Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus
Nyongo hapo jana Desemba 11, 2017 alifanya ziara kwenye machimbo ya Jasi
(Gypsum) ya Mkoani Singida na kuzungumza na Wafanyabiashara na
Wachimbaji wa Madini hayo ambapo aliwahakikishia ushirikiano wa dhati wa
kufikia malengo waliyojiwekea.
Alitembelea maeneo ya machimbo ya
Madini ya Jasi na Viwanda vidogo vya uongezaji thamani ya madini hayo
ikiwemo viwanda vya kusaga madini ya Jasi ambayo unga wake unasafirishwa
nje ya Mkoa huo, viwanda vya kutengeneza chaki vilivyopo Itigi na
kiwanda cha utengenezaji wa mapambo ya majumbani kilichopo Singida
Mjini.
Naibu Waziri Nyongo yupo Mkoani Singida
kwenye ziara ya siku Tatu ya kutembelea maeneo mbalimbali ya uchimbaji
wa madini Mkoani humo ili kujionea shughuli zinazofanywa kwenye maeneo
hayo na kuzungumza na wachimbaji wa madini ili kubaini changamoto
zinazowakabili kwa lengo la kutafuta ufumbuzi wake.
Kwa mujibu wa wachimbaji wa madini
hayo, Madini ya Jasi hutumika kwa matumizi mbalimbali ikiwemo
kutengenezea chaki, hospitalini kwa watu waliovunjika na kutengeneza
viungo bandia, kutumika kutengenezea saruji, urembo majumbani, hutumika
kama insulation kwenye majengo makubwa kwa kuwa Jasi huzuia
moto, kutengenezea midoli na masanamu, kutengeneza meno bandia na pia
hutumika kama mbolea.