Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya
Habari (MAELEZO), Rodney Thadeus akizungumza na Maafisa Habari na
Mawasiliano Serikali wakati wa mafunzo kuhusu mwongozo wa uandishi wa
tovuti za Mikoa na Mamlaka ya Serikali za Mitaa yaliyofungwa leo Ijumaa
Machi 23, 2018 Mkoani Morogoro. Mafunzo hayo yaliandaliwa na Mradi wa
Uimarishaji Mifumo ya Sekta ya Umma (PS3) kwa kushirikiana na Ofisi ya
Rais TAMISEMI kupitia ufadhili wa Shirika la Misaada la Marekani
(USAID).
Baadhi ya Maafisa Habari na
Mawasiliano Serikalini wakifuatiliano mafunzo kuhusu mwongozo wa
uandishi wa tovuti za Mikoa na Mamlaka ya Serikali za Mitaa
yaliyofungwa leo Ijumaa Machi 23, 2018 Mkoani Morogoro. Mafunzo hayo
yaliandaliwa na Mradi wa Uimarishaji Mifumo ya Sekta ya Umma (PS3)
kupitia ufadhili wa Shirika la Misaada la Marekani (USAID).
Afisa Habari kutoka Ofisi ya Rais
(TAMISEMI) Atley Kuni akizungumza na Maafisa Habari na Mawasiliano
Serikali wakati wa mafunzo kuhusu mwongozo wa uandishi wa tovuti za
Mikoa na Mamlaka ya Serikali za Mitaa yaliyofungwa leo Ijumaa Machi 23,
2018 Mkoani Morogoro. Mafunzo hayo yaliandaliwa na Mradi wa Uimarishaji
Mifumo ya Sekta ya Umma (PS3) kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI
kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI kupitia ufadhili wa Shirika
la Misaada la Marekani (USAID).
(NA MPIGAPICHA WETU
………………….
Na Mwandishi Wetu,
MAELEZO
MOROGORO
23.3.2018
MAAFISA Habari na Mawasiliano
katika Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini,
wametakiwa kuongeza kasi ya matumizi ya mitandao ya kijamii ikiwemo
tovuti ili kuleta mageuzi yaliyokusudiwa na Serikali katika kutangaza
shughuli za maendeleo ya wananchi.
Hayo yamesemwa leo (Ijumaa Machi
23, 2018) Mkoani Morogoro na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari
(MAELEZO), Rodney Thadeus wakati wa kufunga mafunzo ya siku nne kwa
Maafisa Habari na Mawasiliano Serikalini yaliyohusu mwongozo wa
uendeshaji wa Tovuti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini
yaliyoandaliwa na Mradi wa Uimarishaji Mifumo ya Sekta za Umma (PS3) kwa
kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI kupitia Ufadhili wa Shirika la
Misaada la Marekani (USAID).
Thadeus alisema Serikali kupitia
Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Wakala ya
Serikali Mtandao (EGA) na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
kwa kushirikiana na Mradi wa Uimarishaji Mifumo ya Sekta ya Umma (PS3)
kwa pamoja waliandaa mwongozo huo ili kuhakikisha kuwa tovuti za Mikoa
na Halmashauri zinakuwa nyenzo muhimu ya taarifa za Serikali.
“Mafunzo mliyoyapata ni vyema
mkahakikishe kuwa tovuti zenu zinaweza kusaidia maendeleo ya wananchi
kwa kutangaza shughuli za maendeleo pamoja na kuzingatia thamani ya
fedha zilizotolewa na wadau wetu wa maendeleo kwa kuleta mabadiliko ya
mwonekano wa tovuti zetu” alisema Thadeus.
Aidha alisema kupitia mafunzo
yaliyotolewa kuhusu mwongozo huo, ni matarajio ya Serikali kuwa tovuti
zote za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa zitakuwa zimesheni habari
zilizoandikwa kwa usahihi pamoja na kuwekwa taarifa za mara kwa mara
hatua itayowezesha wananchi wengi Zaidi kuweza kuzitembelea na kupata
huduma zinazostahili.
Alisema Ofisi yake ipo tayari
kufanyia kazi na Maafisa Habari na Mawasilino waliopo katika Mikoa na
Mamlaka za Serikali za Mitaa iwapo kutajitokeza changamoto yoyote
inayohusu usimamizi, uendeshaji na uboreshaji wa maudhui ikiwemo mafunzo
ya mara kwa mara kwa watendaji wa tovuti hizo.
Thadeus alisema Idara ya Habari
(MAELEZO) itahakikisha kuwa inafanya mawasiliano ya mara kwa mara na
Watendaji Wakuu wa Mikoa na Halmashauri za Wilaya ili kuhakikisha kuwa
Maafisa Habari na Mawasiliano ambao ndio watendaji wa tovuti hizo
wanapata ushirikiano wa kutosha kutoka kwa Wakuu mbalimbali wa Idara na
Vitengo katika Mikoa na Halmashauri zote nchini.
Kwa upande wake, Afisa Habari
kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Atley Kuni alisema malengo ya Serikali ni
kuhakikisha kuwa tovuti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa
zinakuwa kiunganishi baina ya Serikali na wananchi kwa kuhakikisha
zinatangaza taarifa mbalimbali za mafanikio ya Serikali katika miradi
mbalimbali ya maendeleo.
Tumepanga tuwe na jarida maalum
litakalokuwa na habari mbalimbali za mafanikio ya miradi ya maendeleo,
ambazo zitakuwa zikiandikwa na Maafisa Habari na Mawasiliano waliopo
katika Mikoa na Halmashauri ambazo zitakuwa zikiakisi maendeleo
yaliyoweza kupatikana mara baada ya kuanzishwa kwa tovuti hizi” alisema
Kuni.
Aidha aliongeza kuwa Maafisa
Habari na Mawasiliano wa Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa hawana
budi kuongeza ubunifu ili kuhakikisha kuwa tovuti hizo pia zinaweza kuwa
chanzo kikuu cha mapato katikas maeneo yao ya kazi.