WANANCHI WAHAMASISHWA KUCHANGAMKIA FURSA

October 24, 2024

-NI YA UJENZI NA UENDESHAJI WA VITUO VIDOGO VYA BIDHAA ZA MAFUTA VIJIJINI

-MKOPO WA HADI SHILINGI MILIONI 133 KUTOLEWA

Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inahamasisha wananchi kuchangamkia fursa ya mikopo kwa ajili ya Kuwezesha ujenzi na Uendeshaji wa vituo vidogo vya bidhaa za mafuta ya Petroli na Dizeli kwa maeneo ya vijijini.

Meneja Usaidizi wa Kiufundi kwa Waendelezaji Miradi REA, Mhandisi Emanuel Yesaya amesema hayo Jijini Dar es Salaam Oktoba 24, 2024 katika Kongamano la 10 la Jotoardhi (ARGeo-C10).

"Hii ni fursa kwa wajasiriamali, makampuni, vikundi ama mtu mmoja mmoja kupata mkopo nafuu na kuwekeza maeneo ya vijijini kwa kujenga na kuendesha kituo cha bidhaa za mafuta ya petroli na dizeli," alisema Mhandisi Yesaya.

Mhandisi Yesaya alisema Serikali inatambua maeneo mengi ya vijijini yana uhaba wa mafuta na kwamba wananchi wanatumia madumu kuuzia mafuta ya bidhaa za petroli na dizeli ambayo si salama na ni hatarishi kwani inaweza kusababisha mlipuko na ajali za moto.

Alisema ili kuondokana na hatari hiyo sambamba na kumpunguzia mwananchi wa maeneo ya kijijini adha ya kutembea umbali mrefu kufuata bidhaa hizo Serikali kupitia REA imekuja na mpango huo maalum wa mkopo wenye riba ya hadi asilimia 5 ambayo inalipwa ndani ya kipindi cha miaka saba.

"Tunatoa wito kwa wananchi kuchangamkia fursa ambayo imetangazwa na Wakala ya kupata mkopo nafuu wa hadi shilingi milioni 133 kwa ajili ya kujenga na kuendesha vituo vya bidhaa za mafuta maeneo ya vijijini," alisisitiza Mhandisi Yesaya.

Alibainisha kuwa Mkopo huo unahusisha ujenzi wa Kituo cha bidhaa za mafuta ambacho kitakuwa na pampu yenye mikonga miwili mmoja wa Dizeli na mwingine Petroli, matenki ya kuhifadhi mafuta ya ujazo wa kati ya lita 10,000 hadi 15,000 na mwombaji anapaswa kuwa na eneo lisilopungua mita za mraba 924.

Mhandisi Yesaya alitoa wito kwa wananchi kutembelea tovuti ya Wakala ambayo aliitaja kuwa ni www.rea.go.tz ili kupata taarifa zaidi kuhusiana na fursa hiyo ikiwa ni pamoja na Mwongozo wa utoaji mkopo na Fomu ya maombi.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »