
Na Mwandishi Wetu - DAR ES SALAAM,
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki, ameitaka TTCL kuhakikisha wazabuni na wakandarasi wanaotekeleza Awamu ya Pili ya Mradi wa Faiba Mlangoni Kwako wanasimamiwa kwa ufanisi ili kazi zikamilike kwa wakati, kwa ubora na kwa kuzingatia thamani ya fedha.
Mhe. Kairuki amesema usimamizi wa mradi ni muhimu katika kuhakikisha uwekezaji wa Serikali na Shirika unazalisha miundombinu inayodumu na inayotoa huduma bora kwa wananchi.

Ametoa maelekezo hayo wakati wa uzinduzi wa Awamu ya Pili ya mradi huo katika Ukumbi wa Johari Rotana jijini Dar es Salaam.
Amesema mafanikio ya mradi hayatakiwi kuishia katika kujenga Home Pass, bali yanapaswa kuonekana katika huduma zinazotolewa kwa wananchi, kasi ya intaneti na kuridhika kwa wateja.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, CPA Moremi Marwa, amesema utekelezaji wa Awamu ya Pili unafanyika kwa ushirikiano na makandarasi wa ndani na wa kimataifa wakiwemo Huawei, ZTT na Visoll.
Amesema Awamu hiyo inalenga kuongeza zaidi ya Home Pass 400,000, ikiwa ni hatua inayotarajiwa kuongeza upatikanaji wa huduma za intaneti ya kasi.
Marwa amesema TTCL pia imeendelea kutumia teknolojia ya GPON kuongeza ufanisi na kuboresha ubora wa huduma.








EmoticonEmoticon