Ubalozi
wa Uswidi nchini Tanzania umewekeana saini makubaliano na Umoja wa
Mataifa Tanzania ambapo Uswidi imetatoa jumla ya Dola za Marekani
milioni 36 (takribani Shilingi bilioni 80.4) kwa shughuli za maendeleo
katika miaka minne ijayo. Makubaliano hayo yametiwa saini rasmi na
Balozi wa Uswidi nchini Tanzania, Mh. Katarina Rangnitt na Mratibu Mkazi
wa Umoja wa Mataifa, Bw. Alvaro Rodriguez, katika ofisi za Ubalozi wa
Uswidi jijini Dar es Salaam.
Mchango
wa Uswidi utasaidia jitihada za Umoja wa Mataifa za kuhamasisha ukuaji
wa kiuchumi ulio jumuishi na ajira na kuimarisha utawala wa kidemokrasi,
haki za binadamu na usawa wa jinsia. Mchango huo pia utasaidia kuongeza
ushiriki wa wanawake katika siasa na kuondoa vitendo vya ukatili dhidi
ya wanawake na watoto.
Akifafanua
utayari wa dhati wa Uswidi katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya
Tanzania, Balozi Rangnitt alieleza kwamba Uswidi imechagua kusaidia
shughuli za Umoja wa Mataifa zinazoakisi malengo ya maendeleo ya nchi
katika nyanja za haki za wanawake, utawala wa demokrasia na ukuaji wa
uchumi.
Shughuli hizo ni zile zinazomnufaisha kila mmoja katika kipindi ambacho Tanzania inalenga kuwa na uchumi wa kipato cha kati. “Kwa
kupitisha sehemu ya msaada wetu kupitia Mfuko wa Umoja wa Mataifa chini
ya Mpango wa Kufanya Kazi Pamoja, tunashiriki kikamilifu katika
kusaidia ufikiwaji wa malengo ya maendeleo ya Tanzania. Vilevile,
tunatambua bayana kabisa na kuthamini wajibu uliokubaliwa kuwa ndio wa
Umoja wa Mataifa katika kuleta maendeleo endelevu.
- Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa na Mwakilishi Mkazi wa UNDP, Alvaro Rodriguez akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa kutiliana saini makubaliano ya Dola za Marekani milioni 36 (takribani Shilingi bilioni 80.4) kwa shughuli za maendeleo katika miaka minne ijayo kupitia mashirika ya Umoja wa mataifa kwenye hafla fupi iliyofanyika kwenye ofisi za ubalozi huo jijini Dar es Salaam., Kushoto ni Balozi wa Uswidi nchini Tanzania, Mh. Katarina Rangnitt.
Kwa
msaada huu, tunawezesha uchukuaji hatua unaoendana na sera ya nje
inayozingatia haki za wanawake ya Uswidi na pia jitihada zinazolenga,
miongoni mwa mambo mengine, ajira yenye hadhi na haki za watoto. Hii
inadhihirisha mwendelezo wa uhusiano wa karibu na Umoja wa Mataifa na
serikali ya Tanzania wenye lengo la kuleta maendeleo yenye usawa na
jumuishi zaidi,” alisema Balozi.
Akisisitiza
utayari wa kuendelea kuisaidia Tanzania na Umoja wa Mataifa, Balozi
alitumia fursa hiyo kuthibitisha kuyapokea kwa moyo mmoja mageuzi ya
Mfumo wa UN chini ya Mpango wa Kufanya Kazi Pamoja na kutambua njia
fungamanifu zinazotumika na thamani inayopatikana kutokana na mchango wa
mashirika ya UN katika lengo moja kwa kushirikiana na serikali ya
Tanzania, washirika wa kijamii na vyama vya kiraia.
- Balozi wa Uswidi nchini Tanzania, Mh. Katarina Rangnitt akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) katika hafla hiyo fupi ya kutiliana saini makubaliano ya ya Dola za Marekani milioni 36 (takribani Shilingi bilioni 80.4) kwa shughuli za maendeleo katika miaka minne ijayo kupitia mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini.
Akizungumza
baada ya kutiliana saini makubaliano, Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa
na Mwakilishi Mkazi wa UNDP, Bw. Rodriguez alitoa shukrani kwa serikali
na watu wa Uswidi kwa msaada wao endelevu akiipongeza Uswidi kwa kuwa
mshirika wa maendeleo asiyeyumba katika shughuli za Umoja wa Mataifa
Moja na pia kwa Tanzania.
“Uswidi
imekuwa mshirika wa kuaminika wa Tanzania na Umoja wa Mataifa kwa
miongo mingi. Kwa kulenga wale walio wanyonge kabisa katika jamii hii,
rasilimali hii itatoa mchango muhimu sana katika kushughulikia mahitaji
ya wale ‘walio chini sana’ kama inavyoelekezwa katika Malengo ya
Ulimwengu,” alisema.“Mchango huu utauwezesha
Umoja wa Mataifa kuweza kufanya kazi katika masuala mapana mengi kama
vile kuhamasisha fursa za ajira zenye hadhi kwa Watanzania maskini,
kuendeleza kanuni za utawala bora, na nafasi ya uongozi wa wanawake
katika masuala ya siasa na vilevile kuzuia vitendo vya ukatili dhidi ya
wanawake na watoto,” aliongeza.
- Mtaalam wa Mawasiliano wa Umoja wa Mataifa nchini, Hoyce Temu akikabidhi hati za makubaliano kwa Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa na Mwakilishi Mkazi wa UNDP, Alvaro Rodriguez na Balozi wa Uswidi nchini Tanzania, Mh. Katarina Rangnitt wakati wa hafla fupi ya kutiliana saini makubaliano ya dola za Marekani milioni 36 (takribani Shilingi bilioni 80.4) zilizotolewa na Serikali ya Uswidi kwa ajili ya shughuli za maendeleo katika miaka minne ijayo kupita mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini.
- Balozi wa Uswidi nchini Tanzania, Mh. Katarina Rangnitt na Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa na Mwakilishi Mkazi wa UNDP, Alvaro Rodriguez (kulia) wakitiliana saini makubaliano ya dola za Marekani milioni 36 (takribani Shilingi bilioni 80.4) kwa shughuli za maendeleo katika miaka minne ijayo kupitia mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini katika hafla fupi iliyofanyika kwenye ofisi za Ubalozi wa Uswidi jijini Dar es Salaam.
- Picha juu na chini ni Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa na Mwakilishi Mkazi wa UNDP, Alvaro Rodriguez na Balozi wa Uswidi nchini Tanzania, Mh. Katarina Rangnitt wakibadilishana hati za akubaliano ya Dola za Marekani milioni 36 (takribani Shilingi bilioni 80.4) zilizotolewa na Serikali ya Uswidi kwa ajili ya shughuli za maendeleo katika miaka minne ijayo kupitia mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini.
EmoticonEmoticon