Mkuu
wa Mkoa wa Manyara Alexander Mnyeti, amemtumia salamu mbunge wa Jimbo
la Simanjiro James Ole Millya (Chadema) kutumia nafasi hii kuagana na
wananchi wake kwani hawezi kushinda tena ubunge wake mwaka 2020.
Mnyeti
aliyasema hayo wakati akizungumza kwenye uzinduzi wa nyumba sita za
walimu wa shule ya sekondari Emboreet kwa ufadhili wa shirika lisilo la
kiserikali la ECLAT Foundation.
Alisema
Ole Millya anapaswa kuanza kupita kwenye vijiji vya jimbo hilo kwa
ajili ya kuaga wananchi wake sababu hivi sasa wanataka kuongozwa na
mbunge wa CCM.
"Mfikishieni
salamu zangu rafiki yangu Ole Millya kwani tulikuwa naye CCM na
namuhakikishia hawezi kuwa mbunge wa jimbo la Simanjiro mwaka 2020 kwa
sababu CCM italirudisha hivyo aanze kuaga kabla hajaondoka," alisema
Mnyeti.
Hata
hivyo, Ole Millya alisema Mnyeti ni kijana mwenzake wanayeheshimiana na
waliyefahamiana kwa muda mrefu tangu wakiwa UVCCM, hivyo haamini kama
maneno hayo yametoka kinywani mwake.
Alisema
Simanjiro aliyoikuta wakati anachaguliwa mwaka 2015, ilikuwa
imeharibiwa kwa siasa za maji taka, rushwa zinazodhalilisha utu wa watu
na uuzaji wa ardhi uliokithiri.
"Kama
nia yetu ni maendeleo kwa wananchi tunaowaongoza ni muhimu kushirikiana
ili lengo litimie na Mungu akitufikisha mwaka 2020 wananchi waamue nani
wa kumpa kura kwenye nafasi ya Udiwani, Ubunge na Urais," alisema Ole
Millya.
Mnyeti
alitumia nafasi hiyo kumpigia debe mkuu wa wilaya mstaafu Peter Toima
ambaye pia ni Mwenyekiti wa shirika la ECLAT lililowekeza kwenye shule
ya sekondari ya kidato cha sita Emboreet.
"Hili
jimbo lipo wazi kwani linashikiliwa na upinzani, hivyo ndugu yangu
Toima anza kupitapita huku na huku ili uchukue ubunge na mimi nitakuunga
mkono kwa asilimia 100 kwani wewe ni mtu wa maendeleo," alisema Mnyeti
na kuongeza:
"Wana
Simanjiro mkiwa na mtu kama Toima ni sawa na kuwa na wabunge 20 hivyo
msimuache kwani yeye hana ubalozi hata wa nyumba 10 lakini amefanya
maendeleo mengi, nami nitamuunga mkono kwani siyo mbabaishaji," alisema
Mnyeti.
Alisema
Toima anapenda kunyanyua jamii yake kielimu kwani ipo nyuma mno ndiyo
sababu anapaswa kuungwa mkono na kupongezwa kutokana na mchango mkubwa
wa elimu alioutoa kwenye eneo hilo.
Mwenyekiti
wa ECLAT Foundation, Peter Toima alisema shirika hilo lilianza shughuli
za ufadhili wilayani humo na kwenye shule ya sekondari Emboreet kwa
mwaka 2015 hadi mwaka 2019 wametumia bajeti ya sh2.8 bilioni na mradi
ukikamilika baada ya miaka sita zitakuwa zimetumika sh3.5 bilioni.
Toima
alisema shule hiyo ya sekondari Emboreet ndiyo pekee wilayani Simanjiro
yenye kidato cha sita na kwenye matokeo ya kidato cha pili kwa mwaka
huu shule hiyo imeshika nafasi ya kwanza kiwilaya.
"Tuliona
eneo hili la wafugaji linakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa elimu
bora ndiyo sababu tukajenga shule hii ambao sasa hivi zaidi ya wanafunzi
200 wanalala kwenye mabweni ikiwemo wanafunzi 40 wa kidato cha sita,"
alisema.
Alisema
wamepanga bajeti ya sh480 milioni, kwa ajili ya ukamilishaji wa chuo
cha ufundi stadi Veta ambacho ni pekee kilichopo wilayani humo ili
kuwapatia vijana mafunzo ya ufundi.
Alisema
hadi kufikia mwezi Octoba mwaka huu, mradi wa chuo hicho cha Veta,
utakuwa tayari na utaanza kwa wanafunzi 24 watakaojihusisha na masomo ya
ufundi uashi.
Mkuu
wa Mkoa wa Manyara, Alexander Pastory Mnyeti akizungumza na wananchi wa
Wilaya ya Simanjiro kwenye ziara yake ya siku saba ya kukagua miradi
mbalimbali ya maendeleo, kusikiliza kero zao na kuzungumza nao kwa kutoa
maagizo na maelekezo mbalimbali kwa wananchi na viongozi wa eneo hilo.
Mkuu
wa Mkoa wa Manyara, Alexander Pastory Mnyeti akizindua ujenzi wa nyumba
ya walimu wa shule ya kidato cha sita ya sekondari Emboreet, Wilaya ya
Simanjiro iliyojengwa kwa ufadhili wa shirika lisilo la kiserikali la
ECLAT Foundation kwa kuchimba msingi kwa kutumia jembe.
Mkuu
wa Mkoa wa Manyara, Alexander Pastory Mnyeti (mwenye shati la maua)
akimsikiliza Mwenyekiti wa shirika lisilo la kiserikali la ECLAT
Foundation, Peter Kiroiya Toima, juu ya ujenzi wa chuo cha ufundi cha
Veta, ambacho kimejengwa na shirika hilo.