Showing posts with label afya. Show all posts
Showing posts with label afya. Show all posts

SERIKALI KUPITIA BOHARI YA DAWA YAANZA USAMBAZAJI VIFAA TIBA MAJIMBONI VYENYE THAMANI ZAIDI YA BILIONI 14.7/=

January 19, 2024 Add Comment

 BOHARI ya Dawa (MSD) imeanza usambazaji majimboni vifaa tiba vilivyonunuliwa na serikali vyenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 14.7 kwa ajili ya hospitali, vituo vya afya na zahanati lengo ni kupunguza vifo vya mama na mtoto.


Meneja wa MSD, Kanda ya Mashariki yenye mikoa ya Dar es Salaam, Pwani ,Morogoro na Visiwani Zanzibar, Betia Kaema alisema hayo wakati wa makabidhiano wa vifaa hivyo na mkuu wa mkoa wa Morogoro , Adam Malima kwa ajili ya majimbo 11 ya mkoa huo.

Kaema alisema , mkoa wa Morogoro umepatiwa vifaa aina tisa vyenye thamani ya sh milioni 759 na kuanza kusambazwa katika majimbo yote 11 na kila jimbo litapokea vifaa vyenye thamani ya Sh milioni 69.

“ Kama tunavyofahamu Serikali yetu inayoongozwa na Rais Mama Samia Suluhu Hassan , imenunua vifaa kwa ajili ya kupunguza vifo vya mama na mtoto vyenye thamani ya sah bilioni 14.7 na vifaa hivyo vilizinduliwa na Waziri wetu wa Afya kwa ajili ya majimbo ya Tanzania nzima” alisema Kaema.

Kaema alivitaja vifaa vilivyokabidhiwa kwa kila jimbo la mkoa huo na idadi yake kwenye mabano ni Drip stand (330), vitanda vya kawaida vya wagonjwa (330), vitanda vya kujifungulia mama wanajawazito (220) na seti (220) za kujifungulia mama wajawazito.

Alitaja vingine ni shuka (1,320), magodoro (330), Examination table (220), meza ndogo za wagonjwa kuwekea vifaa vyao pale wanapokuwa wamelazwa (165) na Bed side Locker (330).

Kaema alisema hizo zote ni juhudi za serikali katika kuondoa kabisa ama kupunguza vifo vya mama na mtoto wakati wa kujifungua .

“ Kwa sasa serikali imetoa kipaumbele kuimarisha na kuwezesha hospitali zote mikoani ambazo zimeanishwa katika majimbo mbalimbali kuwa na vifaa hivi ili kuweza kuondokana kabisa na vifo vya mama na mtoto wakati wa kujifungua” alisema Kaema .

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima ,alisema serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika miundombonu ya sekta ya afya na kwa sasa imejielekeza katika uboreshaji wa viwango vya utoaji wa huduma za afya nchini.

“ Malengo yetu sisi mkoa baada ya kupokea kwa vifaa tiba hivi ni kwenda kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi na hili tumekuwa tukilihimiza nyakati zote “ Malima .

Mkuu wa mkoa huyo alisema licha ya kupokea vifaa tiba hivyo, mkakati wa mkoa ni kuendelea kutoa elimu kuhusiana na kujikunga na magonjwa mbalimbali na namna ya utumiaji wa vifaa hivyo kwa wagonjwa.

Hivi karibuni Waziri wa Afya ,Ummy Mwalimu alizindua usambazaji wa vifaa vya kuboresha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto vyenye thamani ya zaidi ya sh. bilioni 14.9 ambavyo vitasambazwa katika majimbo 214 na halmashauri nchi nzima.

Ummy alisema usambazaji wa vifaa vya hivyo umelenga kuboresha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto na kuimarisha uzazi salama nchini.



















WANANCHI CHUKUENI TAHADHARI DHIDI YA RED EYES

WANANCHI CHUKUENI TAHADHARI DHIDI YA RED EYES

January 16, 2024 Add Comment



Wizara ya afya imewaasa wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa macho mekundu (Red eyes) Maambukizi ya Kirusi kwenye ngozi ya juu ya gololi ya jicho yajulikanayo kitaalamu “Viral Keratoconjunctivitis” iliyoibuka nchini hivi karibuni.


Hayo yamesemwa leo Januari 15, 2024 na Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Wizara ya Afya Prof Pascal Ruggajo kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Serikali Prof Tumaini Nagu wakati akitoa taarifa ya uchunguzi wa awali ya ugonjwa huo ambao umeripotiwa kuathiri watu wengi nchini.


Prof. Ruggajo amesema dalili ya ugonjwa huo ni pamoja na macho kuwasha, kuchomachoma, kuuma, macho kutoa machozi na kutoa tongo tongo za njano.


"Taarifa za uchunguzi zinaonesha Maambukizi ya Kirusi hiki kwenye ngozi ya juu ya gololi ya jicho yajulikanayo kitaalamu “Viral Keratoconjunctivitis” ni maambukizi yanayosambaa kwa kasi kubwa. Hakuna tiba maalumu kwa ugonjwa huu na hata bila tiba dalili huisha zenyewe ndani ya wiki mbili". Amesema Prof Ruggajo.


Prof. Ruggajo amesema mwenendo wa ugonjwa huo unaonyesha kuna ongezeko kubwa la wagonjwa wanaofika katika Vituo vya kutolea huduma za afya wakiwa wanasumbuliwa na ugonjwa huo. 


“Katika kipindi cha Desembe 22, 2023 hadi Januari 11, 2024 kumekuwa na ongezeko kubwa la watu wanaosumbuliwa na ugonjwa huu kufika katika vituo vya kutolea huduma za afya kwa ajili ya matibabu, kwa mfano katika mkoa wa Dar Es Salaam kuna wagonjwa wapya 869 huku hali ya kawaida katika kipindi cha mwezi Desemba 2023 kulikuwa na wagonjwa 17 pekee” amefafanua Prof. Ruggajo.


Aidha amesisitiza suala la usafi ni jambo muhimu katika kuzuia maambukizi kusambaa kwa wengine Kutokana na tabia ya ugonjwa huu kusambaa kwa kasi, maambukizi haya huleta mlipuko ambao husambaa kupitia kirusi kwa asilimia zaidi ya 80%.


Prof Ruggajo amewashauri wananchi kutokutumia dawa zisizo rasmi na ambazo hazijaandikwa na daktari kwa wakati huo na kutotumia dawa za macho anazotumia mgonjwa mwingine ili kuepuka madhara kwa kuwa dawa za macho ni tofauti na kwa matumizi tofauti.

MAJIMBO 214 KUNUFAIKA NA UGAWAJI WA VIFAA TIBA VYA SHILINGI BILIONI 14.9

January 05, 2024 Add Comment

 Na. WAF - Dar es Salaam 

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu leo Januari 5, 2023 amezindua usambazaji wa Vifaa Tiba (nje ya vilivyopangwa kununuliwa kwenye Bajeti ya 2023/24) vitakavyosambazwa katika majimbo yote 214 nchini Tanzania Bara.

Waziri Ummy amesema Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa fedha za nyongeza Tsh. Bilioni 14.9 mwezi November 2023 na kununuliwa vifaa hivyo ili kuendelea kuboresha huduma za Afya ya uzazi, mama na mtoto.

Miongoni mwa vifaa ambavyo Waziri Ummy amepokea ni pamoja na vitanda vya wagonjwa 3,080, vitanda vya kujifungulia 1,000, magodoro 5,500, mashuka 36,808, pamoja na meza za vutanda 306. 

“Tunategemea kupokea vifaa tiba vingine hivi karibuni ambavyo ni vitanda vya kujifungulia (4280), vitanda vya kufanyia uchunguzi (examination table) 4280, mkoba wa vifaa vya kujifungulia (delivery kit) 4280, kabati za vitanda (bed side lockers) 6420 na stendi ya dripu (6420).” Amesema Waziri Ummy.

Waziri Ummy amesema takwimu zinaonesha asilimia 86 ya wanawake wajawazito Tanzania wanajifungulia katika Zahanati, Vituo vya Afya na Hospitali za Halmashauri, vifaa hivyo vitakwenda kusaidia kuboresha huduma za Afya ya uzazi, mama na mtoto.

Amesema, katika Kila jimbo litapata Vitanda 30, Magodoro 30, Mashuka 60, Bed side locker 30, Drip Stand 30, Meza ya kulia chakula 15, Vitanda vya kujifungulia 10, Delivery set 10 pamoja na Examination bed 10. 

“Waheshimiwa Wabunge watavikuta vifaa hivi kwenye vituo viwili katika kila jimbo ambapo Bohari ya Dawa (MSD) watashusha mzigo huu.” Amesema Waziri Ummy

Mwisho, Waziri Ummy amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuiwezesha Sekta ya Afya kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuboresha huduma za afya ambapo imeweza kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi.

“Vifo vimepungua kutoka vifo 556 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2016 hadi vifo 104 kwa vizazi hai 100,000 ikiwa lengo la Dunia ni Tanzania kupunguza vifo vya wajawazito kufikia vifo 70 kila vizazi hai 100,000 ifikapo mwaka 2030.










TANZANIA YAPIGA HATUA KATIKA VIASHIRIA VYA AFYA YA MAMA NA MTOTO, TAKWIMU ZA VIFO ZASHUKA

January 05, 2024 Add Comment

 



Waziri wa Afya Mh. Ummy Mwalimu amesema taarifa za utafiti wa Demographia ya Afya ya Uzazi na Viashiria vya Malaria (TDHS/MIS) ya mwaka 2022 zinaonesha kuwa Tanzania imepiga hatua katika viashiria vingi vya afya ya mama na mtoto.

Ametoa mfano kuwa Vifo vitokanavyo na Uzazi vimeshuka kutoka 556 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2015/16 hadi 104 kwa kila vizazi hai 100,000 na vifo vya Watoto chini ya miaka mitano vimeshuka kutoka 67 kati ya vizazi hai 1000 mwaka 2015/16 hadi 43 kwa kila vizazi hai 1000. Hii ni sawa na kupunguza vifo vya kinamama wajawazito kutoka 11,000 hadi vifo 2,500 kwa mwaka.

Waziri Ummy Mwalimu ameyasema hayo Leo wakati usinduzi wa usambazaji wa vifaa vya uboreshaji wa huduma za mama na motto uliofanyika kwenye makao Makuu ya Bohari ya Dawa MSD jijini Dar es Salaam Leo Ijumaa Januari 5,2024.

Amesema hizi ni jitihada zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na wadau wa afya katika kuhakikisha kuwa Nchi yetu inafikia malengo ya kitaifa na kimataifa kama vile malengo endelevu ya Milenia 2030 yanayotutaka kupunguza athari za vifo vitokanavyo na uzazi hadi kufikia vifo chini ya 70 katika kila vizazi 100,000 vifo vya Watoto chini ya 38 katika kila vizazi hai 1,000 pamoja na vya Watoto chini 12 katika vizazi hai 1,000.


Ummy Mwalimu ameongeza kuwa serikali imeendelea kuwekeza katika afya ya mama na mtoto kwa kujenga vituo vya huduma za upasuaji wa kumtoa mtoto tumboni (CEmONC) kutoka vituo 340 mwaka 2021 hadi kufikia vituo 523 mwaka 2023. Maboresho ya upatikanaji huduma hizi katika vituo vya kutolea huduma za afya yamesogeza huduma hizo za upasuaji karibu na wananchi. zaidi ya asilimia 75 85 ya wananchi wanapata huduma za Afya ndani ya Kilometa 5 ndani ya maeneo wanayoishi.

Amesema hali kadhalika Serikali imeendelea kuwekeza katika Huduma za Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto kwa kujenga Wodi za uangalizi maalumu (NCU za watoto wachanga) zinazohudumia watoto wachanga walio mahututi kwa mara mbili zaidi kutoka 99 mwaka 2021 hadi 189 mwaka 2023. Hizi ni hatau zinazochukuliwa na Serikali katika kutoa huduma bora za afya na kuokoa maisha ya watoto wanaozaliwa wakiwa chini ya kilo moja.
Sambamba na kuboresha huduma hizo Serikali imeendelea kununua na kusambaza vifaa tiba na dawa hivyo kuongeza wigo wa upatikanaji bidhaa za afya ya uzazi kutoka asilimia 82.5 mwaka 2022 hadi kufikia asilimia 88.2 mwaka 2023.

Aidha amesema Serikali imeendelea kuajiri na kupeleka watumishi wenye sifa katika Vituo vya kutolea huduma za afya nchi nzima kuajiri watumishi wa afya wapatao 28,759 hadi kufikia mwaka 2023.

Akizungumza kuhusu kuhusu Vitanda vua kutolea huduma za afya ya Uzazi, Serikali kwa kushirikiana na wafau amesema selikali imeendelea kuboresha upatikanaji wa vifaatiba hivyo kwa ajili ya huduma za afya ya uzazi ambapo hali ya vitanda vya kutolea huduma kwenye vituo vya afya imeongezeka kutoka vitanda 84,162 (mwaka 2021) hadi vitanda 104,687 (mwaka 2023).

Amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa ununuzi wa vifaa tiba hivi ambavyo vina thamani ya TZS 14,953,854,357 ambavyo ni vitanda vya wagonjwa (3080), vitanda vya kujifungilia (1000), magodoro (5500), mashuka (36808), meza za vitanda (overbed table) 306. Vifaa hivi vitasambazwa katika Majimbo yote 214 nchini Tanzania Bara.

Aidha wizard inategemea kupokea vifaa tiba vingine hivi karibuni ambavyo ni vitanda vya kujifungulia (4280), vitanda vya kufanyia uchunguzi (examination table) 4280, mkoba wa vifaa vya kujifungulia (delivery kit) 4280, kabati za vitanda (bed side lockers) 6420 na stendi ya dripu (6420).

Amesema wizara itagawa kila jimbo vifaa hivyo ambapo Kila jimbo litapata Vitanda 30; Magodoro 30; Mashuka 60; Bed side locker 30; Drip Stand 30; Meza ya kulia chakula 15; Vitanda vya kujifungulia 10; Delivery set 10 pamoja na Examination bed 10. Waheshimiwa Wabunge watavikuta vifaa hivi kwenye vituo viwili katika kila jimbo ambako MSD watashusha mzigo.

Waziri Ummy amesema ana imani kwamba, vifaa hivi vilivyotolewa leo vitachangia katika kuboresha zaidi huduma hizi za mama na mtoto. Aidha ametoa rai kwa Bohari ya dawa kuhakikisha vifaa tiba hivi vinasambazwa kwa wakati.
MAZUNGUMZO YA SIMU HUATHIRI USIKIVU

MAZUNGUMZO YA SIMU HUATHIRI USIKIVU

January 05, 2024 Add Comment





Na. Raymond Mtani BMH-DODOMA

Imeelezwa kuwa kuzungumza kwa njia ya simu kwa muda mrefu kinaweza kuwa chanzo mojawapo cha kupoteza usikivu.

Hayo yamesemwa na Leonard Tibihika, Mtaalamu wa Upimaji Usikivu wa Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) katika mahojiano maalumu kuhusu huduma za uchunguzi wa Usikivu Hospitalini hapo, leo Januari 5, 2024.

“isitafsirike vibaya, si kila anayeongea na simu anahatarisha usikivu, bali yule anayetumia muda mrefu kuongea na simu, kwa sababu mgandamizo wa sauti inayoingia sikioni ukiendelea kwa muda mrefu huathiri Ngoma ya Sikio” Alisema Tibihika.

Watu wengine waliyoko katika hatari ya kupoteza usikivu ni wale wanaofanya kazi katika mazingira ya kelele, alisema Mtalaamu huyo akitolea mfano, wafanyakazi wa viwandani na wanaokesha kwenye klabu za muziki, na wale wenye shughuli katika masoko.

“changamoto anayoweza kukutana nayo mtu anayepoteza usikivu ni kutogundua mapema kuwa usikivu wake hauko katika kiwango cha kawaida, akachukua hatua kwa sababu usikivu hupungua polepole wakati mwingine hadi ambiwe na wengine” Tibihika.

Kuchelewa kugundua kuwa usikivu unapotea, au kugundua na kutochukua hatua za kuchunguzwa ili kutibiwa husababisha watu wengi kufika Hospitali wakiwa katika hatua mbaya kiasi cha kuhatarisha kupoteza usikivu kabisa.

Taarifa za Vituo vya Udhibiti na Kukinga Magonjwa (CDCs) zinadokeza kuwa, Watoto na Vijana wadogo milioni 5.2 na watu wazima milioni 26 hupoteza uwezo wa kusikia kutokana na kuwa kwenye mazingira ya kelele.

Katika moja ya tafiti kuhusu kupoteza usikivu kwa matumizi makubwa ya simu uliyobandikwa katika tovuti ya Shirika la Afya Duniani (WHO), unathibitisha kuwa matumizi ya zaidi ya dakika 60 kila siku yanaweza kuathiri usikivu wa binadamu ndani ya miaka 5.

Tibihika, anatoa wito kwa watumiaji wa simu kwa muda mrefu, kuchukua hatua za kujikinga, pamoja na kuhakikisha wanafanyiwa uchunguzi wa usikivu angalau mara mbili ndani ya miezi 12.

Hospitali ya Benjamin Mkapa, ni miongoni mwa Hospitali tatu za serikali nchini zinazotoa huduma za uchunguzi wa usikivu kwa kufanya vipimo vya aina zote, asilimia kubwa ya wagonjwa wanaopoteza usikivu hubainika kuwa na tatizo la kupasuka Ngoma ya Sikio.