Showing posts with label siasa. Show all posts
Showing posts with label siasa. Show all posts

JESCA MAGUFULI AKABIDHI PIKIPIKI 5 KUSAIDIA UTENDAJI UVCCM GEITA

October 28, 2024 Add Comment

 



Makatibu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wilaya zote za mkoa wa Geita wamekabidhiwa pikipiki tano zenye thamani ya Shilingi milioni 17.

Pikipiki hizo zimetolewa na Ndugu Jesca John Magufuli na kukabidhiwa kwa Katibu wa UVCCM mkoa wa Geita, Ndugu Abel Shamakala ili kuongeza ufanisi wa utendaji wa shughuli mbalimbali za ujenzi wa Jumuiya katika mkoa huo, ikiwa ni pamoja na kuwahi vikao na kufika Kwa vijana na kutafuta kero zao.

Mjumbe wa Baraza Kuu UVCCM Taifa, Ndugu Reuben Saganyika amemshukuru Ndugu Jesca Magufuli kwa mchango wake.

“Hizi pikipiki zitakwenda kufanya kazi, na hasa kipindi hiki cha Uchaguzi, pikipiki hizi zitakwenda kusaka kura za Chama Cha Mapinduzi, zitakwenda kuleta ushindi Kwa Chama Chetu ndani ya mkoa wetu wa Geita, hivyo tunakushuruku sana Dada yetu” amesema Cde. Saganyika.












MHE. PINDA ,SEOM WAKUTANA NA MACHIFU WA BOTSWANA

October 28, 2024 Add Comment


Mkuu wa Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC-SEOM) Mhe. Mizengo Pinda na ujumbe wake wa SEOM wamekutana na kuzungumza na machifu kutoka koo mbalimbali za nchini Botswana katika kikao kilichofanyika jijini Gaborone tarehe 27 Oktoba 2024 ikiwa ni sehemu ya vikao ambavyo SEOM imekuwa ikifanya na wadau mbalimbali wa uchaguzi nchini humo.

Mhe. Pinda ametumia kikao hicho kuwajulisha machifu hao kuhusiana na kazi ya uangalizi wa uchaguzi mkuu wa Botswana kuanzia maandalizi, mwenendo wake na jinsi mambo yalivyo wakati huu wa uchaguzi ikiwa ni kutekeleza jukumu la Uangalizi kwa kuzingatia misingi na miongozo ya uchaguzi wa kidemokrasia iliyowekwa na SADC.

Aliwaambia machifu hao kuwa SEOM imekuwa ikikutana na wadau mbalimbali na kuzungumza nao moja kwa moja na hivyo kupata picha halisi ya jinsi mwenendo na maandalizi ya uchaguzi huo yalivyo na kuongeza kuwa SEOM imepeleka waangalizi wake katika majimbo yote ya uchaguzi ili kuangalia hali inavyokwenda, itakavyokuwa siku ya uchaguzi na baada ya uchaguzi.

Akizungumza katika kikao hicho Kiongozi wa Machifu wa Botswana Chief Gaborone toka kabila la Batlokwa alisema wao kama machifu wana jukumu la kuhakikisha koo zao hazigawanyiki licha ya kuwa wananchi wao ni wafuasi wa vyama vya siasa na kwa kufanya hivyo amani na usalama vitaendelea kuwepo katika maeneo yao.

Alisema wao wakiwa viongozi wa kimila na kijadi nchini humo wana wajibu wa kuwahimiza wananchi kushiriki katika michakato ya siasa ili waweze kuchagua viongozi wa kisiasa ambao wataongoza nchi kwa kipindi husika.

Amesema wao sio wanasiasa ila wanashirikiana na viongozi serikali kuhakikisha wananchi wanashiriki kikamilifu katika shughuli za siasa kwa kufuata sheria, kanuni, taratibu na miongozo iliyopo akitolea mfano wa Tume Huru ya Uchaguzi ya Botswana ilivyowafuata na kuwajulisha juu ya juu ya kufanyika kwa zoezi la uandikishaji wapiga kura na kuwaomba kuwasaidia kufikisha ujumbe huo wa uandikishaji wapiga kura kwa wananchi kwenye maeneo yao.

Naye Chifu Lotlamoreng kutoka kabila la Barolong amesema kama chifu akitaka kujihusisha moja kwa moja na masuala ya siasa ni lazima aondoke katika kazi ya uchifu ili aweze kuwa huru kujihussiha na masuala ya siasa nchini humo.

Wamesema machifu hawajazuiwa kugombea nafasi za siasa ila wanatakiwa wajue kuwa ukiamua kugombea na kushiriki kama mgombea unatakiwa kuondoka katika ofisi ya chifu ili kuepuka mgogoro wa maslahi na sheria Sheria ya Machifu ya mwaka 2008 ambayo inawatambua machifu na Ofisi zao nchini Botswana.

Ameongeza kuwa katiba ya Botswana pia inatambua Ofisi ya Machifu na inawatambua machifu hao ambo wako zaidi ya 500 wakiwamo machifu wananwake ambao wanakaribia 100.

Katika mkutano mwingine, SEOM ilikutana na Kiongozi wa wa Chama cha Real Alternative Bw. Gaontebale Mokgosi ambaye alionyesha wasiwasi kuhusu maandalizi ya uchaguzi huo ambayo yamefanywa na Tume Huru ya Uchaguzi (IEC), akitaja kuchelewa kwa uchapishaji wa karatasi za kupigia kura kama mfano wa mandalizi duni ya uchaguzi huo na wanadhani kuwa IEC haiko tayari kuendesha uchaguzi huru na wa na haki.

Chama hicho kilisisitiza umuhimu wa kuongeza utoaji wa elimu ya wapiga kura na kupendekeza kuwa IEC inapaswa kushirikiana kwa karibu na vyama vya siasa nchini Botswana ili kuhamasisha watu wengi zaidi kushiriki zoezi la kuandikisha wapiga kura na kujitokeza kupiga kura. Pia walisisitiza umuhimu wa ofisi ya ushirikiano wa vyama vya kisiasa kutakiwa kufanya kazi zaidi mwaka huu wa uchaguzi kinyume na ilivyokuwa kwakuwa ofisi hiyo ina jukumu muhimu la kuunganisha IEC, vyama vya kisiasa, na raia kwa ujumla.








MHE. PINDA APOKEA TAARIFA YA MAANDALIZI YA UANGALIZI WA UCHAGUZI NCHINI BOTSWANA

October 21, 2024 Add Comment

 

Mkuu wa Misheni ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ya Uangalizi wa Uchaguzi Mkuu nchini Botswana (SEOM) Mhe. Mizengo Pinda akipokea taarifa ya mandalizi ya uangalizi wa uchaguzi mkuu wa Botswana kutoka kwa Sekretarieti ya SADC jijini Gaborone Botswana tarehe 20 Oktoba, 2024

Mkuu wa Misheni ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ya Uangalizi wa Uchaguzi Mkuu nchini Botswana (SEOM) Mhe. Mizengo Pinda akiwa na wajumbe wa timu ya uangalizi wa uchaguzi mkuu wa Botswana wakipokea taarifa ya maadalizi ya uangalizi wa uchaguzi kutoka kwa Sekretarieti ya SADC jijini Gaborone Botswana tarehe 20 Oktoba, 2024
wajumbe wa Sekretarieti ya SADC waliposhirikikikao cha kuwasilisha kwa taarifa ya maandalizi ya uangalizi ya uchaguzi mkuu wa Botswana kwa Mkuu wa Misheni ya SADC ya kuangalia uchaguzi mkuu wa Botswana Mhe. Mizengo Pinda hayupo pichani


Mkuu wa Misheni ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ya Uangalizi wa Uchaguzi Mkuu nchini Botswana (SEOM) Mhe. Mizengo Pinda ameongoza kikao cha Asasi ya Siasa Ulinzi na Usalama ya SADC TROIKA kupitia taarifa ya maandalizi ya Misheni hiyo nchini Botswana.

Kikao hicho kilichofanyika jijini Gaborone tarehe 20 Oktoba 2024 na kilihudhuriwa na wajumbe kutoka Tanzania ambayo ni Mwenyekiti wa Organ; Malawi  Mwenyekiti ajaye na Zambia ambayo ni Mwenyekiti aliyemaliza muda wake na Sekretarieti ya SADC.

Kikao kimepokea na kujadili taarifa iliyowasilishwa na Sekretarieti ya SADC kuhusu maandalizi ya Uangalizi wa Uchaguzi Mkuu wa Botswana utakaofanyika tarehe 30 Oktoba,2024.

Sekretarieti pia iliwasilisha mgawanyo wa majukumu kwa timu mbalimbali za misheni hiyo katika uchaguzi huo.

Katika kikao hicho Mhe. Pinda amesema ni matumaini yake kuwa maandalizi na Mipango ya Uangalizi itaenda sawa na hivyo kuifanya SEOM kutekeleza jukumu lake kwa tija na ufanisi.

Amesema pia SEOM ıkifanya kazi yake ya uangalizi na kuandaa taarifa za Uangalizi wa uchaguzi huo itasaidia nchi husika kufanya maboresho katika mifumo yake ya demokrasia na hivyo kuwa sehemu ya kukuza demokrasia katika nchi wanachama.

VIONGOZI MLIYOPEWA DHAMANA MSIBAGUE WATU KATIKA KUWATUMIKIA - GAVU

October 18, 2024 Add Comment

Katibu Wa Idara ya Oganazesheni CCM Ndg Issa Ussi Gavu akizungumza wakati wa kufungua kongamano la maombi ya kuliombea Taifa lililoandaliwa na Kanisa la Ufunuo lililopo Ubungo Dar Es Salaam (Picha na Fahadi Siraji)

Katibu Wa Idara ya Oganazesheni CCM Ndg Issa Ussi Gavu amewataka viongozi wa Serikali waliyopewa dhamana ya uongozi kuwatumikia wananchi bila kuwabagua.


Gavu aliyasema hayo hapo jana wakati alipofungua kongamano la kuliombea Taifa lililoandaliwa na Kanisa la Ufunuo lililopo Ubungo jijini Dar Es Salaam.


“Niwahakikishie tutaendelea kumuomba Mwenyezimungu aendelee kuwakumbusha na kuwasimamia viongozi wetu wa Serikali na kila aliyepewa dhamana, kwamba dhamana waliyopewa ni ya kuwatumikia watanzania waliyo wote, dini zote,rangi zote,makabila yote na jinsia zote” alisema.


Aidha amesema Viongozi wa dini ni watu muhimu sana kwani wamekuwa wakiliombea taifa pasipo wengine kufahamu .


"Lakini katika kila jambo unaloliona duniani wapo Viongozi wanaochukua jukumu kwa niaba ya wengine kwenye hili jukumu la kumuomba na kumlilia Mungu niwaombe Viongozi wetu wa kiroho Msichoke endeleeni kuliombea Taifa” alisema na kuongeza


“Maombi yenu Mungu akiyapokea ndio baraka na neema kwa Taifa lenu na Viongozi wetu wa kisiasa Viongozi wetu wa Serikali, Msichoke kutukumbusha pale ambapo panaondoka amani, upendo na utulivu hata shughuli za Ibada hazitapata nafasi ya kuwapa watu Muda wa kuabudu kwa utulivu".


Kongamano hilo ni la siku tano ambapo waumini zaidi ya elfu tatu wanakutana kuliombea taifa.




UBIA WA TWIGA WAONGOZA MCHANGO WA TASNIA YA UCHIMBAJI MADINI KATIKA UCHUMI WA TANZANIA

October 07, 2024 Add Comment

 

Rais na Afisa Mtendaji Mkuu wa Barrick, Mark Bristow akiongea katika mkutano na waandishi wa habari ,viongozi wa serikali na wadau mbalimbali uliofanyika katika mgodi wa bulyanhulu jana,(Kushoto) ni Naibu Waziri wa Madini, Dk.Steven Kiruswa na (kulia) ni Meneja wa Barrick nchini,Melkiory Ngido.
Naibu Waziri wa Madini, Dk.Steven Kiruswa akiongea katika mkutano huo.
Mbunge wa Nyang'hwale,Mh.Hussein Nasor Amar akiongea katika mkutano huo.

Na Mwandishi Wetu.

Naibu Waziri wa Madini, Dk.Steven Kiruswa, amesema ubia kati ya Kampuni ya Dhahabu ya Barrick na Serikali ya Tanzania ni kielelezo cha mafanikio ya ushirikiano wa Serikali na sekta binafsi kwa kuwa unazidi kuleta manufaa nchini na ameomgeza kuwa Serikali itaendelea kuwalinda wawekezaji wenye kuleta mapinduzi chanya katika kukuza uchumi wa nchi .

Akiongea na katika mkutano wa waandishi wa habari wa kupokea taarifa ya utendaji wa migodi ya Barrick na Twiga uliojumuisha wadau mbalimbali uliofanyika katika mgodi wa Bulyanhulu, Dk.Kiruswa, alisema ubia huu umekuwa mfano wa kuigwa kwa kuwa migodi yote inayoendeshwa na Barrick uendeshaji wake umekuwa wa uwazi pia mafanikio yake yanaonekana kutokana na kutoa mchango mkubwa kwa Serikali kupitia kodi mbalimbali, kufanikisha miradi ya kijamii kupitia fedha za uwajibikaji kwa jamii (CSR), kupanua wigo kwa ajira kwa Watanzania na kunufaisha wananchi kupitia utekelezwaji wa sera ya maudhui ya ndani (Local content kwa ufanisi mkubwa) sambamba na uwekezaji katika matumizi ya teknolojia za kisasa cha uchimbaji.

Alisema Serikali haitafumbia macho vitendo vya kuwahujumu wawekezaji wanaofanya vizuri katika uwekezaji wao nchini kwa lengo la kuwakatisha tamaa na kurudisha nyuma mkakati wa Serikali wa kukuza uwekezaji nchini yakiwemo mashirikika yasio ya Kiserikali ya nje ya nchi ambayo yamekuwa yakijifanya kiranja wa kutetea haki za binadamu na kusambaza taarifa za uwongo dhidi ya wawekezaji wa hapa nchini zikijifanya kuwatetea watanzania wanyonge wakati zinatafuta mianya ya kujinufaisha kupitia mgongo wa watanzania.

“Serikali ya Tanzania iko imara na madhubuti katika kusimamia wawekezaji kuhakikisha wanafuata kanuni na sheria zake kupitia taasisi zake mbalimbali zilizoanzishwa kisheria ambazo zinafanya vizuri na wanaokiuka sheria wanachukuliwa sheria na kupewa maelekeza na miongozo hivyo hayo mashiriki yasio ya Kiserikali yaache kuchafua taswira ya nchi kama ambavyo yamekuwa yakifanya kwa muda mrefu kupitia mgodi wa North Mara uliopo wilayani Tarime mkoani Mara” ,alisema.

Aliongeza kuwa kutokana na maombi yaliyokuwa yakitolewa kwa Serikali na viongozi wa wananchi katika maeneo ya migodi ya kuwatengea wachimbaji wadogo maeneo na kuyataka makampuni makubwa yenye teknolojia ya uchimbaji kuwasaidia Serikali imeanza kuyafanyia kazi na imeanza mazungumzo na makampuni makubwa kupitia Wizara ya Madini na taasisi zake zinazosimamia uchimbaji wa madini.

Ubia huo unachangia 51% ya mapato ya Serikali yanayotokana na tasnia ya uchimbaji madini, kwa mujibu wa ripoti ya hivi karibuni ya Mpango wa Uwazi wa Tasnia ya Uchimbaji Madini Tanzania (TEITI). Ubia wa Twiga unajumuisha migodi ya dhahabu ya North Mara na Bulyanhulu.

Migodi yote miwili pia iliongoza katika utendaji wa kiusalama wa tasnia hiyo, huku Bulyanhulu ikishinda Tuzo ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya mwaka huu wakati North Mara ikitajwa na Mamlaka ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya Tanzania (OSHA) kuwa kampuni bora katika kuwahudumia wafanyakazi wenye mahitaji maalumu.

Rais na Afisa Mtendaji Mkuu wa Barrick, Mark Bristow, alisema katika mkutano huo kuwa utafutaji wa madini unaoendelea katika maeneo yaliyotumika na kuachwa karibu na migodi yake ya Bulyanhulu na North Mara unaendelea. Utafiti huo umebainisha fursa zaidi za kuzihuisha na kuzipanua hifadhi za madini ambapo madini yatakwisha au kupungua, jambo litakalosaidia zaidi katika kuongeza uhai na unyumbufu wa migodi hiyo. Aidha, maendeleo mazuri yameshapatikana katika kuyabainisha maeneo mapya ambapo hapakuwahi kuwa na shughuli za uchimbaji madini, yenye uwezo wa kuongeza migodi mipya kwenye kampuni hiyo.

Aidha, Bristow alisema mpango wa Barrick na Twiga wa Kusongesha Mbele Mustakabali wa Elimu umekamilisha awamu yake ya kwanza, ambapo Barrick ilifadhili upanuzi wa miundombinu ya shule zipatazo 64, yenye thamani ya dola milioni 10, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa vyumba vya madarasa vipatavyo 396, mabweni yapatayo 97 na majengo ya maliwato yapatayo 600. Awamu ya pili ya mpango huo umepangwa kuanza katika robo ya nne ya mwaka huu kwa uwekezaji mwingine wa dola milioni 10 ambao utafuatiwa na awamu ya tatu ya dola milioni 10.

Wakati huohuo, Chuo cha Barrick, kilichozinduliwa mwanzoni mwa mwaka na Waziri wa Madini kwenye mgodi uliofungwa wa Buzwagi na ambao hivi sasa ni eneo maalum la uzalishaji (SEZ), tayari kimetoa mafunzo kwa mafomeni, wasimamizi na warakibu zaidi ya 1,000 kutoka katika nchi za Afrika na Mashariki ya Kati. Chuo hiki kiko mbioni kufikia lengo lake la kutoa mafunzo kwa zaidi ya watu 2,000 mwaka huu.

Bristow alisema kulingana na dhamira ya uwazi ya Barrick, kampuni hiyo iliwasilisha taarifa za hivi karibuni za mfululizo wa tuhuma za ukiukwaji wa haki za binadamu zilizokuwa zinatolewa dhidi ya Mgodi wa North Mara kwenye Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Tanzania (CHRGG). Baada ya kutembelea mgodi huo na maeneo ya jirani na kufanya uchunguzi wa kina, tume hiyo ilitoa taarifa iliyothibitisha kwamba hapakuwa na ushahidi wa ukiukwaji wa haki za binadamu katika mgodi wa North Mara na hivyo kuuondolea mgodi huo tuhuma hizo zilizotolewa na baadhi ya mashirika yasiyo yasiyo ya kiserikali ya nchi za nje.

Viongozi mbalimbali wa Serikali kutoka wilaya za Kahama, Msalala na Nyang’hwale waliohudhuria mkutano huo, walipongeza mafanikio makubwa yanayoendelea kupatikana kupitia uwekezaji wa Barrick hususani katika kufanikisha miradi mikubwa ya kijamii kupia fedha za uwajibikaji kwa jamii kwenye sekta ya afya na elimu.
-- Cathbert Angelo Kajuna, Founder and Mananging Director Kajunason Blog, P.O Box 6482, Dar es Salaam. Tel: +255 787 999 774 Alt: +255 735 997 777 www.kajunason.blogspot.com "Everything is Possible Through Peace & Stability'' >>> DO YOUR PART TO PREVENT COVID-19: • Wash your hands frequently • Avoid touching face • Cover coughs and sneezes • Disinfect surfaces regularly • Limit handshaking • Consider postponing travel plans • Avoid large gatherings