Na Grace Michael, Kigoma
MWENYEKITI wa Bodi ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Mama Anne Makinda amesema, Mfuko hautamvumilia mtu yoyote mwenye lengo la kuhujumu huduma zake kwa manufaa yake binafsi na badala yake Mfuko huo utanufaisha wanachama na Watanzania kwa ujumla.
Amesema kuwa ni wakati muafaka kwa wananchi wote kuulinda Mfuko na kujiunga na huduma zake kwa kuwa ni mfumo unaorahisisha upatikanaji wa huduma za matibabu na ndio mfumo unaotumika kote duniani.
Kaimu
Mkurugenzi Mkuu wa NHIF kwa pamoja na Mwenyekiti wa Bodi, Mama Anne
Makinda wakimsaidia Mama mlemavu aliyefika hospitalini hapo kwa lengo la
kuhudumiwa na Madaktari Bingwa.
Mama Makinda ameyasema hayo mkoani Kigoma wakati akizindua mpango wa huduma za Madaktari Bingwa unaotekelezwa kwa wiki nzima mkoani hapa na mkoani Geita kwa ushirikiano wa Mfuko na Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
“Hakuna mtu binafsi atakayetumia Mfuko huu kwa maslahi yake binafsi na sisi Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya hatutakubali kuona mtoa huduma yoyote akiharibu sifa nzuri ama utendaji ambao umeimarishwa kwa kipindi kirefu kwa ajili ya wanachama na wananchi kwa ujumla…tutasimamia huduma zetu kwa nguvu zote,” alisema Mama Makinda.
Mwenyekiti
wa Bodi ya NHIF, Mama Anne Makinda akizungumza na wananchi wa Mkoa wa
Kigoma ambao baadhi yao ni wagonjwa waliofika katika uzinduzi wa huduma
za Madaktari Bingwa mjini Kigoma.
Alionya tabia za baadhi ya watumishi wa sekta ya afya ambao wamekuwa wakitumia nafasi zao kunyanyasa wagonjwa na kusema kuwa huduma za afya ni huduma za msingi ambazo hazitakiwi kuchezewa na mtu yoyote ama kutolewa kwa utashi wa mtu binafsi.
Akizungumzia utaratibu unaoendeshwa na NHIF wa kupeleka madaktari Bingwa alisema kuwa, Mfuko uliamua kuchukua uamuzi wa kutoa huduma hizi za kibingwa katika Mikoa ambayo ina upungufu wa huduma hizo ili kuhakikisha kila Mtanzania anajivunia uwepo wa Mfuko huo.
Kaimu
Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Benrard Konga akitoa maelezo ya awali ya zoezi
la huduma za Madaktari Bingwa wakati wa uzinduzi wa huduma hizo.
“Pamoja na huduma hizi Mfuko unazo fursa nyingi hususan za uboreshaji wa huduma za afya kupitia mikopo ya vifaa tiba na ukarabati wa majengo hivyo tumieni hii fursa kujitathmini ili vituo mshirikiane na Mfuko katika uboreshaji wa sekta hii,” alisema Mama Makinda.
Kwa upande wa Mkuu wa Wilaya ya Kigoma ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa, Samson Anga aliushukuru Mfuko kwa kutoa kipaumbele cha kupeleka madaktari bingwa kwa Mkoa wa Kigoma ambao una mahitaji makubwa ya wataalam hao.
“Kwa kweli niushukuru sana Mfuko huu kwa jitihada mnazofanya na kama ambavyo mnaona hali ilivyo wananchi wamefurika hapa kwa ajili ya kupata huduma hivyo zoezi hili litaleta manufaa makubwa ya afya za wananchi wa Kigoma,” alisema Bw. Anga.
Mkuu
wa Wilaya ya Kigoma Bw. Samson Anga akiongozana na Mwenyekiti wa Bodi
ya NHIF Mama Anne Makinda wakati wakiingia katika Hospitali ya Mkoa wa
Kigoma Maweni.
Akitoa maelezo ya awali Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bernard Konga alisema kuwa zoezi hili limefanyika katika Mikoa 16 na sasa linafanyika kwa mara ya 17 na jumla ya wananchi 13,167 walihudumiwa huku wagonjwa 460 wakifanyiwa upasuaji wa magonjwa mbalimbali.
Bw. Konga alisema kuwa NHIF inatekeleza maagizo ya Serikali ya kusogeza huduma za kwa wananchi na katika huduma hizi Mfuko umejipanga katika kiwango cha juu kuhakikisha zinanufaisha wanachama na wananchi kwa ujumla.
Hata hivyo Bw. Konga ametumia fursa hiyo kuzungumza na wanachama wa Mfuko kwa lengo la kujua changamoto zinazowakabili lakini pia kupata mrejesho wa huduma wanazopata kupitia vituo vilivyosajiliwa na Mfuko.
Utaratibu huu amekuwa akiufanya katika hospitali mbalimbali kwa lengo la kutatua changamoto za wanachama na kuboresha huduma za wanachama na kuweka utaratibu mzuri utakaorahisisha wananchi wengi zaidi kujiunga na NHIF.
Huduma zitakazotolewa ni pamoja na huduma za magonjwa ya watoto, Mfumo wa Mkojo, magonjwa sugu ya ndani ya moyo pamoja na magonjwa ya mfumo wa masikio, pua na koo.
4. Madaktari Bingwa ambao watashiriki katika zoezi la kutoa huduma katika Hospitali ya Maweni Mkoa wa Kigoma.
6. Mwenyekiti wa Bodi ya NHIF, Mama Anne Makinda akisalimiana na wananchi waliofika hospitalini hapo kwa lengo la kupata huduma.
Mwenyekiti wa Bodi ya NHIF, Mama Makinda akizungumza na wananchi waliokuwa wakisubiri huduma za Madaktari Bingwa.
Mama Makinda akisalimiana na mgonjwa mara baada ya uzinduzi wa huduma za Madaktari Bingwa.
Mama Makinda alitumia fursa ya uzinduzi huo kusikiliza mahitaji ya wananchi mkoani Kigoma
Mama Makinda akitoa maelezo kwa Mama Mlemavu ambaye alitaka ufafanuzi wa huduma zinazotolewa na NHIF
EmoticonEmoticon