ZAIDI YA WATOTO LAKI TATU, HUZALIWA WAKIWA NJITI KWA MWAKA- DKT. BITEKO

November 08, 2023

 Na WMJJWM, Dodoma


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Dotto Biteko ametoa wito kwa wadau wa masuala ya Afya ya Watoto nchini, kushirikiana kutokomeza tatizo la watoto waliozaliwa kabla ya wakati (watoto njiti).

Wito huo umetolewa kwa niaba yake na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima wakati wa hafla ya kusherehekea mafanikio ya Ajenda ya Mtoto Njiti (2021) iliyofanyika jijini Dodoma Novemba 07, 2023.

Amesema takribani watoto milioni 15 duniani huzaliwa Njiti huku nchi za Bara la Asia na Afrika hasa kusini mwa jangwa la Sahara, zikiongoza kwa asilimia 80 ya vifo vya watoto hao.

"Inakadiriwa kila mwaka watoto 336,000 huzaliwa njiti nchini Tanzania na zaidi ya watoto 11,500 hupoteza maisha kutokana na changamoto za kuzaliwa njiti. Ni kweli kwamba kiwango cha kuzaliwa kwa watoto njiti hapa nchini kimekuwa kikiongezeka. Hatuna budi kuzidisha mapambano na ningefurahi siku moja itokee taarifa kuwa hakuna vifo vya watoto njiti nchini kwetu," amesema Waziri Dkt. Gwajima.

Waziri Dkt. Gwajima ameipongeza Taasisi ya Doris Mollel Foundation kwa kuzindua na kufanikisha kuhamasisha Wizara ya Afya na wadau wote wanaotoa Bima za afya nchini kujumuisha gharama za matibabu ya watoto njiti katika mifuko yao ya bima pamoja na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kujumuisha elimu ya watoto njiti kwenye masomo ya Sayansi na Baiolojia.

Ameongeza kuwa, Serikali inaweka mikakati ya namna bora ya kupiga hatua katika masuala ya kiafya kwa raia na maisha ya watoto nchini lakini ni muhimu kuongeza juhudi za pamoja na wahisani.

Akizungumza katika hafla hiyo, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora Mhe. Ridhwan Kikwete amebainisha kwamba yeye binafsi akipata nafasi ya kuwasilisha hoja kuhusu sheria ya utumishi na likizo ya uzazi atashauri likizo ya uzazi ifikie miezi sita ili watoto njiti wapate malezi stahiki. Ameongeza kwamba sababu za kuzaliwa watoto njiti ni pamoja na Mila na Desturi pamoja na mimba za utotoni.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Ustawi na Maendeleo ya Jamii Mhe. Fatma Toufiq amesema Taasisi ya Doris Foundation imefanya kazi kubwa na kufikia hatua Serikal kutenga Bajeti ya kuhudumia watoto hao, hivyo Kamati hiyo itaendelea kupigania kuhakikisha sheria ya likizo ya uzazi inapita ili mtoto njiti aweze kupata malezi stahiki. Amewaomba Waheshimiwa Wabunge kupitisha sheria ya wanawake kukaa miezi 6 baada ya kujifungua watoto njiti na wanaume mwezi mmoja.

Awali Mkurugenzi wa Taasisi ya Doris Mollel Foundation, Doris Mollel ameelezea lengo la hafla hiyo ni kujadili namna Serikali na Wadau husika wanavyoweza kufanikisha ajenda kuu ya kisera ya watoto njiti ambayo ni kurekebishwa kwa sheria ya likizo ya uzazi ya sasa kutoka siku 84 hadi 180 ambayo ni moja ya ajenda tatu zilizozinduliwa na Kamati ya Bunge ya Huduma za Maendeleo ya Jamii na Doris Mollel Foundation mwaka 2021.













Share this

Related Posts

Previous
Next Post »