Showing posts with label elimu. Show all posts
Showing posts with label elimu. Show all posts

VETA YAANZA KUTOA ELIMU YA NISHATI YA UMEME JUA NCHINI

October 31, 2023 Add Comment

 

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) Kanda ya Kati, John Mwanja, akizungumza Oktoba 27, 2023 na wahitimu wa mafunzo ya Nishati ya Umeme Jua yaliyoandaliwa na VETA kwa kushirikiana na Chuo cha Ufundi Arusha (ATC). Kulia ni Mkufunzi wa mafunzo hayo kutoka ATC, Daniel Ngwenya na kushoto ni Kaimu Mkuu wa Chuo cha VETA Mkoa wa Singida, , Alphonsina James.

...............................................


Na Dotto Mwaibale, Singida

MAMLAKA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imeanza kutoa elimu ya Nishati ya Umeme Jua katika vyuo vyake vyote nchini ikiwa ni moja ya njia ya kuunga mkono jitihada za Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassanza kuhakikisha nchi inapata umeme wa uhakika.

Akizungumza Oktoba 27, 2023 , wakati akifunga mafunzo ya nishati ya umeme jua ya wiki mbili kwa walimu wa vyuo 12 vya VETA ambayo yameandaliwa na VETA Mkoa wa Singida kwa kushirikiana na Chuo cha Ufundi Arusha (ATC), Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Kati, John Mwanja alisema mafunzo hayo ni ya muhimu hasa katika kipindi hiki ambacho nchi inamgawo wa umeme na inafikiria kuiwasha kwa kutumia umeme huo kupitia wataalamu waliozalishwa na VETA.

“VETA ndio tumepewa majukumu ya kutoa elimu hii kwenye vituo vyetu na kuhakikisha watanzania wote waliopo mijini na vijijini wanaipata,” alisema Mwanja.

Mwanja alisema kupitia wahitimu hao sasa VETA inakwenda kupata walimu wa kufundisha kozi hiyo na kuwa Mkurugenzi Mkuu wa VETA aliwaomba wakuu wa vyuo katika kanda zao kuwaruhusu walimu kuhudhuria mafunzo hayo.

Alisema mafunzo hayo yalianzishwa VETA Mkoa wa Singida ambapo awamu ya kwanza na ya pili yamefanyika hapo na kwa awamu hii waliona yasihusishe watu wa kutoka Singida pekee bali uongezwe wigo wa kuwapata wengi lengo likiwa yasambae kila sehemu ambapo VETA ipo.

Alisema ilipendekezwa hivyo si kwa ajili ya kupata watu wengi bali viwepo vituo vingine kama cha Singida kwenye vyuo vingine kwa ajili ya kupata elimu na wataalam kwenye maeneo hayo.

Alisema kama inavyofahamika majukumu ya VETA ni kufundisha ujuzi na kuwa elimu hiyo ya nishati ya umeme jua ni muelekeo na mpango wa Serikali kutokana na kuwepo kwa changamoto kubwa ya umeme na kuwa moja ya maono ya Serikali ni kuona nchi inapata umeme kutokana na mfumo wa jua.

Alisema wanapotegemea kupata umeme kupitia mfumo huo ni lazima wawepo wataalam wa kutosha wa kufanya kazi hiyo na kuwa kuna wadau wengi kama Chuo cha Ufundi Arusha (ATC) ambao wanafundisha kozi hiyo lakini na VETA wanaowajibu wa kuiunga mkono Serikali wanapotaka kuongeza nishati hiyo kwa kuhakikisha wataalam wanapatikana.

“Haiwezekani wataalam hao wapatikane kwa kutumia kituo cha Singida peke yake hivyo VETA kama wajibu wetu ni lazima wataalam hao wasambae nchi nzima,” alisema Mwanja.

Alisema mahitaji ya VETA ni kutaka kijana aliyopo kule Busokelo mkoani Mbeya au Mwanza na maeneo mengine ya nchi wapate elimu hiyo katika vyuo vilivyopo katika maeneo yao badala ya kwenda Singida jambo litakalowapunguzia gharama na ndio maana Serikali inajenga vyuo vya VETA kila wilaya kwa lengo hilo na kuwa jukumu lao ni kupeleka huduma kwa watumiaji na wadau wao ambao ni hao wanafunzi.

Mwanja alisema kutokana na hali hiyo VETA iliona licha ya kozi hiyo kuanza kutolewa Mkoa wa Singida sasa itolewe katika Mikoa yote kupitia vyuo vya VETA ikiwa ni kuwasogezea huduma watanzania.

Aidha, Mwanja aliwataka wahitimu hao mara watakaporudi kwenye vituo vyao wakawe na mwendelezo wa kwenda kutoa elimu hiyo ambayo pia wanafunzi wanaojifunza fani ya umeme wa kawaida katika chuo hicho wameyapata.

Katika hatua nyingine Mwanja alivitaka vyuo hivyo kujitangaza ili shughuli wanazozifanya zifahamike ikiwa ni pamoja na mafunzo ya nishati ya umeme jua jambo litakalosaidia kufahamaika na akahimiza pia kuanzisha kozi fupi za mafunzo hayo.

“Suala la kujitangaza ni la muhimu tumieni mitandao ya kijamii kuna chuo kimoja kule Ruvuma nilikuta kuna raia wa kigeni kutoka nchi jirani ikiwemo Msumbiji wapo kupata mafunzo nilipouliza walijueje kama kuna hicho chuo walisema kupitia matangazo hivyo ndugu zangu tangazeni vyuo vyetu kwani biashara ni matangazo,” alisema Mwanja.

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Chuo cha VETA Mkoa wa Singida, Alphonsina James aliwashukuru washiriki wa mafunzo hayo kwa ushirikiano mkubwa waliouonesha wakati wa mafunzo na kueleza kuwa kwao ni bahati kubwa kwani katika vyuo 48 ni vyuo 15 pekee ndio vilivyotoa washiriki hao.
Katika risala ya wahitimu hao kwa mgeni rasmi waliomba muda wa mafunzo uongezwe pamoja na uratibu wa mafunzo hayo ufanywe na VETA makao makuu kwa ajili ya uwezeshwaji ambapo pia waliomba kuwezeshwa vifaa vya kufundishia.



Mkurugenzi wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) Kanda ya Kati, John Mwanja, akikabidhi cheti kwa mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo.



Washiriki wa mafunzo hayo wakifuatilia hutuba ya mgeni rasmi wakati wa ufungaji wa mafunzo.

Mgeni rasmi wa ufungaji wa mafunzo hayo Mkurugenzi wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) Kanda ya Kati, John Mwanja (waliokaa katikati), akiwa katika picha ya pamoja na wahitimu wa mafunzo hayo.

WALIMU WA WALEZI SHULE ZA MSINGI, SEKONDARI NA VYUO SHINYANGA WAPATIWA MAFUNZO UANZISHWAJI WA KLABU ZA MAADILI

October 23, 2023 Add Comment

 



Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga, Ibrahim Makana akizungumza wakati akifungua mafunzo kuhusu uanzishwaji wa Klabu za Maadili kwa Walimu wa Malezi wa Klabu za Maadili shule za msingi, sekondari na vyuo katika Mkoa wa Shinyanga.



Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog

Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya imetoa mafunzo kuhusu uanzishwaji wa Klabu za Maadili kwa Walimu wa Malezi wa Klabu za Maadili shule za msingi, sekondari na vyuo katika Mkoa wa Shinyanga.

Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo hayo leo Jumatatu Oktoba 23,2023, Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga, Ibrahim Makana amesema lengo la Klabu za Maadili ni kuwajengea wanafunzi na wanavyuo misingi bora ya maadili tangu wakiwa shuleni au vyuoni.

Amesema Klabu za maadili za wanafunzi ni vikundi vya wanafunzi ndani ya shule au vyuo nyenye jukumu la kuratibu na kufanikisha shughuli za kuelimisha, kuhamasisha na kushirikisha jamii masuala ya maadili na kwamba Klabu hizo zinalenga kuimarisha nidhamu na uzalendo kwa Watanzania.

“Klabu za maadili kwa wanafunzi zina kazi kubwa ya kuelimisha wanafunzi wengine na wananchi kuhusu maadili kupitia nyimbo, kwaya, maigizo, ngonjera, katuni shairi, ngoma na ubunifu mwingine wowote kwa lengo la kujenga tabia njema na kukemea vitendo vya tabia zisizokubalika katika jamii yetu",amesema.

Aidha kutokana na umuhimu wa klabu hizo za Maadili katika kukuza maadili ya Watanzania, amezielekeza shule na vyuo vyote Mkoa wa Shinyanga kuanzisha Klabu za Maadili za wanafunzi na wanachuo ili kuwe na wanafunzi waadilifu.

Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga, Ibrahim Makana 

“Pia Mratibu wa Maadili Mkoa wa Shinyanga unatakiwa kufanya ufuatiliaji wa klabu hizo ngazi ya shule na vyuo ili kuona zinafanya kazi kama ilivyokusudiwa na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa kuwa kuna uhusiano mkubwa kati ya wanafunzi wenye maadili mema na kuongeza ufaulu katika masomo yao”,ameongeza.

Aidha, ameshauri ofisi ya Kanda ya Maadili kutoa mafunzo kila inapoona inafaa kwa lengo la kuimarisha uwezo wa walimu kusimamia klabu hizo ngazi ya shule na vyuo, kwa kufanya hivyo itasaidia kuwaandaa wanafunzi kuwa raia wema, viongozi bora na wazalendo kwa Taifa.

Katika hatua nyingine amemshukuru Gerald Mwaitebele kutoka ofisi ya Maadili Kanda ya Magharibi kwa niaba ya Kamishna wa Maadili kwa kuamua Mkoa wa Shinyanga uwe Mkoa wa mfano katika kuanzisha klabu za Maadili ngazi ya shule na vyuo huku akiishukuru Ofisi ya Maadili kwa kusimamia na kukuza maadili ya viongozi wa umma pia kwa kuanzisha klabu za Maadili katika ngazi ya shule na vyuo.

“Klabu hizi zitasaidia kuwajengea wanafunzi uwezo kujua maadili yanayopaswa kuzingatiwa katika ujenzi wa Taifa letu”,amesema

Katibu Msaidizi, Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Magharibi (Tabora, Kigoma, Shinyanga Simiyu), Gelard Mwaitebele.

Katibu Msaidizi, Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Magharibi (Tabora, Kigoma, Shinyanga Simiyu), Gelard Mwaitebele amewataka walimu kutumia vikao vya wazazi shuleni kufikisha ujumbe wa masuala ya maadili kupitia Klabu za maadili.

“Tumeamua kuanzisha Klabu za maadili kwa wanafunzi ili kuandaa kizazi chenye maadili ili tuwe na taifa bora, tunataka taifa lenye watu wenye maadili ili tuwe na viongozi waadilifu. Tatizo la maadili lipo katika jamii, walimu ingieni kazini. Msiwe na uoga wa kusimamia maadili serikali ipo kazini, Mama, Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan yupo kazini”, amesema Mwaitebele.

Amezitaja sifa za mwalimu wa malezi kuwa ni pamoja na kuwa mwadilifu, mwaminifu, muwazi, mzalendo, mwajibikaji, anayejali, anayethamini utu na mwenye mafanikio katika kazi zake na anayekubalika kimaadili na wanafunzi.

Kwa upande wake, Afisa Maadili Kanda ya Magharibi, Onesmo Msalangi ametaka Klabu hizo zisaidie kulinda maadili katika nchi huku akisisitiza kuwe na ukaribu mkubwa kwa watoto hasa katika kipindi hiki ambacho mambo ya hovyo ni mengi.

“Wafundisheni watoto jinsi kusaidia kazi wazazi. Kuweni makini na hizi TV na simu za mkononi. Kwenye mitandao ya kijamii kuna mema na mabaya, watoto wanaharibika kwa kupewa simu bila uangalizi, tunaharibu kizazi sisi wenyewe, tuwe makini sana na hivi vitu”,amesema Msalangi.
Walimu wa Malezi wa Klabu za Maadili shule za msingi, sekondari na vyuo wakifuatilia mafunzo

“Wafundisheni watoto jinsi ya kutoa taarifa kwa siri ili kudhibiti vitendo viovu shuleni, vyuoni ili kutambua maovu yanayotokea shuleni. Walimu hakikisheni pia mnashawishi wanafunzi wengi zaidi wajiunge kwenye klabu za maadili”,ameongeza Msalangi.

KAMPUNI YA VIVO ENERGY TANZANIA YATOA HUDUMA YA VYOO SAFI KWA SHULE KWA SHULE YA MSINGI KIUNGANI

October 23, 2023 Add Comment

 Kampuni ya Vivo Energy Tanzania, imekabidhi vyoo vilivyokarabatiwa katika Shule ya Msingi ya Kiungani. Ishara hiyo inaonyesha dhamira ya kampuni kutunza mazingira na kuhamashisha uboreshwaji wa afya katika jamii.


Akizungumza katika hafla ya kukabidhi, Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Vivo Energy Tanzania, Bw.Mohamed Bougriba alisema, “Leo tunakabidhi vyoo hivi kama kielelezo cha hamasa yetu ya kushirikiana na wadau mbalimbali katika jamii kuboresha elimu na afya ya watoto. Tunaamini kwa dhati kuwa maboresho haya hayataleta manufaa ya kimwili tu, bali hata ustawi wao wa akili, afya na maisha yao kwa ujumla’

Aliendelea kwa kuhimiza wanafunzi kusoma kwa bidii ili kufikia ndoto zao, akimnukuu Baba wa taifa, Mwalimu Julius Nyerere kwa kusema, "Elimu si njia ya kuepuka umasikini, ni njia ya kupambana nao.’

Naye Mkuu wa Shule ya Msingi Kiungani Bibi Bonvilia Mlay alitoa shukrani zake za dhati kwa kampuni ya Vivo Energy Tanzania huku akisisitiza kuwa vyoo hivyo vipya vitawawezesha watoto wa shule hiyo kupata mazingira safi na salama na hivyo kuwaepusha na maradhi yatokanayo na usafi duni.

Meneja Mawasiliano wa Vivo Energy Tanzania, Grace Kijo pia alitoa shukrani zake za dhati kwa viongozi wa serikali za mitaa waliohudhuria, kwa ushirikiano wao mkubwa katika uendeshaji wa kampuni hiyo. Aliahidi kuendelea kufanya kazi kwa karibu na viongozi wa eneo hilo ili kuleta mabadiliko chanya na ya kudumu kwa jamii.

Vivo Energy Tanzania inaendelea kutekeleza sera yake ya uwajibikaji kwenye jamii, kwa kutambua kwamba kwa kuleta mabadiliko chanya katika ngazi ya elimu, inachangia katika kuboresha jamii kwa ujumla.

Kampuni inajivunia kuunga mkono Shule ya Msingi Kiungani katika dhamira yake ya kuweka mazingira safi na salama kwa wanafunzi wake na inatarajia kuendelea kushirikiana na jamii ili kuleta mabadiliko yenye tija.

Hafla hiyo ilihitimishwa na ushairi kutoka kwa wanafunzi wa darasa la nne wa shule hiyo, ikiwa ni sehemu ya kutoa shukrani kwa Vivo Energy Tanzania.


Mkurugenzi Mtendaji wa  Kampuni ya Vivo Energy Tanzania, Mohamed Bougriba (watatu kulia) na Afisa Elimu wa Manispaa ya Temeke, Abdul Buhety (wapili kulia) wakikata utepe  katika hafla ya kukabidhi choo chenye matundu 16 kilichokarabatiwa na kampuni hiyo kwa shule ya msingi Kiungani iliyopo Kurasini Manispaa ya Temeke jijini Dar es salaam. Kulia ni  Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Bonivilia Malya.

Mkurugenzi Mtendaji wa  Kampuni ya Vivo Energy Tanzania, Mohamed Bougriba (wa pili kulia) akikabidhiwa tuzo ya heshima na Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi  Kiungani iliyopo Kurasini Manispaa ya Temeke ,Bonivilia  Malya mara baada ya  kukabidhi choo chenye matundu 16 kilichokarabatiwa    na kampuni hiyo. Wengine kushoto ni Afisa Elimu Manispaa ya Temeke, Abdul Buhety na kulia ni Meneja Masoko na Mawasiliano Vivo Energy Tanzania, Grace Kijo.

Mkurugenzi Mtendaji wa  Kampuni ya Vivo Energy Tanzania, Mohamed Bougriba akionyeshwa baadhi ya matundu ya vyoo na Mwanafunzi wa Darasa la Sita, Baraka Issa  mara baada ya kukabidhiwa msaada wa ukarabati wa vyoo hivyo.

BINGWA WA MASOMO YA HISABATI ATANGAZWA

October 20, 2023 Add Comment


Chama Cha Hisabati Tanzania (CHAHITA) kimetoa orodha ya wanafunzi 233 kati ya 812 waliofanya vizuri katika shindano la hisababti Nchini Tanzania.

Wanafunzi hao kutoka mikoa 11 ya Tanzania bara na visiwani, walipata asilimia 40 na zaidi ya alama zilizohitajika kwenye shindano hilo na wengine 579 wakipata chini ya asilimia 40.

Mtihani huo ulihusisha makundi mawili, kundi la kwanza likiwa ni wanafunzi wa kidato cha tatu hadi cha nne na kundi la pili ni kidato cha tano hadi sita na washindi.

washindi hao wanatoa wanatoa mwanya wa kupatikana kwa washiriki nane katika shindano la hisabati ngazi ya Afrika mashariki, Afrika na Dunia litakalofamyika mapema mwakani

Akisoma matokeo hayo jDar es Salaam, Mwenyekiti wa CHAHITA Betinasia Manyama,alitaja badhi ya wanafunzi wa kundi la wanafunzi 10 bora wa jumla kidato cha tatu na nne akiwemo Stella Maliti wa Shule Marian Girls ya Pwani, Brown Mafuru wa Marian Boys Pwani na Alice Gonza wa Canossa ya Dar es Salaam.

Kuhusu ya idadi ya shule zilizoshirikia, alisema ni 58 wanafunzi wakiwa 540 ambapo waliopata asilimia 40 na kuendelea ni 167 na chini wastani huo ni 373.

Kwa kidato cha tano na sita, Betinasia alisema walioshiriki ni 272 kutoka shule za sekondari 22, wavulana wakiwa 162 na wasichana 110 takwimu zikionyesha waliopata asilimia 40 na zaidi ni 66 pekee na wenye upungufu na wastani huo wakiwa 206.

Baadhi walioshika nafasi 10 za mwanzo ni Amosi Paulo wa Mzumbe mkoani Morogoro,Elia Wambura wa Iyunga Technical Mbeya na Mwanaarab Said wa Lumumba mjini Magharibi.

Betinasia alisema mtihani wa kuwapata washindi ulifanyika Agosti mwaka huu na washindi nane wanasakwa kuiwakilishi nchi kwenye mashindano ya hisabati Afrika Mashariki, Afrika na Duniani.

“Lengo la mashindano haya ni kupata wanafunzi watakaoiwakilisha nchi kushiriki katika mashindano ya kimataifa,pia kujenga ushirikiano wa kitaaluma na mataifa mbalimbali duniani,baada ya matokeo haya washidi 10 kwa kila jundi watapatiwa zawadi siku ya maadhimisho ya Hisabati Duniani Machi14,2024”alisema.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa CHAHITA Dk Said Sima alisema malengon yao mwakani ni kuhakikisha mikoa yote nchini inashiriki shindano hilo.

Alisema si kila mwanafunzi anashiriki bali ni wale wenye vipaji na uongozi kwenye shule husika ndio huwachagua wahusika kuingia kwenye shindano hilo la mitihani ya hisabati.

“Tunaweka mikakati hawa washindi tuwape elimu ya kutosha ili washiriki kwenye mashindano ya kimataifa vyema,”alisema.

Naye Mkuu wa Idara ya Hisabati Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Sylvester Rugeihyamu alisema lengo la shindano la hisabati ni kutambua na kuibua vipaji kwenye somo hilo,kuchochea na kutambua ubunifu wa uvumbuzi kupitia mitihani

Pia kuwapa motisha wanafunzi kuipenda somo la hisabati akisistiza mitihani hiyo haitumii mitaala inayotumiwa na Baraza l;a Mitihani Tanzania (Necta)

Mikoa ambayo imetoa shule zilizoshiriki kwenye shindano hilo ni Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Mbeya,Arusha,Dodoma, Iringa,Kilimanjaro, Songwe,Mwanza na mjini Magharibi.
Mwenyekiti wa Chama cha Hisabati Tanzania (CHAHITA), Betinasia Manyama, akitangaza matokeo ya mitihani ya mashindano ya hisabati kwa wanafunzi wa kidato cha tatu, nne, tano na sita, katika Idara ya Hisabati, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), jana. Kushoto ni Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Said Sima na kulia ni Mkuu wa Idara ya Hisabati na Mlezi wa CHAHITA, Dk. Sylvester Rugeihyamu. na mpiga picha wetu

Katibu mkuu wa chama cha hisabat Said Sima mara baada ya kutangazwa matokeo ya mitihani ya mashindano ya hisabati kwa wanafunzi wa kidato cha tatu, nne, tano na sita, katika Idara ya Hisabati, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), jana,kulia ni Mkuu wa Idara ya Hisabati na Mlezi wa CHAHITA, Dk. Sylvester Rugeihyamu.

Mkuu wa Idara ya Hisabati na Mlezi wa CHAHITA, Dk. Sylvester Rugeihyamu akizungumza jambo mara baada ya kutangazwa matokeo ya mitihani ya mashindano ya hisabati kwa wanafunzi wa kidato cha tatu, nne, tano na sita, katika Idara ya Hisabati, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), jana,

Picha ya pamoja


ELIMU

WANAFUNZI 56,132 WAPANGIWA MIKOPO YA SH.159.7 BILIONI AWAMU YA KWANZA 2023/2024

October 20, 2023 Add Comment

 NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV


BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetangaza awamu ya kwanza ya Wanafunzi 56,132 wa shahada ya kwanza waliopangiwa mikopo yenye thamani ya shilingi Bilioni 159.7 kwa mwaka wa Masomo 2023/2024.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 20,2023 Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Bw. Abdul-Razaq Badru amesema kuwa kati ya wanafunzi hao, wa kiume 32,264 sawa na asilimia 57% na wa kike ni 23,868 sawa na asilimia 43% na kuanzia leo wanaweza kuona taarifa za mikopo waliyopangiwa katika akaunti walizotumia kuomba mkopo.

Aidha Bw.Badru amesema kuwa maafisa wa HESLB watakuwa katika taasisi za elimu ya juu nchini kuanzia Jumatatu , Oktoba 23,2023 ili kuratibu usajili wa wanafunzi hao katika mfumo wa malipo.

"Kwa wanafunzi wapya, kama walivyoshauriwa wakati wa kuomba mkopo, wafike vyuoni wakiwa na namba za akaunti zao za benki, namba zao za simu zinazopatikana na watasajiliwa katika mfumo wetu wa malipo wa DiDiS baada ya kusajiliwa na Chuo'. Amesema Bw.Badru

Pamoja na hayo Bw.Badru amesema kuwa Serikali imetenga shilingi Bilioni 731 kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi 220,376, kati yao, wanafunzi 75,000 watakuwa ni wanufaika wa mwaka wa kwanza wa shahada ya kwanza na wanafunzi zaidi ya 145,376 ni wanaoendelea na masomo baada ya kufaulu mitihani yao ya mwaka.

Vilevile amewasihi waombaji wa mikopo wa shahada ya Kwanza, Stashahada na wanufaika wa 'Samia Scholrship' kwa mwaka 2023/2024 kuwa watulivu wakati taratibu za uchambuzi na upangaji wa mikipo na ufadhili kwa wanafunzi wenye sifa ukiendelea.

Kwa upande wake rais wa Jumuiya ya Wanafunzi Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (TAHLISO) Bi.Maria Thomas ameipongeza Serikali kwa kuendelea kuongeza bajeti ya mikopo ambapo mwanzo ilikuwa Bilioni 654 hadi kufikia Bilioni 731.

Ameipongeza Bodi ya Mikopo kwa kuendelea kushirikiana nao katika kutatua changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa zikifanyiwa kazi.

Hata hivyo amewaomba wanaufaika wa mikopo watakapopata fedha zao, wazielekeze katika malengo mahususi katika kutimiza ndoto za elimu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) , Bw. Abdul-Razaq Badru (katikati) akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 20,2023 katika Ofisi za HESLB Jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) , Bw. Abdul-Razaq Badru (katikati) akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 20,2023 katika Ofisi za HESLB Jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) , Bw. Abdul-Razaq Badru akisisitiza jambo wakati akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 20,2023 katika Ofisi za HESLB Jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) , Bw. Abdul-Razaq Badru akisisitiza jambo wakati akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 20,2023 katika Ofisi za HESLB Jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) , Bw. Abdul-Razaq Badru akisisitiza jambo wakati akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 20,2023 katika Ofisi za HESLB Jijini Dar es Salaam.


Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) , Bw. Abdul-Razaq Badru (katikati) akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 20,2023 katika Ofisi za HESLB Jijini Dar es Salaam.
rais wa Jumuiya ya Wanafunzi Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (TAHLISO) Bi.Maria Thomas (wa kwanza kushoto) akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 20,2023 katika Ofisi za HESLB Jijini Dar es Salaam.


Mkurugenzi wa upangaji na utoaji mikopo wa HESLB, Dkt. Peter Mmari akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 20,2023 katika Ofisi za HESLB Jijini Dar es Salaam

Baadhi ya Watumishi wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) wakifuatilia Mkutano wa Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) , Bw. Abdul-Razaq Badru na Waandishi wa habari leo Oktoba 20,2023 katika Ofisi za HESLB Jijini Dar es Salaam

(PICHA ZOTE NA EMMANUEL MBATILO)