DKT KAZUNGU AINADI TANZANIA MIRADI YA NISHATI JADIDIFU UAE

January 11, 2025

 



📌Ashiriki mkutano wa 15 wa baraza la Kimataifa la wakala wa Nishati jadidifu IRENA


📌 Asema miradi ya kuzalisha umeme kwa kutumia vyanzo vya nishati jadidifu inazingatia utunzaji wa mazingira


📌Miradi kuinua uchumi wa nchi


📌 Nchi wanachama wa IRENA wakubaliana kutekeleza kwa vitendo na kuweka sera za utunzaji mazingira


Abu Dhabi, UAE


Naibu katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Dkt. Khatibu Kazungu amesema miradi ya kuzalisha umeme kwa kutumia nishati jadidifu inayotekelezwa nchini Tanzania inazingatia umuhimu wa utunzaji wa mazingira na ushirikishwaji wa wananchi kwenye maeneo yanayozunguka miradi hiyo.


Dkt. Kazungu ameyasema hayo leo Januari 10, 2025 mjini Abu Dhabi, Falme za Kiarabu, kwenye Mkutano wa 15 wa Baraza la Kimataifa la wakala wa Nishati jadidifu IRENA wakati wa mjadala wa wazi kujadili athari za mazingira na umuhimu wa miradi ya nishati jadidifu kwenye utunzaji wa mazingira


‘’Tanzania imekuwa ikitilia mkazo umuhimu wa miradi ya nishati jadidifu kwenye utunzaji wa mazingira na imeleta tija kubwa kiuchumi, kijamii na kimazingira’’ amesema Dkt. Kazungu

Aidha, ametaja faida za kiuchumi za miradi ya nishati jadidifu kuwa ni pamoja na ongezeko la ajira wakati wa utekelezaji wa miradi hiyo na kuinua hali ya kipato kwa wananchi wanaoishi kwenye maeneo ya miradi hiyo kwa kutolea mfano wa mradi wa Bwawa la kufua umeme la Mwalimu Julius Nyerere (JNHPP) ambapo takribani ajira 8,000 zimepatikana kupitia mradi huo. 



Vile vile, Dkt. Kazungu ameliambia baraza la IRENA kuwa kwa upande wa utekelezaii wa miradi ya nishati jadidifu kwa upande wa mazingira,imesaidia kupunguza hewa ya ukaa kwenye uso wa dunia yaani green house gases na kuifanya ikolojia kuwa nzuri na kuepusha ukame na kuongeza kuwa miradi mingine ni pamoja na ule wa Kishapu Shinyanga wa Megawati 150 pamoja na miradi ya joto ardhi iliyoko mkoani Mbeya na Songwe ya Kejo na ziwa Ngozi.

Wakitoa uzoefu kwenye nchi zao namna wanavyozingatia utunzaji wa mazingira kwenye miradi ya nishati jadidifu ,Waziri wa Mazingira, Tabianchi na Nishati wa nchini Slovenia Mhe. Bojan Kumer amesena kwa sasa nchi wanachana wa IRENA wanapaswa kuhakikisha masuala ya mazingira yanapewa kipaumbele na kuwekwa kwenye sera za utekelezaji wa miradi ya nishati jadidifu ili kuwepo na uwajibikaji wa kisera kwenye miradi hiyo

Amewataka wabia wa maendeleo na wafadhili wa miradi ya nishati jadidifu kutenga fedha za kutosha kwenye masuala ya mazingira na kuongeza kuwa nchi wanachama wawe na utashi wa kisiasa kutekeleza miradi hii.

Ujumbe wa Tanzania unaogozwa na Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Umeme na Nishati jadidifu Dkt Khatibu Kazungu akiwa ameambatana na Naibu Mkurugenzi Mtendaji uzalishaji Mha Costa Rubagumya, Kamishna Msaidizi wa umeme na Nishati Jadidifu Mha. Imani Mruma, Meneja Tafiti kutoka kampuni ya uendelezaji jotoArdhi Mkufu Tindi

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »