Showing posts with label habari. Show all posts
Showing posts with label habari. Show all posts

KAMISHNA WA UMEME NA NISHATI JADIDIFU AFANYA ZIARA YA UKAGUZI WA MIRADI YA UMEME JIJINI DAR ES SALAAM

June 14, 2025 Add Comment


▪️Aridhishwa na hatua ya utekelezaji wa miradi


▪️Awataka wakandarasi kuzingatia viwango na TANESCO kuongeza usimamizi ili kuepuka ongezeko la gharama


▪️Aisisitiza dhamira ya Serikali ya kuhakikisha Watanzania wanapata umeme wa uhakika


Na. Agnes Njaala, Dar es Salaam


Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu kutoka Wizara ya Nishati, Mhandisi Innocent Luoga, tarehe 12 Juni 2025, amefanya ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme ya Gridi Imara inayoendelea katika Jiji la Dar es Salaam, na kutoa maelekezo muhimu kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) pamoja na wakandarasi wanaotekeleza miradi hiyo.


Miradi hiyo inalenga kuimarisha upatikanaji wa umeme kwa kuboresha miundombinu ya usafirishaji na usambazaji wa umeme nchini, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuhakikisha huduma bora na ya uhakika kwa wananchi.

Akizungumza mara baada ya ziara hiyo, Kamishna amesema ameridhishwa na hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa miradi hiyo, licha ya changamoto mbalimbali za kimazingira, na kusisitiza umuhimu wa kuendelea na jitihada za kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati.


“Nimeridhishwa na hatua zilizofikiwa, lakini nimeagiza wakandarasi waharakishe kazi, vifaa vipatikane kwa wakati, na viwango vya kazi vizingatiwe ili miradi hii itoe matokeo yaliyokusudiwa kwa wananchi,” amesisitiza Mhandisi Luoga.


Akifafanua amebainisha kuwa miradi hiyo ya kimkakati, inayotekelezwa na TANESCO kwa ufadhili wa Serikali, inalenga kuboresha huduma ya umeme kwa wakazi wa Dar es Salaam na maeneo mengine nchini. Aidha, ametoa pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuidhinisha rasilimali fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo muhimu.


Katika maagizo yake, ameitaka TANESCO kuongeza usimamizi kwa wakandarasi katika kuhakikisha upatikanaji wa vifaa kwa wakati, na kusimamia ubora wa kazi ili kuepuka ongezeko la gharama zitokanazo na ucheleweshaji.

Kwa upande wake, Mhandisi Abdallah Chikoyo, Meneja wa Miradi ya Kuzalisha Umeme TANESCO aliyemwakilisha Mkurugenzi Mtendaji , ameahidi kuongeza juhudi katika usimamizi wa miradi na kuweka mipango kazi inayotekelezeka kwa wakati.


“Tumejipanga kuongeza nguvu katika usimamizi wa miradi hii, na kuimarisha ushirikiano na wadau wa maendeleo ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati na kwa ufanisi, tukitimiza wajibu wetu katika kuboresha huduma ya umeme nchini,” amesema Mhandisi Chikoyo.


Ziara hiyo ilikuwa sehemu ya utekelezaji wa wajibu wa Serikali katika kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ambapo Kamishna Luoga alitembelea vituo vya umeme vya Ubungo I, Mabibo, Kinyerezi na Gongo la Mboto. Katika vituo hivyo, kazi ya ufungaji wa mashine umba zenye uwezo mkubwa  (transformers) inaendelea kwa kasi ya kuridhisha, ikiwa ni hatua ya kuimarisha miundombinu ya usambazaji wa umeme jijini Dar es Salaam.

MWENGE WA UHURU 2025 KUPITIA MIRADI YENYE THAMANI YA BILIONI 3 WILAYA YA TANGA

June 14, 2025 Add Comment










Na Paskal Mbunga,TANGA

MWENGE wa Uhuru unatarajiwa kuwasili katika wilaya ya Tanga Jumatatu June 16 mwaka huu na upitia katika miradi saba ya maendeleo yenye thamani ya Sh.Bilioni 3,058,289,671.99.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati akitoa taarifa za ujio wa Mwenge huo,Mkuu wa wilaya ya Tanga Dadi Kolimba alisema wataupokea ukitokea wilayani Mkinga katika uwanja wa shule ya Msingi Mabambani Mtaa wa Mpirani Kata ya Chongoleani.

Aliitaja miradi ambayo itapitiwa na Mwenge ni ujenzi wa madarasa 4 ya Ghorofa ,matundu 13 ya vyoo na ofisi shule ya Msingi Mbuyuni yenye thamani ya Milioni 388,769,596.80 na Ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa ya awali ya mfano shule ya msingi Mwakidila yenye thamani ya Milioni 70,100,000.00.

Mkuu huyo alisema pia miradi mingine ni ujenzi wa ofisi ya mtendaji kata ya Tongoni uliogharimu kiasi cha sh.Milioni 85,000,000.00,ujenzi wa barabara ya Sahare awamu ya kwanza na ya pili yenye urefu wa mita 600 kwa kiwango cha lami uliogharimu Sh.Milioni 489,606,700.00.

“Lakini pia Mwenge utapita katika ujenzi wa Jengo la X-Ray kituo cha Afya Makorora wenye thamani ya Sh.Milioni 84,721,640.00 pamoja na mradi wa ufungaji wa dira za maji za malipo ya kabla awamu ya kwanza wenye thamani ya Sh. 1,872,091,735.00 “Alisema.

Hata hivyo alisema kwamba mradi mwengine ambao utapitiwa na mwenge ni mradi wa kikundi cha vijana cha kutengeneza gypsum wenye thamani ya Sh.Milioni 68,000,000.00

Alisema mbali na miradi hiyo saba mwenge wa uhuru utakagua shughuli za maandalizi ya uchaguzi,kongamano la vijana pamoja na maswala mtambuka.

Mwisho.

GCLA YAWAPA HAMASA VIJANA KUCHANGAMKIA MASOMO YA SAYANSI

June 12, 2025 Add Comment
NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

MAMLAKA ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali imetoa zawadi kwa kuwatunuku vyeti wanafunzi wahitimu 48 na walimu 8 waliofanya vizuri zaidi kwenye masomo ya sayansi kidato cha nne 2023 na kidato cha sita 2024 kwa kutambua bidii na kujituma kwao katika kusoma masomo hayo.

DKT.NCHIMBI AKIFUATILIA BAJETI KUU YA SERIKALI

June 12, 2025 Add Comment
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, akifuatilia Hotuba ya Mapendekezo ya Serikali kuhusu Bajeti Kuu ya Mwaka wa Fedha 2025/2026 akiwa ofisini kwake, katika Ofisi za Makao Makuu ya CCM jijini Dodoma, leo Alhamisi, tarehe 12 Juni 2025. Pamoja naye ni maofisa waandamizi wa CCM Makao Makuu.

WAZIRI DKT.NCHEMBA: SH.TRILION 56.49 KUTEKEKEZA BAJETI 2025/2026

June 12, 2025 Add Comment






Na Saidina Msangi, WF, Dodoma



Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), anamewasilisha Hotuba ya Bajeti Kuu ya Serikali, ambapo ameliomba Bunge ridhaa ya kukusanya na kutumia jumla ya shilingi trilioni 56.49 kwa Mwaka wa Fedha 2025/26.



Dkt. Nchemba ameomba ridhaa hiyo bungeni jijini Dodoma, wakati akiwasilisha mapendekezo ya Serikali kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2025/26, ambapo bajeti hiyo inatarajiwa kugharamiwa na mapato ya ndani ya shilingi trilioni 40.47, misaada shilingi trilioni 1.07 na mikopo ya shilingi trilioni 14.95.



‘‘Kati ya mapato ya ndani yanayotarajiwa, mapato ya kodi ni shilingi trilioni 32.31, mapato yasiyo ya kodi shilingi trilioni 6.48, na mapato ya Mamlaka za Serikali za Mitaa shilingi trilioni 1.68. Aidha, mikopo inajumuisha shilingi trilioni 6.27 kutoka vyanzo vya ndani na shilingi trilioni 8.68 kutoka vyanzo vya nje’’, alifafanua Mhe. Nchemba.



Alieleza kuwa makadirio ya matumizi ya Serikali ya shilingi trilioni 56.49 kwa mwaka 2025/26 yanajumuisha Stahiki za watumishi na michango ya pensheni (Serikali Kuu) shilingi trilioni 9.17 pamoja na ununuzi wa bidhaa na huduma shilingi trilioni 5.58









Aliongeza kuwa matumizi mengine ni malipo ya riba za mikopo shilingi trilioni 6.49; na ruzuku kwa taasisi za Serikali, mashirika ya umma na Mamlaka za Serikali za Mitaa shilingi trilioni 22.17 na shilingi trilioni 7.72 kugharamia malipo ya mtaji kwa deni la ndani na nje.



‘‘Katika Mwaka wa Fedha 2025/26 Serikali inatarajia kuongeza kasi ya ukuaji wa Pato Halisi la Taifa kufikia asilimia 6.0 mwaka 2025 kutoka ukuaji wa asilimia 5.5 mwaka 2024, kuendelea kudhibiti kasi ya mfumuko wa bei na kuhakikisha kuwa unabaki kwenye wigo wa tarakimu moja ya wastani wa asilimia kati ya 3.0 - 5.0 katika muda wa kati’’, alifafanua Mhe. Nchemba.



Aidha, Dkt. Nchemba alisema Serikali inatarajia kuongeza Mapato ya ndani kufikia asilimia 16.7 ya Pato la Taifa mwaka 2025/26 ikilinganishwa na asilimia 15.8 mwaka 2024/25 na mapato ya kodi kufikia asilimia 13.3 ya Pato la Taifa mwaka 2025/26 kutoka asilimia 12.8 mwaka 2024/25.



Dkt. Nchemba alisema vipaumbele vya bajeti ya mwaka 2025/26 ni pamoja na kuendelea kutekeleza na kukamilisha miradi ya kielelezo na ile ya kimkakati, kuimarisha sekta za uzalishaji zenye matokeo chanya katika kukuza uchumi, kuimarisha rasilimali watu hususan katika sekta za huduma za jamii na kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji nchini ili kuvutia ushiriki wa sekta binafsi katika shughuli mbalimbali za kiuchumi.



‘‘Maeneo mengine mahsusi ya vipaumbele ni pamoja na ugharamiaji wa Deni la Serikali; mishahara na stahiki za watumishi wa umma, pamoja na ujenzi na ukarabati wa viwanja vya michezo kwa ajili ya maandalizi ya michuano ya AFCON 2027. Aidha, nipende kuwafahamisha Watanzania kuwa Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 tutaugharamia kwa fedha zetu za ndani’’, alisema Mhe. Nchemba.



Aidha, Dkt. Nchemba alisema katika mwaka 2025/26, Serikali itaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha ukusanyaji wa mapato ikiwemo kuendelea kuhamasisha umma kuhusu kutoa na kudai risiti za malipo za kielektroniki za EFD na kuboresha utaratibu wa ukusanyaji wa mapato kutoka vyanzo vinavyosimamiwa na mamlaka za udhibiti.



‘‘Serikali itaendelea kuboresha Mfumo wa TAUSI ili kuhakikisha vyanzo vyote vya mapato vya Mamlaka za Serikali za Mitaa vinajumuishwa katika mfumo huo, kuongeza ufanisi wa mifumo ya ukusanyaji wa mapato ya mashirika, taasisi za umma na wakala za Serikali ili kuhakikisha gawio na michango stahiki inawasilishwa kwa wakati na kuendelea kutekeleza Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji (MKUMBI)’’, alifafanua Mhe. Nchemba.



MABORESHO YA MIFUMO YA KODI



Dkt. Nchemba alisema Serikali inalenga kufanya maboresho ya mfumo wa kodi, ikiwemo baadhi ya viwango vya kodi, tozo na ada zinazotozwa chini ya sheria mbalimbali pamoja na kuboresha taratibu za ukusanyaji na usimamizi wa mapato ya Serikali ili kuwa na mfumo wa kodi ambao ni tulivu na wa kutabirika unaolenga kuchochea shughuli mbalimbali za uzalishaji mali ndani ya nchi.



Mapendekezo ya kurekebisha mfumo wa kodi kwa mwaka 2025/26 yanatarajiwa kuiongezea Serikali jumla ya shilingi milioni 4,260,023.77 ambapo baadhi ya mapendekezo hayo ni kusamehe kodi ya ongezeko la thamani kwenye viuatilifu vinavyotambulika kwa HS Codes 3808.61.00, 3808.62.00 na 3808.69.00, ili kuwapa unafuu wakulima ya kupata dawa za kuua wadudu mashambani na hivyo kuongeza uzalishaji wa mazao nchini.



Kusamehe kodi ya ongezeko la thamani kwenye miamala ya ununuzi wa bima mtawanyo inayofanywa baina ya kampuni za bima na zile za bima mtawanyo ili kuongeza ushindani wa kampuni za ndani, kukuza Sekta ya Bima na kuhamasisha matumizi ya bima katika kukabiliana na majanga nchini.



Kutoza kodi ya ongezeko la thamani kwa kiwango cha asilimia 0 kwenye bidhaa za nguo zinazotengenezwa kwa kutumia pamba inayolimwa nchini kwa kipindi cha mwaka mmoja ili kuleta unafuu kwa wakulima wa pamba na viwanda vinavyotengeneza nguo nchini.



Kutoza kodi ya ongezeko la thamani kwa kiwango cha asilimia 0 kwenye mbolea inayozalishwa ndani ya nchi kwa kipindi cha miaka mitatu ili kuleta unafuu kwa wakulima na walaji hasa katika kipindi hiki ambacho dunia imetoka kwenye mdororo wa kiuchumi duniani.



Kusamehe kodi ya ongezeko la thamani kwenye mafuta ya kula yanayozalishwa ndani ya nchi kwa kutumia mbegu zinazozalishwa nchini kwa muda wa mwaka mmoja ili kuendelea kuleta unafuu wa bei ya mafuta ya kula nchini.



Kufuta Msamaha wa kodi ya ongezeko la thamani unaotolewa kwenye ununuaji na uingizaji wa gaming supply. Hatua hii inalenga kuleta usawa katika utozaji wa kodi kwa kuwa michezo mingine kama vile mpira wa miguu ipo katika wigo wa utozaji wa kodi ya ongezeko la thamani. Hatua hii inatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 322,022.5.



Kuweka sharti la msamaha wa kodi ya ongezeko la thamani kwenye matairi ya trekta yanayotumika kwenye shughuli za kilimo yanayotambulika kwa HS Code 4011.70.00; dam liners zinazotambulika kwa Heading 39.20; forks (HS Code 8201.90.00); reki (HS Code 8201.30.00); na shoka (HS Code 8201.40.00) kutolewa baada ya kupata ridhaa ya Waziri mwenye dhamana ya masuala ya kilimo.



Kufuta msamaha wa kodi ya ongezeko la thamani kwenye lami zinazotambulika kwa HS Code 2713.20.00 na 2715.00.00 ili kuendana na azma ya Serikali ya kupunguza misamaha isiyo na tija ili kulinda mapato ya Serikali na kupunguza matumizi yanayohusiana na utoaji wa misamaha ya kodi. Hatua hii inatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 85,606.2.



Kusamehe kodi ya ongezeko la thamani kwenye magazeti yanayozalishwa nchini pekee ili kupunguza gharama za magazeti hayo na hivyo kuwezesha upatikanaji wa taarifa muhimu. Hatua hii inatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 1,274.4.



Kusamehe kodi ya ongezeko la thamani kwenye gesi asilia inayouzwa kwenda kwenye vituo vya kushindilia gesi kwa ajili ya matumizi ya magari ili kuweka unafuu kwa wawekezaji, kuvutia uwekezaji wa vituo vya kusambazia gesi asilia iliyosindikwa kwenye magari na kupunguza utegemezi wa mafuta na uzalishaji wa hewa ya ukaa.



Kusamehe kodi ya ongezeko la thamani kwenye matanki na mitungi ya gesi ya kupikia zinazotambulika kwa HS Code 7311.00.10 pamoja na mitambo ya kuondoa hewa ukaa yenye HS Code 8417.80.00 inayotumika katika uzalishaji wa mikaa mbadala. Hatua hii inalenga kupunguza gharama za upatikanaji wa bidhaa hizi ili kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.



Kujumuisha masoko mtandao na huduma za masoko za kimtandao kwenye wigo wa tafsiri ya neno wakala wa huduma za kimtandao ili kutanua wigo wa kodi kwa kuweka ufafanuzi utakaopelekea kutatua changamoto zilizopo katika utozaji na usimamizi wa kodi ambapo tafsiri iliyopo sasa haijumuishi huduma hizo katika utozaji kodi. Hatua hii inatarajia kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 116,073.4.



Kuweka unafuu wa kutoza kodi ya mapato kwa kundi la pikipiki ya miguu miwili, pikipiki ya miguu mitatu (Bajaji) na magari ya kubeba mizigo yenye uzito usiozidi Kilogramu 500 ikiwemo Guta kwa kuweka utaratibu mpya wa kukadiria kodi ya mapato kwenye vyombo hivyo. Maboresho ya viwango vya kodi elekezi yanalenga kuweka unafuu wa kodi kwa kundi husika na hivyo kurahisisha utekelezaji wa sheria.



Kupunguza tozo ya ushuru wa huduma kutoka utaratibu wa sasa wa kutoza kiwango kisichozidi asilimia 0.3 ya pato ghafi kwenda kiwango mfuto cha asilimia 0.25 ya pato ghafi. Lengo la hatua hii ni kupunguza gharama za ufanyaji biashara na uwekezaji nchini pamoja na kuendana na masharti ya Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara (MKUMBI).



Kupunguza kiwango cha ada ya ushuru wa hoteli (hotel levy) kutoka asilimia 10 hadi asilimia 2. Lengo la hatua hii ni kupunguza gharama za ufanyaji biashara na uwekezaji nchini.



Kufuta ada za upakiaji (loading) na upakuaji (offloading) zinazotozwa na Mamlaka za Serikali za Mitaa zinazohusiana na usafirishaji wa mizigo. Lengo la hatua hii ni kupunguza gharama za ufanyaji biashara na uwekezaji nchini ili kuendana na masharti ya Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara nchini (MKUMBI).



Kupunguza ada ya usajili wa pikipiki za biashara kutoka shilingi 340,000 hadi shilingi 170,000 kwa miaka mitatu ambapo ada husika italipwa wakati wa usajili wa awali pekee. Kupunguza ada ya leseni ya uendeshaji wa pikipiki, bajaji na guta kutoka shilingi 70,000 hadi shilingi 30,000.



KUGHARAMIA BIMA YA AFYA



Serikali inapendekeza kuanzisha vyanzo mbadala vya mapato ili kupunguza nakisi ya kibajeti kwa kufanya marekebisho katika sheria mbalimbali. Aidha inapendekezwa asilimia 70 ya mapato yatakayoongezeka ipelekwe kwenye Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti UKIMWI (ATF) na asilimia 30 ipelekwe kwenye Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kwa Wote. Marekebisho hayo ni kama ifuatavyo:



Kufanya marekebisho ya Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, SURA 147 ili kuongeza ushuru wa bidhaa kwenye vinywaji vya kilevi vinavyozalishwa na vinavyoingizwa kutoka nje ya nchi kama ifuatavyo: shilingi 20 kwa bia zinazotambulika kwa Heading 22.03; shilingi 30 kwa mvinyo unaotambulika kwa Heading 22.04, 22.05, na 22.06; shilingi 50 kwa spirits na vinywaji vingine vinavyotambulika kwa Heading 22.08.



Kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, SURA 147 ili kuongeza kiwango cha ushuru wa bidhaa kwenye huduma za mawasiliano ya kielektroniki kutoka asilimia 17 hadi asilimia 17.5.



Kufanya marekebisho ya Sheria ya Ushuru wa Barabara na Mafuta, SURA 220 ili kutoza kiasi cha shilingi 10 kwa kila lita ya mafuta ya Petroli, Dizeli na Mafuta ya Taa pamoja na kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Madini, SURA 123 ili kutoza kiwango cha asilimia 0.1 kwenye thamani ya soko ya madini.



Kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Michezo ya Kubahatisha, SURA 41 ili kuongeza kiwango cha kodi kwenye zawadi ya ushindi (Winning tax) kwenye michezo ya kubashiri matokeo (sports betting) kutoka asilimia 10 hadi asilimia 15; na kwenye michezo ya kasino ya ardhini (land based casino) kutoka asilimia 12 hadi asilimia 15.



Kutoza magari na mashine (heavy machines) zinazoingizwa kutoka nje ya nchi kama ifuatavyo: Shilingi 50,000 kwa magari yenye ukubwa wa injini (CC) kati ya 0 -1000; Shilingi 100,000 kwa magari yenye ukubwa wa injini (CC) kuanzia 1001-1500; Shilingi 150,000 kwa magari yenye ukubwa wa injini (CC) kuanzia 1501-2500; Shilingi 200,000 kwa magari yenye ukubwa wa injini (CC) kuanzia 2501 na zaidi; Shilingi 250,000 kwa mashine (Excavators, Bulldozers, Fork Lifts) zenye Heading 84.29 na 84.27.



Kutoza shilingi 500 kwa kila tiketi inayotolewa na mtoa huduma za usafirishaji kwa njia ya treni na kutoza shilingi 1000 kwa kila tiketi inayotolewa na mtoa huduma za usafirishaji kwa njia ya anga. Hatua hizi kwa pamoja zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa shilingi milioni 586,404.9.



KUBORESHA MAZINGIRA YA BIASHARA



Ili kuiwezesha nchi kuwa na sera bora za biashara na kuweka mazingira mazuri ya ufanyaji biashara baina ya wazawa na wageni, Serikali inatarajia kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Utoaji wa Leseni za Biashara ikiwemo:



Kufuta kifungu cha 3(4) kinachozipa nguvu mamlaka za utoaji wa leseni za biashara kufunga biashara pale ambapo wafanyabiashara wamekiuka masharti ya Sheria husika. Lengo la hatua hii ni kuwaondolea kero wafanyabiashara na pia kutekeleza maelekezo ya Serikali ya kutofunga biashara.



Kuongeza kifungu cha 8(7) ambacho kinampa mamlaka Waziri mwenye dhamana na masuala ya biashara kuainisha shughuli za kibiashara ambazo hazipaswi kufanywa na wageni. Utaratibu wa utekelezaji wa kifungu hiki utafanywa kupitia Amri (Order) itakayotolewa na Waziri ambayo itakua na orodha ya shughuli za kibiashara ambazo hazipaswi kufanywa na wageni.



Dkt. Nchemba alisema bajeti hii inaendeleza na kukamilisha utekelezaji wa miradi, Kuchochea uchumi shindani na shirikishi, kuimarisha uzalishaji wa bidhaa viwandani na utoaji huduma, kukuza uwekezaji na biashara, kuchochea maendeleo ya watu na kuendeleza rasilimali watu ili kuhakikisha ufikiwaji wa malengo ya Dira 2025.