Ratiba ya Uchaguzi wa Kamati ya Uongozi ya Bodi ya Ligi Kuu
Tanzania (TPLB) utakaofanyika kesho Jumapili, Oktoba 15 mwaka huu,
itaanza saa 2.00 asubuhi hadi saa 7.15 mchana.
Saa 2.00 asubuhi, Wajumbe na viongozi wengine watawasili Ukumbi wa
mikutano wa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, kabla ya mkutano huo
kufunguliwa saa 3.00 asubuhi na Rais wa TFF, Wallace Karia atayekuwa
Mgeni Rasmi.
Kwa mujibu wa Ratiba, tunatarajiwa kuwa na mkutano na wanahabari saa 7.15 mchana mara baada ya mkutano wa Baraza hilo.
Jumla ya wajumbe 44 watashiriki Mkutano huo wa uchaguzi wa Baraza Kuu
la TPLB. Wajumbe hao ni klabu 16 za Ligi Kuu, klabu 24 za Ligi Daraja
la Kwanza na wawakilishi wanne wa klabu za Ligi Daraja la Pili.
Nafasi ya Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na wajumbe wa kuwakilisha
klabu za Ligi Kuu zitapigiwa kura na klabu 16 pekee za Ligi Kuu.
Wagombea saba wamepitishwa kuwania uongozi wa TPLB baada ya Kamati ya
sasa kumaliza muda wote. Kamati mpya ya Uongozi itakayochaguliwa katika
uchaguzi huo unaosimamiwa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF utakaa madaraka
kwa kipindi cha miaka minne.
Waliopitishwa kwenye kinyang’anyiro hicho baada ya orodha ya mwisho
iliyotolewa Oktoba 9, mwaka huu ni Clement Andrew Sanga kutoka Yanga na
Hamad Yahya Juma wa Mtibwa Sugar wanaowania uenyekiti wa TPLB.
Wengine ni Shani Christoms Mligo wa Azam FC ambaye ni mgombea pekee
wa nafasi ya Makamu Mwenyekiti. Nafasi tatu za kuwakilisha klabu za Ligi
Kuu kwenye Kamati ya Uongozi zimevutia wagombea wawili; Hamisi Mshuda
Madaki (Kagera Sugar) na Ramadhani Marco Mahano (Lipuli).
Almasi Jumapili Kasongo kutoka Ashanti United FC ni mgombea pekee
aliyejitokeza kuwania nafasi ya uwakilishi wa klabu za Ligi Daraja la
Kwanza. Klabu za Daraja la Kwanza zina nafasi mbili.
Klabu za Ligi Daraja la Pili zina nafasi moja kwenye Kamati ya
Uongozi ya TPLB, na mgombea pekee aliyejitokeza kuwania nafasi hiyo
Edgar William Chibura kutoka Abajalo FC.
EmoticonEmoticon