Benki ya CRDB yaandika historia kuorodhesha Kijani Bond Soko la Hisa Luxembourg

July 01, 2025

 

Luxembourg, 1 Julai 2025 – Benki ya CRDB imeweka historia kwa kuorodhesha rasmi hatifungani yake ya kwanza ya kijani maarufu kama ‘Kijani Bond’ katika Soko la Hisa la Luxembourg (LuxSE). Hatua hii inaifanya Benki ya CRDB kuwa miongoni mwa benki za kwanza za biashara Kusini mwa Jangwa la Sahara kuorodhesha hatifungani ya kijani iliyotolewa nchini katika soko hilo la kimataifa na pia kuonekana katika Soko la Hisa la Kijani la Luxembourg (LGX), jukwaa linaloongoza duniani kwa masuala ya fedha endelevu.

Kijani Bond ilizinduliwa kwa mafanikio nchini Tanzania ikivutia wawekezaji wengi na kukusanya zaidi kwa thamani ya Shilingi Bilioni 171.8 (sawa na Dola za Marekani Milioni 65.7). Kuorodheshwa kwake katika orodha rasmi ya Dhamana za Soko la Hisa la Luxembourg (LuxSE SOL) ni ushuhuda wa kuongezeka kwa mahitaji na uwezo wa Afrika kuwekeza katika miradi ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi huku ikivutia masoko ya mitaji ya kimataifa.

Hafala ya kuorodheshwa kwa hatifungani hiyo imefanyika katika kwenye makao makuu ya LuxSE, ikihudhuriwa na Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji na Luxembourg, Bw. Juma Ali Salum, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Mussa Nsekela, Afisa Mkuu wa Biashara na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya LuxSE, Arnaud Delestienne, pamoja na viongozi wengine waandamizi kutoka Benki ya CRDB, LuxSE na Orbit Securities Tanzania mawakala wa uuzaji wa dhamana hiyo ambayo pia imeorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).

Akizungumza katika hafla hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, alisema: “Kuorodheshwa kwa Kijani Bond si tu hitimisho la mchakato wa kifedha, bali ni mwanzo wa ushirikiano mpya kati ya Afrika na Ulaya katika kufadhili uchumi wa kijani. Tuna fahari kuwa waanzilishi katika nyanja hii kwa kufanikisha ukusanyaji wa zaidi ya Dola Milioni 65.7 kupitia dhamana yetu ya kwanza ya kijani, ambayo ilispata mafanikio ya zaidi ya asilimia 429. Leo, tunaipeleka safari yetu ya uendelevu katika jukwaa la kimataifa, si kwa ajili ya kupata fedha pekee, bali pia kuinua viwango vyetu vya ufadhili endelevu. Huu ni ujumbe kwa dunia: Afrika ipo tayari kuongoza katika ufadhili endelevu kwa ubunifu, uadilifu, na dhamira ya kweli.”

Kijani Bond ni hatifungani ya kwanza ya aina yake nchini Tanzania na miongoni mwa kubwa zaidi Kusini mwa Jangwa la Sahara kwa wakati wa kutolewa. Fedha zilizopatikana kupitia dhamana hii tayari zinaelekezwa katika sekta mbalimbali zenye mchango mkubwa kwa maendeleo endelevu ikiwemo: Nishati mbadala, Kilimo kinachohimili mabadiliko ya tabianchi, Nishati safi ya kupikia, Majengo rafiki kwa mazingira, Usafiri wa kijani, Maji safi na huduma bora za usafi wa mazingira, pamoja na miradi mingine inayozingatia mabadiliko ya tabia nchi.

Kwa upande wake, Arnaud Delestienne, Afisa Mkuu wa Biashara wa LuxSE, alisema: “Tunafurahia kuikaribisha Benki ya CRDB na hatifungani yake ya kijani katika soko letu. Huu ni ushahidi wa namna masoko ya mitaji ya kimataifa yanavyoweza kusaidia kupata fedha kwa ajili ya huduma muhimu na kuchochea mabadiliko ya kijani barani Afrika. Pia ni uthibitisho wa nafasi ya Afrika kama mshirika muhimu katika maendeleo ya fedha endelevu duniani.”

Akitoa salamu kutoka kwa Serikali ya Tanzania, Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji na Luxembourg, Juma Ali Salum, alieleza:

“Tukio hili ni la kujivunia kwa taifa letu na ni kielelezo cha dhamira ya Tanzania katika kushiriki kikamilifu katika ajenda ya kimataifa ya mabadiliko ya tabianchi chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Kijani Bond ya Benki ya CRDB inaonyesha dhamira ya nchi yetu kuwa mfano wa maendeleo jumuishi na yanayozingatia mabadiliko ya tabianchi.”

Benki ya CRDB ikiwa ni taasisi iliyoidhinishwa na Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (UN-GCF), inaendelea kujijengea nafasi thabiti kama kiongozi wa ufadhili endelevu katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati. Kuorodheshwa kwa Kijani Bond katika Soko la Hisa la Luxembourg kunaiwezesha benki kupanua wigo wake wa kupata mitaji ya kimataifa huku ikiimarisha mchango wake katika kusaidia jitihada za serikali kukuza uchumi wa kijani.
Kupitia dhamana hiyo, Benki ya CRDB tayari imefanikiwa kuwezesha maelfu ya wanawake na vijana kuanzisha na kukuza biashara zao, kusaidia wakulima kutumia mbinu za kilimo kinachohimili mabadiliko ya tabianchi, pamoja na kuboresha maisha ya watu katika jamii mbalimbali nchini Tanzania Kwa taarifa zaidi kuhusu Dhamana ya Kijani ya CRDB Bank, tafadhali tembelea: 🔗 https://www.luxse.com/security/TZ1996105155/416649

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »