WAFANYAKAZI wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Kanda ya Mashariki wamefanya mazoezi ya kukimbia umbali wa takribani kilomita saba katika eneo la Coco Beach jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya kujiweka katika hali nzuri ya kiafya na utayari wa kutekeleza majukumu yao.
Akizungumza baada ya zoezi hilo leo Agosti 22, 2026 Jijini Dar es Salaam, Mhifadhi Mwandamizi wa TFS, Sunday Nachule, kwa niaba ya Kamanda wa Kanda ya Mashariki, amesema mazoezi hayo ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha askari wanakuwa timamu muda wote kwa ajili ya kutekeleza majukumu yao.
Amesema TFS itaendelea kuhamasisha watumishi wake kushiriki katika mazoezi ya mwili mara kwa mara ili kujenga afya na utayari wa kiutendaji.
Katika zoezi hilo, wanafamilia wa TFS wamepata pia fursa ya kufanya mazoezi pamoja na Mbunge wa Jimbo la Buchosa, Eric Shigongo, ambaye amewapongeza kwa juhudi hizo na kuwataka kuendelea na mazoezi.
Shigongo amesema misitu ni muhimu kwa uhai wa binadamu kutokana na mchango wake katika upatikanaji wa hewa safi na maji, hivyo wananchi wanapaswa kushirikiana na Serikali katika kuilinda.
Ametaja maeneo ya Buhindi na Lubondo yaliyopo katika Jimbo la Buchosa kuwa miongoni mwa maeneo yenye misitu inayosimamiwa na TFS, akisisitiza umuhimu wa wananchi kutunza rasilimali hiyo.
“Bila misitu hakuna uhai. Kwa hiyo nawaomba Watanzania waendelee kutunza misitu kwa sababu ni chanzo cha hewa na maji,” amesema Shigongo.
Aidha, ameipongeza TFS kwa kazi inayofanya katika kulinda na kuhifadhi misitu nchini, akieleza kuwa wananchi wanapaswa kuwa wadau wa uhifadhi kwa kuhakikisha rasilimali hiyo inalindwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.











EmoticonEmoticon