DKT. KIKWETE ASHAURI MBINU ZA KUPAMBANA NA ATHARI ZA MABADILIKO YA TABIANCHI KWENYE KILIMO

February 13, 2025
Rais Mstaafu Dkt Jakaya Mrisho Kikwete akiwa na Rais wa Ethiopia Taye Atske Selassie, Rais Mstaafu wa Nigeria Goodluck Jonathan, Waziri Mkuu Mstaafu wa Niger Ibrahim Mayaki, na Waziri Mkuu Mstaafu wa Ethiopia Mhe. Hailemariam Desalegn katika kongamano la kimataifa kuhusu umwagiliaji na uzalishaji wa kilimo himilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, lililofanyika siku ya Jumatano mjini Addis Ababa, Ethiopia.

Rais Mstaafu Dkt Jakaya Mrisho Kikwete akiwa na Rais wa Ethiopia Taye Atske Selassie, Rais Mstaafu wa Nigeria Goodluck Jonathan, Waziri Mkuu Mstaafu wa Niger Ibrahim Mayaki, na Waziri Mkuu Mstaafu wa Ethiopia Mhe. Hailemariam Desalegn katika kongamano la kimataifa kuhusu umwagiliaji na uzalishaji wa kilimo himilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, lililofanyika siku ya Jumatano mjini Addis Ababa, Ethiopia.


Rais Mstaafu Dkt Jakaya Mrisho Kikwete akishiriki katika  kongamano la kimataifa kuhusu umwagiliaji na uzalishaji wa kilimo himilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, lililofanyika siku ya Jumatano mjini Addis Ababa, Ethiopia. 


Addis Ababa, Februari 13, 2025 -

 Rais Mstaafu Dkt. Jakaya mrisho Kikwete ameungana na viongozi mbalimbali wa Afrika katika kongamano la kimataifa kuhusu umwagiliaji na uzalishaji wa kilimo himilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, lililofanyika siku ya Jumatano mjini Addis Ababa, Ethiopia.

 

Katika mkutano huo, viongozi hao walijadili changamoto zinazokumba sekta ya kilimo barani Afrika, ambapo asilimia 80 ya watu wa bara hili wanategemea kilimo kama chanzo cha kipato na chakula.

 

Washiriki wengine wa kongamano hilo walikuwa Rais wa Ethiopia Taye Atske Selassie, Rais Mstaafu wa Nigeria Goodluck Jonathan, Waziri Mkuu Mstaafu wa Niger Ibrahim Mayaki, na Waziri Mkuu Mstaafu wa Ethiopia Mhe. Hailemariam Desalegn.

 

Katika mjadala ulioongozwa na Mhe. Hailemariam Desalegn, viongozi hao walibainisha kuwa mabadiliko ya tabianchi yameathiri sekta ya kilimo, huku ukame, mafuriko, vimbunga, na mvua zisizotabirika vikisababisha kushuka kwa uzalishaji wa chakula. Hali hii inazidi kuhatarisha usalama wa chakula barani Afrika.

 

Kwa upande wake, Dkt. Kikwete alisisitiza kuwa Afrika inahitaji mabadiliko makubwa ya kiutendaji kwa kuwekeza katika Kilimo cha kisasa kinachotegemea umwagiliaji, Mbegu zinazohimili ukame na mabadiliko ya tabianchi, Mbolea bora na pembejeo za kisasa pamoja na kuongeza idadi ya mabwana shamba ili kuwasaidia wakulima kuachana na kilimo cha mazoea.

 

Kuhusu uzalishaji duni wa Chakula katika Afrika, Dkt. Kikwete alitaja changamoto nyingine zinazokwamisha maendeleo ya sekta ya kilimo kama ukosefu wa mikopo kwa wakulima, masoko ya uhakika, na kiwango kidogo cha usindikaji wa mazao.

 

Alisisitiza kuwa serikali peke yake haiwezi kutatua matatizo haya, bali inahitaji kushirikiana na sekta binafsi ili kuhakikisha uzalishaji wa chakula unakuwa endelevu.

 

Akitoa mfano wa mafanikio nchini Tanzania, Dkt Kikwete alitaja mradi kama wa Ushoroba (corridor) wa Kukuza Kilimo Kusini mwa Tanzania (SAGCOT) na Jenga Kesho iliyo Bora kupitia Kilimo (BBT), ambazo zinalenga kuimarisha sekta ya kilimo nchini.

 

Akifungua kongamano hilo, Rais wa Ethiopia Taye Atske Selassie, alieleza jinsi nchi yake ilivyojitegemea kwa asilimia 100 katika uzalishaji wa ngano kutokana na mipango madhubuti ya kilimo cha umwagiliaji.

 

Alisisitiza kuwa ushirikiano kati ya nchi za Afrika ni muhimu ili kubadilishana uzoefu wa kuboresha uzalishaji wa chakula.

 

Katika kipindi hiki ambapo mataifa yaliyoendelea yamepunguza misaada yao kwa Afrika, viongozi hao walikubaliana kuwa Afrika haina budi kuwekeza katika teknolojia za kilimo na miradi ya uzalishaji wa chakula kwa njia endelevu.

 

Na kwa kutambua umuhimu wa mijadala kama hii, kongamano hili linatarajiwa kufanyika kila mwaka ili kuimarisha mshikamano wa Afrika katika kupambana na changamoto za tabianchi na usalama wa chakula.

 

MWISHO

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »