Arusha, 24 Oktoba, 2024
Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) iimeeleza itaendelea kufanya kazi kwa bidii kila siku ili kuhakikisha miundombinu yake ya barabara na madaraja inakuwa bora na fursa kwa watumiaji wa ndani na nchi jirani za Jumuia ya Afrika Mashariki na Jumuia ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Kauli hiyo imetolewa leo na Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Mohamed Besta katika mkutano wa 17 wa Ufuatiliaji na Tathmini ya Sekta ya Uchukuzi unaofanyika jijini Arusha kuanzia tarehe 23 hadi 25 Oktoba, 2024.
“TANROADS ni taasisi muhimu katika uwezeshaji wa usafiri na usafirishaji nchini ambapo tumeendelea kufanya kazi kwa bidii sana ili kuhakikisha miundombinu yetu inakuwa bora zaidi, kwa kusimamia miradi mikubwa yote ambayo ni chachu ya maendeleo katika uchumi wa nchi yetu,” amesema Mha. Besta.
Mha. Besta amesema malengo ya TANROADS ni pamoja na kukuza ubora wa barabara katika majiji kwa kujenga madaraja ya juu na kufanya upanuzi wa barabara kuu zinazoingia katika majiji makuu, zikiwemo za Jiji la Arusha, ambapo sasa wanakamilisha usanifu wa barabara ya Arusha hadi Tengeru na USA River, na katika mkoa wa Kilimanjaro ujenzi wa barabara ya Kibosho na daraja la Kikavu na kwa Jiji la Mwanza barabara unganishi ya Usagara kwenda daraja la J.P Magufuli na upanuzi wa barabara ya Ubungo hadi Kimara kwa Jiji la Dar es Salaam.
Amesema pia TANROADS itaendelea kujenga madaraja ya juu katika Jiji la Dar es Salaam eneo la makutano ya Morocco na Mwenge, pia yatajengwa Jijini Arusha na sehemu nyingine nchini, na yote haya yanafanyika na kusaidia wananchi wanapata usafiri wa haraka.
Hatahivyo, ametoa wito kwa watumiaji wa barabara kuhakikisha wanazitunza kwa kufuata viwango vilivyowekwa vya uzito wa magari na kutozidisha uzito kwenye magari ya mizigo, na kuacha tabia ya kutoa alama za barabarani kwa kuzifanyia matumizi mengine ambayo hayajakusudiwa, maana wanahatarisha usalama wa watumiaji wa barabara hizo.
EmoticonEmoticon