Na Jumia Travel Tanzania
Hivi unajua kwamba binti wa miaka nane, Roxy Getter, kutokea Florida nchini Marekani amekuwa ni mwanamke wa kwanza mwenye umri mdogo zaidi kupanda mlima Kilimanjaro mpaka kileleni mnamo mwezi Julai mwaka 2017? Kama hiyo haitoshi, Mmarekani Kyle Maynard, ambaye hana mikono wala miguu mwaka 2012 aliweza kuupanda Mlima Kilimanjaro mpaka kileleni mwenyewe bila ya msaada wowote? Licha ya kuupanda mlima huu wengine wamekuwa wakijiwekea nia ya kufanya mambo mbalimbali kwa mara ya kwanza wakiwa kileleni kama vile kundi la wachezaji wa kike 30 wa mpira wa miguu kutokea mataifa 20 walivyofanikisha azma yao ya kucheza mechi kwa dakika zote 90 kwenye urefu wa mita 4000 mwezi Julai mwaka huu!
Kuupanda Mlima Kilimanjaro ambao ndio unashikilia rekodi ya kuwa mrefu zaidi barani Afrika ukiwa na urefu wa mita 5,895 (sawa na futi 19,341) na unaoweza kupandika kwa urahisi zaidi duniani ni miongoni mwa malengo wanayojiwekea watu mbalimbali katika maisha yao kutoka kila kona ya dunia.
Yapo mambo mengi ambayo inabidi kuyafahamu kwanza kama una ndoto ya siku moja kuja kuupanda Mlima Kilimanjaro. Jumia Travel ingependa kukushirikisha dondoo zifuatazo ambazo wapandaji wengi huzitumia kabla ya kukata shauri la kufunga safari kwenda kuupanda mlima huo.
Tafiti kampuni sahihi itakayokusaidia kukuongoza kuupanda Mlima Kilimanjaro. Zoezi la kuupanda Mlima Kilimanjaro sio jambo rahisi ambalo mtu yeyote anaweza kujiamulia kufanya hivyo. Unahitajika uzoefu na utaalamu wa hali ya juu na ndiyo maana kuna watu na kampuni yenye vibali kujihusisha na shughuli hizo. Hivyo basi ili kufanikisha lengo lako itakuwa ni vema ukawasiliana na makampuni hayo, yapo mengi kwa hapa nchini na kuchagua lipi linafaa zaidi.
Panga bajeti mapema. Kama shughuli nyingine yoyote ile itakulazimu kutumia kiasi cha fedha ili kufanikiwa kuupanda mlima huu. Gharama hizo ni kwa ajili ya kugharamia safari nzima ambayo kwa kawaida huanzia siku tano mpaka kumi, chakula, malazi, mavazi, matibabu nakadhalika. Vyote hivi hushughulikiwa na kampuni utakayoichagua kukuongoza. Kwa hiyo itakubidi kuwasiliana nayo mapema ili ujue itakugharimu kiasi gani.
Tambua majira yapi ni muafaka kwa kuupanda mlima. Kwa sababu Mlima Kilimanjaro upo pale siku zote haimaanishi kwamba unaweza kuupanda muda wowote utakaojisikia wewe. Majira ya mwaka huwa yanabadilika, kuna masika, baridi, kiangazi, upepo na vinginevyo. Ushauri kutoka kwa makampuni yanayofanya kazi ya kuwapandisha watu mlima unahitajika ili kukuhakikishia safari yako itakuwa ni salama na yenye mafanikio. Kwa mujibu wa watu waliokwishaupanda mlima huu wanapendekeza miezi ya kuanzia Januari mpaka Machi na kuanzia Juni mpaka Oktoba. Kati ya miezi ya Januari na Machi hali ya hewa ni nzuri na kunakuwa hakuna watu wengi. Kuanzia Juni mpaka Oktoba, kunakuwa wa watu wengi kutokana na kipindi hiko kugongana na likizo za majira ya kiangazi kwa nchi nyingi za Ulaya na Marekani, lakini hali ya hewa ni nzuri na ya kuvutia. Ni vema kuiepuka miezi yenye mvua nyingi ya Aprili, Mei na Novemba, lakini pia unasisitizwa kubeba nguo za kukukinga na baridi kali linalopatikana kileleni mwa mlima huo kwa kipindi chote cha mwaka.
Chagua njia sahihi na rahisi kuupanda Mlima Kilimanjaro. Zipo njia saba za kuweza kukufanikisha kuukwea mlima huu mpaka kileleni zikiwa zinatofautiana kwa ugumu, msongamano wa watu, na mazingira ya kuvutia, hivyo kuchagua ile iliyo sahihi zaidi ni sehemu muhimu kwako pindi unapofanya maandalizi. Njia tatu za Machame, Umbwe na Marangu zinapatikana upande wa Kusini; mbili za Shira na Lemosho zinapatikana kutokea Magharibi na Rongai kwa upande wa Kaskazini Mashariki. Njia ya saba ni kutokea upande wa Magharibi kuanzia Lemosho kuuzunguka Mlima Kilimanjaro ikiwa imevumbuliwa siku za hivi karibuni. Muda utakaoutumia njiani mpaka kufika kileleni utategemea na njia utakayoichagua, ambapo kwa kawaida ni kuanzia siku tano mpaka kumi. Kwa mujibu wa wataalamu na waliowahi kuupanda mlima wanapendekeza kwamba njia zinazoweza kukufanikisha kumaliza zoezi zima ni zile zinazochukua muda mrefu na kupandwa kwa mwendo mdogo au wa kawaida. Hali hii huwaruhusu wapandaji kuendana na mabadiliko yanayotokana na kukwea miinuko mirefu na mikubwa. Njia ya Marangu ndiyo inayofahamika kama rahisi zaidi lakini Rongai, Lemosho na zile za upande wa Kaskazini zimeonyesha mafanikio kwa kiasi kikubwa.
Je itanichukua muda gani kukamilisha zoezi zima la upandaji mlima? Mpaka unafanikiwa kuupanda Mlima Kilimanjaro itategemea ni njia ipi utakayoichagua. Lakini kwa kawaida ili kukamilisha zoezi zima itakulazimu kutumia siku kuanzia tano mpaka kumi ukiwa njiani kuelekea kileleni. Wazoefu na wataalamu wanapendekeza muda mwingi utakaotumika kuupanda mlima huo ndio nafasi kubwa ya kufika kileleni huwepo. Na hii ni kutokana na urefu wake, njia ilivyo na mabadiliko ya hali ya hewa kuendana na afya ya mpandaji. Sio watu wote wanaoupanda Mlima Kilimanjaro hufika kileleni, wapo wanaofanikiwa, wengine wanaoishia njiani kwa kuchoka au kwa matatizo ya kiafya na wengine hufariki dunia. Hivyo ni vema kuyajua haya mapema na kujiandaa kukabiliana nayo, cha msingi ni kutokulazimisha kuendelea na safari pale unapoona mwili wako haukuruhusu kufanya hivyo ili kujipanga kwa wakati mwingine.
Nipande mwenyewe au pamoja na watu wengine? Hakuna sheria inayomlazimu mtu kuwa na watu wengine ili kuupanda Mlima Kilimanjaro. Lakini ni lazima kuwepo kwa waongozaji wenye uzoefu na utaalamu wa shughuli hiyo kwani zipo changamoto kadhaa njiani mpaka kufika kileleni. Ingawa kwa sababu zoezi zima ni kufurahia tukio hilo huwa inapendeza ukiongazana na watu wengine, inaweza kuwa mke, mume, familia, ndugu, jamaa na marafiki.
Vitu gani unahitajika kubeba kwenye begi lako? Wasiliana na kampuni itakayokuongoza kuupanda mlima ili wakupatie maelekezo ya vitu muhimu vya kupakia kwenye begi lako. Wao ndio wenye utaalamu wa vitu vinavyohitajika pamoja na uzito wa mzigo utakaoweza kuumudu mpaka kufika kileleni. Kutokana na umbali wa safari ni vema kubeba vile unavyoshauriwa kuvibeba na vitakavyohitajika njiani ili kujiepusha na usumbufu utakaoweza kujitokeza.
Nawezaje kujiandaa kwa kupanda mlima? Kukwea mwinuko wenye urefu wa mita 5,895 sio jambo rahisi kwani linahitaji maandalizi ya muda mrefu hususani kama sio mtu unayefanya mazoezi mara kwa mara. Kama jambo lingine lolote unalotaka kulifanikisha maandalizi ya mapema yanahitajika. Hivyo basi maandalizi kama vile kufanya mazoezi ya kuuweka mwili wako katika hali nzuri ili kukabiliana na mabadiliko yoyote ni muhimu, muone daktari ili kufanya uchunguzi wa afya yako kama itakuruhusu kupanda mlima lakini pia kwa wenye uwezo hukata na bima ya afya kabisa ili kugharamia matatizo ya kiafya yatakayojitokeza.
Vipi kuhusu matatizo ya kiafya? Ni vema kuchukua tahadhari ya hali ya juu kuhusiana na afya yako kabla, wakati na baada ya kuupanda mlima huu mrefu zaidi barani Afrika. Hakikisha unafanya uchunguzi wa afya yako kabla ya kukata shauri la kufanya hivyo, waweke wazi waongozaji wa safari kuhusu afya yako, hakikisha kampuni utakayoitumia ina vifaa vya kitaalamu kukusaidia pindi matatizo ya kiafya yatakapojitokeza, lakini pia itakuwa ni vema kwenda kufanya uchunguzi wa afya yako baada ya kufanikiwa na zoezi zima la upandaji wa mlima.
Hakuna jambo linaloshindikana chini ya jua, kila kitu kinahitaji dhamira ya dhati, maandalizi ya kutosha na bidii kuhakikisha linafanikiwa. Kwa mbinu hizo chache zilizoshirikishwa na Jumia Travel kwako wewe msomaji, tunaamini kwamba sasa utakuwa umepata mwanga wa kutosha juu ya vitu gani unavyotakiwa kuvifahamu kabla ya kwenda kupanda mlima huu ambao watu mbalimbali wanasafiri maelfu ya kilometa kuja kuupanda.
EmoticonEmoticon