Serikali Mpya ya Lesotho yashauriwa kutekeleza Mageuzi - SADC

June 05, 2017
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushrikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Augustine Mahiga na Mkuu wa Timu ya waangalizi ya SADC ya uchaguzi wa Lesotho akiwasilisha taarifa ya awali kuhusu uchaguzi huo .
Waziri Mahiga akiendelea kuwasilisha taarifa ya awali ya uchaguzi wa Lesotho jijini Maseru .
Waziri Mahiga bado anasoma taarifa ya awali ya uchaguzi wa Lesotho kwa wajumbe. 



Serikali Mpya ya Lesotho yashauriwa kutekeleza Mageuzi - SADC

Serikali itakayoingia madarakani baada ya Uchaguzi wa Wabunge uliofanyika nchini Lesotho Julai 3, imeshauriwa kutekeleza kikamilifu na kwa nia ya dhati maazimio yote ya Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika SADC yanayohusu mageuzi kwenye sekta muhimu za katiba, sheria na mahakama, ulinzi na usalama, utumishi na sekta ya umma na vyombo vya habari kwa muda muafaka ili kuimarisha utawala bora na wa kidemokrasia nchini humo. 

Mnamo mwezi Machi mwaka 2017, baada ya Mfalme Letsie wa III wa Lesotho kutangaza tarehe ya uchaguzi mkuu, kikao cha juu cha maamuzi cha Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC Summit), kilielekeza Serikali mpya itakayoshinda uchaguzi na kuingia madarakani, itekeleze maazimio hayo kwa kuweka muda maalum na vigezo vya utekelezaji ili kuepuka chaguzi za mara kwa mara. 

Msimamo huo wa Jumuiya ya SADC umetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania Mheshimiwa Augustine P. Mahiga, Mwenyekiti wa Kamati ya Asasi ya Ushirikiano ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC alipokuwa akitoa taarifa ya awali ya timu ya uangalizi siku mbili baada ya zoezi la upigaji kura kukamilika. 

Mheshimiwa Mahiga alisema, japokuwa zoezi la kuhesabu kura bado linaendelea, ni dhahiri kuwa wapiga kura nchini Lesotho wanatarajia mageuzi makubwa kutoka kwenye Serikali mpya yatakayoandika historia mpya nchini Lesotho, ambayo imafanya chaguzi tatu kuu ndani ya miaka mitano. 

Mapendekezo mengine yaliyotolewa kwenye taarifa hiyo ya awali ya SADC yanaitaka Serikali mpya kupitia na kufanyia mageuzi mfumo mzima wa uchaguzi ambao kwa sasa unatoa fursa kwa wabunge kuhama chama bila kupoteza ubunge wao (Floor Crossing). Alisema mfumo huo unayumbisha mfumo wa siasa na wa kibunge kwenye Falme ya Lesotho. 

Kwenye upande wa ulinzi na usalama wa raia wakati wa uchaguzi, taarifa hiyo ilisifu Tume Huru ya Uchaguzi ya Lesotho kwa kuendesha kwa weledi mkubwa zoezi la upigaji kura na kushirikiana na Jeshi la Polisi kuimarisha usalama vituoni kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi. 

Hata hivyo taarifa za awali za waangalizi wa kimataifa zimeeleza kuwa Jeshi la Lesotho pia lilionekana kwenye baadhi ya maeneo, nje ya vituo wakiimarisha ulinzi kwa mujibu wa sheria ya jeshi hilo. Balozi Mahiga alieleza kuwa japokuwa uwepo wa jeshi hakuathiri mwenendo mzima wa upigaji kura, bado kuna umuhimu wa kufanya mageuzi ndani ya vyombo hivyo ili kuainisha majukumu ya kila taasisi na kuondoa muingiliano wa kimajukumu kama ilivyo sasa. 

Mapendekezo mengine yaliyotolewa na Jumuiya ya SADC kwa Serikali mpya nchini humo ni kuweka mazingira bora yatakayowezesha wanawake na watu wanaoishi na ulemavu kushiriki kikamilifu kwenye shuguli za kisiasa bila ubaguzi. Vilevile kuifanyia mageuzi sekta ya habari nchini na kuwawezesha wananchi kupata habari za uhakika na kwa wakati.

Matokeo ya uchaguzi wa Wabunge yanaendelea kutangazwa ambapo na yanatarajiwa kukamilika ndani ya siku mbili ambapo upinzani mkali unaonekana baina ya Chama cha Democratic Congress kinachoongozwa na Waziri Mkuu wa sasa Mhe. Pakalitha Mosisili na Chama cha All Basotho Convention kinachoongozwa na Waziri Mkuu wa zamani Mhe. Thomas Motsoahae Thabane.
Imetolewa na:

Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, 
Maseru, Lesotho, 05 Juni 2017

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »