Na Dk. Reubeni Lumbagala
Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni chama kikongwe nchini, sasa kimetimiza miaka 48 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1977. Ukongwe wa chama hiki, si tu katika umri wake tangu kuanzishwa kwake, lakini pia uzoefu wake, kwa maana ya kuwa na rundo la watu wazoefu lakini pia katika kuwa na sera nzuri na bora zinazogusa maisha ya wananchi hasa katika kuwaletea maendeleo kwa kuzingatia kuwa msingi wa mamlaka unatoka kwa wananchi.
Kwa kuwa lengo kuu la chama chochote cha siasa ni kushika dola, naiona CCM ilivyodhamiria kikamilifu kuendelea kushika dola kwa kuhakikisha kuwa kinasuka vyema kikosi chake ili kurahisisha ushindi katika uchaguzi mkuu wa Oktoba, 2025.
Kwa sauti moja, katika Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM Taifa uliofanyika kwa siku mbili mfululilizo kuanzia Januari 18 hadi 19, 2025 jijini Dodoma, uliwapitisha Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya chama hicho, na Dk. Hussein Mwinyi kugombea Urais kwa upande wa Zanzibar.
Kazi kubwa na zuri zilizofanyika Tanzania Bara na Zanzibar hasa katika utekelezaji wa ilani ya CCM ya mwaka 2020-2025, imekuwa ni kielelezo tosha cha kuwapendekeza wawili hao waendelee na awamu nyingine ya uongozi wa nchi yetu ili waendelee kumalizia programu zao mbalimbali na wananchi waendelee kufaidi matunda ya maendeleo yanayosimamiwa kikamilifu na Dk. Samia Suluhu Hassan na Dk. Hussein Mwinyi (kwa upande wa Zanzibar).
Kukubalika kwao kwa wananchi ambao ni mashuhuda wa kazi nzuri zilizofanyika katika mitaa, vitongoji, vijiji, wilaya na mikoa yao hususani utekelezaji wa miradi ya maendeleo na ya kimkakati ambayo inagusa maisha yao moja kwa moja, kunamaliza mjadala wa kuwa wanatosha au hawatoshi kuendelea kushika nafasi zao.
Vitendo vina sauti kubwa kuliko maneno, na hapa nawaona Dk. Samia Suluhu Hassan na Dk. Hussein Mwinyi katika majukwaa ya kampeni watakavyokuwa wakionesha kazi nzuri walizozifanya, na kuja na kazi mpya ambazo zitakuwa katika Ilani ya uchaguzi ya chama hicho ya mwaka 2025-2030 ili waendelee kuwatumikia wananchi.
Katika kusuka kikosi bora zaidi cha CCM, Katika Mkutano Mkuu Maalum huo, uliridhia pendekezo la Rais Dk. Samia la kumpendekeza Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Emmanuel Nchimbi kuwa mgombea mwenza wake katika uchaguzi utakaofanyika Oktoba 2025.
Dk. Nchimbi ambaye sasa ni suala la muda tu lakini ndiye Makamu wa Rais ajae, ni mwanasiasa mwenye sifa nyingi ambaye pengine ukitafuta mtu kama yeye kwenye kambi ya upinzani unaweza usimpate!
Huyu ni mwanasiasa msomi, aliyekulia ndani ya chama, akishika nafasi mbalimbali za ndani ya chama na serikalini kama vile Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Mkuu wa Wilaya (DC), Mbunge wa Songea Mjini, Naibu Waziri, Waziri kamili, Balozi nchini Brazil na Misri na Katibu Mkuu wa CCM Taifa. Huyu mwamba ni kiungo muhimu katika kikosi cha CCM kuelekea uchaguzi wa mwaka huu.
Sambamba na hilo, Mkutano Mkuu Maalumu huo pia ulimchagua kwa kishindo mwanasiasa mkongwe nchini, Stephen Wasira kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara) kufuatia kujiuzulu kwa Abdulrahman Kinana mwaka jana.
Stephen Wasira nae ni kiungo muhimu katika chama. Ana uzoefu mkubwa katika chama na serikali kwani ameshashika nyadhifa nyingi kwenye TANU na CCM, amewahi kuwa Mkuu wa Mkoa, Mbunge, Naibu Waziri, Waziri kamili. Baada tu ya kuchaguliwa na wajumbe kwenye Mkutano Mkuu Maalum, Wasira alisema; "Kazi ya chama hiki imeelezwa kwenye ibara ya 5 ya katiba ya CCM ambayo ni kushinda uchaguzi, kukamata dola ya Jamhuri ya Muungano na Zanzibar na serikali za mitaa. Sasa kazi tuliyonayo ni kukamata dola ya Jamhuri ya Muungano na Jamhuri ya Zanzibar. Ndugu zangu Waislamu wanasema kanzu ya Ijumaa inafuliwa Alhamisi, sasa hivi wamebadilisha, wanasema tufue Jumatano, sasa Jumatano imeshapita tumechukua serikali za mitaa, Sasa tujiandae ifikapo Oktoba, kazi ya kuchukua dola inakamilika."
Wasira ni miongoni mwa Watanzania wenye uwezo mkubwa wa kujenga hoja na majibu ya uhakika. Mtu ambaye ukija na hoja za kistaarabu na kiakili atakujibu kistaarabu na hoja za mihemuko, ubabe na upuuzi pia utakujibu kwa 'saizi' yako.
Kwa hakika, upatikanaji wa viongozi hawa wanne: Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar, Mgombea Mwenza kwa upande wa Tanzania Bara na Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara) ambao wote sina mashaka nao katika uadilifu, uchapakazi, uzalendo, naamini kikosi kipo imara na ushindi utapatikana.
Mara kadhaa, viongozi wa CCM wamekuwa wakisisitiza kuwa kuelekea kwenye uchaguzi, watakaoteuliwa ni wale wanaokubalika na wananchi ili kurahisisha ushindi. Naamini baada ya kupatikana viongozi hawa, uteuzi wa viongozi bora utazingatiwa pia katika upande wa wagombea wa nafasi za ubunge na udiwani.
Ama kwa hakika ukiweka kando kazi zenye kuonekana zilizofanywa na serikali ya CCM timu hii inatisha kulinganisha na watu ninaowaona kwenye vyama vya upinzani ambao wengi ni wanaharakati waliojaa mihemuko badala ya kujipamba na sera mbadala. Watu wanaodhani kwamba adui yao ni katiba na Tume ya uchaguzi kumbe ni kushindwa kuonesha sera mbadala!
Ndio maana nasema, kwa CCM hii yenye kikosi bora kuanzia juu hadi chini, inashindwaje kwenye uchaguzi wa Oktoba, 2025? Muda utaongea na ilipeleka salamu kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka jana.
Maoni: 0620 800462
EmoticonEmoticon