• *_BoT yanunua dhahabu yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 570_*
• *_Asisitiza dhamira ya Tanzania kuwa miongoni mwa mataifa 10 yenye hifadhi kubwa ya dhahabu Afrika_*
• *_Abainisha kuongezeka kwa mapato yatokanayo na madini ya dhahabu_*
📍 *Dodoma*
Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, amebainisha kuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imenunua tani 2.6 za dhahabu inayochimbwa na kusafishwa hapa nchini ikiwa ni sehemu ya juhudi za kukabiliana na changamoto ya upungufu wa fedha za kigeni, kuboresha akiba ya fedha za kigeni, na kuimarisha thamani ya shilingi ya Tanzania.
Amesema hayo leo Januari 22, 2024, jijini Dodoma, wakati akiwasilisha taarifa kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, taarifa inayohusu utendaji wa viwanda vya kusafisha dhahabu nchini kwa kipindi cha Machi hadi Desemba 2024 pamoja na mwenendo wa ununuzi wa dhahabu unaotekelezwa na BoT.
*Mwenendo wa Ununuzi wa Dhahabu BoT*
Kwa mujibu wa Waziri Mavunde, tarehe 1 Oktoba 2024, Tume ya Madini ilitoa tangazo linalowataka wachimbaji na wafanyabiashara wa dhahabu kutekeleza takwa la Kifungu cha 59 cha Sheria ya Madini Sura 123, ambalo linawataka kutenga asilimia 20 ya dhahabu na kuiuzia BoT kupitia viwanda vya usafishaji vilivyoidhinishwa.
“Mheshimiwa Mwenyekiti, Tangu kutolewa kwa tangazo hilo hadi Januari 21, 2025, BoT imefanikiwa kununua tani 2.6 za dhahabu kutoka kwa wachimbaji wa kati, wachimbaji wadogo, na wafanyabiashara wa dhahabu. Thamani ya dhahabu hiyo ni zaidi ya shilingi bilioni 570 kwa mujibu wa bei ya soko la dunia ya tarehe 22 Januari 2025” amesema Mhe. Mavunde.
Halikadhalika, Waziri Mavunde amesisitiza kuwa, kupitia mpango huo wa BoT, lengo la Serikali ni kuifanya Tanzania kuwa moja ya mataifa 10 yenye hifadhi kubwa ya dhahabu barani Afrika kwa ustawi wa taifa.
*Ongezeko la Mapato ya Serikali*
Kwa upande wa mapato, Waziri Mavunde amebainisha kuwa, mwenendo wa ukusanyaji wa mrabaha kwa upande wa madini ya dhahabu umeendelea kuimarika na kwamba kuanzia Julai 1, 2024 hadi Desemba 31, 2024, Serikali iliingiza shilingi bilioni 400.22 kutokana na mauzo ya kilogramu 34,826.75 za dhahabu, ikiwa ni ongezeko la asilimia 5.55 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2023, ambapo kilogramu 32,995.54 ziliuzwa na Serikali kupata shilingi bilioni 278.86.
*Maendeleo ya Kiwanda cha Kusafisha Makinikia – Kahama*
Katika hatua nyingine, Waziri Mavunde aligusia maendeleo ya Kiwanda cha Kusafisha Makinikia cha Tembo Nickel Refining Limited, kitakachojengwa Kahama, mkoani Shinyanga katika eneo ambalo awali lilikuwa likitumiwa na Mgodi wa Buzwagi, ambao umesitisha shughuli za uzalishaji wa dhahabu.
Amefafanua kuwa mradi wa Kiwanda hicho ni moja ya miradi machache barani Afrika inayozalisha bidhaa iliyotayari kwa matumizi, hivyo unatarajiwa kuleta tija kubwa kwa uchumi wa nchi, sambamba na kuimarisha Mchango wa Sekta ya Madini.
*Faida za Mpango wa BoT*
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Dkt. Mathayo David, amepongeza juhudi hizo na kueleza kuwa hatua hiyo itasaidia kuimarisha shilingi ya Tanzania, kuimarisha akiba ya dhahabu, na kuiweka nchi katika orodha ya mataifa yenye hifadhi kubwa ya dhahabu ulimwenguni.
Juhudi hizo ni sehemu ya mikakati ya Serikali kupitia Wizara ya Madini kuhakikisha kuwa Sekta ya Madini inatoa mchango mkubwa zaidi kwa uchumi wa Taifa na ustawi wa wananchi.
EmoticonEmoticon