Na. Mwandishi Wetu, Dar.
UONGOZI mpya wa Chama cha Waandishi wa habari Mkoa wa Dar es Salaam (Dar es Salaam Press Club) DPC chini ya Mwenyekiti wake Bakari Kimwanga, umekabidhiwa rasmi ofisi tayari kwa majukumu mapya ya kuendesha Klabu hiyo kutoka kwa mtangulizi wake, Sam Kamalamo.
Hafla ya makabidhiano hayo imefanyika katika ofisi za DPC zilizopo Posta Mtaa wa Samora na kushuhudiwa na wajumbe wapya wa Bodi sambamba na Wakili wa Kujitegemea, Rafael Awino.
Tukio hilo la makabidhiano limefanyika kwa upekee na uwazi kwa pande zote huku Uongozi uliopita na wa sasa kila mmoja akiahidi ushirikiano kwa mwenzake.
Akizungumza baada ya makabidhiano hayo, Kimwanga amesema:
"Tumekuja kunusuru Klabu, kwa kuwa hatutaki iende shimoni.
Kimwanga ameongeza kwa kuwa wanategemeana, wataendelea kuheshimu Uongozi uliopita na hata kuomba ushauri kila watakapohitaji.
"Tunahitaji taasisi iliyo huru, itakayosimamia umoja maadili na taaluma miongoni mwa Wanachama wake. Tusihukumu kwa mabaya, tukumbuke mema ya wale waliopita.
...Tuchukue na kuanza na mema, twende nayo kwa manufaa yetu sote." Ameeleza Kimwanga.
Aidha, Amesema Klabu inahitaji kujenga heshima ya kipekee, kurejesha matumaini hivyo anakwenda kusimamia uchukuaji wa maamuzi magumu, Akisisitiza mshikamano na kufanya kazi kwa pamoja baina ya Wanachama na viongozi.
Februari 28, 2025 katika ukumbi wa mikutano wa Anatouglo Ilala, DPC ilifanya Mkutano wake Mkuu na Kimwanga alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Chama hicho baada ya kutangazwa rasmi na Mwenyekiti wa Kamati huru ya uchaguzi Wakili wa Kujitegemea, Raphael Awino.
Aidha, katika tukio hilo la makabidhiano ,wengine walioshuhudia ni pamoja na Makamu Mwenyekiti, Mary Geoffrey, na Wajumbe watano, ambao ni Selemani Jongo, Penina Malundo, Andrew Msechu, Khamis Miraji na Veronica Mrema.
Mwisho.
EmoticonEmoticon