Waziri
wa Afya Mahmoud Thabit Kombo akitoa maelezo kwa wajumbe wa Baraza la
Wawakilishi katika mkutano wa kushajihisha wajumbe hao kuhusu kifua
kikuu, Ukimwi na homa ya Ini katika Hoteli ya Ocean View Kilimani Mjini
Zanzibar.
Spika
wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid ambae alikuwa Mwenyekiti wa
mkutano huo akiufungua rasmi katika Hoteli ya Ocean View (kulia)
Mnadhimu wa Baraza Ali Salim Haji na (kushoto) Waziri wa Afya Mahmoud
Thabit Kombo.
Baadhi
ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wakifuatilia ufunguzi wa mkutano wa
kuwashahishaji kuhusu Kifua kikuu, Ukimwi na homa ya Ini uliofanyika
Hoteli ya Ocean View Kilimani Mjini Zanzibar.
Mratibu
wa huduma za homa ya Ini Zanzibar Dkt. Sania Shafi akiwaelezea Wajumbe
wa Baraza la Wawakilishi hali halisi juu ya homa ya Ini katika mkutano
uliofanyika Hoteli ya Ocean View Kilimani Mjini Zanzibar.
Mwakilishi wa Jimbo la Magomeni Rashid Makame Shamsi akitoa mchango katika mkutano huo.
Meneja
Kitengo Shirikishi Kifua kikuu, Ukimwi na homa ya Ini Dkt. Farhat Ahmed
akijibu maswali ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi katika mkutano wa
kuwashajihisha kuhusu maradhi hayo katika Hoteli ya Ocean View Kilimani
Mjini Zanzibar. Picha na Makame Mshenga.
Na Ramadhani Ali – Maelezao Zanzibar
Wajumbe
wa Baraza la Wawakilishi wameshtushwa na idadi kubwa ya vifo
vinavyotokana na homa ya Ini wakati wananchi wengi hawana uelewa juu ya
maradhi hayo na Serikali haijaandaa mikakati imara ya kupambana nayo.
Wajumbe
hao walieleza hisia zao wakati wakichangia mada ya hali halisi ya homa
ya Ini katika mkutano wa kushajihisha wajumbe hao kuhusu maradhi ya
Kifua kikuu, Ukimwi na Homa ya Ini ulioandaliwa na Kitengo Shirikishi
cha maradhi hayo katika Hoteli ya Ocean View Kilimani.
Mwakilishi
wa Jimbo la Magomeni Rashid Makame Shamsi alisema wakati homa ya Ini
inaongoza kwa kusababisha vifo vingi zaidi ikilinganisha na maradhi
mengine haikuzungmzwa katika Bajeti ya mwaka huu ya Wizara ya Afya.
Amesema
kukosekana taarifa ya homa Ini ndani ya Bajeti ya Wizara huku wananchi
hawana uelewa juu ya homa hiyo itapelekea kuenea kwa kasi na kupoteza
maisha ya wananchi.
Mwakilishi
wa kuteuliwa Ahmada Yahya ameishauri Wizara ya Afya kupitia Kitengo
Shirikishi kutoa taaluma zaidi kwa wananchi ili kuwa na uelewa mpana wa
homa ya Ini na njia za kujikinga nayo.
Spika
wa Baraza la Wawakilishi ambae alikuwa Mwenyekiti wa mkutano huo
ameishauri Kamati ya Bajeti ya Baraza hilo kuangalia uwezekano wa
kukipatia fedha Kitengo Shirikishi cha Ukimwi, Kifua Kikuu na homa ya
Ini ili kiweze kukabiliana nayo.
Mratibu
wa huduma za homa ya Ini Zanzibar Dkt. Sania Shafi aliwafahamisha
wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuwa homa hiyo ni janga kama yalivyo
maradhi ya Ukimwi na Kifua kikuu hivyo mashirikiano ya pamoja
yanahitajika katika kukabiliana nayo.
Aliwaeleza
wajumbe hao kuwa njia kuu za maambukizi ya homa ya Ini ni sawa na zile
za maambukizi ya Virusi vya Ukimwi lakini virusi vya homa ya Ini
vinakasi zaidi.
Alisema
mtu anapopata homa ya Ini hupoteza uwezo wa kufanyakazi kwa vile Ini
linaharibika na husababisha kupata saratani na hatimae kupoteza maisha.
Aliwashauri
vijana kujiepusha kufanya vitendo vinavyosababisha kupata Virusi vya
Ukimwi kwa vile maradhi hayo yanauhusiano mkubwa na homa ya Ini.
Alisema
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Afya kwa kufahamu
athari ya homa ya Ini inaendelea kufanya tafiti na hivi karibu itafungua
kliniki katika hospitali kuu ya Mnazimmoja kwa ajili kushughulikia homa
hiyo.
EmoticonEmoticon