amesema sekta hizo zimeajiri makundi yote jumuishi yakiwemo ya watu wenye ulemavu, vijana, wazee na watoto kwa jinsia na hali tofauti na watu wote.

Waziri Mkuu amesema zaidi ya hayo, sekta hiyo inakuza ujasiriamali na biashara ndogondogo na za kati. ”Sote tumewashuhudia wasanii wakianzisha biashara, kuzirasimisha na kuziweka katika mfumo unaotambuliwa na mabenki ili  kuzitumia kama dhamana kwenye taasisi za kifedha ili kupata mitaji kwa shughuli mbalimbali.”


Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa wasanii wote nchini wajitahidi kutengeneza kazi bora zaidi na kurasimisha shughuli zao za sanaa katika mamlaka husika za binafsi na Serikali ili kila msanii awe rasmi na aweze kunufaika na fursa zilizopo.

Amesema Sekta za Utamaduni na Sanaa inatoa mchango mkubwa katika uchumi kote ulimwenguni, ambapo Ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Biashara na Maendeleo (UNCTAD) ya mwaka 2022, imebainisha kuwa sekta hizo zilichangia asilimia 3.1 ya Pato la Dunia (GDP), huku ikitoa asilimia 6.2 ya ajira sawa na ajira milioni 50 duniani kote.


Waziri Mkuu amesema kwa kutambua umuhimu wa sekta za utamaduni na sanaa, Serikali imefanya jitihada mahsusi za kuendeleza sekta hizo.  Jitihada hizo ni pamoja na kuimarisha mifumo kisera na rasilimalifedha kwa ajili ya kuendeleza shughuli za kisekta.


Pia, Waziri Mkuu amesema sambamba na kutunga sera, Serikali imetunga sheria na kanuni zilizoleta mageuzi ya shughuli za utamaduni na sanaa. ”Mifumo hiyo ya kisheria, imewezesha shughuli za utamaduni na sanaa kuondoka kwenye dhana ya kuwa burudani pekee na kuwa ajira rasmi zinazochangia kukuza pato kwa mtu binafsi na Taifa.


Amesema hatua hiyo kwa upande mwingine ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020-2025 Ibara ya 241 inayoielekeza serikali kuboresha tasnia ya sanaa nchini ili kuiendesha kibiashara  na  kuongeza upatikanaji wa fursa zaidi za ajira kwa makundi yote ya jamii.


Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Profesa Palamagamba Kabudi amesema Mkutano huo ni wa pili katika mfululizo wa mikutano ya wadau wa Mfuko wa Utamaduni na Sanaa Tanzania inayolenga kuwakutanisha ili kubadilishana uzoefu, kujadili mafanikio na changamoto zilizopo na kuweka mikakati ya pamoja ya kukabiliana nazo.


Akizungumzia kuhusu mahitaji ya mikopo kwa wasanii amesema ni makubwa kuliko mtaji walionao na kwa upande mwingine wadau wanaomba kiasi cha juu cha mkopo kinachotolewa cha shilingi milioni 100 kiongezwe mara dufu ili kiendane na uhalisia wa uwekezaji kisekta.


“Tumetoa mikopo yenye masharti nafuu kwa zaidi ya miradi 580 ya wasanii, hii inaonesha kwamba Serikali imedhamiria katika kuiinua sekta ya Utamaduni na Sanaa kama kichocheo cha maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Hadi sasa tumefanikisha marejesho kwa asilimia 96 hadi sasa, jambo ambalo linaonesha uwajibikaji wa wanufaika.”


Amesema wakati wizara inaendelea na jitihada za kutafuta vyanzo vingine endelevu vya fedha, wanamshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada za makusudi za kuhakikisha bajeti ya Mfuko wa Utamaduni inaongezeka kila mwaka ambapo katika mwaka wa fedha 2025/2026 imefikia sh bilioni nne kutoka shilingi bilioni 1.6 mwaka 2023/2024.