Showing posts with label habari. Show all posts
Showing posts with label habari. Show all posts

BALOZI DK.NCHIMBI AMWAKILISHA RAIS SAMIA KUMUAGA HAYATI SONGAMBELE MKOANI RUVUMA

June 02, 2025 Add Comment



Na Mwandishi Wetu,Songea

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, amemwakilisha Rais na Mwenyekiti wa CCM Taifa ,Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika shughuli ya kuaga mwili wa Hayati Alhaj Mustafa Mohamed Songambele iliyofanyika nyumbani kwa marehemu eneo la Mahenge, mjini Songea mkoani Ruvuma.

Akizungumza katika shughuli hiyo, Dkt. Nchimbi amemuelezea Hayati Songambele kama mmoja wa mashujaa waliotoa mchango mkubwa katika kupigania uhuru wa Tanzania na kujenga misingi ya taifa jipya baada ya ukoloni.


Dk.Nchimbi amesema Hayati Songambele alikuwa miongoni mwa waanzilishi wa Chama cha TANU na alishiriki kikamilifu katika harakati za kujenga taifa huru na lenye mshikamano.


"Tuendelee kujifunza kutoka kwa wazee hawa ambao wamefariki wakiona amani na upendo wa Tanzania ukiendelea, heshima pekee tunayoweza kuwapa ni kuendeleza mshikamano, amani na maendeleo ya nchi yetu…


“Tuendelee kujua sisi ni Taifa moja, tuna wajibu wa kupendana na kujiepusha na vishawishi vyote ambavyo vinaweza vikavuruga amani na kuvunja mtangamano wa kitaifa," alisema Dkt. Nchimbi.


Dkt. Nchimbi aliongeza kuwa Rais Dkt. Samia ameguswa sana na msiba huo, akimwelezea Hayati Songambele kama kiongozi mwenye moyo wa kipekee wa kulitumikia taifa kwa hali na mali, na kwamba wananchi wa Ruvuma wana kila sababu ya kujivunia mchango wake mkubwa.


Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas Ahmed, amesema kifo cha Mzee Songambele ni pigo kubwa kwa Taifa, akieleza kuwa marehemu alikuwa ni hazina ya busara na kumbukumbu muhimu ya historia ya Tanzania.


"Hakuwa tu kiongozi bali alikuwa taa na mwelekeo katika giza la ukoloni, aliyesimama kidete kwa ujasiri, hekima, na moyo wa kizalendo katika kuijenga Tanzania mpya. Alisimama kwa haki, kupitia juhudi zake na viongozi wenzake wa wakati huo, tunauona leo mwanga wa uhuru, umoja, na amani uliodumu kwa zaidi ya nusu karne," alisema Kanali Ahmed.


Akizungumza kwa niaba ya familia, Mtoto wa Hayati Songambele, Rajab Songambele amesema wataendelea kuyaenzi na kuyatekeleza mema yote waliyofundishwa na Mzee wao ili yadumu kwa vizazi vijavyo.

Hayati Alhaj Mustafa Mohamed Songambele alikuwa ni mmoja wa waanzilishi wa Chama cha TANU akiwa miongoni mwa wanachama wa kwanza 30 wa chama hicho, na alipata kadi ya uanachama namba 27.

Alizaliwa Mei 25, 1925 katika eneo la Bombambili, Manispaa ya Songea, mkoani Ruvuma na amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 100.






TASAC YATOA ELIMU YA UTUNZAJI MAZINGIRA DODOMA

June 02, 2025 Add Comment



Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania TASAC, leo tarehe 02 Juni, 2025 limetoa elimu ya utunzaji wa mazingira majini kwa wadau waliotembelea banda lao jijini Dodoma.

TASAC imetoa elimu hiyo kwa wadau na wananchi wa Dodoma katika Maadhimisho ya Wiki ya Mazingira Duniani 2025 yanayofanyika kuanzia tarehe 01 - 05 Juni, 2025 jijini humo. 



Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wataalamu wa TASAC wameeleza wananchi namna wanavyotekeleza majukumu yao ikiwa ni pamoja na jukumu la kusimamia na kudhibiti Usalama, Ulinzi na Utunzaji wa Mazingira pamoja na kupambana na umwagikaji wa mafuta majini.

Baadhi ya wadau waliotembelea banda hilo ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dkt. Ladislaus Chang’a ambapo amepongeza juhudi za TASAC katika kutumia taarifa za hali ya hewa zinazotolewa na TMA.

TASAC ni moja ya taasisi za umma zinazoshiriki maadhimisho hayo yenye kauli mbiu: “Mazingira Yetu na Tanzania Ijayo Tuwajibike Sasa, Dhibiti Matumizi ya Plastiki”. Kilele cha maadhimisho hayo ni tarehe 05 Juni 2025.

NSSF YAWATAKA WAAJIRI KULIPA MICHANGO KWA WAKATI WASISUBIRI MPAKA WAPELEKWE MAHAKAMANI

June 01, 2025 Add Comment




Na Oscar Assenga,Tanga

MFUKO wa Taifa wa Hifadhi za Jamii (NSSF) umewataka waajiri kuhakikisha wanalipa michango ya watumishi wao kwa wakati na wasisubiri mpaka wapelekwe mahakamani kutokana na kutokuiwasilisha .

Hayo yalisemwa leo na Meneja wa NSSF Mkoa wa Tanga Nuhu Mbaga katika maonyesho ya 11 ya Biashara na Utalii yanayoendelea katika eneo la Mwahako Jijini Tanga.

Ambapo alisema wanashiriki maonyesho hayo kwa lengo la kutoe elimu kwa wananchi juu ya mafao mbalimbali wanayoyatoa wanapojiunga nao.

Alisema kwamba wanatakiwa kulipa michango kwa sababu ipo kwa mujibu wa sheria na wasipofanya hivyo kifungu cha 72 wanaweza kukitumia kwa ajili ya wao kupelekwa mahakamani.

“Hivyo nitumie nafasi hii kuwataka waajiri tusisubiri mpaka mpelekwe mahakamani bali wahakikisheni mnatekeleza wajibu wenu kupeleka michango ya watumishi wenu”Alisema

Aidha alitumia wasaa huo kuwahamasisha wananchi waliojiajiri kufika kwenye banda lao kuweza kupata elimu ya kuweza kujiunga na kunufaika na mafao mbalimbali yanayotolewa kwenye mfuko huo ikiwemo ya kupata matibabu kama ilivyo kwa wengine

“Yote haya ni kutokana na sera nzuri ya awamu ya sita chiini ya Rais Dkt Samia Suluhu kwa sababu mtu akiwa na afya njema ataweza kwenda kujishughulisha na kufanya kazi ya kupata kipato cha mtu mmoja mmja na kuweza kujikwamua kiuchumi”Alisema

GCLA KANDA YA KATI YATOA MAFUNZO YA KUKABILIANA NA MAJANGA YA KEMIKALI KWA WAKAZI WA RUAHA MBUYUNI

May 31, 2025 Add Comment
Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilolo, Eston Kyando (aliyesimama) akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa makundi mbalimbali ya viongozi wa Kata ya Ruaha Mbuyuni juu ya namna ya kukabiliana na majanga ya kemikali ikiwemo ajali za magari yanayosafirisha kemikali. Mafunzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa shule ya msingi Mbuyuni A, Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa, Mei 30, 2025. Kulia ni Meneja wa Usajili wa Kemikali na Maabara za Kemia, Musa Kuzumila.