Showing posts with label habari. Show all posts
Showing posts with label habari. Show all posts

KAMPUNI YA SUNKING YAUNGA MKONO AGENDA YA RAIS SAMIA

March 28, 2025 Add Comment

 

Kampuni ya sola ya SunKing imeendelea kusogeza karibu zaidi huduma kwa wananchi baada ya kufungua duka jipya katika eneo la stendi ya Kona ya Kayenze jirani na Kisesa, Wilaya ya Magu mkoani Mwanza.

Akizungumza Ijumaa Machi 28, 2028 wakati wa hafla ya ufunguzi wa duka hilo, Msimamizi wa Biashara wa kampuni hiyo, Juma Mohamed amesema hadi sasa jumla ya maduka 65 yamezinduliwa kote nchini na mkakati ni kuendelea kufungua maduka zaidi ili kuwafikia wananchi wengi zaidi.

"Kazi yetu ni kubuni, kutengeneza na kusambaza mitambo inayotumia nishati ya jua (sola) yenye uhakika wa mwanga ang'avu na salama kwa matumizi ya wananchi. Hili litakuwa duka la nne Mwanza ambapo tayari tumefungua Buhongwa, Buzuruga, Buswelu" alisema Mohamed.

Mohamed amebainisha kuwa kampuni hiyo ina mitambo ya gharama nafuu inayotolewa kwa mkopo kuanzia shilingi 350 kwa siku huku ikiwa na mitambo yenye uwezo wa kuwasha vifaa mbalimbali ikiwemo taa, TV na friji.

Ameongeza kuwa kampuni ya SunKing inaunga mkono jitihada za Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan zinazohamasisha nishati safi ili kuondokana na matumizi ya nishati chafu hatari kwa mazingira ikiwemo mkaa, kuni na mafuta ya taa.

Akizungumza kwa niba ya Mkuu wa Wilaya ya Magu, Afisa Tarafa ya Sanjo- Perpetua Chonja amewahimiza wananchi kuepuka matumizi ya nishati chafu ikiwemo vibatari kwani moshi wake ni hatari kwa macho na mapafu na badala watumie taa za SunKing kama nishati mbadala kwa hasa umeme unapokatika.

Chonja ameipongeza kampuni ya SunKing kwa kuunga mkono jitihada za Raid Dkt. Samia ambaye amekuwa akihamasisha nishati safi ikiwemo mitungi ya gesi ambapo kwa Tarafa ya Sanjo jumla ya majiko 800 yametolewa kwa wananchi.

Kwa upande wake balozi wa SunKing, mwanamuziki Mrisho Mpoto amesema bidhaa za SunKing ni bora kwani zinatoa nishati ya kutosha hata wakati wa mawingu huku pia ikitoa fursa kwa mtu yeyote kuwa wakala wa kuuza bidhaa hizo ambapo hadi sasa ina zaidi ya mawakala elfu tatu nchini.

Nao baadhi ya wananchi akiwemo Beatrice Michael na Kipara Luhiji wamesema bidhaa za SunKing ni mkombozi hasa kwa wajasiriamali wanaofanya shughuli zao nyakati za usiku ambapo hupata mwanga ang'avu ambao pia huwasaidia wanafunzi kujisomea wakiwa nyumbani.
Na George Binagi- GB Pazzo, Mwanza
Afisa Tarafa ya Sanjo wilayani Magu, Perpetua Chonja (wa tatu kulia) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa duka jipya la SunKing katika eneo la Stendi ya Kona ya Kayenye iliyopo Kijiji cha Isangijo Kata ya Bukandwe wilayani Magu. Wa tatu kushoto ni Msimamizi wa Biashara SunKing, Idd Mohamed. Wengine ni viongozi mbalimbali Kata ya Bukandwe.
Afisa Tarafa ya Sanjo wilayani Magu, Perpetua Chonja (wa tatu kulia) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa duka jipya la SunKing katika eneo la Stendi ya Kona ya Kayenye iliyopo Kijiji cha Isangijo Kata ya Bukandwe wilayani Magu. Wa tatu kushoto ni Msimamizi wa Biashara SunKing, Idd Mohamed. Kulia ni Balozi wa SunKing, Mrisho Mpoto.
Afisa Tarafa ya Sanjo wilayani Magu, Perpetua Chonja (wa pili kulia) akikata keki kuashiria uzinduzi wa duka jipya la SunKing katika eneo la Stendi ya Kona ya Kayenye Mwanza. Kulia ni Msimamizi wa Biashara SunKing, Idd Mohamed. Wengine ni viongozi wa Kata ya Bukandwe.
Afisa Tarafa ya Sanjo wilayani Magu, Perpetua Chonja (wa pili kulia) akimlisha keki Balozi wa SunKing, Mrisho Mpoto.
Afisa Tarafa ya Sanjo wilayani Magu, Perpetua Chonja (wa pili kulia) akimlisha keki mmoja wa wananchi.
Uzinduzi wa bidhaa za SunKing katika eneo la stendi ya Kona ya Kayenze Mwanza.
Wakazi wa Mwanza wakifuatilia uzinduzi wa duka jipya la SunKing katika eneo Kona ya Kayenye jirani na Kisesa.
Mmoja wa wakazi wa Mwanza akipatiwa huduma ya sola kutoka kampuni ya SunKing.

Mawakala wa SunKing wakiwa kwenye picha ya pamoja na mwanamuziki Mrisho Mpoto.
Burudani.

KAMATI YA PIC YARIDHISHWA NA THAMANI YA FEDHA KATIKA MRADI WA MAJI SAME MWANGA KOROGWE.

March 28, 2025 Add Comment

 NA WILLIUM PAUL, MWANGA.


WAJUMBE wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) imeridhishwa na ubora wa mradi wa maji Same Mwanga Korogwe ambao umegharimu zaidi ya Bilioni 400 na kudai kuwa thamani ya fedha inaonekana katika mradi huo.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Augustine Vuma mara baada ya kutembelea mradi huo ambapo alisema kuwa, hali ya upatikanaji wa maji kwa sasa katika miji ya Mwanga na Same ni ya kuridhisha kwani wananchi wanapa maji kwa masaa 24.

“Kamati imeridhishwa na ubora wa mradi pamoja na upatikanaji wa maji kwa sasa hivyo kamati inaipongeza Serikali ya awamu ya sita inayoongpzwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi kujenga mradi huo na zimetolewa kwa wakati” alisema Vuma.

Alisema kuwa, jukumu la sasa kwa Wizara ya maji kupitia mamlaka yake ya Mwanga Same ni kutunza mradi huo kwa kushirikiana na Wananchi ili uendelea kuwa bora na kudumu muda mrefu ili kuhakikisha kuwa wananchi hawarudi kule walipotokea kukosa maji au kupata kwa mgao.

Aidha wameiagiza mamlaka hiyokuhakikisha inatekeleza mpango wa usambazaji maji kikamilifu katika maeneo ya mamlaka ili kuwafikiwa wahitija na kutimiza adhima ya Serikali ya kuwafikia wananchi wengi huduma.

Alisema kuwa, mamlaka hiyo inatekeleza mpango wa ulinzi wa vyanzo vya maji na miundombinu yake pamoja na kuweka mpango wa muda mfupi na mrefu wa ukarabati wa miundombinu ya maji ili kuhakikisha mradi unaendeshwa kwa ufanisi na katika hali ya uendelevu ambapo jambo hilo litapelekea mradi huo kutoa tija.

“Mamlaka ya maji Same Mwanga hakikisheni mnaimarisha mkakati wenu wa ushirikiano wa kibiashara na wadau mbalimbali wakiwemo wateja wakubwa ili kuweza kuwafikia kihuduma jambo ambalo litawezesha kuongeza wigo wa kiwango cha ukusanyaji wa mapato pamoja na kutoa elimu kwa wananchi ili waweze kulipia Ankara za maji kikamilifu na kwa wakati ili kuepuka changamoto za madeni ambayo imekuwa kikwazo kwa mamlaka nyingi nchini” alisema Vuma.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa mamlaka ya Maji Same Mwanga (SAMWASA), Mhandisi Rashid Mwinjuma alisema kuwa, kupitia mradi huo kwa sasa wananchi wa Mwanga na Same wanapata maji ya uhakika masaa 24, ambapo hali hiyo imesaidia mapato yameongezeka kutoka milioni 40 kwa mwezi hadi kufikia milioni 70.

Mhandisi Mwinjuma alisema kuwa, hata wateja wameongezeka kutoka 4000 hadi kufikia 6000 huku akidai kuwa mwamko wa wananchi kuomba kuunganishiwa huduma ya maji umekuwa mkubwa.

“Kwa sasa tunajukumu la kuendelea kusambaza mtandao wa maji ili kuwafikia wateja wengi ili kusaidia kukusanya fedha za kuweza kuendeshea mradi huu na kwa siku tumekuwa tukipokea wastani wa watu 50 wanaotaka kuunganishiwa na huduma ya maji lakini tumeendelea kutoa elimu ili watambue umuhimu wa kulipia Ankara zao kwa wakati” alisema Mhandisi Mwinjuma.




SimBanking kugawa milioni 240, magari matano kwa wateja wake

March 27, 2025 Add Comment

Ikizindua msimu wa tano wa kampeni ya yake ya Benki ni SimBaking, Benki ya CRDB imetangaza kutenga zawadi kiasi cha shilingi milioni 240 pamoja na magari matano.
Akizindua kampeni hiyo, Mkurugenzi wa Wateja Wadogo na wa Kati wa Benki ya CRDB, Bonaventura Paul amesema kwa mwaka huu benki imejipanga kutoa magari manne aina ya Toyota IST na Toyota Harrier ‘New Model’ moja kwa wateja watakaoibuka kuwa vinara katika matumizi ya SimBanking katika kukamilisha miamala yao na huduma nyingine.

Bonaventura amesema azma ya Benki ya CRDB siku zote ni kuhakikisha inatoa huduma zinazokidhi mahitaji ya wateja wake na jamii ya Watanzania kwa ujumla hivyo itaendelea kuwekeza kwenye ubunifu wa kidijitali ili kukidhi mahitaji yaliyopo na yatakayojitokeza.

Katika kampeni ya mwaka huu ya SimBanking amesema kutakuwa na washindi wa kila siku na kila wiki watakaopata zawadi za fedha taslimu na gari aina ya Toyota IST na mshindi wa jumla ataondoka na Toyota Harrier.

“Tumetenga zaidi ya shilingi milion 240 zitakazotolewa kwa washindi wetu na kila baada ya miezi miwili tutatoa zawadi ya gari aina ya IST wakati mshindi wa jumla tutakayemtangaza mwishoni mwa mwaka atapata gari aina ya Toyota Harrier. Magari haya yote tutakayoyatoa kwa washindi wetu ni ‘New Model’ na yamekatiwa bima kubwa. Kwa wanafunzi wa vyuo, kuna simu za kisasa aina ya Iphone 16 zitakazokuwa zinatolewa kila baada ya miezi mitatu,” amesema Bonaventura.

Kwa miaka mitano ya kuendesha kampeni ya Benki ni SimBanking, amesema kumekuwa na mwitikio mkubwa ambao kwa sasa kwani kila mwezi takriban wateja milioni moja wanafanya miamala mingi kupitia programu hiyo inayowaruhusu kukamilisha malengo yao wakiwa mahali popote ndani ya saa 24.

Bonaventura amesema Benki ya CRDB inaamini katika kutoa huduma bora na za kisasa ili kuchangia maendeleo ya wateja wake na taifa hivyo kuhitaji kuwekeza katika ubunifu unaoendana na mabadiliko ya teknolojia duniani. Amesisitiza kuwa SimBanking ni kati ya huduma bora inayotambulika duniani kutokana na urahisi, usalama na uhakika wa kukamilisha miamala kidijitali.

“SimBanking ni kati ya huduma za Benki yetu ya CRDB ambazo zimeleta mapinduzi makubwa katika kuchochea ujumuishi wa huduma za fedha nchini. Kwa zaidi ya muongo mmoja sasa tangu kuanzishwa kwake mwaka 2011, SimBanking imetoa fursa kwa Watanzania wengi kujiunga na mfumo rasmi wa huduma za benki.





TBS YASISITIZA UMUHIMU WA KUHAKIKI USAHIHI WA VIPIMO ( UGEZI ) WA VIFAA VYA HOSPITALI , KULINDA AFYA ZA WATANZANIA.

March 27, 2025 Add Comment


Na Mwandishi Wetu.

Machi 26 , 2025 Shirika la Viwango Tanzania ( TBS ) limewasihi Watumiaji mbalimbali wa Vifaa Tiba kuhakikisha wanapeleka Vifaa vyao TBS katika Maabara ya Taifa ya Ugezi ili kuhakiki Usahihi wa Vipimo wa Vifaa hivyo utakaowasaidia kuwa na uhakika wa majibu yanayotolewa na Vifaa hivyo suala litakalopelekea kujenga uaminifu na kulinda Afya za Wateja wanaowahudumia.



Akizungumza na Waandishi wa Habari Mapema Leo hii katika Makao Makuu ya Shirika hilo Ubungo Jijini Dar Es salaam Afisa Vipimo Mkuu kutoka Maabara ya Taifa ya Ugezi iliyopo TBS Bwn. Joseph Mahilla amesema ni muhimu sana kufanya Uhakiki wa Usahihi wa Vipimo ( Ugezi ) kwenye sekta ya Afya kwa maana ya Viwanda vinavyotengeneza madawa ( pharmaceutical Industries ) *wanatakiwa kufanya ugezi ili dawa zinazozalishwa ziwe na ubora unaotakiwa* , pamoja na maeneo yote yanayotoa Huduma za Afya kama Hospitali , Vituo vya Afya na Zahanati ili kulinda Afya za Watanzania kwa maana kifaa kinapofanyiwa Ugezi kitatoa majibu sahihi yatakayomwezesha Daktari au mtu yeyote katika Sekta ya Afya kutoa maelekezo sahihi kwa mteja.


" Mfano katika Hospitali , Vifaa vinapokua vimefanyiwa Ugezi vitatoa majibu sahihi ya Vipimo ambayo yatamwezesha Daktari kujua mgonjwa ana tatizo gani na kuchukua hatua stahiki za kupambana na ugonjwa husika kwa haraka sana, *daktari hutoa matibabu kutegemea Majibu yaliyotoka maabara, hivyo kama maabara imefanyiwa ugezi daktari atatoa matibabu sahihi kwa mgonjwa na kumhakikishia usalama wake, hii pia itapunguza upotevu wa muda na fedha kwa kufanya ufuatiliaji wa matibabu sehemu nyingine ama kupewa dawa wakati hakuna ugonjwa. Kufanya ugezi kunachangia maendeleo katika Jamii " amesema Mahilla .

Kwa upande wake Bi. Clara Mwinami Afisa Vipimo TBS ametoa wito kwa Hospitali ambazo hazijafanya Ugezi wa Vifaa katika Maabara zao kufika TBS kwa maana Uhakiki wa Usahihi wa Vipimo wa Vifaa vyao utawasaidia kuaminika kwa Huduma wanazozitoa .

Bi. Clara alimalizia kwa kusema kuwa Shirika la Viwango Tanzania TBS kupitia Maabara yake ya Metrolojia wanatoa Huduma ya Ugezi katika maeneo mbalimbali ambayo wana Umahiri na wamepata Ithibati katika Maabara zaidi ya Saba kutoka SADCAS kwa maana majibu wanayoyatoa ni sahihi na yanakubalika kote ulimwenguni.

COSTECH WAKABIDHI RASMI ENEO LA MRADI KWA MKANDARASI KWA AJILI YA UJENZI WA JENGO JIPYA LA STI JIJINI DODOMA

March 26, 2025 Add Comment

 

TUME ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) imekabidhi rasmi eneo la mradi kwa mkandarasi TIL Construction Limited kwa ajili ya kuanza ujenzi wa jengo jipya la Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (STI)  jijini Dodoma.

Akizungumza baada ya kukabidhi eneo hilo la mradi Machi 25,2025 jijini Dodoma  Mratibu Msaidizi wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) kutoka COSTECH, Dkt. Aloyce Andrew, amesema hatua hiyo inalenga kurahisisha utoaji wa huduma kwa wadau wa taasisi hiyo.

"COSTECH ina jengo Dar es Salaam lakini tumeamua kujenga Dodoma kwa ajili ya kuwahudumia wadau wetu kwa ukaribu zaidi...,Jengo hili litakuwa na sehemu ya kuhudumia wabunifu, kuatamia kampuni changa, na kuratibu masuala ya utafiti," amesema Dkt. Andrew.

Amesema ujenzi wa jengo hilo, ambalo litajengwa eneo la Azina jijini humo  lenye mita za mraba 4,800, unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 12 kufuatia kusainiwa kwa mkataba Machi 24, 2025.

Kwa upande wake, Mshauri Elekezi wa mradi huo kutoka Kampuni ya MEKON, Benedict Martin, amesema wamekuwa wakihusika katika usanifu wa jengo hilo tangu mwaka jana (2024) baada ya kushinda zabuni kutoka COSTECH.

"Tulishirikiana na COSTECH kuhakikisha jengo hili linakidhi mahitaji yao yote. Pia tuna uhakika kwamba mkandarasi tuliyempata ana uwezo wa kutekeleza mradi huu kwa ubora unaotakiwa," alisema Martin.


Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa TIL Construction Limited, Ding Fubing, ameahidi kwamba kazi itafanyika kwa ufanisi na kumalizika kwa wakati.

"Tunaanza rasmi kesho kwa kulisafisha eneo lote, na baada ya wiki mbili hadi tatu, tutaingia kwenye ujenzi wenyewe. Tunaahidi kufanya kazi nzuri na kukamilisha mradi kwa muda uliopangwa au hata kabla," alisema Fubing.


Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi wa COSTECH, Imanuel Mgonja, amesema taasisi hiyo ina imani na mshauri elekezi pamoja na mkandarasi, akiwashukuru kwa kujitolea kuhakikisha mradi unatekelezwa kwa ubora unaohitajika..