WANANCHI KUNUFAIKA NA HUDUMA ZA KIJAMII MRADI WA LNG MKOANI LINDI

December 19, 2025


📌*Ndejembi asisitiza TPDC kutanguliza uzalendo katika utekelezaji wa mradi*


Waziri wa Nishati Deogratius Ndejembi ameeleza kuwa utekelezaji wa mradi wa kubadilisha gesi asilia kuwa kimiminika ( LNG)  unatarajiwa kuwanufaisha wazawa kwa kiasi cha takribani dola za Marekani milioni 10 (USD 10M) pindi mradi huo utakapoanza kupitia shughuli za uwajibikaji kwa jamii (CSR), pamoja na kuliingizia taifa mapato mbalimbali yakiwemo kodi za zuio na kodi ya mapato ya kampuni. 

Akizungumza katika kikao na Watendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC)  kilichofanyika katika Ofisi za Wizara ya Nishati, Mtumba jijini Dodoma, Waziri Ndejembi amesema kuwa mradi huo utakaotekelezwa katika kijiji cha Likong'o mkoani Lindi ni wa kimkakati kwa maendeleo ya taifa, hivyo ni muhimu kufuata taratibu na miongozo iliyopo ili kuhakikisha Watanzania wananufaika kikamilifu na rasilimali hiyo.

Ameongeza kuwa Halmashauri zitafaidika moja kwa moja kupitia miradi ya maendeleo itakayotekelezwa katika maeneo husika.

Ndejembi amesema mradi huo utafungua fursa kwa sekta nyingine za uzalishaji ikiwemo sekta ya madini na sekta nyingine muhimu, hatua itakayochochea ukuaji wa uchumi wa taifa.

 Katika kikao hicho amesisitiza umuhimu wa kutoa elimu kwa Watanzania mapema kuhusu mradi huo wa gesi asilia na faida zake ili kujenga uelewa na uungwaji mkono wa wananchi.

Kwa upande mwingine  Mhe. Ndejembi, amewataka wataalamu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kuzingatia uzalendo na kutanguliza maslahi mapana ya taifa katika utekelezaji wa mradi wa kuchakata gesi asilia kuwa kimiminika ( LNG).



Share this

Related Posts

Previous
Next Post »