SERIKALI, SEKTA BINAFSI KUENDELEA KUSHIRIKIANA KUTUMIA TEKNOLOJIA ZA KISASA KUTOA HUDUMA BORA

October 04, 2024



Na WAF, DAR ES SALAAM

Serikali kupitia Wizara ya Afya imezitaka Hospitali zote nchini ikiwemo za Sekta binafsi kuwekeza kwenye matumzi ya teknolojia na miundombinu za kisasa katika kutoa huduma za Afya ili kuendana na mabadiliko ya sasa ya sayansi na teknolojia.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa wizara ya Afya Dkt. John Jingu leo October 4,2024 alipotembelea Hospitali Binafsi ya Kairuki iyopo jijini Dar es Salaam na kujionea hatua mbalimbali za maendeleo ya utoaji wa huduma bora za afya katika Hospitali hiyo.

“Ajenda yetu Kubwa kwa sasa ni ubora wa huduma unaoendana na mazingira ya sasa hivi na mazingira ya dunia ya sasa ni ya kiteknolojia, tumetoka kuwapongeza wenzetu wa Hospitali ya Kairuki kwa uwekezaji mkubwa walioufanya, Lakini pia mnafahamu Serikali imewekeza kwenye Hospitali za umma na kununua vifaa vya teknolojia mbalimbali za kisasa ambazo zinatuwezesha kuto huduma bora.” Amesema Dkt. Jingu

Adha Dkt. Jingu ameipongeza Hospitali ya Kairuki na nyinginezo za sekta binafsi kwa namna zinavyojipambanua katika kutoa huduma bora za Afya na kuwa wadau wakubwa wa serikali kwa kusaidia utoaji huduma kwa wananchi.

“Kiufupi huduma zinatolewa vizuri, sekta binafsi ni mdau Mkubwa sana katika maendeleo lakini katika eneo hili ni mdau muhimu sana kwenye utoaji wa huduma za Afya. Ukija hapa utaungana na mimi katika hili na kuona sekta binafsi inahakikisha watanzania wanakuwa na afya njema.” Amesema Dkt. Jingu

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu amezitaka Hospitali na watoa huduma za Afya ikiwemo sekta binafsi kuzingatia miongozo ya Afya katika kutoa huduma pamoja na huduma za upandikizaji mimba ambazo zimeanza kutolewa hapa nchini na kutaka huduma hizo kusambazwa vijijini.

“Wizara ya Afya inatengeneza miongozo na sera lakini pia inalea Hospitali na Vituo binafsi vya kutolea huduma ili tushirikiane kwa pamoja kutoa huduma kwa wananchi. Tumeanzisha pia huduma ya upandikizaji mimba watu wanahitaji huduma hii hivyo kuwa na huduma hizi nyingi zaidi ni wajibu wetu na tutaendelea kuhamasishana ili huduma hizi zifike mbali.” Amesema Prof. Nagu

Dkt. Asser Mchomvu ni Mkurugenzi Mkuu wa hospitali ya kairuki amesema hospitali itaendelea kuwekeza katika utoaji wa huduma bora ikiwemo huduma ya sasa ya uondoaji uvimbe bila kupasua ambayo hadi sasa imeshafanyika kwa wananchi zaidi ya mia moja.

“Zamani upasuaji ulikuwa unafanyika kwa kukata,ambapo kwanza unabaki na kidonda kisha kovu, lakini sasa hivi teknolojia imeongezeka unaweza kuondoa uvimbe bila kupasua na mtambo huo tunao hapa haukuachi na kidonda wala kovu.” Amesema Dkt. Mchomvu      

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »