Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii imeahidi kutoa ushirikiano kwa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi wakati wote wa kutekeleza majukumu yake.
Kauli hiyo imetolewa leo tarehe 15 Januari, 2026 na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Timetheo Mnzava wakati wa kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge na Wizara ya Ardhi kilichokuwa na lengo la kuifahamu wizara ya ardhi na taasisi zake.
Pamoja na kuifahamu wizara na taasisi zake, Kamati za Kudumu za Bunge zinatakiwa kufahamu baadhi ya sera na sheria kulingana na majukumu ya kila kamati kama ilivyofafanuliwa kwenye nyongeza ya 8 ya Kanuni za Kudumu za Bunge chini ya Kanuni ya 140 ya Kanuni za Bunge inayoelekeza Kamati kupitishwa kwenye majukumu yake ya msingi na Kamati ya Bajeti kufanya maandalizi ya Hoja zitakazojadiliwa na Bunge.
Mwenyekiti huyo wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii ambaye ni Mbunge wa jimbo la Korogwe vijijini amesema, kelele ni nyingi katika masuala ya ardhi lakini wao kama kamati wataendelea kuwa pamoja na wizara kuhakikisha migogoro ya ardhi inatatuliwa na kazi ya kushughulikia changamoto za sekta ya ardhi inakuwa nyepesi.
Kwa upande wake Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo aliwashukuru wajumbe wa kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii kwa michango yao aliyoieleza kuwa ina lengo la kuboresha sekta ya ardhi nchini.
"Sisi wizara tutahakikisha tunapokea ushauri na maoni yenu na kuyafanyia kazi ili tuwe na matokeo chanya katika sekta ya ardhi" amesema mhe Dkt Akwilapo.
Vikao vya Kamati za Kudumu za Bunge ni kwa ajili ya maandalizi ya Mkutano wa 2 wa Bunge la 13 unaotarajiwa kuanza Jumanne, tarehe 27 Januari, 2026.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Kaspar Mmuya, Katibu Mkuu Mhandisi Anthony Sanga, Naibu Katibu Mkuu Bi Lucy Kabyemera, wajumbe wa Menejimeti pamoja na Wakuu wa taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo.
-----------------mwisho------------






EmoticonEmoticon